Naamini kuwa hii ni kazi ya kwanza ya tungo ya mashairi ya Kiswahili kuandikwa katika ukamilifu wa kitabu kupitia mkusanyiko uliotokana na kuandikwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter. Na kama ndivyo basi roho na moyo wangu ni burdan kwa kuwa mtangulizi katika hili.
Mitandao ya kijamii sasa imekuwa sehemu ya maisha yetu, na ipo hapa kwa kudumu maana jinsi ilivyopendwa na kutumiwa, mtu ungeweza kujiuliza ni vipi dunia ilikosa mfumo huu wa mawasiliano, lakini kama wasemavyo wahenga kila zama na mambo yake.

Basi ndipo nami nilipoona fursa katika zama hizi, ambapo kwa wengi tunaamini pamoja na kuwepo njia nyingi za mawasiliano ya kijamii lakini mfumo wa Twitter ndio unaonekana kupendwa na wale wanaotaka mijadala migumu na pia ya kisomi. Hutumika na watawala, wana diplomasia, walimbwende na wasanii na wana michezo wenye hadhi , na kina sisi makabwera, pangu pakavu hujigaragisha humo humo.
Katika Twitter lazima mtumiaji ajifunze kupeleka jumbe zake kwa herufi 140 ikiwemo mapengo au nafasi baina ya neno na neno. Kwa hivyo huhitaji utumiaji wa akili kupanga ujumbe katika herufi 140, seuze kuandika shairi lenye sifa ya kishairi katika nafasi hiyo ya herufi 140.
Kwa sasa mashairi katika Twitter si jambo geni duniani na yapo katika kila lugha. Wataalamu wa mashairi ya Kiingereza ya Twitter wameshatoa majina kama “micropoetry” na pia “twihaiku”. Hili la ‘twihaiku” linatokana na mashairi ya Kijapani ya kale ambayo huandikwa kwa ustadi mkubwa kwa mistari isiyozidi 4. Mfumo huo kwa Kijapani huitwa Haiku
Ila mimi nimeamua kuyaita mashairi ya kwenye Twitter kwa jina la “Tungo Twiti” na kwa jina hili naleta kazi yangu kwa wasomaji wa Kiswahili.
Muundo wa mashairi katika mkusanyiko huu wa Tungo Twiti ni kuwa mashairi yafuate mfumo wa Twitter wa herufi 140; yawe na mistari isiyopungua saba na isiyozidi 15; yawe na mstari angalau mmoja ambao una neno moja tu; yasiwe na jina au anuani ili yawe huru kwa msomaji na pia kuokoa nafasi; yawe ya mapokeo au ya kisasa wakati wa kuandikwa twitani; unayoweza kutumia nambari ndani yake au alama yoyote kama ile zile za hesabu kugawa, kuzidisha, kutoa na kujumlisha kwa mfano mashairi ya Kufanyiza na Kapuni na mwisho likipewa anuani au jina katika kitabu au nje ya twitta itakuwa ni ya neno moja tu.
Ila wakati mashairi haya au diwani hii inakamilika mara wamiliki wa mtandao wa Twita wakasikiliza maoni ya watumizi wake, lakini pia kuonyesha kuwa mtandao wa jamii una badilika kwa kasi sana, basi wakatangaza kuwa sasa herufi zitazidi kutoka 140 hadi 240, na mimi nikaingia katika jahazi hilo kama inavyoonekana katika mashairi ya mwisho mwisho katika diwani hii.
Pia katika Tungo Twiti, kama ulivyo utamaduni wa Twitter na kwa uhaba wa nafasi basi yawezekana fikra ikawasilishwa kwa zaidi ya Twitter moja lakini ikabakia na maudhui yale yale, tabaan katika mkusanyiko huu au diwani hii, baadhi ya tungo zikiambatana kwa zaidi ya moja, zimebakia na jina au anuani moja ya msingi na inayofunganisha baina yao – kwa mfano shairi Zimbabwe, Aibu na Maliwatoni.
Nakiri pia kuna mashairi yametokana na majibizano na watu wengine mtandaoni kama vile lile la Maliwatoni ambapo kulikuwa na majibizano mimi na Bwana Dan Nkurlu na nikachota ule utunzi wa upande wangu, ila fikra ya awali ilikuwa ni yake.
Mashairi haya yamekusanywa ndani ya muda wa miezi 6 ya mwaka 2017 na kipindi kigumu katika siasa za Tanzania ambapo demokrasia imeonekana kuzongwa na moshi angani na mbigili ardhini. Ni kipindi cha matukio mengi na mengi yao yamenaswa katika diwani hii. Ni kipindi ambacho nikiwa katikati ya muda wangu wa kutumikia Bunge, nikiwa Mwakilishi wa wananchi wa JImbo la Malindi, Zanzibar nikiona nimeingia siasani kipindi kizito sana.
Lakini pia matukio ya kijamii nayo yamejumuishwa kwa wingi, maana kadri tuendavyo kumekuwa na mabadiliko ya kutisha katika jamii ya Kitanzania kiasi ambacho mtu waweze ukajiuliza kama watu ni wapi tuelekeako. Twitani watu hujiuliza masuala magumu na kujibishana hoja nzito.
Kwa jumla mashairi haya au mkusanyiko huu umeakisi mapigo ya moyo wa taifa na mzunguko wake wa damu ili kutoa picha halisi ya mwili Tanzania ulivyo yaani vilio vyake, hasira zake, jaka lake la moyo, jitimai yake, kafara zake, figisu zake, vitimbi vyake na mihanga yake kwa upande mmoja na upande mwengine cheko zake, deko zake, dhihaka zake, matumaini yake na kadhalika.
Ni diwani ambayo inapaza sauti zinazotokana na msokotano na watawala, ambapo watawala hawapendi sauti hizo zije juu maana huona ni dosari kwao wakati ni faida na huimarisha uongozi. Uongozi ni kusikia na husikii kama hujaambiwa, na yule ambae hataki kuambiwa na ustawi wa mawazo huru, hupungukiwa sifa za uongozi, japo atabaki uongozini kama vile kwa mazingaombwe tu.
Nataraji mkusanyiko huu utafungua mengi katika tajuri la Kiswahili, ambalo hazina yake haijawahi kupungua bali inazidi kwa watumiaji wa lugha hii kujaza ndani yake mapya na ya msingi zaidi kuijenga lugha hiyo yetu adhimu.
TANBIHI: Kuagizia diwani hii, tafadhali bonyeza hapa.
Asante kwa ujumbe huu, nazidi kuboreka kwa mafunzo haya kwa kuwa kwangu pia kalamu haipo mbali sana nami. Jabari akuzidishie mengi mazuri maishani.