Majuzi Rais John Magufuli alimuapisha Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) akiweka msisitizo kwamba anataka kuona wala rushwa wanafungwa jela haraka iwezekanavyo.
Kwa maneno yake mwenyewe Rais Magufuli, “mambo makubwa ambayo taifa linapambana nayo yanatokana na rushwa…” na kwamba kama Tanzania ikifanikiwa kuipunguza rushwa angalau kwa asilimia 80, basi itakuwa imeyatatua matatizo yake mengi sana.
Hakuna anayepinga kwamba Tanzania, ambayo imeongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) – chama chake yeye Rais Magufuli – muda wote wa kuwa kwake taifa huru, imeoza kwa rushwa. Inanuka, imeoza, kila mahala, kila sekta!
Lakini katikati ya uoza huo, au pengine kwa sababu ya uoza huo, ndipo unapokuta hii tabia yetu mbovu ya kuuzungumzia uchafu kwa maneno yanayochuja kimaana. Mojawapo likiwa ni hili la kuuita ufisadi kuwa ni rushwa. Rushwa tu!
Ukweli ni kuwa rushwa ni kitu kidogo sana panapohusika uoza wenyewe hasa uliopo. Rushwa ni utowaji na au upokeaji wa kitu (mara nyingi huwa pesa) kwa ajili ya kutoa au kupokea huduma, ambayo kimsingi ingelikuwa haki kutolewa bila ya kitu hicho.

Wengi wetu tunadhani rushwa ni sawa na ule msamiati wa Kiingereza ‘corruption’, ndiyo maana hata hiyo taasisi inayoshughulika na kadhia hiyo inaitwa TAKUKURU kwa kuwa tunasema inafanya kazi ya kupambana na kuzuia rushwa.
Na kwa kuwa tunakosea kwenye kuipa jina lake halisi hali hii tunayokabiliana nayo, ndio maana tunazunguka mumo humo, tukiamini kwamba kubadilisha sura kwenye chombo chenye mamlaka ya kupambana na hali hii kunatosha kuimaliza.
Ukweli ni kwamba kuiangalia hali kwa jicho lake halisi kuna nafasi kubwa mno kwenye kuzifikia hizo asilimia 80 anazolenga Rais Magufuli kwenye vita hivi vikubwa na, kwa hakika, vyenye maana kwetu sote.
Tanzania inaliwa na ufisadi na sio rushwa pekee, na tena ufisadi mkubwa zaidi ni ule wa kisiasa, ambao umejengewa mihimili kwa miaka 50 ya utawala wa CCM, kiasi cha kuufanya uonekane hali ya kawaida kwenye maisha ya kila siku.
Ufisadi wa kisiasa unakwenda mbali zaidi ya pale rushwa ya kutoa na kupokea fedha inapoishia. Huu ni utumiaji mbaya wa madaraka unaofanywa na maafisa wa serikali na, au, wa taasisi za kisiasa kwa maslahi binafsi. Aina zake ni za viwango tafauti, na hiyo rushwa moja tu miongoni mwao.
Katika upana wake utakuta pia udugunaizesheni, wizi wa kura, milungula, wizi wa mali ya umma na ubadhirifu, kwa kutaja machache.
Ufisadi huu wa kisiasa, kwa hakika, ndio mama wa maovu mengine yote katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uovu wa madawa ya kulevya, ujambazi, ukahaba na umasikini wa watu wetu, kwa mfano, ni matokeo ya ufisadi wa kisiasa ambao umekuwa ukiila nchi yetu kwa zaidi ya miongo mitano sasa.
Bahati mbaya ni kuwa ufisadi huu una khulka moja ya hatari sana: kuzoeleka. Kila anayechukua nafasi ya uongozi wa umma katika serikali au taasisi ya kisiasa huona sawa kwake kuwa fisadi, na kwa hakika jamii humtarajia awe hivyo. Kwamba atumie fursa ile kujinufaisha binafsi, awatishe wengine, awakomowe, awaangamize ili yeye awe hapo alipo .
Ndio maana maafisa wa tume za uchaguzi huiba kura kwa ajili ya kuwanufaisha wanasiasa wanaowapa vyeo, wagombea hununua wapiga kura, polisi hula mkono kwa mkono na wahalifu, maprofesa hupasisha au kufelisha wanafunzi vyuoni kwa kuzingatia maslahi yao binafsi. Alimradi ni mchafukoge.
Jamii hii ya mchafukoge ni muakisiko wa ufisadi wa kisiasa uliopea na kuzoeleka. Utamaduni wa chukua chako mapema, wa iba ulindwe na kemea udhibitiwe (kama wanavyoonekana kudhibitiwa wapinzani sasa), ndio unaojenga fikra za Watanzania uwaonao mbele yako leo.
Si hasha, kwa hivyo, kusikia hata miongoni mwa kada za hao waitwao wasomi leo hii wakisema: “Naye Tundu Lissu kazidi kidomodomo.” Kwao wao ufisadi ni ada ya maisha ya kila siku.
Kilele cha utamaduni huu huwa ni kile kinachoitwa kleptocracy (rule by thieves), yaani utawala wa wizi – wizi wa kura, wizi wa mali, wizi wa matumaini, wizi wa kesho ya wanyonge walio wengi.
Ufisadi una hatari kubwa na ya pekee katika maendeleo ya taifa. Katika siasa, hufifisha na wakati mwengine kuua kabisa mfumo wa kidemokrasia na utawala wa sheria, maana ufisadi una kiburi cha kuingilia kati chochote ambacho kinaonekana kiko dhidi yake. Ukweli ni kwamba demokrasia na utawala wa sheria ni adui kwa ufisadi; na kilipo kimoja chengine hakikai.
