Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi ndiye aliyekuwa rais wa pili wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya 1964 na akaja kuondolewa na Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1984 katika kile kinachoitwa “Kuchafuka Hali ya Hewa ya Kisiasa Zanzibar”. Miaka 10 baadaye alichapisha kitabu chake kinachozungumzia sakata zima la yeye kuondolewa madarakani na kuelezea msimamo wake juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ismail Jussa anatupitisha kwenye kurasa zake kuchota mafunzo yaliyomo.
Tag: jamhuri ya muungano wa tanzania
Serikali inapojibu mabomu ya Lissu kwa risasi za maji
Inaonekana mtazamo wa serikali ya Rais John Magufuli kumuelekea mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, unaanza kubadilika.
Kutoka kumkamatakamata kila akitoa kauli na kumweka ndani kisha kumfungulia mashitaka yasiyo kichwa wala miguu, sasa serikali imeamua kujibizana naye neno kwa neno, ‘bandika-bandua’ wasemavyo vijana wa mjini.
Sasa leo Lissu akisema jambo kuhusu serikali, ngojea kauli ya msemaji wa serikali hiyo kesho yake. Hii ni hatua nzuri sana, mara nyingi zaidi kuliko ule anaouita mwanamuziki Ibrahim Musa (Roma Mkatoliki) kama ‘uhuni wa kishamba.’
Uhuni wa kishamba ni pamoja na huu wa kukamatamata wanasiasa wa upinzani ovyo, kuwapiga, kuwatesa na kisha kuwafungulia mashitaka yasiyo mashiko alimradi tu kuwasumbua, kuwavunjia heshima na haki zao za kibinaadamu na kuwapotezea muda wao.
Kwa hivyo, ni jambo la kusifiwa kuwa serikali inaamua kuachana na tabia isiyo sahihi, angalau kwa kuanza na huyu mwanasheria anayetambuliwa kwa misimamo ya kimapinduzi, Lissu.
Huenda tabia hii ikachukuliwa pia dhidi ya wengine wasiokuwa wanasheria, lakini ambao wanaamini kuikosoa serikali iliyopo madarakani kwa mijadala na midahalo ni njia bora zaidi kuliko kugeukia uasi wa silaha na matumizi ya nguvu.
Hata hivyo, inapoamua kutenda hivi, serikali bado inapaswa kujipanga. Isiwe inakurupuka kama kule kwenye huo uitwao ‘uhuni wa kishamba.’ Vyenginevyo, itakuwa inapata matokeo yale yale – ya kubwagwa kwa aibu na fadhaa.
Kwa aliyefuatilia mara mbili tatu ambazo ofisi ya msemaji maalum wa serikali imeamua kumjibu Lissu, atagundua kirahisi namna ofisi hiyo inavyotumia staili ile ile ya kukurupuka hadi sasa, na matokeo yake kuja na majibu mepesi kwa maswali mazito ambayo mnadhimu huyo wa kambi ya upinzani bungeni anayaibua.
Mfano wa karibuni kabisa ni huu wa majuzi, ambapo Lissu aliibua suala la kuzuiliwa kwa ndege aina ya Bombardier Q400-Dash 8 iliyonunuliwa na serikali ya Rais Magufuli nchini Canada kutokana na deni la dola milioni 37.8 (shilingi bilioni 87) ambalo serikali ya Tanzania inadaiwa kwa kuvunja kwake mkataba na kampuni moja ya ujenzi, Stirling Civil Engineering Ltd.
Kwa mujibu wa Lissu, kampuni hiyo ina hati ya mahakama inayoipa haki ya kuzuia mali za Tanzania sio tu nchini Canada, bali pia Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Uingereza na hata nchi jirani ya Uganda.
Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Lissu aligusia pia taarifa ya kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia Mining kuifungulia serikali ya Tanzania kesi kwenye mahakama ya usuluhishi ikidai pia mamilioni ya dola kwa kuzuiwa mchanga wake wa dhahabu, maarufu kama makinikia. Acacia wamefungua kesi hiyo hata kama bado mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanaendelea.
Hicho ndicho cha msingi alichokibainisha Lissu kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, ingawa kiliambatana na makandokando mengine kama vile kusema kuwa ukweli huo ulifichwa na serikali kwa kuwa ni matokeo ya tabia ya serikali hiyo kufanya mambo kwa kuripuaripua bila kufuata taratibu.
Sasa sikiliza majibu ya kaimu msemaji rasmi wa serikali, Zamaradi Kawawa, kwenye hili. Kwanza, kwamba ni kweli Bombardier-4000 imezuiliwa, lakini jitihada zinaendelea kuikwamua na kuifikisha Tanzania muda mfupi ujao.
Pili, kwamba kuzuiwa kwa ndege hiyo kunatokana na kampeni inayoendeshwa na wanasiasa wetu wasioitakia mema Tanzania.
Tatu, kwamba serikali ya Rais Magufuli haibaguwi kwenye maendeleo.
Nne, kwamba serikali hiyo inawafuatilia kwa karibu wanasiasa wanaokwamisha maendeleo kwani pia ni hatari kwa usalama wa taifa.
Wengi walioyasikia majibu haya walivunjwa moyo tangu sentensi ya kwanza kabisa kuanza kusomwa na kaimu msemaji huyo wa serikali. Sababu ni kuwa Lissu kwenye uwasilishaji wa ‘bomu’ lake alikuja na ushahidi mzito na wa moja kwa moja dhidi ya serikali.
Kwamba serikali ilikuwa imevunja mkataba wa ujenzi barabara mwaka 2009 na kampuni hiyo. Kwamba ikashitakiwa. Kwamba ikashindwa kesi. Kwamba ikakataa kulipa fidia. Kwamba ikakata rufaa. Kwamba ikashindwa rufaa. Ikaamuriwa kulipa tena. Ikakataa. Sasa ndege yake imekamatwa. Kwamba ni baada ya ndege kukamatwa kwa deni, ndipo Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga, akaenda nchini Canada kusaka njia ya kulimaliza hilo kimya kimya.
Yote haya hayajibiki kwa kusema kuwa ndege italipiwa na itafika nyumbani na Watanzania waendelee kuiamini serikali yao. Waiamini kwa msingi upi kwenye hili, wakati haikuwahi hata siku moja kusema kuwa ndege iliyotakiwa kufika mwezi mmoja nyuma haikufika kwa sababu gani? Na hata alipokuja mtu kutamka hadharani, sababu za kuchelewa kwake kufika, serikali inamrukia mtu huyo kuwa anakwamisha maendeleo?
Mambo matatu yanazuka sasa hapa, sio kwenye suala lenyewe la Bombardier tu, bali kwenye tabia yenyewe ya serikali kuyaendea maswala muhimu ya nchi. Kwanza, serikali hii inayojipambanua kwa kupambana kwake na ufisadi, wizi na ubadhirifu katika sekta ya umma, imeuficha udhaifu wake nyuma ya ukali wa kiongozi mkuu, Rais Magufuli.
Kwamba pale guo la ukali huo wa Rais Magufuli linapovuliwa, basi kinachodhihirika ni serikali isiyo viunganishi na muunganiko. Waliofuatilia suala hili hili, wanajuwa kuwa huko kwenye mitandao ya kijamii, Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi Makame Mbarawa alishakanusha siku moja tu nyuma juu ya kushikiliwa kwa Bombardier. Huyu ni mjumbe wa baraza la mawaziri. Lakini siku moja baadaye, msemaji wa serikali anakiri kuwa ni kweli inashikiliwa. Hii inaonesha kuwa huko ndani, nje ya ukali wa Rais Magufuli, kuna vikuku vya mkufu wa mawasiliano ndani ya utawala vimekatika. Na huo ni udhaifu mkubwa.
Pili, miaka miwili baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli ameshindwa kupanga timu yake ya mkakati vyema. Bado utendaji wake na wa timu yake unakwendana na mapigo ya kinachoendelea mitandaoni na kwenye majukwaa ya kisiasa.
Mawasiliano baina ya serikali na umma yanajengwa na kipi kimeibuliwa na ‘waropokaji’ huku nje – mitandaoni, majukwaani, mitaani. Ujanja wa kuziwahi taarifa mapema ili kuchomeka wazo ambalo serikali inataka liwe wazo kuu kwa wananchi haumo ndani ya vichwa vya timu ya mkakati ya Rais Magufuli.
Tatu, na la mwisho, serikali inadanganya kwa jina la uzalendo. Kuanzia Rais Magufuli mwenyewe hadi wanaomfuata chini yake, kauli yao kubwa ya kukumbizia takataka chini ya zulia ni kwamba taifa letu linahitaji uzalendo wa hali ya juu, ambao kwa maoni yao ulikuwa umekosekana siku nyingi huko nyuma.
Wakati hilo ni sahihi kabisa, kisichokubalika ni kwa serikali hiyo hiyo kuficha ukweli au kudanganya kwa wananchi ili kujenga mapenzi yasiyo ya kweli kwa serikali yao.
Ingelikuwa vyema kabisa kile kinachohubiriwa na Rais Magufuli majukwaani, kwamba yeye ni msema kweli, kikawa ndicho kinachoakisika katika mtiririko mzima wa wanaomfuata chini yake. Na inapobainika kwamba kimakosa serikali ilidanganya au ilificha ukweli uliopaswa kufahamika na umma kwa wakati muafaka, basi iwe tayari kuomba radhi haraka na kwa ufanisi.
Mapenzi na uzalendo hujengwa juu ya ukweli na uwazi.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 22 Agosti 2017.
