KISWAHILI KINA WENYEWE

Alimaye ‘pantosha’, atavuna ‘pankwisha’

Mazungumzo ya swahibu na mwandani wangu yalikuwa na maana kubwa leo kwa sababu ya misemo miwili ya Kiswahili aliyonitolea na kunifafanulia. Mmoja ni huo uliobeba jina la makala hii: “Alimaye pantosha, atavuna pankwisha.”

Kwa hakika, Kiswahili kina bahari pana sana ya fasihi na hekima zake. Hufika mahala nikawa ninajiuliza hawa tunaowaita wahenga walikuwa na akili kubwa kiasi gani hasa hata wakawa waliweza kutoa kauli za miaka elfu kadhaa nyuma na hadi leo maneno yao yanasimama kama shujaa vitani. Hayaanguki. Hayatikisiki.

Angalia busara iliyofumbatwa na msemo huu ambayo inaweza kufumbuliwa na kumuongoza mtu maisha yake yote kuelekea ustawi na mafanikio. Waswahili wamesambaa kote upwa wa Afrika ya Mashariki na bara yake, ambako kilimo ni miongoni mwa njia kuu za uchumi, hivyo takribani kila  Mswahili anaijuwa misamiati inayoambatana na kilimo na ulimaji.

Mimi ambaye nimelelewa na kukulia kwenye nyumba ambayo wazazi wote walikuwa wakulima, ninajuwa maana ya kulima panapotosha, maana hata mimi mwenyewe zama za ubarobaro wangu nilikuwa naiishi kauli hiyo. Kwa mfano, katika moja ya mashamba yetu ya mpunga, baba yangu alikuwa ananikatia kipande ambacho nilitakiwa kukilima ndani ya kipindi maalum kwa kuambatana na msimu ili kuwahi usiaji. Kipande chenyewe kingenichukuwa muda wa wiki kadhaa kama si mwezi mzima hata kama si kikubwa, kwa sababu kila asubuhi nilikuwa nakwenda kupiga majembe mawili matatu kisha ninajisemea “pashatosha kwa leo”.

Wenzangu wanaopiga majembe 100 kwa siku wanamaliza kipande kama changu kwa siku tatu, mimi naselelea nacho, lakini kwa kuwa kimewekwa mpaka wa pegi na kamba, ndio kinakuwa kimeniganda hicho. Matokeo yake ni kuwa zinaweza kunyesha mvua za usiaji, nami sijamaliza kuburuga, na hatimaye nikawa mtu wa mwisho kusia na pengine kipande changu kikawa cha mwisho kuwa na mpunga mzuri. Nikavuna ‘pankwisha’. Yaani ama nisingelivuna kitu au ningelivuna kidogo mno kiasi cha kwamba nikidondoa mashuke matano sita, ndio mavuno yote yamekwisha!

Naam, leo mwandani na swahibu yangu amenirejesha kwenye kumbukumbu za utotoni na msemo ambao sikuwa nimewahi kuusikia, lakini ambao nimewahi kuuishi katika uhalisia wake – shamba, kilimo, ukulima, mazao. Ameurudisha sasa ukiwa na maana pana zaidi kwangu, kwa kuwa umeondoka shambani na kusafiri moja kwa moja kuingia maishani mwangu na mwetu, kwa ujumla.

Hapa ndipo unapogundua kiwango cha juu cha hekima za wahenga wa Uswahilini. Kwamba kauli zao hazina mipaka ya kiwakati wala kijiografia – ni za muda wote, ni za mwahala mote. Hata huku Ulaya niliko, hata baada ya miaka takribani 20 ya kuacha kubeba jembe langu kwenda shambani kulima, bado msemo huu una maana kubwa kabisa. Unaniambia kuwa ikiwa ninafanya mambo yoyote yanayohusu ustawi wa maisha yangu kwa mtindo wa kivivuvivu (pantosha), basi sitakuwa na mafanikio makubwa wala ya kudumu (pankwisha).

Na hii ninaichukuwa kutoka kiwango cha chini kabisa cha mtu binafsi (mimi na maisha yangu), kisha ninapandisha ngazi hatua kwa hatua – kifamilia, kikazi, kijamii, kitaifa na hadi kimataifa – na majibu yake yanakuwa ni yale yale.  Wafanyakazi wanapokuwa hawazitowi nyoyo zao zote kwa kile wanachokifanya na wakawa  hawawekezi nishati, akili na muda kwa jambo ambalo lina maslahi kwenye kazi yao, hawezi kupata maslahi hayo na hivyo hawataweza kuendelea. Ndivyo ilivyo kwa jamii, ndivyo ilivyo kwa taifa, ndivyo ilivyo kwa mataifa.

Najuwa kuna misemo mingine ya Kiswahili ambayo inaweza kuwa inapingana na msemo huu, kama ule usemao ‘Jitihada haiondoshi kudura’, lakini busara ya kila msemo ni kuutafasiri kwa muktadha wake. Huu wa leo ukiutafsiri vyema kwenye muktadha wake unakupa moyo kwamba kila unapojitahidi kufanya mengi zaidi na kujitoa zaidi kwa ajili ya jambo lako, basi matokeo yake yatakuwa tafauti na yule ambaye anafanya jambo lake kivivu na kiviya.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.