Kongamano la siku tatu la kimataifa juu ya taaluma za Kiswahili limemalizika mchana wa leo katika mji wa Bayreuth, kusini mwa Ujerumani, kwa wataalamu na washiriki kutoka zaidi ya mataifa na vyuo vikuu 20 ulimwenguni kuazimia haja ya kuunganisha nguvu kukipa Kiswahili uthubutu na nafasi yake kinachostahiki kwenye ulimwengu wa sasa kwani tayari kimejipambanua chenyewe kuwa lugha inayoliwakilisha na kulisemea bara zima la Afrika.
Ingawa dhima kuu ya kongamano hili la 28 la Kiswahili mwaka huu, ilikuwa ni kulinganisha mitazamo ya matumizi ya lugha hii katika nyanja za isimu, fasihi na utamaduni, siasa za uzalendo na umoja wa Afrika zilitanda takribani mijadala ya mada zote. Katika siku hii ya mwisho ya kufungia kongamano, wataalamu wameweka msisitizo juu ya nafasi ya Kiswahili katika ulimwegu wa sasa, na haja ya Waswahili wenyewe kuhakikisha kuwa hawawi nyuma kwenye kukijengea Kiswahili nafasi yake katika jukwaa la kimataifa. Dokta Aldin Mutembei wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema nafasi ya Kiswahili haiwezi tena kupuuzwa na dunia, kwani “tayari ni sauti ya Waafrika”.
Mwangwi wa siasa hizo za kizalendo pia uliakisika kwenye mada ya matumizi ya lugha mkato katika utumaji wa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu za mkononi, ambapo mhadhiri wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Ghana, Bi Josephine Dzahene-Quarshie, yeye mwenyewe akiwa mzaliwa wa Ghana, aliiambia DW kwamba miaka takribani 50 tangu mwasisi wa taifa la Ghana, Dk. Kwame Nkrumah, kutamka kwamba Kiswahili ndicho kiwe lugha ya Afrika moja iliyoungana, ukweli huo bado umesalia “ingawa ndoto ya Afrika Moja haijatekelezwa.”
Kongamano la safari hii liliwakutanisha washiriki kutoka Tanzania, Kenya, Msumbiji, Rwanda, Ghana, Ujerumani, Italia, Marekani, Uingereza, Austria na Ufaransa. Jumla ya mada hamsini ziliwasilishwa na kujadiliwa, kutoka zile zilizolinganisha tanzu ya ushairi katika fasihi ya Kiswahili hadi zile zilizolinganisha lahaja, maneno na matumizi ya lugha katika mataifa yanayotumia Kiswahili.
Vile vile, washiriki walitumia sehemu ya muda wao katika siku ya kwanza ya kongamano hili kuukumbuka mchango wa Omar Babu Marjan, ambaye alikuwa mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Cologne hapa Ujerumani, mwandishi na mshairi, aliyefariki dunia siku mwanzoni mwa mwaka huu.
Alikuwa ni Profesa Ken Walibora, rafiki na mshirika wa karibu wa Marehemu Omar Babu katika zama za uhai wake, ndiye aliyerejesha simanzi kwa kuwaghania washiriki sehemu ya wimbo wa taarab ambao Omar Babu alipenda kuuimba.