Kwa hivyo, kwa jamii kama yetu, ambayo imejikita katika uoza wa kupindukia wa ufisadi, mafisadi wenyewe hawataki kabisa kuona mfumo wa demokrasia ukistawi ama utawala wa sheria ukisimama. Si ajabu, kwa hivyo, kuona wakiingilia kati taratibu za kawaida za kidemokrasia na za utawala wa sheria kila pale wanapoona zinachukuwa mkondo wake.
Ya kuharibiwa kila mara kwa chaguzi za Zanzibar, kwa mfano, kwa kupelekwa majeshi yenye silaha nzito nzito ni katika hizo jitihada za ufisadi kupingana na demokrasia na utawala wa sheria.
Ufisadi katika chaguzi hupelekea ofisi za umma kukaliwa na watu wasiotokana na ridhaa ya umma na hivyo nao matokeo yake huzikalia ofisi hizo kwa maslahi yao binafsi na sio kwa maslahi ya umma, maana sio uliowaweka ofisini.
Leo hii Rais Magufuli anapolilia ukosefu wa uzalendo miongoni mwa wenzake serikalini – wanaofikia hadi kusaini mikataba ya kuuza madini kiholela – anapaswa kujiuliza namna hao watiaji saini walivyofika hapo madarakani. Je, ni kwa demorasia au kwa ufisadi wa kisiasa?
Ufisadi katika vyombo vya kutunga sheria hupunguza au huondosha kabisa uwajibikaji na uwakilishi wa kweli katika vyombo hivyo; ufisadi kwenye mahakama huiweka rehani haki ya wananchi; na ufisadi kwenye utawala husababisha ukosefu wa uadilifu katika utowaji wa huduma za kijamii.
Kwa jumla, ufisadi hukokozoa kabisa uwezo wa kitaasisi wa serikali, kwani husababisha taratibu kupuuzwa, rasilimali kuporwa, na ofisi za umma kuuzwa na kununuliwa kama bidhaa nyengine yoyote.
Ufisadi wa kisiasa ukipevuka huufanya hata uhalali wa serikali iliyopo madarakani uhojike na vivyo misingi ya demokrasia na kuaminiana itoweke. Ni mapema, pengine, sasa kwa wananchi wa Tanzania kuhoji uhalali wa serikali yao, lakini kwa mwenendo huu tunaokwenda nao, si muda mrefu tena ujao, hilo la kuhoji litakuwa wajibu wetu wa mwanzo!
Lakini wakati tukisubiri wakati huo ufike, sote ni mashahidi wa namna ambavyo ufisadi wa kisiasa unadumaza maendeleo ya kiuchumi kwa kuchochea ubadhirifu na ukosefu wa ufanisi.
Watanzania wameshuhudia mali za nchi zikiibiwa mbele ya macho yao: mchanga wa dhahabu unasafirishwa makontena kwa makontena, meli za kigeni zinavua tani kwa tani za samaki kwenye bahari yao, na wenye vyeo wanajikopesha na kujikatia juu kwa juu kutoka hazina ya taifa.
Na hayo hayajasimama kwa kuwa Rais Magufuli kasema anataka kuwaona wala rushwa wakifungwa jela. Yatasimama kwa kuuita ufisadi kwa jina lake halisi na kuutendea kama ututendeavyo – kuuwa maana nao unatuuwa.
Haitoshi kila siku kulia majukwaani na kwenye vichwa vya habari magazetini. Kuuzungumzia ufisadi kwa jina la rushwa hakutoshi. Kueleza ushahidi wa rushwa hiyo ilivyolimaliza taifa pia hakutoshi.
Hakutoshi, maana baada ya kuwa mashahidi na walalamikaji miaka yote 50 ya taifa huru, kumetusaidia nini? Kwa karibuni miongo mitano yote, hiyo imekuwa hali ambayo taifa hili limeishi nayo.
Leo hii tunajikokota kwenye mstari wa mwisho wa umasikini duniani, watoto wetu wakifa kwa maradhi na njaa, na bado tumeendelea kuwa mashahidi na walalamikaji ambao tunalizunguka tatizo lenyewe, badala ya kutua katikati yake – penye ufisadi wa kisiasa.
Kwa hivyo, si mwanajeshi John Mbungo anayepaswa kuvaa magwanda yake kupambana na ufisadi huu wa kisiasa, maana si ajabu kuwa hata yeye mwenyewe ni matokeo ya mfumo uliousimamisha ufisadi wa aina hiyo, na ndio maana hata amiri jeshi wake anataka tu akahakikishe anawafunga wala rushwa. Wala rushwa tu!
Ni wananchi wanaopaswa, kwanza, kuufahamu ufisadi wa kisiasa ambao Tanzania imekulia nao. Kisha, pili, kuuchukia kwelikweli, na mwisho, la tatu, kuchukuwa hatua dhidi ya uoza huu kwa njia halali.
Miongo hiyo mitano ya ufisadi wa kisiasa imewashuhudia watawala wale wale wakiwazoesha kuupenda na kuushabikia ufisadi na kuufanya kuwa utamaduni wao. Wamewapotosha vya kutosha. Wamefanywa waone jambo la kawaida kutoa na kupokea rushwa. Wamewafanya wautarajie ufisadi na wautegemee kama njia ya kupita kufika waendako.
Wanapaswa sasa kukataa na kusema hapana. Hapana kwa ufisadi wa kisiasa. Hapana kwa mafisadi wa kisiasa.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHALISI la tarehe 28 Agosti 2017.