Magufuli anawauzia Watanzania tamaa ya maendeleo kwa gharama ya demokrasia yao
Kwa hakika, Rais John Magufuli anaonekana kuwalazimisha raia wake kufanya naye biashara ya gizani. Yeye awauzie maendeleo, nao wamlipe kwa gharama ya demokrasia angalau hadi mwaka 2020 wakati wa kampeni za uchaguzi mwengine.
Lakini je, biashara hii inawezekana kwa taifa ambalo lilishaonja ladha ya demokrasia kwa robo karne nzima mtawaliya? Je, ili kupata maendeleo ni lazima kuitia rehani misingi ya kikatiba, mgawanyo wa madaraka, haki za binaadamu na uhuru wa mtu binafsi?
Akizungumzia dhana ya demokrasia, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anasema: “Demokrasia haihusiani pekee na ile siku moja kila baada ya miaka minne au mitano pale panapoitishwa chaguzi, bali inahusiana na mfumo wa serikali unaohishimu mgawanyo wa madaraka, uhuru wa mawazo, wa kidini, wa kujieleza, wa kujiunga na kujikusanya na pia utawala wa sharia. Utawala wowote unaokanyaga misingi hii, hupoteza uhalali wake wa kidemokrasia, hata kama awali uliingia madarakani kwa kushinda uchaguzi.” (Tafsiri ni yangu).
Dk. Chris Sausman, Mkurugenzi wa Chime Communications Group, anayatafsiri maendeleo kwa umbo la pembe tatu. “Kwanza ni mchakato ambao ndani yake muna mkururo wa hatua zinazopelekea – au zinazotegemewa kupelekea – matokeo ya aina fulani makhsusi, pili ni mkakati ndani ya mipango na sera na, tatu, ni matokeo ya mikondo miwili ya kwanza kupitia kiwango cha mtu binafsi – pale anapokuwa na kuutumia uhuru wake, kiwango cha jamii – pale inapoweza kutoka hatua moja ya kimaisha kwenda nyengine na kiwango cha kiuchumi – pale uchumi wa jumla unapoimarika.” (Tafsiri ni yangu).
Namna dhana hizi mbili za demokrasia na maendeleo zinavyoungana zinatuambia kuwa biashara anayoifanya Rais Magufuli na Watanzania haitakuwa na mwisho mwema, hata kama sasa kunatolewa takwimu za mapambio.
Kama anavyosema Mkuu wa Madhehebu ya Shia Ismaili duniani, Aga Khan, “kimsingi maendeleo na demokrasia vimeungana na kuimarika kwa thamani ya maisha ya binaadamu. Uwezo wa kuifahamu (na kuihishimu) mifumo ya kikatiba, uwepo wa vyombo vya habari huru na vyenye kujumuisha wote, asasi imara za kijamii na dhamira ya kweli katika kuelekea utangamano na majadiliano ya kijamii. Hii ndiyo misingi mikuu ya kufikia lengo la maisha bora. Demokrasia inaweza tu kudumu kama inaonesha, muda wote na mwahala mote, kwamba ni njia bora kabisa ya kufikia lengo hilo.” (Tafsiri ni yangu).
Tanzania inapitia kwenye moja ya vipindi vigumu sana vya historia yake ya hivi karibuni. Baada ya kujaribu kuujenga mfumo wa kidemokrasia kwa miongo miwili na nusu, sasa jitihada hizo zinarudi nyuma kwa kasi ya ajabu.
Misingi mikuu ya demokrasia inashambuliwa kila uchao na serikali ya Rais Magufuli, akiamini kuwa ana uhalali wa kufanya lolote atakalo kwa kuwa tu madaraka ya juu yamo mikononi mwake.
Hata miaka miwili haijatimia vyema tangu ale kiapo cha utiifu kwa Katiba, Rais Magufuli ameshathibitisha kuwa yeye si muumini wa misingi mikuu ya Katiba yenyewe, kama vile mgawanyo wa madaraka na hishima kwa uhuru na haki za binaadamu.
Kwa mfano, mara kadhaa muhimili wa utawala kupitia kwake na wateule wake, umekuwa ukiingilia muhimili wa bunge kuwafunga midomo wabunge, kuzima mijadala yenye maslahi kwa taifa na hata kuzuwia matangazo ya bunge hilo kuoneshwa moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa, ambayo inaendeshwa kwa kodi ya wananchi.
Wakati akizuwia matangazo hayo kwa kisingizio cha gharama na kubana matumizi ya serikali na pia kuwapa muda wananchi kufanya kazi, shughuli za kisiasa zake na za chama chake, CCM, hupewa nafasi ya kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya umma, vinavyolipiwa kwa fedha ya umma na katika wakati wa kazi.
Ndani ya kipindi hiki kifupi, wabunge kadhaa wameshakamatwa, kupigwa, kuwekwa vizuizini na hata kufungwa jela, na katika baadhi ya mifano wakiwa ama bungeni au majimboni mwao katika shughuli zinazohusiana na nyadhifa na madaraka yao kama wabunge na au viongozi wa vyama vyao.
Ndani ya kipindi hiki kifupi, Rais Magufuli ameshatoa kauli kadhaa zinazoingilia moja kwa moja uhuru wa mahakama na vyombo vyengine vinavyohusiana moja kwa moja na upatikanaji haki kama vile ofisi ya mwendesha mashitaka, polisi na idara za upelelezi, kwa kuwatia hatiani hadharani wale wote anaowashuku.
Matokeo yake, kwa kuwa tuna aina ya Katiba inayompa mkuu wa nchi nafasi ya uungu mtu, walio chini yake kwenye vyombo hivyo wanajipendekeza kuigeuza kila “kauli ya rais” kuwa ukweli, hata kama kwa kufanya hivyo wanazikanyaga sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea wenyewe kama taifa.
Ndani ya kipindi hiki kifupi, Tanzania imejikuta ikirejea kwenye zama za giza – ikitajwa kuwa na matukio ya utekaji nyara, upoteaji watu, ukamatwaji ovyo ovyo unaofanywa na vyombo vya dola, na hata mauaji dhidi ya raia na pia dhidi ya askari wetu, ambao wana jukumu la kuwalinda raia hao.
Ndani ya kipindi hiki kifupi, kesi kadhaa zimefunguliwa na serikali yake dhidi ya wananchi wa kawaida wanaotumia mitandao ya kijamii kuelezea maoni na mawazo yao kuhusiana na mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya nchi. Sambamba na hilo, magazeti kadhaa yamefungiwa na vyombo vya habari vimevamiwa na waandishi wa habari kushambuliwa, kupigwa na hata kuwekwa ndani, wakati wakiwa kwenye majukumu yao ya kukusanya na kusambaza habari.
Ndani ya kipindi hiki kifupi, Rais Magufuli ameirejesha Tanzania kwenye mfumo wa chama kimoja kwa kuzuwia shughuli zozote za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na hata ya ndani, sikwambii maandamano na midahalo ya kitaifa hadi mwaka 2020, kwa kile anachodai ni kumpatia muda wa kutekeleza ilani ya chama chake aliyoinadi kwenye kampeni za uchaguzi wa 2015.
Mara kadhaa, polisi yake imewatia nguvuni viongozi wa upinzani wakiwa kwenye shughuli zao za kisiasa, ingawa haifanyi hivyo kwa viongozi wa CCM wakiwa kwenye shughuli kama hizo.
Tumeshuhudia kiwango kikubwa kabisa cha kukosewa hishima taratibu za kinchi kwenye teuzi, utenguwaji, utendaji na hivyo uwajibikaji wa watumishi wa sekta ya umma. Kila mmoja, kutoka raia wa chini kabisa hadi afisa wa juu serikalini, anaishi kwenye khofu ya kulengwa na kuandamwa si kwa sababu ya makosa anayoyatenda, lakini kwa sababu ya ‘hisia’ za mtawala mkuu wa nchi, ambazo nazo hutokana na taarifa zisizo sahihi anazofikishiwa na wale alioamua pekee kuwaamini na kuwakubali ‘ukweli’ wao.
Kila mtu na kila taasisi ambayo ni tishio kwa ‘ukweli wa hisia’ za mtawala, basi haiko salama. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo viliisababisha kwa mara ya kwanza CCM kushindwa kupata asilimia 60 ya kura za urais ndani ya miaka 25 vinanyanyaswa kusudi na vyombo vya dola.
Chama cha Wananchi (CUF) ni mmoja wa wahanga wakubwa wa kipindi hiki kifupi cha utawala wa Rais Magufuli, kwa kuwa kinaonekana kukataa kuwa sehemu ya ‘ukweli wake wa hisia’ kwamba rais pekee ndiye anayemiliki maoni, mawazo, na njia sahihi kwa kila kinachojiri, likiwemo suala tete la ‘uhuni’ uliofanywa na CCM na vyombo vya dola dhidi ya maamuzi sahihi ya wananchi wa Zanzibar ya tarehe 25 Oktoba 2015.
Kwa ufupi, ndani ya utawala huu wa awamu ya tano, misingi ya kidemokrasia, kama ilivyotajwa hapo juu na Kofi Annan, inakanyagwa na utawala wa Rais Magufuli. Yote kwa jina la kumpa yeye nafasi ya kuleta maendeleo aliyoyaahidi kwa wananchi.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 24 Julai 2017.
