UCHAMBUZI

Lissu wa dhahabu

Mkononi mwangu nina kitabu kiitwacho ‘A Golden Opportunity? Justice & Respect in Mining’ (Fursa ya Dhahabu? Haki na Heshima kwenye Madini) cha mwaka 2008. Waandishi wake ni wawili – Mark Curtis na Tundu Lissu. Ni matokeo ya utafiti uliofanywa na wawili hao wakiwa chini ya Baraza la Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na uchapishaji wake kufadhiliwa na Shirika la Misaada la Kikristo la Norway. Continue reading “Lissu wa dhahabu”

UCHAMBUZI

Serikali inapojibu mabomu ya Lissu kwa risasi za maji

Inaonekana mtazamo wa serikali ya Rais John Magufuli kumuelekea mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, unaanza kubadilika.

Kutoka kumkamatakamata kila akitoa kauli na kumweka ndani kisha kumfungulia mashitaka yasiyo kichwa wala miguu, sasa serikali imeamua kujibizana naye neno kwa neno, ‘bandika-bandua’ wasemavyo vijana wa mjini.

Sasa leo Lissu akisema jambo kuhusu serikali, ngojea kauli ya msemaji wa serikali hiyo kesho yake. Hii ni hatua nzuri sana, mara nyingi zaidi kuliko ule anaouita mwanamuziki Ibrahim Musa (Roma Mkatoliki) kama ‘uhuni wa kishamba.’

Uhuni wa kishamba ni pamoja na huu wa kukamatamata wanasiasa wa upinzani ovyo, kuwapiga, kuwatesa na kisha kuwafungulia mashitaka yasiyo mashiko alimradi tu kuwasumbua, kuwavunjia heshima na haki zao za kibinaadamu na kuwapotezea muda wao.

Kwa hivyo, ni jambo la kusifiwa kuwa serikali inaamua kuachana na tabia isiyo sahihi, angalau kwa kuanza na huyu mwanasheria anayetambuliwa kwa misimamo ya kimapinduzi, Lissu.

Na Mohammed Ghassani

Huenda tabia hii ikachukuliwa pia dhidi ya wengine wasiokuwa wanasheria, lakini ambao wanaamini kuikosoa serikali iliyopo madarakani kwa mijadala na midahalo ni njia bora zaidi kuliko kugeukia uasi wa silaha na matumizi ya nguvu.

Hata hivyo, inapoamua kutenda hivi, serikali bado inapaswa kujipanga. Isiwe inakurupuka kama kule kwenye huo uitwao ‘uhuni wa kishamba.’ Vyenginevyo, itakuwa inapata matokeo yale yale – ya kubwagwa kwa aibu na fadhaa.

Kwa aliyefuatilia mara mbili tatu ambazo ofisi ya msemaji maalum wa serikali imeamua kumjibu Lissu, atagundua kirahisi namna ofisi hiyo inavyotumia staili ile ile ya kukurupuka hadi sasa, na matokeo yake kuja na majibu mepesi kwa maswali mazito ambayo mnadhimu huyo wa kambi ya upinzani bungeni anayaibua.

Mfano wa karibuni kabisa ni huu wa majuzi, ambapo Lissu aliibua suala la kuzuiliwa kwa ndege aina ya Bombardier Q400-Dash 8 iliyonunuliwa na serikali ya Rais Magufuli nchini Canada kutokana na deni la dola milioni 37.8 (shilingi bilioni 87) ambalo serikali ya Tanzania inadaiwa kwa kuvunja kwake mkataba na kampuni moja ya ujenzi, Stirling Civil Engineering Ltd.

Kwa mujibu wa Lissu, kampuni hiyo ina hati ya mahakama inayoipa haki ya kuzuia mali za Tanzania sio tu nchini Canada, bali pia Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Uingereza na hata nchi jirani ya Uganda.

Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Lissu aligusia pia taarifa ya kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia Mining kuifungulia serikali ya Tanzania kesi kwenye mahakama ya usuluhishi ikidai pia mamilioni ya dola kwa kuzuiwa mchanga wake wa dhahabu, maarufu kama makinikia. Acacia wamefungua kesi hiyo hata kama bado mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanaendelea.

Hicho ndicho cha msingi alichokibainisha Lissu kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, ingawa kiliambatana na makandokando mengine kama vile kusema kuwa ukweli huo ulifichwa na serikali kwa kuwa ni matokeo ya tabia ya serikali hiyo kufanya mambo kwa kuripuaripua bila kufuata taratibu.

Sasa sikiliza majibu ya kaimu msemaji rasmi wa serikali, Zamaradi Kawawa, kwenye hili. Kwanza, kwamba ni kweli Bombardier-4000 imezuiliwa, lakini jitihada zinaendelea kuikwamua na kuifikisha Tanzania muda mfupi ujao.

Pili, kwamba kuzuiwa kwa ndege hiyo kunatokana na kampeni inayoendeshwa na wanasiasa wetu wasioitakia mema Tanzania.

