Ya leo ilikuwa kali kuliko siku zote. Hadi nikajisikia kukovyoka badala ya kuenda chafya tu. Nilikuwa na ahadi ya kukutana na mwenzangu mahala fulani. Saa moja kabla akanitumia ujumbe wa maandishi kwa simu kuulizia ikiwa miadi yetu ipo pale pale, nami nikajibu ‘ndio’ ila nilikuwa namalizia kufanya kadhaa na kadhaa. “Lakini hauwezi kumalizia shuuli zote izo kwa lisaa limoja.” Akaniandikia. “Kwa hisani yako kama Kiswahili kinakupa tabu, bora niandikie kwa Kiingereza au Kijerumani.” Nikamtumia ujumbe.
Nimekuwa nikisikia matumizi haya ya kuweka ‘a’ ndani ya kiambishi cha ukanushi wa kitenzi kwa nafsi ya pili umoja kwa wakati uliopo muda mrefu sasa. Nimekuwa nikisikia maneno yenye sauti za ‘gh’, ‘kh’, ‘tw’, ‘dh’ na hata ‘th’ yakitamkwa na baadhi ya wakati hata kuandikwa vibaya. Nimekuwa nikisikia na kusoma kugonganishwa na kubadilishwa herufi ‘h’ na ‘a’ kwenye maneno kadhaa. Nimekuwa nikisikia vivumishi vya majina katika kundi la LI-YA (Umoja) vikiwekwa kiambishi ‘li-‘.
Nikawa ninakereka nafsini mwangu, bali nikawa sijapata pa kutoa joto langu. Leo nimepapata.
Sio ‘hauwezi’, ni ‘huwezi’
Ukanushi wa kitenzi kwa nafsi ya kwanza, pili na tatu umoja, una silabi moja yenye herufi mbili tu kama hivi ifuatavyo:
Nafsi Kiambishi
Mimi Si-
Wewe Hu-
Yeye Ha-
Kwa hivyo, hakuna “wewe hauwezi”, “wewe hautaki”, “wewe hauli” na kadhalika. Hiyo herufi ‘a’ baina ya ‘h’ na ‘u’ haitakiwi kuwapo. Sarufi ya Kiswahili, kwa maana ya muundo na matumizi yake, hairuhusu hilo.
Sio ‘shuuli’, ni ‘shughuli’
Kwa sababu ambazo mimi ninazihusisha na ama na ujinga wa ukabila na au chuki za udini, kumezuka tabia ya kuziondoa sauti za Kiarabu kwenye maneno ya Kiswahili yenye asili ya lugha hiyo kwa hoja kwamba Kiswahili ni Kibantu tu na hakiwezi kuwa na matamshi ya Kiarabu.
Kwa mfano, neno kama ‘magharibi’ sasa hutamkwa magaribi, maaribi au maharibi. Neno ‘ghali’ sasa hutamkwa hali, gali au ali. Neno khofu, sasa ni hofu au ofu. Hata majina, kama vile Khamis, hutamkwa Hamis au Amis. La baba yangu, Khelef, hutamkwa Helef au Elef.
Mifano ni mingi mno, nami ninachoweza kusema hapa ni kusimamia hoja ya weblog hii kwamba Kiswahili kina wenyewe, na kwamba ladha ya maji ni kata, kuzi ni urembo. Kwa Mswahili wa kweli, sauti za gh, kh, tw na nyenginezo, ni sehemu ya sauti za lugha yake. Tabu inatupata pale wasiokuwa Waswahili kujivika wao madaraka ya kukisemea Kiswahili.
Sio ‘lisaa limoja’, ni ‘saa moja’
Miongoni mwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili, kuna utata wa ikiwa nomino ‘saa’ inaingia kundi gani la majina kati ya I-ZI na LI-YA. Mimi nasimamia hoja kwamba neno hilo lina maana mbili kwenye lugha hii: moja inamaanisha wakati au muda na nyengine inamaanisha chombo au kifaa kinachoelezea huo wakati. Linapotumika kukusudia wakati, basi kundi lake ni LI-YA; na linapotumika kumaanisha chombo, kundi lake ni I-ZI.
Tunasema, kwa hivyo, “masaa mengi yakapita kabla majibu kutoka” (tukikusudia muda au wakati) na “saa za siku hizi si nzima, ukinunua leo kesho zimeshavunjika” (tukikusudia chombo au kifaa).
Kwa kundi lolote kati ya hayo mawili na kwa maana yoyote ya neno ‘saa’ kati ya hizo mbili, bado umoja wake ni saa si lisaa na kivumishi chake ni moja si limoja. Kikiwa chombo ni saa moja, ukiwa muda ni saa moja. Hili neno lisaa limoja ni upotoshaji wa kudhani kuwa kilicho kwenye kundi la LI-YA kitaanza na ‘Li-‘. Ni upotofu maana maneno mengine yaliyo kwenye kundi hilo, hayapewi muundo huo. Kwa mfano, hao wanaosema lisaa limoja, hawasemi litunda limoja, ligazeti limoja wala lijambo limoja.
Kwa hakika, katika kundi hili, vivumishi ambavyo katika umoja huongezwa kiambishi ni kama -pya, -eusi, -ekundu, na -eupe kwa kutaja baadhi yao ambavyo navyo kiambishi kinachowekwa ni ‘j-‘ na wala sio ‘li-‘. Tunasema, kwa hivyo, jiwe jipya jeusi na sio lijiwe lipya leusi.
Yatoshe hayo kwa leo.
AHSANTE KAKA KWA UFAFANUZI WAKO HUU.
NATUMAI SOMO HILI PIA LITAWASAIDIA NA WENGINE WENGI AMBAO HAWAJUI KUTAMKA MATAMSHI SANIFU YA LUGHA YA KISWAHILI, NINAWASHAURI WASIONE AIBU KUJIFUNZA. KWANI INAONEKANA MAKOSA HAYA NI JANGA TAKRIBANI KWA WATUMIAJI WENGI WA KISWAHILI, HUSUSANI HAPA TANGANYIKA.
NA KUNA MANENO MENGINE KAMA KUSEMA: “Kale kabuzi kangu kamekufa” Siendagi sokoni leo” NA MENGINE MENGI. KWA HAKIKA TUSIPOKUWA WAANGALIFU KUWAFUNDISHA HAWA WANAOJINASIBISHA NA UTUMIAJI SANIFU WA LUGHA YA KISWAHILI, LADHA HALISI YA LUGHA YETU ITATOWEKA.
TUIENZI LUGHA YETU HII, AMBAYO NI TUNU HATA KWA MATAIFA YA UGHAIBUNI.
SABAHULKHER.