*Siasa za Muungano na hatima ya uchumi wa Zanzibar
Kwa miaka yote hii 45 ya Muungano, habari imekuwa ndiyo hiyo. Kwa jina la Tanzania, Tanganyika imeendelea kujizolea kila kilicho cha Zanzibar kukipeleka kwenye Muungano kwa kisingizio cha kuuimarisha; na Zanzibar inazidi kufa kwa kuwa inaingiza kila chake kwenye tumbo la Mfalme Jeta lisiloshiba! Na baya zaidi ni kuwa Tanganyika inaambiwa haipo, basi Zanzibar imekosa mshirika wa kuongelea naye matatizo ya Muungano, maana anayeiwakilisha Tanganyika ni huo huo Muungano!
1. Utangulizi
Kuna msemo wa Kiingereza unaosema: “When the hunted knows how to hunt, the hunting game is no more!” Yaani pale kiwindwa kinapojuwa kuwinda, mchezo wa kuwindana huwa umekwisha.
Tangu Waziri Mkuu Mizengo Pinda atoe kauli yake Bungeni mwaka jana, kwamba Zanzibar si nchi, vuguvugu la Wazanzibari kuzungumzia khatima ya nchi yao ndani ya Muungano huu, ambao unatimiza miaka 45, halijapoa. Ingawa ni mapema mno kujitangazia ushindi, lakini si vibaya kupongezana kwamba hatua tunayoichukua sasa ni ya haki na ya halali, kwetu na kwa nchi yetu. Ni alama ya mapambano ya jamii ya watu wanaoamini kwamba wamekuwa wakikandamizwa na ambao, kama ilivyo kanuni ya kimaumbile, wana wajibu wa kunyanyuka kujipapatua dhidi ya ukandamizwaji huo.
Nimetakiwa kuzungumzia mawili matatu kuhusu mada hii kubwa, pana na kongwe. Nami nitafanya hivyo kwa kadiri niwezavyo. Lakini kabla ya kuingia undani wa mada yenyewe, naomba nitoe tanbihi. Kwanza, nimealikwa hapa kama kijana wa kawaida tu wa Kizanzibari na sio msomi. Kwa hivyo, nisitarajiwe kuwa nitafuata utamaduni wa wasomi, ambao wanalaumiwa kuwa ni wazito wa kufanya maamuzi, wasiri wa kueleza misimamo yao na kutokusema moja kwa moja wanachokimaanisha, wakikhofia kukosolewa na wasomi wenzao au kupoteza heshima zao za kitaaluma. Badala yake, nitarajiwe kwamba nitazungumza kama kijana, kwa ari nyingi, jazba kidogo na uwazi wa kutosha, maana sina lolote la kupoteza katika zaidi ya minyororo iliyofungwa nchi yangu ya Zanzibar!
Pili, uchambuzi wangu huu unaongozwa na hoja tatu zifuatazo: Moja, bila ya kuzingatia maandiko yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, uchambuzi huu unatambua kwamba Tanganyika na Serikali yake ni vitu hai, vipo na vinaishi. Kwamba hii iitwayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo hiyo hiyo Tanganyika yenye mipaka na jina jipya, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ndiyo hiyo hiyo Serikali ya Tanganyika.
Mbili, Serikali hiyo ya Tanganyika, ambayo imepewa jina la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina sera yake maalum kuelekea Zanzibar ambayo, ingawa kimaandishi haikuandikwa popote, lakini kiuhalisia inasomeka kila mahala. Sera hiyo inasema: “Kuwa na Jamhuri ya Muungano imara, ni kuwa na Zanzibar dhaifu; na kuwa na Zanzibar imara ni kuwa na Jamhuri ya Muungano dhaifu.” Kwa hivyo, linapokuja suala la nafasi ya ‘siasa za Muungano kuelekea uchumi wa Zanzibar’, huo ndio ninaoutambua kuwa mtazamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kama uchambuzi huu utakavyothibitsha.
Tatu, kihistoria, Wazanzibari wameandaliwa kuuangalia Muungano huu katika sura ya Shirikisho, ambalo lilichukuwa baadhi tu ya mamlaka kutoka kila upande, yaani Tanganyika na Zanzibar, na kubakisha sehemu nyengine ya mamlaka hayo kwa serikali za nchi husika. Hiyo ndiyo dhana inayoakisika katika Katiba ya Zanzibar. Lakini Watanganyika wameandaliwa kuuangalia Muungano huu kama ni wa serikali moja tu, ambapo hawaoni mipaka ya kimamlaka baina ya Zanzibar na Tanganyika. Hiyo ndiyo dhana inayoakisika katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Mambo haya matatu, kwa hivyo, ndiyo muongozo wa uchambuzi huu. Ni maoni yangu kwamba ndani ya Muungano huu, Tanganyika imekuwa ikitumia sura zake mbali mbali inazojidhihirisha kuinafiki (kuichoma kisu mgongoni) Zanzibar, kwa upande mmoja, na kuitia kabari Zanzibar, kwa upande mwengine.
2. Suala la Bodi ya Sarafu na Namna Zanzibar Ilivyochomwa Kisu Mgongoni na Tanganyika
Turudi kwenye historia kidogo kuona namna ambavyo Tanganyika imeutumia Muungano kuinafiki Zanzibar kwa hadaa na ghilba. Wazungu huita hali hii “knife on the back.” Nyaraka zilizopatikana kutoka Crown Agency London, Uingereza, zinaibua siri nzito ambayo inafunua namna Tanganyika ilivyotumiliwa na kujikubalisha kutumikia matakwa ya mkoloni, Muingereza, ili kuinyima Zanzibar nguvu za kiuchumi kwa makusudi. Ni suala la Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB).
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wakati wa ukoloni zile nchi zilizojulikana kama East African Territories – Kenya, Uganda, Tanganyika, Zanzibar, Somalia na Aden – zilikusanywa pamoja katika Bodi ya EACB. Baada ya kupatikana kwa uhuru, Aden na Somalia ziliamua kujiondoa kwenye Bodi hiyo, lakini nyingine ziliendelea. Zanzibar haikuwa inajuwa kuwa kumbe wakati huo, tayari Tanganyika ilishatakiwa na mkoloni wake, Uingereza, kuhakikisha kwamba uwezo wa Zanzibar kifedha na kiuchumi unaporomoshwa kwa kadiri ilivyowezekana ikianza na kuuondoa uwakilishi wake kwenye Bodi hiyo.
Mwaka 1964, kulikuwa kuwe na mkutano wa Bodi hiyo. J.B. Loynes, ambaye alikuwa na dhamana katika Wizara ya Makoloni ya Uingereza alimuandikia H. R. Hirst, ambaye alikuwa katibu wa Bodi kwamba: “…isipokuwa kama kuna kauli madhubuti kutoka Dar es Salaam inayothibitisha kuhudhuria kwa Zanzibar (na tusiwe sisi tunaozua suala hilo), haitokuwa sawa kwa Bodi kumualika mwakilishi kutoka Zanzibar kwa sasa. Kusema kweli, italeta fadhaa kuona wale wenye nia ya kujitenga huko Visiwani wanapewa kichwa.”
Hata hivyo, Hirst alikuwa amefahamishwa na Jacob Namfua, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wa Tanganyika, kuwa suala la kuiondoa Zanzibar kwenye Bodi hiyo lilikuwa ni kinyume na Mkataba wa Muungano, maana mpaka wakati huo suala la sarafu halikuwa la Muungano. Barua ya Namfua kwa Hirst ya Juni 9, 1964, inaeleza: “Nimeagizwa kutamka kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Muda inayoongoza Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, katika vikao vya siku za mbele vya Bodi, utaendelea kwa utaratibu ule ule kama ilivyokuwa kabla ya Muungano. Makubaliano ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar hayahamishi moja kwa moja mambo ya sarafu kuingia katika Serikali ya Muungano na mpaka yatakapofanywa mabadiliko kama itakavyokubaliwa, uanachama wa Bodi ya Sarafu unabaki kama ulivyo.”
Lakini inaonekana kuwa Uingereza ilikwishaamua kwamba iwe iwevyo, Zanzibar haikutakiwa kabisa kuwemo kwenye Bodi hiyo. Kwa hivyo, Loynes akamuandikia tena Hirst Septemba 8, 1964 akimwambia: “Tunaweka wazi kwamba hatuitaki Zanzibar katika kikao chetu kinachofuata na natumai lazima kutakuwa na njia zinazoweza kuwaweka nje. Lile ambalo ningependa kufanya kwa sasa ni kukumbusha juu ya suala hili, ili kuhakikisha kwamba hakuna makabrasha yanayovuka bahari hadi tutapokuwa na uhakika wa msimamo wetu.”
Kufika hapo, Tanganyika kwa kuwa ilikuwa yenyewe tangu mwanzo haina dhamira njema na khatima ya Zanzibar kiuchumi na, kwa kuwa, ilikuwa tayari kutumikia hata maslaha ya wale ambao Mwalimu Julius Nyerere alikuwa huku nje akiwaita mabeberu, ikapiga magoti kutimiza matashi yake na matakwa ya Muingereza.
Mgao wa ziada wa fedha za Bodi ulifanywa Oktoba 1964 na fungu la Zanzibar hapo, na kuanzia hapo, lilikwenda katika kasha la Tanganyika katika Crown Agency (rejea barua ya W.H. Tweed ya Oktoba 1, 1964).