Tatu, kwamba serikali ya Rais Magufuli haibaguwi kwenye maendeleo.

Nne, kwamba serikali hiyo inawafuatilia kwa karibu wanasiasa wanaokwamisha maendeleo kwani pia ni hatari kwa usalama wa taifa.

Wengi walioyasikia majibu haya walivunjwa moyo tangu sentensi ya kwanza kabisa kuanza kusomwa na kaimu msemaji huyo wa serikali. Sababu ni kuwa Lissu kwenye uwasilishaji wa ‘bomu’ lake alikuja na ushahidi mzito na wa moja kwa moja dhidi ya serikali.

Kwamba serikali ilikuwa imevunja mkataba wa ujenzi barabara mwaka 2009 na kampuni hiyo. Kwamba ikashitakiwa. Kwamba ikashindwa kesi. Kwamba ikakataa kulipa fidia. Kwamba ikakata rufaa. Kwamba ikashindwa rufaa. Ikaamuriwa kulipa tena. Ikakataa. Sasa ndege yake imekamatwa. Kwamba ni baada ya ndege kukamatwa kwa deni, ndipo Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga, akaenda nchini Canada kusaka njia ya kulimaliza hilo kimya kimya.

Yote haya hayajibiki kwa kusema kuwa ndege italipiwa na itafika nyumbani na Watanzania waendelee kuiamini serikali yao. Waiamini kwa msingi upi kwenye hili, wakati haikuwahi hata siku moja kusema kuwa ndege iliyotakiwa kufika mwezi mmoja nyuma haikufika kwa sababu gani? Na hata alipokuja mtu kutamka hadharani, sababu za kuchelewa kwake kufika, serikali inamrukia mtu huyo kuwa anakwamisha maendeleo?

Mambo matatu yanazuka sasa hapa, sio kwenye suala lenyewe la Bombardier tu, bali kwenye tabia yenyewe ya serikali kuyaendea maswala muhimu ya nchi. Kwanza, serikali hii inayojipambanua kwa kupambana kwake na ufisadi, wizi na ubadhirifu katika sekta ya umma, imeuficha udhaifu wake nyuma ya ukali wa kiongozi mkuu, Rais Magufuli.

Kwamba pale guo la ukali huo wa Rais Magufuli linapovuliwa, basi kinachodhihirika ni serikali isiyo viunganishi na muunganiko. Waliofuatilia suala hili hili, wanajuwa kuwa huko kwenye mitandao ya kijamii, Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi Makame Mbarawa alishakanusha siku moja tu nyuma juu ya kushikiliwa kwa Bombardier. Huyu ni mjumbe wa baraza la mawaziri. Lakini siku moja baadaye, msemaji wa serikali anakiri kuwa ni kweli inashikiliwa. Hii inaonesha kuwa huko ndani, nje ya ukali wa Rais Magufuli, kuna vikuku vya mkufu wa mawasiliano ndani ya utawala vimekatika. Na huo ni udhaifu mkubwa.

Pili, miaka miwili baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli ameshindwa kupanga timu yake ya mkakati vyema. Bado utendaji wake na wa timu yake unakwendana na mapigo ya kinachoendelea mitandaoni na kwenye majukwaa ya kisiasa.

Mawasiliano baina ya serikali na umma yanajengwa na kipi kimeibuliwa na ‘waropokaji’ huku nje – mitandaoni, majukwaani, mitaani. Ujanja wa kuziwahi taarifa mapema ili kuchomeka wazo ambalo serikali inataka liwe wazo kuu kwa wananchi haumo ndani ya vichwa vya timu ya mkakati ya Rais Magufuli.

Tatu, na la mwisho, serikali inadanganya kwa jina la uzalendo. Kuanzia Rais Magufuli mwenyewe hadi wanaomfuata chini yake, kauli yao kubwa ya kukumbizia takataka chini ya zulia ni kwamba taifa letu linahitaji uzalendo wa hali ya juu, ambao kwa maoni yao ulikuwa umekosekana siku nyingi huko nyuma.

Wakati hilo ni sahihi kabisa, kisichokubalika ni kwa serikali hiyo hiyo kuficha ukweli au kudanganya kwa wananchi ili kujenga mapenzi yasiyo ya kweli kwa serikali yao.

Ingelikuwa vyema kabisa kile kinachohubiriwa na Rais Magufuli majukwaani, kwamba yeye ni msema kweli, kikawa ndicho kinachoakisika katika mtiririko mzima wa wanaomfuata chini yake. Na inapobainika kwamba kimakosa serikali ilidanganya au ilificha ukweli uliopaswa kufahamika na umma kwa wakati muafaka, basi iwe tayari kuomba radhi haraka na kwa ufanisi.

Mapenzi na uzalendo hujengwa juu ya ukweli na uwazi.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 22 Agosti 2017.