KISWAHILI KINA WENYEWE

Si kila nomino yaweza kugeuzwa kitenzi

Lugha ina sifa moja kubwa ya kuwa chombo cha mawasiliano. Nje ya mawasiliano, lugha haina manufaa mengine. Ingawa mawasiliano yenyewe, baadaye, huzaa manufaa kadhaa wa kadha kwa jamii ya kibinaadamu. Katika kuwasiliana – na kwa kuwa ndiyo kazi pekee ya lugha – mwanaadamu hutumia kila mbinu inayowezekana ili kuyarahisisha mawasiliano yenyewe.

Lakini ukweli huu ndio unaotutega wengi kwenye matumizi ya lugha. Kwamba kwa kuwa tunaamini lugha ipo kurahisisha mawasiliano, basi hudhani kuwa tumepata kibali cha kuitumia lugha hiyo vyovyote, almuradi tu tumeyarahisisha mawasiliano.

‘Vyovyote’ hivyo huwa ni pamoja na kukiuka kanuni na taratibu za lugha na au kutumia kanuni moja kwa kila neno na kila mazingira. Hoja? Tunarahisisha mawasiliano.

Hapa nitapiga mfano wa namna uchanganyaji wa kanuni za lugha kuiharibu lugha yenyewe kwa hoja ya kurahisisha mawasiliano, na hivyo kutufanya tunase kwenye mtego wa kuivuruga lugha tunayodai kuitukuza. Miongoni mwa kanuni za lugha ni kwamba aina moja ya neno huweza kugeuzwa (kwa kanuni ya uambishaji) kuwa aina nyenginezo za maneno. Angalia hata hili neno rahisi linavyoweza kuwekwa viambishi na kugeuka maana yake:

Rahisi – kivumishi, kielezi
Rahisisha – kitenzi, maana yake ‘fanya kitu kiwe rahisi
Urahisi – nomino 1, kwa maana ya hali ya kuwa rahisi
Urahisishaji – nomino 2, kwa maana ya namna au njia za kufanya kitu kuwa rahisi.

Lakini  ambapo neno rahisi linaweza kugeuzwa aina mbalimbali za maneno kupitia kanuni ya uambishaji, si kila kivumishi au kielezi kinaweza kugeuzwa kuwa kila aina ya neno. Nakusudia kuna vivumishi vinavyoweza kufanywa nomino, kwa mfano, lakini haviwezi kuwa kitenzi. Vivyo hivyo, si kila nomino inayoweza kuwa kitenzi na kadhalika, na kadhalika.

Kwa mfano, neno baya ni kivumishi. Linaweza kuwekwa kiambishi awali u na kuwa nomino ubaya. Lakini haliwezi kugeuzwa kitenzi kama kivumishi rahisi kilivyofanywa hapo juu na kuwa bayisha, ikikusudiwa fanya kitu kiwe kibaya au kufanywa nomino ubayishaji kwa maana ya njia ya kufanya kitu kuwa kibaya. Hilo haliwezekani kwa neno hili.

Nitapiga mfano mwengine. Kwa hoja hiyo hiyo ya kurahisisha mawasiliano, kanuni za lugha zinakubali kuyageuza baadhi ya maneno yenye kuundwa na vishazi (neno zaidi moja) kuwa neno moja. Neno kupata bahati au kuwa na bahati huweza kuwa kubahatika. Tunasema “Fulani amebahatika sana, kumaliza masomo tu akapata kazi”. Lakini kupata au kuwa na pesa sio kupeseka.

Kwa nini basi kanuni moja ikubalike kwenye neno moja la aina hiyo hiyo na isifanye kazi kwenye neno jengine? Kwa sababu Kiswahili ni lugha. Na kama zilivyo lugha zote za kibinaadamu, hii nayo ni mkusanyiko wa sauti za nasibu. Ina kanuni zake lakini kanuni zake ni zile zilizotokea kukubaliwa na wenyewe wenye lugha na sio zipangwazo kwenye mabaraza na makongamano.

Hapo patoshe kwa leo.

2 thoughts on “Si kila nomino yaweza kugeuzwa kitenzi”

 1. Majadiliano kati ya Mohammed Ghassany na Ally Mahadhy kuhusu mada hii kupitia Facebook:

  Ally Mahadhy: “Maalim Ghassany, lakini lugha si inasifa ya kiumbe hai, bimaana inazaliwa, inakuwa na inakufa? Je huoni kuwa itakuwa tunazuia ukuaji wa lugha ya kiswahili ikiwa hatutaruhusu kuzuka kwa maneno mapya ya lugha au kubadilikia kwa sarufi za maneno kutokana na muda au sehemu ya watu husika! Na nnavyojuwa kiswahili ni kimoja kama lugha, lakini kina lahaja tofauti, lahaja za kipemba haziwi sawa na za kiunguja, jee kivipi watamani lahaja za wa Tanganyika ziwe sawa na za kipemba? Kwanini tusiache lugha itimize sifa zake hizo tatu, yaani ishazaliwa, sasa inakuwa na baadae ife? Naomba maarifa zaidi maalim wangu!”