Ghilba hii ‘ilihalalishwa’ kwa Toleo la Sheria, Mswada Na. 43, la Juni 18, 1965, ambapo ilielezwa: “Mambo yafuatayo sasa yanatengwa kwa Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na yanatangazwa kuwa Mambo ya Muungano: mambo yanayohusiana na sarafu na mzunguko wake – na shughuli za benki, fedha za kigeni na udhibiti wa viwango vya kubadilishana fedha, na kifungu kidogo (1) cha kifungu 68 cha Katiba ya Muda hivi sasa kinarekebishwa kwa kuongeza mambo yaliyotajwa kama jambo jipya (xii) katika tafsiri ya ‘Mambo ya Muungano.”
Kwa hakika huu, kama alivyokuwa akiuita Marehemu Ali Nabwa, ulikuwa ni “ujambazi wa hali ya juu” dhidi ya Zanzibar! Ulikuwa uonevu wa dhahiri uliofanywa na Nyerere, Amir Jamal (aliyekuwa Waziri wa Fedha) na Edwin Mtei (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo) kwa kuchochewa, kuongozwa na kudhibitiwa na watawala, wakoloni Waingereza.
Ni wazi kuwa, kwa Tanganyika kutimiza matakwa ya Uingereza, kulikuwa ni kujidhalilisha yenyewe mbele ya mkoloni huyo, na ndiyo maana hata katika nyaraka hizo nilizozitaja unaiona dharau ambayo Waingereza waliionesha kwa viongozi hao wa Tanganyika. Kwa mfano, Loynes alimtaja mara moja Mtei kama kitakataka tu (Nabwa, 2003).
Lakini japokuwa hii ilikuwa ni aibu kwa upande wa Tanganyika, ilikuwa ni aibu iliyowasaidia kuzivunja nguvu za Zanzibar kiuchumi na imekuwa ndiyo hasara kwa upande wa Zanzibar, kwani baada ya hapo zilifuatia rasimu kwa rasimu za barua iliyokuwa inatakikana kuhalalisha kutolewa kwa Zanzibar nje ya Bodi, huku Loynes akisisitiza kwamba lugha iwe makini kiasi kwamba wao (wapanga njama hizi) wasiweze kutambulika, maana wote walijuwa kuwa wanayoyafanya yalikuwa kinyume na sheria.
Yaliofuata hapo ni historia ya mzozo mmoja mkubwa katika Muungano unaohusisha nafasi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na nani anamdai mwenzake – baina ya Zanzibar na Tanganyika – katika Muungano huu.
3. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Kabari za Tanganyika kwa Zanzibar
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianzishwa kutokana na Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 1965 ili kuchukua jukumu la kifedha lililokuwa likisimamiwa na EACB iliyokuwa na Makao yake Makuu Nairobi, Kenya.
Lakini kuanzishwa kwa BoT hakukuja hivi hivi tu, bali kwenyewe kulikuwa ni matokeo ya dhuluma iliyofanyiwa Zanzibar kwenye EACB kama ilivyooneshwa hapo juu. Ili kufanikiwa kuitupa Zanzibar nje ya Bodi hiyo, Tanganyika iliingiza haraka haraka shughuli za matumizi ya sarafu na utawala wa mabenki katika Muungano.
Kwa kutumia Katiba ya Muda ya Muungano (1965), Sheria Na 43 ya 1965 (1965 Act. No. 43 of 1965), Serikali ya Tanganyika ilipeleka Bungeni marekebisho ya kifungu Na. 85 cha Katiba hiyo na kuongeza kifungu kidogo Na. XII cha Orodha ya Makubaliano ya Muungano kinachohusu masuala ya fedha, mabenki, sarafu, fedha za kigeni na udhibiti wa fedha za kigeni kuwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano kama inavyosemeka.
Gazeti la Serikali ya Muungano la tarehe 18 Juni 1965 ndilo lililotangaza kufanyika marekebisho hayo ambayo ni kinyume kabisa na Makubaliano ya Muungano ya 1964. Baada ya kufanyika marekebisho hayo, Edwin Mtei aliandika barua rasmi kwa Katibu wa EACB na kumueleza kwamba kuanzia Disemba 29, 1965 kwamba kuanzia hapo ni yeye Mtei ndiye angeliiwakilisha Tanzania katika Bodi hiyo. Kwa hakika, hili lilikuwa ndilo jambo lililokuwa likitakiwa na Waingereza.
Baada ya kukamilika kufanyika marekebisho haya ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano, Waziri wa Fedha wa wakati ule wa Tanganyika, Amir Jamal, alimuandikia barua Mwenyekiti wa EACB na kumuagiza rasmi kwamba haki zote na amana zote za Zanzibar zilizokuwemo katika Bodi hiyo, zipelekwe katika Benki Kuu chini ya Serikali ya Muungano na kwamba kuanzia pale ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania pekee ndiye tu atakayeiwakilisha Tanzania katika Bodi hiyo. Haya yalifanyika baada ya kulazimisha kuingizwa kifungu Na. XII katika Orodha ya Mambo ya Muungano ambacho hakikuwemo kabisa katika Makuabaliano ya Muungano ya 1964 (Duni, 2008).
Uchambuzi huu unaiita hii kuwa ni kabari ya kijambazi ya Tanganyika kwa uchumi za Zanzibar. Kuyatia masuala ya fedha katika Orodha ya Mambo ya Muungano ulikuwa ubabe wa makusudi maana ni jambo ambalo, kisheria, lisingeweza kufanyika bila ya idhini ya Zanzibar na pia wizara ya fedha ya Muungano haikuwa na haijawahi kuwa ya Muungano hadi leo. Kama kulikuwa na kitu cha Muungano hadi wakati huo kwenye masuala ya fedha, ilikuwa ni usimamizi wa taratibu na utoaji wa sarafu na udhibiti wa mwenendo wa kubadilisha thamani ya shilingi tu.
Serikali ya Muungano haikuwa imepewa idhini ya kusimamia fedha za Zanzibar na kile ilichokifanya kwa kuzitwaa fedha za Zanzibar hakiwezi kupewa jina jengine la kiungwana zaidi ya wizi uliofanywa kwa jina la Dola. Maana kilichofuatia baada ya hapo ni kuwa, fedha hizo ziliingizwa kuanzisha mtaji wa BoT, ambayo leo hii Zanzibar inaambiwa haina chake.
Ukweli ni kuwa BoT ina mchango wa Serikali ya Zanzibar ambao ulitokana na mgawo wake ilioupata baada ya kuvunjika kwa EACB. Kumbukumbu zinaonesha kwamba wakati wa kuanzisha kwa BoT, Bodi ya EACB ilikuwa imeshapeleka paundi za Kiingereza 82, 840 kama ni mchango wa Zanzibar katika uanzishwaji wa Benki hiyo.
Duni (2008) anaeleza vyema hisabu halisi ya mtaji wa BoT na mchango wa Zanzibar katika mtaji huo, kwamba benki hiyo ilianzishwa kwa mtaji wa paundi milioni moja (1,000,000) za Kiingereza ambayo ilikuwa ni sawa na milioni 20 za Afrika Mashariki kwa wakati huo, ambapo Serikali ya Tanganyika ilitoa paundi 668,884, ya Zanzibar ikatoa hizo 82,840 na kasoro ya kujalizia ili kufikia pauni 1,000,000 – yaani paundi 248,276 – ikajazwa na Serikali ya Muungano, ambayo Zanzibar ni sehemu yake.
Hisabu ya mtaji wa BoT inaelezeka hivi:
Mchangiaji Kiwango cha Mchango (kwa Paundi)
Tanganyika = 668,884
Zanzibar = 82,840
Jumla Ndogo (Tanganyika na Zanzibar) = 751,724
Serikali ya Muungano = 248,276
Jumla Kuu = 1,000,000
Katika hili la BoT, hoja ya Zanzibar sio tu kwamba Zanzibar ina amana yake katika uanzishwaji wa benki hiyo ambayo, hata hivyo, kwa miaka yote hii Serikali ya Muungano hawataki kuitambua, lakini zaidi ni kuwa sheria iliyoianzisha benki hiyo ilikuwa na misingi ya kibeberu, ambapo iliipa Serikali ya Muungano nguvu zote za kumiliki na kusimamia fedha huku ukiipopotoa kabisa Zanzibar. Kwamba pamoja na mchango wake wa asilimia 11.02 katika mtaji ulioanzisha BoT, Serikali ya Zanzibar haikutajwa kabisa kwenye sheria hiyo.
Badala yake sheria hiyo, kwa makusudi, inaiteremsha hadhi Serikali ya Zanzibar kwa kuilinganisha kuwa sawa na Serikali ya Mkoa. Hii maana yake ni kuwa, kama ambavyo serikali za mikoa haziwezi kukopeshwa, ndivyo ilivyo pia kwa serikali ya Zanzibar. Leo hii, ikiwa Serikali ya Zanzibar inataka kukopa BoT, inalazimika kufanya hivyo kwa kupitia Serikali ya Muungano tu, na si vyenginevyo. Lakini kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano na Katiba zote mbili ambazo zilipaswa kuutafsiri Mkataba huo, Serikali ya Zanzibar ndiyo yenye jukumu la kusimamia uchumi wa Zanzibar. Ni vipi Serikali inaweza kusimamia uchumi ikiwa haina mamlaka kwenye fedha na njia za kuzipata fedha hizo?
Kuinyima Serikali ambayo ina jukumu la kusimamia uchumi wa watu wake nguvu za kukopa na kufanya mikataba inayohusiana na fedha na taasisi nyengine ni unyongaji wa makusudi, na kwa bahati mbaya Zanzibar imejikuta katika kitanzi hicho.
