Jamani napata dhiki, nakujuvyeni
Au niite hilaki, niambieni
Kwani imezidi dhiki, kweli huzuni
Tamu hatuzidiriki
Tamu hatuzidiriki, siji kwanini
Kitu hata hakiliki, cha husudani
Chaporwa na mafataki, chatupwa chini
Tamu hatuzidiriki
Vipo vilivyo shambani, tuli mtini
Mara viwa pakachani, kwenda sokoni
Mwenye shamba wamhuni, yu masikini
Tamu hatuzidiriki
Twajitafutia dhiki, is’o kifani
Kwani hatutendi haki, ya duniani
Twamtendea dhihaki, Mola Manani
Tamu hatuzidiriki
Pupa inatusumbua, fikirieni
Mwaka hakijatiamia, ni ladha gani
Eti unakichukuwa, wewe fatani
Tamu hatuzidiriki
Sasa tuwa paka shume, kula wenetu
Jamani hayo kinyume, cha wetu utu
Wala si ujanadume, unyama mwitu
Tamu hatuzidiriki
Khelefu na Athmani, nawe Hamadi
Niambeni kwanini, hatufaidi –
Kula ladha ya maini, tukaburudi?
Tamu hatuzidiriki
Sir Haji nasubiri, yenu majibu
Nami nitayahubiri, kistaarabu
Wanaotenda ya shari ,niwe tabibu
Tamu hatuzidiriki
Mzee Haji (Sir Haji)
23 Novemba 2011