KISWAHILI KINA WENYEWE

Vitenzi Vitatu: Kuwa, Kuwako na Kuwa na

Kiswahili kina vitenzi hivi vitatu, ambavyo licha ya kuwa na maumbile yanayokaribiana, vina maana tafauti. Vitenzi hivyo ni kuwa, kuwako na kuwa na. Hiki kitenzi kuwako kinaweza pia kuandikwa kuwapo au kuwamo kwa mujibu wa muktadha unaohusika; lakini hiyo si mada kwa leo. Mada ni kuangalia mgusano na muachano wa vitenzi hivi vitatu vya kuwa, kuwako na kuwa na.

1. Kuwa na Kuwako

Waingereza wana kitenzi to be na Wajerumani wana kitenzi sein kumaanisha vitenzi viwili tafauti vya Kiswahili vya kuwa na kuwako. Katika Kiswahili, tunatumia kitenzi kuwa kuelezea “dhati” na kuwako kuelezea “uwapo wa dhati yenyewe”. Na kwa sababu ya kuwasilisha maana tafauti, ndio maana pia unyambuaji na uambishaji wa vitenzi hivi viwili katika Kiswahili ni tafauti, ingawa kwenye Kijerumani na Kiingereza huwa ni mmoja.

Kwa mfano, katika Kiingereza na Kijerumani ninapotaka kuzungumzia dhati na uwapo wangu, ninaweza kusema:

Kiingereza:
i. I am Mohammed (dhati)
ii. I am in Germany (uwapo)

Kijerumani:
i. Ich bin Mohammed (dhati)
ii. Ich bin in Deutschland (uwapo)

Kwa Kiswahili ninatumia vitenzi viwili tafauti:

i. Mimi ni Mohammed (dhati)
ii. Mimi nipo Ujerumani (uwapo)

Vitenzi hivi, kuwa na kuwako, vinapishana na kukutana pia katika uambishaji na unyumbuaji wake. Ambapo kitenzi kuwa hubadilisha kabisa mzizi wake wa neno kinapokuwa katika wakati uliopo, kitenzi kuwako hubakia na kiambishi chake –ko (au –po au –mo) katika wakati uliopo. Lakini vyote viwili, kuwa na kuwako, kubakia na neno zima kama mzizi katika wakati uliopita, ujao, hali kamilifu na shurutia na kuwekewa tu viambishi awali vya nafsi, nyakati na hali hizo.

Hebu tutafsiri maelezo haya kwenye mifano hii:

1.1. Kuwa (wakati uliopo)

i. Mimi ni mwanafunzi
ii. Wewe ni mwanafunzi (inaweza pia kuwa “wewe u mwanafunzi)
iii. Yeye ni mwanafunzi (inaweza pia kuwa “yeye yu mwanafunzi)
iv. Sisi ni wanafunzi (inaweza pia kuwa “sisi tu wanafunzi)
v. Nyinyi ni wanafunzi (inaweza pia kuwa “nyinyi mu wanafunzi)
vi. Wao ni wanafunzi

1.2. Kuwa (wakati uliopita)

i. Mimi nilikuwa mwanafunzi
ii. Wewe mulikuwa wanafunzi
iii. Yeye alikuwa mwanafunzi
iv. Sisi tulikuwa wanafunzi
v. Nyinyi mulikuwa wanafunzi
vi. Wao walikuwa wanafunzi

1.3. Kuwako (wakati uliopo)

i. Mimi nipo Ujerumani
ii. Wewe upo Ujerumani
iii. Yeye yupo Ujerumani
iv. Sisi tupo Ujerumani
v. Nyinyi nipo Ujerumani
vi. Wao wapo Ujerumani

1.4. Kuwako (wakati uliopita)

i. Mimi nilikuwapo Ujerumani
ii. Wewe ulikuwapo Ujerumani
iii. Yeye alikuwapo Ujerumani
iv. Sisi tulikuwapo Ujerumani
v. Nyinyi mulikuwapo Ujerumani
vi. Wao walikuwapo Ujerumani

2. Kuwa na

Katika maana, kitenzi kuwa na kinasimamia dhana ya umilikishi. Tunasema, kwa mfano, ‘Juma ana gari’, tukimaanisha anamiliki au angalau imo kwenye himaya yake. Dhana hii ya umilikishi ndiyo pekee inayomaanishwa na kitenzi hiki, kwa mintarafu kuwa hakiwakilishi dhana nyengine yoyote kama ambavyo kitenzi kama hiki kwenye Kiingereza (to have) na Kijerumani (haben) hufanya kazi nyengine ya kuwa kitenzi kisaidizi cha ama hali timilifu (kwenye Kiingereza) au, na pia, kisaidizi cha wakati uliopita (kwa Kijerumani).

Waingereza husema, kwa mfano: ‘I have seen him’ au Wajerumani: ‘Ich habe ihn/sie gesehen’, zote mbili zikimaanisha: ‘Nimemuona’. Mote humo kimetumika kwa maana ya ziada ya kuwa kitenzi kisaidizi. Nasema maana ya ziada, maana katika maana yake ya msingi inakutana na hii ya Kiswahili ya ‘kuwa na’ – umilikishi. Sentensi ‘I have some money’ ya Kiingereza na ‘Ich habe Geld’ ya Kijerumani zote zinamaanisha ‘Mimi nina pesa’ kwa Kiswahili.

Unyambuaji na uambishaji wa kitenzi kuwa na, hata hivyo, hautafautiani sana na kitenzi kuwako. Vyote viwili hubakia na sehemu yake ya mwisho kama mzizi (-ko kwenye kuwako na na kwenye kuwa na) katika wakati uliopo na kubakia na neno zima kama mzizi katika wakati uliopita, ujao, hali kamilifu na shurutia na kuwekewa tu viambishi awali vya nafsi, nyakati na hali hizo.

Tena tutumie mifano hii kubainisha tunachokusudia:

2.1 Kuwa na (wakati uliopo)

i. Mimi nina gari
ii. Wewe una gari
iii. Yeye ana gari
iv. Sisi tuna gari
v. Nyinyi muna gari
vi. Wao wana gari

2.2. Kuwa na (wakati uliopita)

i. Mimi nilikuwa na gari
ii. Wewe ulikuwa na gari
iii. Yeye alikuwa na gari
iv. Sisi tulikuwa na gari
v. Nyinyi mulikuwa na gari
vi. Wao walikuwa na gari

3. Makosa Yanayofanywa

Kuna watumiaji wa Kiswahili ambao kimakosa hulazimisha unyumbuaji na uambishaji wa vitenzi hivi vitatu – kuwa, kuwako na kuwa na – kwa kufuata utaratibu wa muundo wa A-AWA kwenye kundi la YU-A-WA. Kwa kufanya hivyo, husema kwa mfano: “Huyo Juma ako wapi sasa?“ wakimaanisha “Huyo Juma yuko wapi sasa?“. Husema pia “Watu wako na kazi nyingi sana hapa“ makusudi yakiwa “Watu wana kazi nyingi sana.“

Hivyo sivyo kabisa!

1 thought on “Vitenzi Vitatu: Kuwa, Kuwako na Kuwa na”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.