4. Suala la Mafuta na Gesi: Chetu Chao, Chao Chao
Mwaka 1999 nilikuwa mwanafunzi wa Diploma ya Lugha katika chuo hichi hichi ambacho leo natoa mhadhara huu. Wakati huo tulikuwa tunaelekea katika uchaguzi wa 2000 na suala la nishati ya mafuta na gesi lilikuwa limeanza kuonekana kuwa lingeliweza kuwa sehemu muhimu ya kampeni za uchaguzi huo.
Baada ya kuwa Wazanzibari wengi tumejifunza ukweli kwamba suala hilo lilishaingizwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano zaidi ya miaka 10 nyuma ya hapo, tena kwa njia sizo, mimi niliandika shairi nililoliita Chetu Chao, Chao Chao na kulibandika kwenye ubao wa habari za wanafunzi. Kwa idhini yenu, naomba ninukulu baadhi ya beti za ushairi huo:
Naandika kwa kilio, machozi hadi viatu
Wino ndilo kimbilio, na shahidi Mola wetu
Nayawahi haya leo, bado ningalithubutu
Nawahi huu ubao, bado ungali ni wetu
Sababu hatuna chetu, vyote vishakuwa vyaoNisaidieni kilio, tulieni wanakwetu
Tulie kwa tufanywayo, tuporwapo haki yetu
Iyoneni hiyo hiyo, yatolewa ndani mwetu
Wanayo wenenda nayo, wasema yao si yetu
Ya Ilahi Mola wetu, hebu lete hukumoyo!Utesi si kusudiyo, naicha gowe si kitu
Bali hichi ni kiliyo, chozi letu na wenetu
Twalia tupokonywao, tupokwapo kilo chetu
Twalia watupokao, na kale wali wenzetu
Cha kwao wao si chetu, lakini chetu ni chaoTazamani muonao, onani hii papatu
Haya wayachukuwayo, yetu siye mali yetu
Wazitwaa hata nyoyo, hata hizi roho zetu
Na miili ndiyo hiyo, sasa waujia utu
Punde ‘takuwa vibutu, yote washakwenda nayo!Ni uchungu unipao, na nguvu na jasho letu
Kwani chao kiwe chao, chetu kisiwe ni chetu?
Kwetu kuwapo ni kwao, kwao hakuwini kwetu?
Mungu hakuwapo vyao, shuruti watwae vyetu?
Kwa nini hatuna chetu, tulichonacho ni chao!?
Mwaka 2003, nikiwa mwandishi wa makala za uchambuzi katika gazeti huru la Dira Zanzibar, niliandika makala refu – Kazi yao kunanusha tu – kulalamika kwamba, Serikali ya Zanzibar ilikuwa ikijaribu kuficha ukweli kwamba shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi katika eneo la nchi ya Zanzibar zilikuwa zimeshaanzishwa na kampuni ya Antrim Energy ya Canada, lakini zikiwa zinasimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Mafuta la Tanzania (TPDC), ambalo lenyewe hakikuwa chombo cha Muungano. Kwamba mpaka hapo tayari Wazanzibari tulikuwa tumeshasukumwa nje ya duara la kufaidika na rasilimali hiyo kwenye ardhi yetu.
Sasa, mwaka wa 10 kumi tangu kubandika shairi hilo kwenye ubao wa habari za wanafunzi wa chuo hichi na mwaka wa sita tangu kuchapishwa kwa makala hiyo na Dira Zanzibar, sioni kuwa ninaweza kukisema kitu kizuri zaidi kuhusu hila za Serikali ya Muungano panapohusika nishati hizi, kuliko kile kilichosemwa na Serikali yenyewe ya Zanzibar katika Baraza la Wawakilishi kupitia Waziri wake wa Nishati, Ardhi, Ujenzi na Mazingira, Bwana Mansour Yussuf Himid, tarehe 2 Aprili, 2009.
Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Serikali ya Zanzibar, ni kuwa, kumbe Serikali ya Muungano ilishaingia mkataba na Antrim Energy kuanza kazi za kukusanya taarifa za kitaalam za nishati ya mafuta katika eneo linalohusisha kilomita 100 za kisiwa cha Pemba na kilomita 100 kwa kisiwa cha Unguja na kilomita 200 kwa eneo la bahari kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 3.5 kwa mika miwili ya mwanzo kuanzia Aprili 2002 mpaka Aprili 2004. Kwa kipindi cha miaka miwili nyengine kinachofuatia – yaani kuanzia Aprili 2004 mpaka Aprili 2006, Antrim walitakiwa wachimbe kisima cha utafiti wa mafuta kwa maeneo ya Kaskazini Pemba kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 4.
La kukumbushwa hapa ni kwamba mkataba huu wa mamilioni ya dola ulifungwa tangu mwaka 1997 katika makubaliano yaliyofanywa baina ya kampuni hiyo na Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania Bara, ambayo si ya Muungano, tena bila ya ridhaa ya Serikali ya Zanzibar.
Na, hakika si wizara tu ambayo si ya Muungano, bali hata TPDC lenyewe si la Muungano. Hili ni shirika lililoanzishwa kwa tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Mei, 1969 na Sheria ya Makampuni ya Umma ya 1969 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kurekebishwa na Sheria mpya ya mwaka 1992 inayotumika hivi sasa huko Tanzania Bara (Himid, 2008).
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar halijawahi kupitisha sheria ya kulifanya shirika hilo kuwa la Muungano kama yalivyo matakwa ya Katiba ya Zanzibar katika Sura ya 13 Kifungu Namba 132 (1). Kwa hakika, kwa mujibu wa Serikali ya Zanzibar, “japokuwa TPDC ina sura na tafsiri ya chombo cha Muungano kinachosimamia utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi, hususan kwa masuala yanayohusiana na mafuta na gesi asilia, haupo. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawakilishwa na mjumbe mmoja tu kutoka Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi ndani ya bodi ya TPDC.”
Hansard za Baraza la Wawakilishi la Zanzibar zinaonesha kuwa wajumbe wa Baraza hilo wamesema mara kadhaa kwamba suala la mafuta na gesi kuwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano lilifanywa ‘kinyemela’ katika wakati wa Mwalimu Nyerere. Kiogozi wa sasa wa Kambi ya Upinzani, ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Bwana Abubakar Khamis Bakary, anasema kwamba anakumbuka kwamba waliposhtukia hilo, walimkabili Mwalimu Nyerere na kumueleza, naye akakiri kuwa ni kweli liliingizwa kimakosa na kwamba angeliagiza liondolewe hadi hapo mjadala utakapokuwa umefanyika na makubaliano kufikiwa. Lakini inaonekana kwamba Mwalimu Nyerere hakuona ulazima wa kutembea juu ya maneno yake panapohusika maslahi ya Zanzibar. Kwa Nyerere, na kwa viongozi wengi wa Tanzania Bara, chao ni chao na chetu pia ni chao!
Sasa nini athari za kuliingiza na kulibakisha suala la nishati za mafuta na gesi asilia katika mikono ya Serikali ya Muungano? Kwanza kama nilivyokwishatangulia kuhoji mwanzoni, Serikali ya Muungano na Serikali ya Tanganyika ni kitu kimoja, na kwamba Serikali hiyo ina siasa yake kuelekea Zanzibar, ambayo inasema kwamba: “ukiwa na Zanzibar imara, utakuwa na Muungano dhaifu” na vivyo kinyume chake.
Kwa hivyo, mtu akifuatilia uzoefu wa namna Zanzibar ilivyochomwa visu vya mgongo kwenye suala la Bodi ya Sarafu na kisha kuja kutiwa kabari kwenye suala la Benki Kuu, ni wazi kuwa Zanzibar haitaweza kufaidika kiuchumi na nishati hizo zilizomo kwenye ardhi zake. Kwa kuwa suala la mapato, kwa mfano, ni la Muungano, basi ni wazi kuwa Zanzibar itakosa mapato yote yatakayotokana na usajili wa makampuni ya uchimbaji wa mafuta, na utoaji wa leseni pamoja na kuzipasisha.
Serikali ya Zanzibar ina kumbukumbu ya namna ambavyo Kampuni ya Zantel imekuwa ikilipa jumla ya dola za Kimarekani 3,000,000 (karibuni shilingi bilioni nne) kila mwaka kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ndiyo inayotoa leseni, huku Zanzibar ikiwa haipati hata shilingi. Zantel pia inalipa mrahaba wa dola 200,000 za Kimarekani (takribani shilingi milioni mia tatu) kwa Tanzania Bara hivi sasa.
Kufupisha maneno katika suala hili la mafuta na gesi asilia, lilikuwa ni pigo la makusudi la kiuchumi kuliweka katika Orodha ya Mambo ya Muungano na ingawa sasa Serikali ya Zanzibar imeonekana kujikakamua kutaka kulirudisha katika mamlaka ya Zanzibar, lazima tukiri ukweli kwamba tuna kazi ngumu ya kusaidiana na serikali yetu kufanikisha hilo. Uzoefu ni kwamba, Muungano umekuwa kama yule Mfalme Jeta, anayetajwa na Sheikh Shaaban Robert katika hadithi ya Kusadikika, ambaye ingawa mito, bahari, maziwa, tani za magogo, mawe na udongo hutiririka kuingia kinywani mwake, bado kila wakati hulia: “Njaa! Njaa! Kiu! Kiu!”
