Pale hadithi mbili zinapokutana njiani – moja ikiikimbia jana yake na nyengine ikiikimbilia kesho yake – panakuwa na fursa ya kujihakiki upya sio tu kama fanani na hadhira, bali pia kama wahusika wa hadithi zenyewe na kama watenda na watendwa wa mifumo yetu ya kisiasa na kijamii.
Ndicho kitu cha kwanza ambacho hadhira ya mchezo wa maonesho, Puma, anachoweza kujifunza. Puma, mchezo ulioandikwa, kutayarishwa na kuongozwa na Mkawasi Mcharo Hall, ni igizo linaloakisi majeraha ya Wakenya kutoka yale ya mapambano ya uhuru zaidi ya nusu karne iliyopita hadi vidonda vya mauaji ya baada ya uchaguzi wa 2006. Lakini je, sanaa inaweza kutumika kuyaponya majeraha haya na kuwapa Wakenya fursa ya kusonga mbele kama taifa moja?
Usimulizi wa hadithi
Usimuliaji hadithi una njia nyingi kwenye jamii za Waswahili, ikiwemo hii ya sanaa za maonesho, ambayo huikusanya hadhira sio kwa namna ile ya “paukwa-pakawa, mwanangu mwana siti, kijino kama chikichi”, bali kwa kuwashuhudia mafanani na watambaji wakionesha kwa vitendo mkasa ambao vyenginevyo ungesimuliwa kwa mdomo.
Kote kwenye historia yake, mwanaadamu ameitumia sanaa kujisemea na kuyasemea yanayomzunguka, ndio sababu ya sanaa kuitwa mdomo wa jamii, na ndio maana kuna ulazima wa sanaa kuakisi jamii husika. Ndipo mchezo huu wa Puma ulipo pia.
“Mchezo huu ni kuhusu makutano ya hadithi mbili. Upande mmoja, kuna msichana ambaye yupo kileleni mwa kutimiza ndoto yake kubwa maishani na, upande mwengine, kuna mwanamme mtu mzima ambaye anakimbia mateso yake ya nyuma. Wanakutana, na kile kinachotokea kwenye makutano haya ndicho kinachokuwa hadithi ya mchezo wenyewe,” anasema Mkawasi.
Na kweli. Ndani ya Puma muna hadithi mbili zinazokutana – moja ni ya Mwalimu Kulungu, mtendwa wa mauaji ya 2006 – 2007 nchini Kenya, ambaye alimpoteza mke wake na mtoto wake mchanga, aliyezaliwa usiku ule ule yalipoanza machafuko baada ya uchaguzi mkuu.
Kwenye jukwaa la Jumba la Maonesho la Taifa jijini Nairobi mwanzoni mwa mwezi Disemba 2015, mwandishi alimshuhudia muhusika huyu akitamba kwa malalamiko na maumivu: “Siku ile jirani yangu alikuja na kuniambia kuwa kuna watu wanakuja kuichoma moto nyumba yangu. Tulikuwa tumejenga nyumba yetu hapo, lakini sasa tulionekana kama wageni, kama watu wa kabila lisilofaa. Nilikuwa mwalimu kwenye Mavani Forest, nikingojea shule zifunguliwe kwa mwaka mpya. Nilikuwa na nafasi kubwa ya kuwa msaidizi mwalimu mkuu. Siku hiyo mke wangu alikuwa nyumbani, tulikuwa tukitegemea kupata mtoto wa kwanza baada ya kuhangaika muda mrefu kwenye ndoa yetu….”
Upande mwengine ni hadithi pia ya Tunu, bintiye Salma ambaye ana ndoto ya kuimba mbele ya Rais wa Jamhuri ya Kenya siku taifa lao linapotimiza nusu karne. Ndoto yake inajikuta kwenye mtihani, pale pumu (na sio puma) ilipompandia njiani akikimbilia kuitimiza ndoto hiyo. Mwenzake, Kalole, anasikika akimuhimiza ajiinuwe na waende hivyo hivyo: “Kimbia Tunu. Kimbia…. Tutachelewa… tutakuta sherehe zimekwisha. Na kumbuka ulisema baba yako anakuja kukuona ukiimba. Lazima uharakishe Tunu.”
Hadithi ndani ya hadithi
Lakini ndani ya hadithi hizi mbili zinazokutana, ndimo pia munamoibuka hadithi nyengine tata na changamano kwenye jamii ya Kenya. Mojawapo ni ya mama yake Tunu, Salma, ambaye sio tu kuwa anabeba machungu ya kuzaa na mchungaji wa kanisa anayemkana bintiye, bali pia taifa linalomkana yeye na jamii yake nzima ya Wanubi wa Kibera.
“Kwa muda wote nimechukuliwa kuwa mimi si raia halali wa nchi hii. Nchi yangu mwenyewe. Nchi waliyozaliwa baba na mama yangu. Mimi ni Mnubi. Daima nimekuwa nikipigania kupata elimu na kazi ya heshima. Lakini, hapana, wanatoa madai yasiyowezekana. Eti nilete vyeti vya kuzaliwa vya bibi na babu zangu. Lakini waliishi Kibera miaka mia kadhaa iliyopita, nimesema. Tunafukuzwa kwenye maofisi ya serikali kama kuku waliokwenda kuchafua nyumba za matajiri,” analalamika Salma.
