BLOG POSTS

TUFUNUWE KITABU: Mafunzo kutoka “Pan-Africanism or Pragmatism?” cha Prof. Issa Shivji

Wiki iliypota, Ismail Jussa alichambua kitabu cha “The Partner-ship: Miaka 30 ya Dhoruba” kilichoandikwa na Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi, na leo anachambua cha Profesa Issa Shivji, Pan-Africanism or Pragmatism?”, ambacho ni muakisiko wa kile cha Marehemu Jumbe.

UCHAMBUZI

Kuimaliza CUF ni kuimaliza Zanzibar

Kikiwa kama chama kikubwa cha kitaifa, Chama cha Wananchi (CUF) kinafanana na vyama vingine vingi vya kisiasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kina jambo moja kubwa ambalo kimejipambanuwa kutoka vyama vyenziwe. Nalo ni falsafa yake juu ya nafasi ya Zanzibar kwenye Muungano huo.

Hiki ni chama pekee kilichojikita kwenye “Siasa za Muungano” kama mtaji wake mkuu wa kisiasa upande wa Zanzibar. Hakuna chama chengine chochote ambacho kina dira ya kuifanya Zanzibar kuwa mshirika mwenye nguvu za kweli ndani ya Muungano huu kama ilivyo CUF.

Na hapa ndipo tatizo lenyewe lilipo. Siasa za Muungano. Zile ambazo zinasema kuwa “ili uwe na Muungano imara basi lazima uwe na Zanzibar dhaifu” na ambazo zinaiona Zanzibar imara kama jambo hatari kwa Muungano huo.

Kwa waumini wa siasa hizo za Muungano, chochote kinachoipa Zanzibar taswira ya uimara ni kitu cha kuchukiza na kisicho na uhalali wa kuishi. Kinapaswa kuangamizwa mara moja, tena kwa kadiri ambavyo inawezekana.

Hiki kinachoendelea sasa hivi dhidi ya CUF kina mashiko yake kwenye ukweli huu wa utekelezaji wa siasa za Muungano kuelekea Zanzibar.

Kwa muda wote, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992, CUF imekuwa mwiba mbaya kooni mwa waumini wa siasa hizo za Muungano walio ndani na nje ya visiwa vya Zanzibar.

Na Mohammed Ghassani

Waumini hao hasa ni watiifu kwa makao makuu ya siasa zenyewe, Chimwaga, na ambao kwa hakika hasa sio kwamba wanaupenda Muungano kama Muungano, bali wanaupenda Muungano ule ambao kwawo, nchi moja iko juu ya nyengine kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Waumini wa siasa hizo wametekeleza hujuma kubwa kubwa dhidi ya Zanzibar kabla ya Muungano wa 1964 na tangu siku za awali kabisa za Muungano wenyewe, mara tu baada ya Mzee Abeid Karume kung’amuwa mtego alionasishwa na mwasisi mwenzake wa Muungano huu.

Tangu awamu hiyo ya kwanza, takribani hakuna kipindi kilichopita salama bila ya kukuta alama, taasisi au watu wanaowakilisha taswira ya nguvu za Zanzibar ndani ya Muungano wakinyakuliwa, kudunishwa, kudhalilishwa na hata kuangamizwa kabisa kabisa.

Wazalendo wa Kizanzibari waliokuwa wasomi na wenye fikra nzito nzito za kimageuzi kutoka pande zote za ushindani wa kisiasa visiwani Zanzibar, akina Ali Muhsin Barwani, Amani Thani, Abdulrahman Mohamed Babu, Abdallah Kassim Hanga, Kanali Ali Mahfoudh, Salim Ahmed Salim, na wengine kadhaa walijikuta wakimezwa ndani ya tumbo la Tanganyika na kisha ama kuselelea huko ama kuangamia kupitia mkono wa huko.

Katika kitabu chake cha Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar Union, Profesa Issa G. Shivji anazungumzia mzozo mkubwa uliokuwepo kati ya Mzee Karume na Mwalimu Julius Nyerere, hata kabla ya wino wa sahihi kwenye Makubaliano ya Muungano haujakauka.

Katika siku za mwisho mwisho za uhai wake, Mzee Karume alikuwa hazungumzi moja kwa moja na Mwalimu Nyerere na hata panapokuwa na jambo la wawili hao kuzungumzwa, lilipaswa kupitishwa kwa mawaziri wao waandamizi.

Mwisho, Aprili 1972, akiwa kama alama ya nguvu ya Zanzibar kwenye Muungano, maisha ya Mzee Karume yakakatishwa, huku maswali kuhusu wahusika wa mauaji hayo hadi leo yakibakia bila majibu, lakini tuhuma kwamba msimamo wake kuhusu Muungano ulichangia kifo hicho, zipo miongoni mwa Wazanzibari.

Miaka mitano baada ya kuuawa kwa Mzee Karume, taasisi imara kabisa iliyowasilisha na kuwakilisha nguvu za Zanzibar, chama cha Afro-Shiraz (ASP), nacho kikauliwa kwa maslahi ya kuundwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichotokana na chenye nguvu zake upande wa Tanganyika.