Ikiwa Wazanzibari kupitia serikali yao wataweza mara hii kuizuia mifereji ya mafuta na gesi asilia yao isielekee kwenye kinywa cha Mfalme Jeta, basi hilo litakuwa tukio la kihistoria, amblo sio tu litazinusuru fedha zao, bali pia litawapa fakhari ya kutimiza matakwa ya Katiba yao, ambayo katika kifungu chake cha 10 (3), kinaipa jukumu Serikali ya Zanzibar kudhibiti uchumi wa nchi kufuatana na misingi ya madhumuni yaliyoelezwa na Katiba hiyo na katika utaratibu unaohakikisha huduma bora kabisa kwa Wazanzibari.
Hilo litanusuru pia mambo mengine yanayohusiana na maendeleo ya kiuchumi, kama vile ardhi, ajira, misitu, bima, uvuvi na bahari, mwenendo wa biashara na suala zima la uhamiaji na ongezeko la idadi ya watu katika nchi ya Zanzibar.
Nimesema katika mwanzo wa nukta hii, kwamba tabia ya kisiasa na kiuchumi (politico-economic behavior) ya Tanzania Bara imejengeka juu ya msingi wa kibeberu, Chetu Chetu, Chao Chetu. Katika kanuni za hisabati, tabia hii hujua kujumlisha na kuzidisha tu na sio kutoa na kugawa. Kwa mfano, inafahamika kuwa Tanzania Bara imeanza kuchimba gesi na kuuza tangu mwaka 2003, na japokuwa hilo ni jambo la Muungano, hakuna wakati Serikali ya Zanzibar imewahi kushirikishwa kwa namna yoyote ile.
Vile vile, ardhi ya Tanganyika ina madini mengi na ya aina nyingi. Kwa kuwa madini hayo, kama ilivyo kwa mafuta na gesi hupatikana kutoka ardhini, mantiki ingelitusukuma kuona kwamba vyote kwa pamoja vingelikuwa vya Muungano. Lakini Mwalimu Nyerere alikumbuka kuweka gesi na mafuta tu; na akasahau kuyafuta, sio dhahabu, almasi, uranium, tanzanite, makaa ya mawe, rubi na chuma. Yote ni kwa kuwa chao ni chao, na chetu pia ni chao!
5. Mchango wa Kuuendesha Muungano: Upatu wa Kizungumkuti
Katiba ya Jamhuri ya Muungano haina sehemu yoyote inayotaja matumizi ya Tanzania Bara kama Tanzania Bara ndani ya Muungano au angalau matumizi kwa mambo yasiyo ya Muungano kuhusiana na Tanzania Bara. Badala yake, Katiba imeingiza vifungu 133 mpaka 144 ambavyo vinahusika na Mambo ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano na ambavyo vinaashiria kuwepo kwa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano tu.
Hiki ni kizungumkuti kilichomo kwenye Katiba yetu na ambacho kinaonesha sura halisi ya Muungano wetu. Kwamba Katiba inaelezea wazi kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar na pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo ina madaraka ya kushughulikia mambo yote ndani ya, na kwa Jamhuri ya Muungano na yote mengine ndani ya, na, kwa Tanzania Bara, lakini haiitengi Tanzania Bara katika matumizi na, hivyo, mchango wake kwa Muungano.
Tuchukulie mfano na ukweli huu: kuna mfuko mkuu kwa Jamhuri ya Muungano ambao unaingiza mapato yote au pesa zote kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Hapa tafsiri safi na isiyo na mashaka ni kwamba, mfuko huu unapaswa kutumiwa kwa mambo ya Muungano tu, kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba. Lakini, Tanzania Bara haina mfuko mkuu kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano yanayohusu Tanzania Bara tu, ingawa Zanzibar inao mfuko wake mkuu kwa mambo yasiyohusu Muungano, yanayohusu Zanzibar tu. Sasa kwa nini matumizi ya Tanzania Bara kwa mambo yasiyo ya Muungano yagharamiwe na mfuko mkuu wa Jamhuri ya Muungano?
Huu ndio ambao uchambuzi unauita ‘Upatu wa Kizungumkuti’, ambao kwa bahati mbaya sana unaonekana kutokufahamika au, yumkini, kupuuziwa na wasomi wa Tanzania Bara, ambao mara kadhaa huandika wakihoji kwamba Zanzibar haichangii kitu katika Muungano, bali ni Tanzania Bara (Muungano) ndiyo huchangia. Kwa mfano, Teddy Maliyamkono katika kitabu chake, The Political Plight of Zanzibar, anahoji kwamba baina ya mwaka 1983-84 na 1998-99, Tanzania Bara iliipa Zanzibar takirbani dola za kimarekani milioni 835, ambayo ni sawa na kusema “Bara inampa kila Mzanzibari zawadi ya dola 1,202 kwa mwaka, ambayo pia ni sawa na mapato ya Serikali ya Zanzibar kwa miaka sita.”
Anasema pia kwamba Zanzibar hailipii mchango wake kwa Muungano kama inavyofanya Tanzania Bara, na kwa hivyo, Zanzibar inafaidika sana na Muungano kwa kuwa inabebwa sana.
Sisi Wazanzibari tunaudhika kuambiwa tunabebwa, maana si kweli na ni kauli ya kutudhalilisha. Kwanza, bila ya shaka, Maliyamkono anazungumzia mzunguko wa fedha baina ya Zanzibar na Tanzania Bara kupitia njia mbali mbali, hasa za miradi, biashara kati ya serikali mbili na, pengine, mgawo wa kawaida wa Muungano, ambayo tunaambiwa Zanzibar hupewa asilimia 4.5 ya misaada kutoka nje inayoingia kwenye Muungano. Ikiwa hivyo ndivyo, basi hiyo si ‘takrima’ kwa Zanzibar, bali ni haki, kwa upande mmoja, na ni matokeo ya kibiashara, kwa upande mwengine.
Pili, anayoizungumzia kuwa ni serikali ya Tanzania Bara, ambayo inatoa pesa kupeleka Zanzibar – hata kama ingelikuwa ni kweli Serikali hiyo inatoa – basi anazungumzia serikali hewa isiyokuwepo. Iliyopo hasa ni Serikali ya Muungano, ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na kwa hivyo inapofanya jambo kwa Zanzibar ni kama vile inavyofanya hivyo kwa Tanzania Bara.
Lakini, tatu, kwa kuwa kama nilivyotaja hapo juu, hakuna mgawanyiko wa kimamlaka katika Katiba baina ya Serikali ya Tanzania Bara na ile ya Muungano, ukweli ni kuwa Tanzania Bara haichangii chochote kwenye Muungano, maana haipo. Kwanza pangelikuwa pana serikali ya Tanzania Bara, halafu ndio tukazungumzia serikali hiyo kutekeleza majukumu yake, likiwemo hilo la kuuchangia Muungano. Hichi ndicho kizungumkuti chenyewe.
Tupige mfano mwengine wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha. Kifungu cha 133 cha Katiba ya Tanzania kinazungumzia Akaunti ya Fedha ya Pamoja (Joint Finance Account) ya Jamhuri ya Muungano, ambapo zitatiwa fedha kutoka michango ya serikali mbili kwa viwango vitavyowekwa na Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Finance Commssion). Kwa hiyo, kikatiba ni Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zenye wajibu wa kuchangia huduma na uendelezaji wa Muungano na sio Tanzania Bara, maana Katiba haiitambui kuwa na taasisi zake yenyewe.
Ni hapa ndipo sasa unapoona kwamba kumbe kulitakiwa kuwepo na Serikali ya Tatu ya Tanzania Bara, maana ilivyopaswa hasa iwe ni hivi: suala la mapato lihusishe Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika. Hapo pasingekuwa na hoja wala haja ya Tume ya Pamoja ya Fedha, ambayo, hata hivyo, mfumo wa kuteuliwa kwake unalalamikiwa.
6. Matokeo: Ng’ombe Wetu Kundini mwa Msegeju
Mimi si mmoja ya wale wanaoamini kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na dhamira njema walizokuwanazo wale tunaowaona kuwa waasisi wake, Sheikh Abeid Karume wa Zanzibar na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika. Sikubali kwamba msukumo wa kuungana kwa nchi hizi ulikuwa ni hisia za umoja na udugu wa Afrika (pan-africanism). Na, kwa hakika, nakerwa sana na hoja kwamba Zanzibar iliuhitaji Muungano huu kwa sababu ya ulinzi na kujiimarisha kiuchumi. Yote hayo yalitumiliwa tu, lakini hazikuwa sababu hasa za kuutosa utaifa wa mataifa mawili haya.
Masuala haya yanayohusu ‘Siasa za Muungano katika uchumi wa Zanzibar’ yanadhihirisha kuwa malengo ya kuunganishwa Tanganyika na Zanzibar yalikuwa zaidi, au hata nje kabisa, ya udugu wa Afrika. Mifano na matukio kadhaa wa kadha, ambayo kutokana na uchache wa muda sikuweza kuyataja hapa, yanaonesha kuwa baina ya Karume na Nyerere palikuwa na dhamira tafauti za kuingia kwenye Muungano.
Mwandishi Sheila Rule katika makala yake, Easygoing Isle, an Uneasy Match with Mainland, katika gazeti la New York Times la Aprili 22, 1987, anaandika:
The sheik (Abeid Karume) was afraid that the deposed Arab Sultan, who had escaped to Britain, might mobilize an army overseas and retake Zanzibar, according to longtime residents. He quickly sought protection from outside attack from Mr. Nyerere, then President of Tanganyika. Mr. Nyerere, himself concerned that Zanzibar might become a Communist base in East Africa, offered Sheik Karume, who was later assassinated, a union instead of an army.
