Mmojawapo miongoni mwa washairi maarufu wa Tanzania, Khamis Amani Nyamaume (1926-1971), katika shairi lake labeti nne, liitwalo ‘Saa’, alitunga akasema:
Saa za huku na huko, zimekosana majira
Sababu ni mzunguko, haufuati duara
Sasa rai iliyoko, ni kubadilisha dira
Saa zatupa majira, mafundi zitengezeni…
Mafundi zitengezeni, hasa saa za minara
Na zetu za ukutani, zipate mwenendo bora
Kazi hii twawapeni, msambe ni masikhara
Saa zatupa majira, mafundi zitengezeni…
(DIWANI YA USTADH NYAMAUME, Shungwaya Publishers, Nairobi, 1976; Mkuki na Nyota Publishers, Dar es Salaam, 2004).

Naanza kwa kuwaomba mniwie radhi kwa kuwarudisha nyuma, kwenye mjadala mfupi tuliokuwa nao kuhusu neno “kandarasi”. Mwanzo, nilikuwa nimekata shauri niyaache yapite; nisiendelee nao mjadala huu. Lakini, kisha, nikaona kwamba nisipoendelea nao nitakuwa naudhulumu mjadala wenyewe, naidhulumu lugha ya Kiswahili, na pia nitakuwa naidhulumu nafsi yangu. Na dhuluma si njema. Sababu iliyonipa kuurudia mjadala huu ni kwamba naona ulipelekwa kwengine: uliacha paa ukashika makuti!!
Kwa vile muda mrefu umepita, kabla ya kuungia pale tulipoachia, naona itakuwa vizuri mwanzo tujikumbushe kidogo mambo yalivyokwenda. Tulilokuwa tukilijadili ni kama neno lifaalo ni “kandarasi” au “mkandarasi”, na kama wingi wake ni “kandarasi” au “wakandarasi”. Kwa vile aliyeuliza (Bwana Charles Hilary) alilinasibisha neno hilo na binadamu, maoni yangu yakawa ni kwamba neno lifaalo ni “kandarasi”, na wingi wake ni “makandarasi” – kama ambavyo twasema balozi/mabalozi, shekhe/mashekhe, fundi/mafundi, na kadhalika.
Dkt. Chipila alikuwa na maoni tafauti na yangu: kwamba sawa ni “mkandarasi” na wingi wake ni “makandarasi”. Na sababu aliyoitoa ya kutilia nguvu maoni yake hayo ni kwamba, “Maneno ya mkopo ndiyo yanayokataa /m-/ au /mu-/. Maneno yenye asili ya Kibantu yanabeba /m-/ au /mu-/.” Na akatupa mifano: mtoto/watoto, mtoro/watoro, mzazi/wazazi.
Kwa kauli yake hii, na kwa maoni yake kuhusu swali lililoulizwa, yadhihirika kuwa Dkt. Chipila amelikubali neno hilo kuwa limo katika mkumbo wa maneno yenye asili ya Kibantu. Kwa vile pia neno “fundi” linakataa kiambishi /m-/, ndipo nami nikauliza: kwani neno hilo nalo ni la “mkopo”? Jawabu ya Dkt. Chipila ikawa ni: “Nakiri ujinga wangu kuhusu asili ya neno ‘fundi’.” Na leo naongeza swali jengine: Je, ni ipi asili ya haya maneno mengine, ambayo katika umoja nayo pia yanakataa kiambishi /m-/, lakini katika wingi wayo yanakubali kiambishi /ma-/ – ingawa yatumiliwa kwa watu pia? Kwa mfano, shemeji (shemegi), pwagu, zuzu, sakubimbi, bingwa, nyakanga, gwiji, bwege, gunge, sogora. Zaidi ya hayo, leo pia nauliza, tuna hakika gani kwamba hili neno “kandarasi” halina asili ya lugha ya kigeni?
Hata hivyo, hayo maoni ya Dkt. Chipila, kwamba sawa ni mkandarasi/wakandarasi, hayakunishughulisha sana. Hayakunishughulisha kwa sababu – kama nilivyopata kueleza wiki chache zilizopita tulipokuwa tukielezana kuhusu swala jengine – katika lugha hii tuliyonayo sasa, kuna baadhi ya maneno ambayo yamebadilishwa maana zake, mengine yamebadilishwa yanavyoandikwa, na mengine yamebadilishwa matamshi yake, kiasi cha kwamba hivi leo baadhi ya watu hata hawaoni tena kinyezi (kinyaa) kuyatumia hivyo, au kuyaandika hivyo, au kuyatamka hivyo. Wakati mwengine mabadiliko kama hayo huwa hayaepukiki, haswa kwa lugha kama hii iendeleayo kukua kwa kasi, na ambayo kila uchao yazidi kupata wazungumzaji na waandishi wapya. Kwa hivyo, basi, hivi leo tafauti kama hizo zimekuwa zikitumiwa kuwa ni mibadala, na huwapa watu hiari ya kulitumia wanalolitaka, bila ya kuingia makosani.
Yaani, kwa mfano, hivi leo – katika hiki Kiswahili Sanifu tulichonacho – wako watamkao au waandikao ‘ahsante’ (au hata ‘ahsanta’), na kwa wengine ni ‘asante’; au wasia/wosia/usia; arbaini/arubaini/arobaini; thalathini/thelathini; thamanini/themanini; ghorofa/orofa; tafauti/tofauti.
Au, kwa baadhi ya watu, neno ‘tahadhari’ limekuwa ni nomino, hali ya kwamba kwa asili lilikuwa ni kitenzi, ambacho nomino yake ilikuwa ni ‘hadhari’: yaani mtu anatahadhari au anafanya hadhari, au anakuwa hadhari. Au baadhi ya watu kusema au kuandika ‘kugharamiwa’ badala ya ‘kugharimiwa’; kwa sababu kitenzi cha awali kabla ya neno hili kunyambuliwa, ni ‘gharimu’. Kwa mfano, twasema, “Vitu hivi vimenigharimu shilingi mia tano.” (Au labda baadhi ya watu wamevutika kusema ‘kugharamiwa’ kwa sababu nomino yake ni ‘gharama’?) Lakini hatuwasikii au kuwaona watu kama hao wakisema, au wakiandika, ‘kubarakiwa’ badala ya ‘kubarikiwa’ licha ya kwamba nomino ni ‘baraka’; wala hakuna asemaye au aandikaye ‘kuhasariwa’ ingawa nomino yake ni ‘hasara’; na mengineyo kama hayo.
Tafauti nyengine tuliyonayo katika Kiswahili Sanifu ni kuhusu yale maneno ambayo wengine huyaunganisha, na wengine huyatenganisha. Kwa mfano, hapohapo/ hapo hapo; sawasawa/ sawa sawa; vilevile/ vile vile, na kadhalika.
YATAENDELEA, inshaAllah.
Ahsante mwalimu
Shukrani mwalimu nimekuelewa vyema.