Ndimi mvuvi halisi, kulla vuvi nalijuwa
Nivuwaye mikambisi, na papa wenye khatuwa
Wala sivui vingisi, mishipi haisumbuwa
Nimekwambiya elewa
Sivuwi bahari ndogo, hatia nanga fuoni
Havisimbika vigogo, vilivyozama majini
Na wala Sivuwi ngogo, vidagaa na mbinini
Siwavui asilani
Jabali hulijilisi, jishipi nikalitupa
Haotea mifulusi, na nguru na mijipapa
Si kasikazi si kusi, khabari yangu nakupa
Wala sivui kwa pupa
Na nivuapo malema, huingia ndani ndani
Maji yangu ni ya pima, thalatha u thalathini
Na ndiyo ninayozama, lema halibwaga tini
Uliza mimi n’nani?
Na nivuapo maziyo, mavuvi ya kizamani
Kwa hino hali niliyo, huvua kwa kutamani
Hatafuta kiteweyo, cha wali mwema kombeni
Haandaa siniani
Ela uvuvi wa juya, kuvua siutamani
Sababuye ‘takwambiya, ufahamiwe mwendani
Ni kwambakwe huingiya, samaki waso thamani
Kama wewe mwafulani
Ni kuu yangu bahari, elewa sana elewa
Huko hakwendi vihori, wala vyenu vimashuwa
Shoti nahodha hodari, kisha ende kwa ngalawa
Na milango kuijuwa
“Malenga wa Mvita: Diwani ya Ustadh Bhalo Ahmad Nassir” ukurasa wa 34