Tafsiri isiyo rasmi ya kauli hii ni kuwa: Kwa mujibu wa wakaazi wa muda mrefu (wa Zanzibar), Sheikh Abeid Karume alikuwa akikhofia kwamba Sultan wa Kiarabu, aliyekuwa amekimbilia Uingereza, angeliitisha jeshi huko nje na kuja kuichukua tena Zanzibar. Hivyo, haraka akatafuta ulinzi dhidi ya mashambulizi kutoka nje kutoka kwa Bwana Nyerere, aliyekuwa Rais wa Tanganyika. Nyerere, mwenyewe akiwa na khofu kwamba Zanzibar ingeweza kuwa kituo cha Ukomunisti katika Afrika Mashariki, akampa Karume Muungano badala ya jeshi (la kumlinda).
Akiandikia mtandao wa Socialist Website, tarehe 15 Novemba 2000, Ann Talbot, anasema katika makala yake Nyerere’s Legacy of Poverty and Repression in Zanzibar:
Nyerere was looking at Lumumba’s fate when he initiated the union with Zanzibar. He knew that he would not survive if he allowed the movement in Zanzibar to continue and could demonstrate his usefulness to imperialism by bringing Zanzibar into a union with Tanganyika.
Tafsiri yake isiyo rasmi ni kwamba: Nyerere alikuwa anakabiliwa na khatima kama ya Patrice Lumumba wa Kongo Kinshasa (ambaye alikuwa ameuawa na mawakala wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa kushindwa kwake kudhibiti siasa za Kikomunisti zisienee ndani ya eneo la Afrika ya Kati na kujiegemeza mno na Urusi), wakati alipoanzisha Muungano na Zanzibar. Alijuwa kwamba asingelibakia hai kama angeliruhusu harakati kama hizo kuendelea Zanzibar na kwamba angeliweza kuonesha ni mtu wa manufaa kwa mabeberu kwa kuiingiza Zanzibar kwenye Muungano na Tanganyika.
Hata hivyo, katika utenzi wake, Tamko la Mzanzibari, mwandishi wa uchambuzi huu anauchukulia Muungano na Mapinduzi kuwa ni kitu kimoja kama vile ambavyo Prof. Shivji (2008) anavyouunganisha mgogoro wa Zanzibar na kero za Muungano. Hoja ni kwamba, palipinduliwa ili paunganwe, na hivyo, hata kama ilitokezea kwamba wakati wa kuunganishwa nchi hizi, sababu za Ukomunisti wa kina Abdirahman Babu zilikuwepo, hiyo ilikuwa ni sadfa tu na ikatumiliwa vilivyo.
Kwangu mimi, tangu mwanzo, wote wawili, Karume na Nyerere, kila mmoja kwa upande wake, alijuwa anachokifanya. Kwa Karume, Muungano huu ulikuwa kama ngome tu ya kulindia madaraka yake dhidi ya wale aliowaona kuwa maadui zake. Kwa hali hiyo, kila siku alijijuwa yuko katika Muungano ambao aliuhitaji kwa lengo hilo moja tu, huku akiendelea kujiaminisha kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka yote na ya mwisho kuhusu Zanzibar. Zaidi ya hapo, hakuwa na habari na Muungano (Shivji, 2008). Wazanzibari wengi leo wanaamini kuwa kama angelikuwa hai, basi Muungano huu leo hii usingefikia miaka 45, maana kwake yeye ungelikuwa umeshatimiza matarajio yake ya kumlinda.
Lakini Nyerere naye alikuwa na dhamira yake ya kuivuta Zanzibar kwenye Muungano. Tangu mwanzo kabisa, alikuwa anajuwa anachokifanya katika suala hili la kizungumkuti. Alijuwa, kwa mfano, kwamba kwa kulififilisha tu jina la Tanganyika, hakuwa anaiuwa nchi hiyo wala kuzivunja nguvu zake, bali alikuwa anatanua himaya kwa kuipa nchi yake jina na mipaka mipya. Alichokuwa akikitafuta ni kile kielezwacho kwenye nyimbo moja ya kikwetu:
Msegeju yuna ng’ombe
Ng’ombeze
Nami n’na ng’ombe yangu
Anambia tuchanganye
Sitaki
Kwaheri nakwenda zangu
Hadithi ya nyimbo hii ni kwamba, kulikuwa na wachugaji wawili wa ng’ombe: mmoja (mwimbaji) alikuwa na ng’ombe mmoja tu na mwengine (Msegeju) alikuwa na kundi kubwa la ng’ombe. Lakini pamoja na kuwa na kundi hilo kubwa, bado Msegeju alimtaka (kwa kumlazimisha) mwimbaji wachanganye ng’ombe wao. Mwenzake ndipo akaimba kwa malalamiko kwamba anatenzwa nguvu kumchanganya ng’ombe wake mmoja kwenye kundi lile kubwa, naye jambo hilo hakulitaka. Akihofia kuja kumpoteza ng’ombe wake mmoja kwenye kundi kubwa la mwenzake, akaamua kuaga: “kwaheri nakwenda zangu!”
Msegeju ni Nyerere na Karume ndiye mwimbaji mwenye ng’ombe mmoja. Lakini bahati mbaya ni kwamba Karume alipotakiwa na Nyerere kumchanganya ng’ombe wake kwenye kundi, alikubali kwa matarajio ya kulindiwa ng’ombe huyo. Bahati mbaya zaidi, kama alivyokhofia mwimbaji, Karume naye akafa hajaweza kumuengua ng’ombe huyo kutoka kundi lile wala kufaidika naye, ingawa kila mara alilalamika. Wakati Karume alipoaga kwenda zake, yule ng’ombe alimuacha mule mule kundini, lakini lile kundi akaliwacha mikononi mwa Nyerere. Sasa ng’ombe wa Karume yumo kwenye kundi la ng’ombe wa Nyerere na, kwa hivyo, ni wa Nyerere. Watoto wa Karume wanalilia urathi wa baba yao, lakini u wapi? Watoto wa Nyerere wanasema wale ng’ombe wote wamerithi kutoka kwa baba yao!
Mzee wangu, Arham Ali Nabwa, alikuwa akikuita huku ndiko ‘kufa dungu msooni.’ Msemo maarufu kwenye mchezo wa kitoto wa gololi, ambapo aliyekufa dungu msooni hulazimika kutoka mchezoni akiwa amepoteza kila kitu na huku kutakiwa zote ‘alizokula’ mwanzo azitowe. Akaondoka pangu pakavu, keshabunwa, kwa lugha ya kitoto.
Kwa miaka yote hii 45 ya Muungano, habari imekuwa ndiyo hiyo. Kwa jina la Tanzania, Tanganyika imeendelea kujizolea kila kilicho cha Zanzibar kukipeleka kwenye Muungano kwa kisingizio cha kuuimarisha; na Zanzibar inazidi kufa kwa kuwa inaingiza kila chake kwenye tumbo la Mfalme Jeta lisiloshiba! Na baya zaidi ni kuwa Tanganyika inaambiwa haipo, basi Zanzibar imekosa mshirika wa kuongelea naye matatizo ya Muungano, maana anayeiwakilisha Tanganyika ni huo huo Muungano!
Lakini kimsingi, wakati Muungano unasainiwa, haikuwa dhamira (angalau ya Karume) kupoteza kila kitu. Kwa hakika, mnasaba wa Mkataba wa Muungano unaonesha kwamba palikusudiwa kuwepo kwa mamlaka tatu: ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano. Hivyo ndivyo muundo ulivyokusudiwa uwe. Kwamba hautekelezwi hivyo, hilo ni suala jengine.
Na kwa nini muundo huu hautekelezwi? Ni kwa sababu tangu mwanzoni kabisa palikuwa na dhamira mbaya ya kisiasa kwa upande wa Tanganyika, ambayo ilikusudia hasa kuikalia Zanzibar kwa gharama yoyote iliyostahili. Kwa hivyo, kama nilivyotangulia kusema, Muungano huu tulionao haukuchimbukia kwenye nia njema kama tunavyoambiwa.
Lakini kwa nini palikuwa na dhamira mbaya?
Kuna sababu zaidi ya moja, hapa nitazitaja tatu. Kwanza, dhamira ya Muungano huu ilikuwa ni kuitumilia Zanzibar kiuchumi. Hadi tunapata uhuru wa Disemba 1963 na kufanya Mapinduzi ya 1964, Zanzibar ilikuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa zimeendelea sana kwa viwango vya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tanganyika waliopata uhuru miaka 3 kabla yetu, walikuwa katika hali ngumu kiuchumi. Kwa nafasi yake ya kijiografia, Zanzibar ni mlango wa kuingilia na kutokea katika soko kubwa la Afrika ya Mashariki. Kwa nafasi yake ya kihistoria, Zanzibar ni kituo cha usambazaji. Nyerere alikihitaji kituo hiki kuiendeleza Tanganyika yake. Ni bahati mbaya sana kwamba hakuwa na ujanja wa kutosha kuweza kutumia fursa hiyo ya kiuchumi iliyonayo Zanzibar kwa miaka 20 ya utawala wake badala yake akazifanya zote mbili, Tanganyika na Zanzibar, kuwa masikini zaidi kuliko alivyozikuta. Ujamaa wake ulikuwa ni wa kuugawa umasikini kwa watu wake na na sio wa kuwaondoshea umasikini huo (Talbot, 2000).
