Moyo usighururike, ukavamia dunia
Iache usiishike, mbali nayo bora kuwa
Wala usipaparike, joto la roho kungia
Hino si njema rafiki, hayebu mtu dunia
Waliila waloila, matumboni hayekaa
Bali kupata madhila, ‘kaitema kwa fazaa
Wakabaki lahaula, laitani nengejua
Hiino ndio dunia, ino i tele hadaa
Dunia kiti cha basi, paondokwapo pakawa
Humilikipo nafasi, yako maliyo ikawa
Uzitowo wa unyusi, hugwapo ukasikiwa
Yache dunia ipite, akherayo fikiria
Dunia hii i fyuka, si jambo la kuchezea
‘kiidasa yafyatuka, kitanzini kushangia
Wabaki wapaparika, ‘sijuwe pa kutokea
Shikamanana na yano, ndipo utaongokewa
Dunia haishindika, daima shindi i yoyo
Majabari huanguka, yakaramba zake nyayo
Waponao hupofuka, fimbo ‘kawa dira zao
Tamakani ewe moyo, sighilibike sikia
Dunia i danganyifu, usipotamburikiwa
Utaiona chekefu, ukadhani wachekewa
Tahamaki watilifu, ndani ya domo la chewa
Huno ndo wangu waadhi, ipuze ino dunia
Dunia ina wahaka, wa mja kutotuliya
Kila kukicha wataka, zaidi ya ulopewa
Yakupeleka kupoka, wastahikio pewa
Usifate mwendo uno, takupoteza dunia
Rabi ziongoze nyoyo, zetu siye waja wako
Zipende uyapendayo, zitii amri zako
Zifanye tu yalo ndiyo, yaso siyo yawe mwiko
Na siku ya hukumuyo, tufungiye peponiko.
Hamad Hamad
5 Mei 2011
Copenhagen
Umekuwa mtu hadhi, kuuasa wako moyo
Mfano wako ni ngazi, kwa wengine kuwa nao
Dunia haina radhi, imekosa kwa Molao
Thamaniye ni ajizi, muda mdogo ‘lonao
Kwavyo nami napongeza, Dunia kujiepusha
Gonga hodi wakwambie, dunia ni yetu sote
Wala haina wenyewe, kwa hilo usiogope
Wewe umo mie nimo, ili mambo yaongoke
Dunia ni hii hii, mambo mengi yana tope
Ukiyaweza si ndwele, ‘kishindwa usitoweke