Baada ya hujuma hii ya kuimaliza ASP kufanikiwa, hapakuwa tena na mpaka wa kukichukuwa kila kilichomo Zanzibar, iwe taasisi, mtu au alama inayoashiria nguvu za Zanzibar ndani ya Muungano. Kuanzia maamuzi hadi utekelezaji.

Ndicho kilichomkumba Marehemu Mzee Aboud Jumbe Mwinyi kwa kuvuliwa nafasi zake zote za uongozi wa kichama na kiserikali na hatimaye naye maisha yake yakamalizikia akiwa kapotezwa kabisa kwenye ramani ya siasa za nchi.

Ndicho kilichokuja baadaye kuwakumba vijana wa wakati huo ambao walikuwa alama ya nguvu ya Zanzibar ndani ya Muungano, akina Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohamed, Soud Yussuf Mgeni, Juma Ngwali, Maulid Makame, Shaaban Khamis Mloo, Juma Duni Haji na wenzao, ambao sio tu kuwa walivuliwa nyadhifa zao bali pia waliwekwa jela.

Mwanzoni kabisa, mara tu baada ya Katibu Mkuu wa sasa wa CUF, Maalim Seif, kutoka kizuizini alikokuwa amewekwa baina ya Mei 1989 na Novemba 1991, alikutana na Mwalimu Nyerere katika kile kilichoitwa “mazungumzo ya siri ya Msasani.”

Ingawa hakuna hata mmoja aliyekisema hasa walichokizungumza wawili hao, lakini inasemekana kuwa Mwalimu Nyerere alimuambia Maalim Seif kuwa afanye afanyavyo kwenye siasa zake, lakini kamwe asije akathubutu kuugusa Muungano, akimtishia kuwa akiuchezea Muungano “asingelibaki salama!”

Lakini Maalim Seif na CUF yake, inaonekana, hawakutaka kumkubalia Mwalimu Nyerere. Waliendelea kuugusa Muungano, nao wakaendelea kukabiliana na adhabu za kuugusa huko.

Miongoni mwa adhabu hizo ni mauaji ya Januari 2001, ambapo kwa mujibu wa ripoti ya shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch iliyopewa jina la “Risasi Zilinyesha Kama Mvua”, mashuhuda wanasema wauaji, watesaji na wabakaji wao walikuwa wakirejelea kauli za kisiasa zinazohusiana na upinzani wa wana-CUF dhidi ya Muungano.

Kwa hivyo, hata maandamano yale kwa watawala ilikuwa ni alama ya Wazanzibari kuinuka dhidi ya Muungano na yalipaswa kuangamizwa kwa namna yoyote.

Hapo katikati, kuanzia mwaka 2009, Zanzibar ilianza tena kurudi kwenye siasa za umma dhidi ya mfumo uliopo wa Muungano, ambazo zilichangiwa pakubwa na Maridhiano yaliyoasisiwa na Rais Amani Karume na Maalim Seif.

Kwa Maridhiano hayo, Kura ya Maoni ya Julai 31 ikaamuwa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, pamoja na Mabadiliko ya Katiba yaliyoitangaza rasmi Zanzibar kuwa ni nchi.

Yote haya yalikuwa ni alama za ukaidi dhidi ya siasa za Muungano. Ishara za kuipa nguvu Zanzibar. Asasi huru za kijamii, kama vile Jukwaa la Katiba la Zanzibar na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho), zikapata uhuru wa kuelezea hayo kinagaubaga, lakini kila mtu anafahamu yaliyowakumba viongozi wake ambao wamebambikiziwa kesi za ugaidi kwa mwaka wa nne sasa.

Ukweli kwamba uchaguzi wa Oktoba 2015 ulichafuliwa, na ambao CUF unadai kushinda na jumuiya huru za ndani na nje ya nchi zinasema ulikuwa huru na wa haki zaidi kuwahi kutokea visiwani Zanzibar, una mahusiano ya moja kwa moja na siasa za Muungano kuelekea Zanzibar na msimamo wa CUF kuelekea Muungano huo.

Kwa hivyo, hivi leo kwamba CUF imeingizwa kwenye mzozo mkubwa kabisa wa kiuongozi, ambapo kundi linalosaidiwa kwa hali na mali na vyombo vya dola linaendesha hujuma za waziwazi zinazotishia uhai wa chama hicho, ni kwa kuwa chama hicho kimesimama kama alama ya Zanzibar imara ndani ya Muungano.

Alama hii ikiachiwa nayo kwenda, kama ambavyo alama nyengine huko nyuma zimewachiwa kwenda, itaongezea idadi kwenye orodha ya maangamizi kwa Zanzibar.

Kuiangamiza Zanzibar kama nchi na kama mshirika muhimu wa Muungano ni hatua muhimu kuelekea ile sera ya “serikali moja, nchi moja, chama kimoja.”

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 31 Julai 2017