Chembelecho (au chambilecho, au chambacho) msemo wa Kiswahili, “Kipya kinyemi, kingawa kidonda.” Ni dasturi ya baadhi ya watu kuvutiwa na kipya kitokacho kwengine, hata kama tangu hapo wanacho chao wenyewe kifananacho na hicho cha kigeni. Hili swala la maneno kama “mubashara” lina tanzu mbili. Utanzu wa kwanza ni huo wa kupenda kukimbilia maneno ya kigeni, hata kama tunayo yetu wenyewe yenye maana hiyo hiyo. Kama ilivyokwisha elezwa, kabla ya habari “mubashara” tumekuwa tukisema habari/ ripoti za moja kwa moja, au za papo kwa papo (wala si “papo” pekee).