  Mohammed Ghassany: “Bwana Ali tabia ya kuzaliwa, kukua na kufa kwa lugha ndiyo hiyo hiyo inayotumiwa kimakosa kama hoja ya kukivuruga Kiswahili. Matokeo yake ndiko huko kukiuwa, maana mwisho wa siku tukikubali kila ‘Kiswahili’ kiwe Kiswahili kwa hoja ya kuwa kila pahala pana tabia zake, hapatakuwa tena na Kiswahili. Hali ni sawa na Kiingereza. Huzungumzwa Nigeria, Jamaica na kwengineko, lakini haisemwi wala haikubaliki kuwa hivyo ndivyo ‘viingereza’ sahihi. Kutumia lugha fulani hakukufanyi uwe mwenye lugha hiyo. Kila lugha ina wenyewe na wenyewe hao ndio kanuni na kawaida zao za kisarufi hufuatwa kuwa msingi wa lugha hiyo.

  Ama kuhusu la lahaja, sipingani nalo. Lakini lahaja hata ziwe nyingi vipi, hazivunji kanuni za lugha husika. Kimrima kwa mfano, hakisemi kuwa kila neno lazima liwe na wingi na umoja, hakilazimishi kila kitenzi kugeuzwa nomino. Kunaweza na tafauti za sauti au herufi chache lakini sio kugeuza sarufi nzima.

  Na mwisho dhana ya kuzaliwa, kukuwa na kufa inarejea kwenye uhalisia wa mwanaadamu. Hivyo kama mwanaadamu azaliwavyo na wazazi wake, na lugha inao wake na ina kwao. Si yule anayeitwa mtoto wa mitaani. Mtoto huyu akikuzwa vyema atakuwa mwema, na akikuzwa vibaya atakuwa mbaya. Nasi hatutaki mwana huyu akuwe vibaya wala afe. Ndio maana tukashika kalamu.”

  Ally Mahadhy: “…na vile vile kama mwanaadamu akuavyo, kuzeeka na mwisho hufa, na lugha (kiswahili) haina budi kupitia hali hizo! Sababu hata hao walomzaa (kiarabu, kibantu, kigiriki, kingereza nk) wengine washazeeka na wengine washakufa! Si twasikia siku hizi kuna kingereza cha marekani, cha nigeria, cha kichina, cha uingereza, cha malkia n.k, pia kuna kiarabu cha misri, cha lebanon,cha saudia n.k! Ha vyereje kusiwe na kiswahili cha mrima, kenya, mombasa n.k! Nahisi juhudi hizi ni sawa na kuzuia kifo kwa binaadam, wakati ishaandikwa kila nafsi itaonja mauti! Endelea kunipa darsa maalim wangu.”

  Mohammed Ghassany: “Tamathali ya uhai wa roho moja ya binaadamu na roho ya lugha ni tamu kuitumia, lakini ni vigumu kuitilia uzito. Sababu ni kuwa, tukichukuliwa uwiano wa sawa kwa sawa, baina ya mtoto kuzaliwa, kukuwa, kuwa mkubwa, kuoa/kuolewa, kuzaa, kuzeeka, na kufa, lugha huikuti humo.

  Kwa mfano, je kuna wakati ambapo lugha ilikuwa mtoto mchanga asiyeweza kujishika? Kuna wakati ilikuwa kijana ikiwa na nishati na nguvu za kutosha? Kuna wakati ilizeeka na kuwa dhaifu ya kutoweza kumudu harakati za maisha? Kwani uhai wa lugha upo kwenye nini hasa hata upimwe kwenye uhai wa mwanaadamu?

  Maswali kama haya, ambayo kwa hakika majibu yake yako wazi, ndiyo yanayothibitisha kwamba kuimithilisha lugha na mwanaadamu ni kwa sababu za tamathali na sio mantiki yake. Viwili hivi havifananishiki hivyo. Uhai wa lugha upo kwenye matumizi. Isipotumiwa lugha hufa.

  Lakini nukta kubwa kwa hakika si kufa kwa Kiswahili, bali ni kuharibiwa kwa lugha hii. Kuchafuliwa na halafu wachafuaji wakajipa haki na madaraka ya kusema hicho wakifanyacho ni kukihuisha Kiswahili – kukipanua, kukifanya kiende na wakati na mabadiliko, na mengine kadhaa wa kadha. Sipingi mabadiliko kwenye lugha, napinga maharibiko kwenye lugha.”

