Shutuma kwamba utawala wa awamu ya tano wa Rais John Magufuli unaibinya roho demokrasia changa ya taifa hili kubwa kabisa Afrika Mashariki zina mashiko yake kwa kuangalia rikodi ya yale yanayotendwa dhidi ya vyama vya upinzani na viongozi wao, asasi za kijamii na hata vyombo vya habari, viwe vipya ama vikongwe.
Lakini wale wanaokosoa kwamba utawala huu unafanya mambo bila ya kuwa na itikadi au falsafa maalum inayouongoza, nao pia wanakosea. Ukweli ni kuwa kinachofanywa sasa na Rais Magufuli na timu yake kina mashiko yake kwenye mojawapo ya matapo makongwe kabisa kwenye taaluma ya uchumi wa kidola.
Tapo hilo ni lile linaloamini kwamba, kwanza, maendeleo yana tafsiri ya ukuwaji wa uchumi kupitia miundombinu na ubanaji matumizi na, pili, maendeleo hayo yanawezekana pale tu ambapo pana mfumo wa kirasimu na utawala wa mkono wa chuma. Ushahidi wa wanaoamini hayo wanautoa kwenye mifano ya Rwanda na baadhi ya mataifa ya Amerika Kusini na Asia, ambayo ni kigezo cha namna udikteta unavyofanikiwa kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.
Wasomi akina Walter Galenson, Karl De Schweinitz na Samuel Huntington wanahoji kwamba demokrasia inajikita zaidi kwenye mahitaji ya muda mfupi ambayo yanagharimu uwekezaji na ukuwaji wa uchumi. Kwa maoni yao, “demokrasia inatishia faida na, hivyo, kupunguza uwekezaji na basi haiendani na maendeleo ya kiuchumi.“ Watetezi hao wanahoji kwamba udikteta una uwezo mkubwa zaidi wa kulazimisha upatikanaji wa akiba na hatimaye kuanzisha ukuwaji mkubwa wa uchumi.
Akitetea mtazamo huo, Vaman Rao aliandika maneno haya mwaka 1984: “Maendeleo ya kiuchumi ni mchakato unaohitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali watu, vitu na fedha. Mipango ya uwekezaji kama huo inahusisha makato kwenye matumizi ambayo yanaweza kuwa machungu sana kwa watu wa chini ambao ndio wengi wao kwenye mataifa yanayoendelea. Serikali zinapaswa kuchukuwa hatua kali kabisa na kulazimisha zitekelezwe kimabavu ili kuweza kuzalisha ziada inayohitajika kwa uwekezaji. Endapo hatua hizo zitapigiwa kura na wananchi, hapana shaka zitashindwa. Hakuna chama chochote cha siasa kinachoweza kutegemea kushinda uchaguzi wa kidemokrasia kwa kutumia hoja ya kuwataka wananchi wajitowe muhanga leo ili wawe na maisha mazuri kesho.” (Tafsiri ni yangu).

Hadi hapo, kwa wale wanaodhani kuwa chini ya Rais Magufuli, Tanzania inaendeshwa mzobemzobe huku mkuu akiwa hajuwi aendako, wanapaswa kuhakiki upya wanayoyaamini. Inawezekana muda wa kuwepo kwake madarakani usitoshe kumfikisha anakolunga, lakini haina maana kuwa hakujuwi – angalau kwa kuzingatia tapo hili la kitaaluma ya uchumi wa kidola.
Ubakaji demokrasia hauwezi kuwa dawa ya ukuwaji uchumi
Lakini je, kwa kuungwa kwake mkono na wasomi kama hao niliowataja, kunaufanya mtazamo wa kuyachagua maendeleo kwa gharama ya kuiua demokrasia kuwa sahihi? Jibu langu ni hapana. Mtazamo huu si sawa hata kidogo, kwa sababu sio tu kwa kuwa una fasili finyu sana ya maendeleo (kwa kusisitiza ukuwaji wa uchumi kupitia uwekezaji wa miundombinu pekee), bali pia unapingana na hata ushahidi wa wazi na tafiti kadhaa za kisayansi duniani, zikiwemo zile zilizofanywa kwenye mataifa yetu ya Dunia ya Tatu na yale yaliyojikwamua kiuchumi yaitwayo sasa Dunia ya Kwanza.
Wasomi Douglass C. North na Barry R. Weingast, kwa mfano, waliandika hivi mwaka 1989: “Dola ya kikandamizaji kila siku inakuwa tayari kuigeuza jamii kuwa windo lake kwa kisingizio cha kujenga uchumi. Ni taasisi za kidemokrasia pekee ndizo zinazoweza kuizuwia dola hiyo kwa maslahi ya umma. Udikteta wa aina yoyote ile ni chanzo kikuu cha ukosefu wa ufanisi, maana serikali ambayo jukumu lake la msingi ni kuweka mfumo wa kulinda uwekezaji, uzalishaji na usambazaji inajigeuza kuwa ndio mtendaji wa pekee wa kila kitu.”