Kwenye makutano ya hadithi hizi, mtazamaji anakutanishwa uso kwa uso na matokeo machungu ya dhuluma ya kijamii na kisiasa kwa watoto wa taifa la Kenya, mojawapo ni jaala ya akina Boss na rafikiye – watoto wanaoishi mazingira magumu mitaani, maarufu kama chokoraa. Na ndani yao, licha ya magumu wanayopitia, unakutana na sura nyengine ya ubinaadamu. Ni wao wanaosaidiana na Mwalimu Kulungu, Bibi Truvera na Kolela kumpeleka Tunu hospitalini.
Ujumbe wa hadhira kwenda nao nyumbani
Ndani ya kipindi cha nusu karne ya uhuru wake, taifa la Kenya limepitia kwenye masaibu kama haya, ambayo ingawa ni hadithi za mtu mmoja mmoja, jamii moja moja na hata mtaa mmoja mmoja, lakini kwa ujumla wake ndizo zinazojenga moja ya taswira za Kenya iliyotusimamia mbele yetu.
Na zote zimo kwenye onesho la Puma, ambalo baada ya kuliangalia kwa makini, hadhira inaondoka na ujumbe mmoja mzito – nao ni kwamba jamii inapaswa kuponyeshwa majeraha yake.
Ndivyo alivyoniambia Kate, ambaye alikuwa sehemu ya hadhira iliyoangalia pamoja nami onesho hili: “Ukifiria zile ghasia zilizotokea, ni sisi vijana ndio ambao tulizifanya kwa wingi. Na sisi kama watu tuliofanya ghasia zile hatukupona madonda yetu, tutayahamishia haya kwa watoto wetu. Na hilo si jambo zuri.”
Lakini kwa hadithi kusimuliwa ikasimulika katika onesho la jukwaani na kuifanya hadhira iondoke na ujumbe halisi ambao mtayarishaji alitaka kiwe kifurushi cha mwisho kabisa kubebwa na hadhira yake kwenda nacho nyumbani, kunahitaji ubunifu mkubwa wa sio dhamira ya onesho, bali pia lugha na ujenzi wa wahusika.
Uhalisia wa wahusika
Nje ya jukwaa, nilikutana na waigizaji wenyewe. Mmoja wao ni Robert, ambaye kwenye Puma ndiye Mwalimu Kulungu anayekimbia hisia kali za mateso ya jana yake na kujificha nyuma ya hasira. “Mimi ndiye niliyebebeshwa dhamana nzima ya mchezo. Nilipaswa kuzitoa nguvu na hisia zangu zote ili ujumbe ufike kuwa haya yaliyotokea, basi tena. Imetosha!”
Kuna pia Janet, ambaye kwenye mchezo anacheza nafasi ya Truvera, mwanamke msakaji mali ambaye inamchukuwa muda mrefu kuja kuujuwa ubinaadamu lakini anapoujuwa tu, anausimamia kwa nguvu sake zote.
Yeye aliniambia mapenzi yake kwa sanaa ni makubwa mno kiasi cha kwamba ndio pumzi na uhai wake. “Nikipewa uhusika, huuingia ndani yake na nikaishi humo, hadi mtu akiniona njiani husema kuwa nilivyo jukwaani ndivyo nilivyo kwenye uhalisia.”
Hili la kuuvaa uhusika na kuugeuza uhalisia, ndilo pia analosema muhusika Kolela, kijana wa miaka 20 aliyeigiza nafasi ya mtoto wa shule ya msingi, na kweli ukimuona sura yake na ukamsikia sauti yake jukwaani haikupitikii hasa kuwa si kitoto cha miaka minane.
“Yote inaanzia kwenye uzingatiaji. Kisha kitu cha pili ni kujiweka kwenye ule wakati wenyewe. Na jambo la tatu ni kufuatilia.”
Kuisimulia hadithi kama njia ya kuponya majeraha
Si jamii nyingi ulimwenguni zenye uthubutu wa kugeuka nyuma kuyaangalia madonda ya kihistoria yaliyosababishwa na ama mifumo yao ya kisiasa au kijamii. Badala yake, wengi huhiyari kuangalia mbele kwa kuamini kuwa kufukuwa makaburi kunaweza kuwa na maana mbaya kwa utulivu wa kijamii uliopatikana baada ya maafa kama yale ya Kenya ya mwaka 2006.
Hawa ni wale wanaoamini kuwa mtendwa ana wajibu wa kunyamaza, ikiwa kuyasema mateso aliyopitia kutamaanisha kuivuruga jamii yake. Hali kama ya Zanzibar baada ya mavamizi ya mwaka 1964 ambayo yaliangamiza maelfu ya roho za wasiohatia inahusika kwenye mfano huu. Hadi leo, Wazanzibari walioumizwa na uvamizi huo wanahisabiwa kama hawana haki ya kuelezea maumivu yao!
Lakini huo si mtazamo wa Mkawasi, ambaye anasema lazima jamii iisemee mikasa yake, watu wapewe nafasi ya kufunua madonda yao ili yaponywe. “Ni muhimu kusimamisha haki, maana bila ya haki hatuwezi kusonga mbele kama Wakenya na kama Waafrika. Hadithi zetu zitufanye tusisahau, kwani tukisahau tutarejea tena.”
Kwa hivyo, inahitaji ujasiri wa kiuandishi kuichukuwa hadithi chungu ya jamii yako na kuigeuza kuwa kipande cha sanaa, ambacho kinalenga kupaundaunda pale palipokwishabovuka!