  Ally Mahadhy: “Maalim wangu, naam lugha yoyote inapita huko kuna wakati inakuwa mtoto mchanga nipale inapokuwa haifahamiki na watu wengi katika jamii au katika sehemu fulani, na kwa maana hiyo haipati watu wakubadilisha! Kipindi twafananisha na mtoto mchanga asiejiweza, ni mfano wa kiswahili wakati huo kikizungumzwa na wa mwambao tu, kilikuwa hakijulikani huko mrima, na baadae hukuwa kikawa na nishati mithili ya kijana, wakati huu ni ule kinapokuwa kinaeleweka na kuzungumzwa na jamii kuubwa, lakini bado hawatokei wanaokibadilisha, kwa maana wanakipokea na kukizungumza kama kilivyo, lakini kinapoanza kusanifiwa kwa kuongezewa maneno au kugeuzwe baadhi ya silabi za maneno yake kwa minajili ya kukidhi lafudhi ya walioipokea lugha hiyo au kukidhi wakati husika, kwa mfano wakati huo kiswahili kilipokuwa kijana baro baro kulikuwa hakuna tarakishi (computer) hivyo kuzuka kwa maneno mapya kuhusu hiyo tarakishi kwa wakati huu ni ukuaji pia, kama ilivyo kubadilika kwa maneno kulingana na jamii husika (akhsante ikawa ahsante na mwisho asante)…na ndio maana mwisho hufa, sababu baadae kikisha kukuwa sana, kupita kiasi, kinapoteza uasili wake, haitajulikana neno lipi ni sahihi kabisa na lipi nilakuzuka tu, mapitio hayo hayawezi kuzuiwa kwa nguvu za kibinaadam abadan! Lakini mabadiliko hayo hayawi dhambi wala kuwa makosa, kwa maana msingi wa lugha yoyote ni kuelewana wakati wa kuwasiliana (kufikisha ujumbe), kwa hiyo madhali jamii itaendelea kuelewana kupitia lugha hiyo mpya ya wakati huo ambayo itaendelea kuitwa kiswahili! Lakini kwa maelezo yako maalim wangu, ni wapi tunatakiwa tuseme kwamba haya ni mabadiliko ya lugha (ambayo hupingani nayo) na wakati gani tuseme haya ni maharibiko (unayopingana nayo)? Nikimaanisha nini tofauti ya maharibiko na mabadiliko katika lugha? Majibu ya hayo kwa muktadha huu ntakuwa nimemaliza kujifunza katika darsa hii! Natanguliza shukrani nyingi!”

  Mohammed Ghassany: “Naam, Ally. U wapi mstari baina ya mabadiliko na maharibiko? U pale ‘kusema’ inapokuwa ‘kusemaga’ (maharibiko) na pale kitu kilichovumbuliwa nje ya jamii ya Waswahili kikaja kwenye jamii hiyo na Waswahili wakakitohowa kulingana na kanuni za lugha yao, kama Computer kuitwa Kompyuta kwenye kundi la I-ZI ambapo hata zikiwa nyingi huwa si tena Kompyutaz kama ilivyo computers kwenye lugha yake ya asili (mabadiliko). Wala sina tatizo na wanaokichukuwa Kiswahili halafu wakakitumia kwa ndimi zao kama chombo cha mawasiliano kukidhi matakwa yao kwa wakati fulani, mahala fulani na hali fulani. La hasha! Ugomvi wangu ni pale watumiaji hao wanapokirudisha sasa Kiswahili hicho kwetu na kutwambia sisi Waswahili: “hiki hasa ndicho Kiswahili!” Wajamaica, Wanigeria, Wacarrebean, wamekichukuwa Kiingereza, wakakitumia kwa ndimi zao, lakini mwisho wa siku hawakumrudishia Muingereza wakamwambia kuwa sasa ndicho akitumie. Hapana! Hutumia mseto wao baina yao ‘kuyarahisisha mawasiliano’, lakini wakikirudisha wanasema mulichotupa ndicho Kiingereza.

  Ufupi wa mambo ni kuwa, Kiswahili kina wenyewe. Si kila mtumiaji wa Kiswahili ni Mswahili na hivyo hana haki ya kuilazimisha njia yake ya matumizi ya Kiswahili, kuwa kanuni za Kiswahili. Kiswahili kama zilivyo lugha zote kina kanuni zake.”

  Ally Mahadhy: “Ahsante sana maalim wangu. Hapa nimejfunza mengi mno. Usichoke kunifunza kwa jengine litakalo ni tatiza! Wengine sie ni wazito kuelewa mpaka tudadisi sana.”

  Mohammed Ghassany: “Katika masuala ya elimu, hakuna anayepoteza. Kila mtu anapata faida kubwa. Mimi nimefaidika zaidi na uchambuzi wako, Ally Mahadhy.”

  1. tusaidie hili swali…Kwakutumia kanuni maridhawa onesha tofauti zilizopo baina ya uambishaji na unyambulishaji..

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.