Dunia ni shahidi wa kupinduka kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kibinafsi kwenye mataifa yaliyoujaribu udikteta hata katika yale ambayo leo hii utawala wa Rais Magufuli unayachukulia kuwa ni kigezo cha kufuatwa. Kuanguka kwa uchumi wa Nicaragua chini ya dikteta Somoza, wa Jamhuri ya Dominik chini ya Trujillo, Ufilipino chini ya Marcos na Ulaya ya Mashariki chini ya tawala za kikomunisti si mambo ya kuigwa.
Athari za ubakaji wa demokrasia ndani ya ‘Tanzania ya Magufuli’
Ndani ya kipindi hiki kifupi cha utawala wa awamu ya tano unaoikanyaga misingi ya kidemokrasia, Tanzania imo kwenye wakati mgumu sana kimaendeleo. Hali ya maisha imezidi kuwa ngumu, imani ya wananchi kwa mfumo inapotea na imani ya wawekezaji wa kati na wa juu inatikisika, licha ya ripoti za kutunga zitolewazo na taasisi za kidola kuonesha kuwa mambo yako shwari.
Bei za bidhaa muhimu kwa matumizi ya kila siku kama vile unga, mchele, sukari na madawa ni ya juu sana, vituo vya afya havina madawa, mashuleni kuna msongomano na ukosefu wa vifaa.
Hoteli kadhaa zimeripoti anguko la asilimia hadi 60 la mauzo yao ndani ya kipindi hiki cha utawala wa Rais Magufuli, huku kukiwa na wimbi la wafanyabiashara wanaohamishia biashara zao nje ya nchi kwa sasa, si kwa kuwa ni wakwepaji kodi kama inavyotakiwa iaminike, bali kwa kuwa hawana hakika ya mitaji yao nchini kutokana na staili ya matamko ya kuripuka na kutaka sifa ya mkuu wa nchi.
Yote haya ni kwa kuwa utawala usiohishimu misingi ya kidemokrasia hukaribisha ghasia – ghasia kwenye nafsi za watu, ghasia kwenye maisha yao, ghasia kwenye mifumo ya kiuchumi na kisiasa. Hizi ni ghasia za kimyakimya lakini zina mahusiano ya moja kwa moja na ukosefu wa maendeleo. Tanzania ya Magufuli – kama mwenyewe anavyopenda kuiita – sasa inapitia kwenye kipindi hicho cha ghasia.
Dawa ni kuimarisha viwili kwa pamoja
Mwaka 1972, muongo mmoja baada ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere aliuvunja mfumo uliotoa mamlaka kwa serikali za mikoa kwa minajili ya kuimarisha madaraka na nguvu za serikali kuu iliyopo Dar es Salaam, lakini wakati akikaribia mwisho wa utawala wake, alinukuliwa akisema kwamba: “Kuna mambo ambayo nisingeliyafanya endapo ningeweza kuanza upya. Mojawapo ni kuvunja mamlaka ya serikali za mikoa.”
Hili linatuzinduwa kuwa daima kwenye utawala, jambo la busara ni kutoa uhuru zaidi wa kidemokrasia kwa wananchi na sio kuubana. Ushiriki wa wananchi kwenye uendeshaji wa mambo yao ni jambo la muhimu sana kama jamii hiyo inataka kweli kuyafikia maendeleo.
Ingawa miaka 25 ya siasa za vyama vingi haikuwa na ukamilifu, ikizongwa na matatizo mengi na wakati mwengine ya kuvunja moyo, lakini Tanzania ilikuwa inapiga hatua kidogo kidogo. Hatua hizo zilipaswa kuendelezwa na sio kurejeshwa nyuma kama ambavyo inaonekana wazi hivi sasa.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina serikali isiyohishimu mgawanyo wa madaraka, isiyohishimu uhuru wa kimsingi kama vile uhuru wa mawazo, uhuru wa kujieleza, na uhuru wa kujiunga na kujikusanya na pia utawala wa sharia, ni taifa lenye utawala uliopoteza uhalali wake wa kidemokrasia, hata kama awali uliingia madarakani kwa kushinda uchaguzi.
Kama kweli tunataka kuwa na maendeleo, tunapaswa kuziunganisha dhana hizi mbili pamoja, kwani kimsingi maendeleo na demokrasia duniani yameungana na uimarishaji wa thamani ya maisha ya binaadamu.
Serikali ya Rais Magufuli inapaswa kuifahamu na kuihishimu mifumo ya kikatiba, vyombo huru vya habari na vyenye kujumuisha wote, asasi imara za kijamii na dhamira ya kweli ya kuelekea utangamano na majadiliano ya kijamii.
Hii ndiyo misingi mikuu ya kufikia lengo la maisha bora. Demokrasia inaweza tu kudumu kama inaonesha, muda wote na mwahala mote, kwamba ni njia bora kabisa ya kufikia lengo hilo.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kabisa na gazeti la Mwelekeo la tarehe 18 Julai 2017.