KISWAHILI KINA WENYEWE

Mkosha hukoshwa

Unaijua methali ya Kiswahili “Mkosha naye hukoshwa”? Katika maana ya kawaida ni kwamba maiti katika mila za Waswahili hukoshwa na kufanyiwa taratibu nyengine kabla ya kuzikwa. Ukiwacha watu wa karibu wa familia, wakoshaji huwa ni watu maalum kwenye jamii. Mara nyingi ni watu wazima, wenye busara za hali ya juu na wanazuoni.

Hekima ya kuteuliwa watu hawa ni uwezo wao wa kutunza siri za marehemu, maana Uswahili unamtambua hata maiti kuwa ni mja mwenye haki zake kubwa, zikiwemo haki za mambo yake ya ghaibu. Kwa hakika hasa, Waswahili wanamtambua maiti kuwa na haki na nguvu kubwa zaidi, pengine hata ambazo hakuwahi kuwa nazo katika uhai wake.

Katika maana yake ya matumizi, methali hii inakusudia kuwa hata yule mtu anayefanya jambo kubwa kabisa dhidi au kwa ajili ya mwenziwe, basi naye kuna siku jambo kama hilo litatendwa kwake. Kuna siku mkosha maiti naye atakufa na atakuwa marehemu anayehitaji kukoshwa. Siku hiyo hatakuwa mkosha maiti tena, atakuwa muoshwa. Atakoshwa.

Juzi, mtangazaji wa Radio Maisha FM ya Nairobi, Geoffrey Mung’ou, alizungumza nami kwa ajili ya kipindi chake cha Magwiji wa Lugha kinachorushwa moja kwa moja na redio hiyo ya Kenya. Tangu nimeanza kazi ya utangazaji kwa mwaka wa tano sasa huu, sijawahi kuhojiwa na kituo cha redio isiyokuwa Idhaa yangu ya Kiswahili ya Deutsche Welle hapa Bonn, Ujerumani.

Badala yake, ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano, nimeshafanya mahojiano mara zaidi ya 50 na watu wa kila aina – kutoka viongozi wakubwa wa kisiasa Afrika ya Mashariki hadi wananchi wa kawaida mitaani.

Majuzi ilikuwa zamu yangu. Mkosha nikakoshwa na mkoshaji alikuwa ni Geoffery Mung’ou. Sikiliza hapo chini namna nilivyokuwa nikimiminiwa maji.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.