Pili ni kuitumilia Zanzibar kujijenga kisiasa. Tanganyika ilihitaji kujitanua na Nyerere alihitaji sifa ya kuonekana mwanasiasa wa Kiafrika anayethubutu. Kuitwaa Zanzibar ilikuwa andasa yake hata kabla ya Uhuru wa Tanganyika wa 1961. Mara nyingi alikuwa amesema kwamba hakuwa tayari kuwa na jirani wa Kiarabu na Kiislam mlangoni pake. Aliumwa na hilo na kuichukua Zanzibar hata halikuwa suala la kufikiria mara mbili. Zile hadithi alizokuwa akizitoa Nyerere kwamba ni Karume ndiye aliyeshauri waungane, na kisha kumuambia kuwa yeye Nyerere awe Rais na yeye Karume awe makamu, zina shaka sana. Karume alivyokuwa akiupenda ukubwa, haingii akilini kwamba aliutoa sadaka uraisi wake kiasi hicho.
Sababu ya tatu iliyo nyuma ya Muungano huu ni ya kidini, ambayo ilichochewa sana na Uingereza, ambayo inalaumiwa kuyawezesha Mapinduzi ya 1964; lakini ikawa na tahadhari kuelekea Muungano ikikhofia kwamba athari ya Uislamu iliyoko Zanzibar ingelikuwa imepata jukwaa lake Tanganyika kama ingelikuwa nchi moja. Lakini katika mtindo wa kutumiliana, Nyerere akashinda ushawishi wake kwa kuonesha kwamba sio tu kuwa Zanzibar kuna hatari ya Uislam, lakini pia kuna hatari ya Ukomunisti, ambao kuudhibiti kulihitaji kuiingiza katika makucha yake. Akasaidiwa katika hilo na likawa kama lilivyokuwa na leo ndio huu Muungano tulionao (Ghassany, 2008).
Sababu hii inaogopwa sana kutajwa kwa kuwa siasa za leo za kilimwengu zimefanikisha kuubatiza Uislam jina la ugaidi. Wengi wa wanaojiita wasomi, au watu walioendelea, hawataki kujihusisha na Uislam wala kuuhusisha Uislam na Uzanzibari. Mimi si mmoja wao. Nisiwe msomi wala mtu niliyeendelea, lakini nitasema kwamba chuki za Nyerere dhidi ya Zanzibar zilichangiwa pia na imani yake ya kidini. Nyerere hakuupenda Uislam na aliwachukia Waislam. Hilo linathibitishwa na historia ya kwao, Tanganyika, inayoonesha hivyo. Soma kitabu cha Mohammed Said, Maisha ya Abdulwahid Sykes, cha Padri Joachim Sullivan, Kanisa Katoliki na Siasa za Tanzania, cha Dk. Hamza Njozi, The State and Islam in Tanzania na, au, makala ya Ousamne deSonghai, Islam: The Influence of Zanzibar Empire, ikiwa unataka ushahidi madhubuti.
Waingereza pia, tangu mwanzoni mwa karne ya 14 wamekuwa na vita maalum dhidi ya Uislam na Waislam. Unashauriwa kusoma kitabu In the Balance: Themes in Global History cha Walton na wenzake au kile cha Asaf Hussein, Western Conflict with Islam, kujifunza namna ambavyo Dola za Magharibi zimekuwa zikuangalia Uislam na hivyo Zanzibar, kama kitovu cha Uislam kwa ukanda huu wa Afrika, ilivyochukuliwa kwa kuhusishwa na hisia za Dola ya Uthmaniyya; na kwa hivyo ikawa lazima kidhibitiwe kwa namna yoyote ile.
Japokuwa Waingereza hawakufikia upeo mkubwa zaidi wa kuitosa Zanzibar, lakini angalau walifanikiwa kuichora vibaya historia ya Visiwa hivi kwa kutumia ukabila, na kisha wakazunguka kwa mlango wa nyuma kusaidia kufanikishwa kwa Mapinduzi ya 1964 na hatimaye ndio Muungano ukaja.
8. Neno la Mwisho: Mapinduzi Daima na, au, Zanzibar Daima?
Nimetangulia mwanzo kusema kwamba uchambuzi huu unaongozwa na hoja ya kuwa Wazanzibari na Watanganyika wana malezi tafauti kuhusiana na sura ya Muungano. Ambapo Watanganyika wanauangalia huu kuwa ni Muungano wa Serikali Moja, Wazanzibari wanauangalia kuwa ni wa shirikisho la Serikali Tatu. Hata hivyo, si serikali moja wala tatu zilizoandikwa popote katika sheria kuu zinazoongoza sehemu hizi mbili, isipokuwa tabia, matendo na maono ya watu yanasomeka hivyo. Ndiyo maana, si rahisi kwa Mtanganyika kumkuta anajiita kwa jina hilo, maana kwa wengi wao Tanganyika imeshapotea, lakini kila mara utamkuta Mzanzibari akijiita na akijinasibisha kwa Uzanzibari wake.
Huu ni uamuzi wa kimapinduzi kwa pande zote mbili za Muungano. Kwa Tanganyika ni wa kimapinduzi kwa kuwa umeweza kupindua fikra za karibuni vichwa milioni 37 na kuvifanya viamini kitu kimoja. Kwa Zanzibar ni wa kimapinduzi kwa kuwa vichwa milioni moja tu, ambavyo vinafanya chini ya asilimia 3 tu ya Watanzania wote na vinakaa chini ya asilimia moja tu ya ardhi yote ya Tanzania, vimeweza kuhimili kubakia na hisia za kutokuridhika kwa miaka 45 ya Muungano huu. Lazima tukiri kwamba ni ujasiri tu ndio unaomuwezesha mwanaadamu kuweza kukaa na fundo la moyo kwa miaka mingi kama hii.
Kubwa zaidi kwetu ni kukiri kwamba kuna kutokuridhika huko kwa upande wa Zanzibar, ndipo tuweze kusaidiana kuyageuza mateso yetu kuwa faraja. Kukubali huko kutayaendeleza Mapinduzi ya kweli ya Zanzibar kwa kuyapa maana katika maisha ya kila siku na ya kila mmoja wetu. Kwamba Mapinduzi hasa ni matokeo ya kutokuridhika, ambako huletwa na mgogoro kati ya njia ambazo watu wanaouona ukweli na njia ambazo wangelipenda ukweli huo uwe (Khan & McNiven, 1990). Zanzibar inauona ukweli kuwa Muungano huu, katika hali uliyo, ni tatizo kwake na, sasa, ingelitaka kuuona kuwa ni sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo. Huko hakuwezekani ila kwa Mapinduzi; na hayo si mapinduzi ya mapanga na marungu, wala bunduki na mizinga, bali ya fikra na mkakati, ambayo yanatakiwa yapitie hatua tano zifuatazo:
i. Hatua ya matayarisho kwa ajili ya mapinduzi
ii. Hatua ya kuporomoka kwa mfumo mkongwe
iii. Hatua ya kuharibika kwa mahusiano makongwe
iv. Hatua ya kujenga mahusiano mapya
v. Hatua ya kuuimarisha mfumo mpya
Ama kwa kujijua au kutojijua, tayari tumeshapita kipindi cha kwanza cha matayarisho kwa ajili ya mapinduzi, ambacho kilitawaliwa na woga wa wananchi na mateso ya watawala. Kilikuwa ni kipindi ambacho, ingawa palikuwa na kiwango kikubwa cha kutokuridhika na jinsi Muungano huu unavyoikandamiza Zanzibar, si Wazanzibari wengi waliokuwa na uthubutu wa kukusema kutokuridhika huko. Bali hata wale wachache waliothubutu, walisemea vibuyuni ambako ama walichokisema kilimalizwa huko huko au wenyewe walimalizwa kwa njia zao za kumalizana.
Sasa tulipo, kwa maoni yangu, ni katika hatua ya pili ya mapinduzi, ambapo mfumo mkongwe wa Muungano usio na maslahi kwa Zanzibar unaelekea kuporomoka. Kawaida kipindi hichi ni matokeo ya kupotea kwa uongozi (leadership vacuum) ndani ya kundi la watawala, ambapo mgawanyiko wa makundi humfanya kila mmoja kutenda vyake. Mara nyingi hatua hii haifikiwi mpaka ajitokeze kiongozi anayejiona kuwa mwanamageuzi kutaka kuunusuru mfumo mkongwe; na akafeli. Turgot na Necker walijaribu kuunusuru ufalme wa Ufaransa kabla ya mwaka 1798 na Stolpyin akafanya jaribio kama hilo nchini Urusi kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini wote walishindwa (Khan & McNiven, 1990).
Huwa ni wakati ambapo, kutokana na mtikisiko wake, mfumo mkongwe huwa kama tayari umeshakufa kitambo, lakini kwa kuwa watu wanaothubutu kuyathibitisha mauti yake hawajatokea, basi huendelea kuwepo tu ukiendea upepo na kudura ya Mungu. Nabii Suleiman (A.S) alifariki siku nyingi, lakini watumishi wake wakaendelea kutumika wakidhani bosi wao amekaa kitini akiwasimamia, hadi mchwa alipokuja kuila fimbo yake. Kuna watu waliojuwa kuwa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Ufaransa imeshakufa tangu mwaka 1934, lakini maziko yake yalikuja kufanywa mwaka 1940.
Wazo ninalojaribu kuliwasilisha kwenu hapa ni kwamba, kuna siku yale yale matakwa ya Wazanzibari, kama yalivyoelezwa kupitia Ripoti za Tume za Jaji Nyalali na Jaji Kisanga, ndiyo yatakayoiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala sio Katiba hizi zilizopo sasa; na viashiria vya utabiri huo vimeanza kujengeka sasa.
Changamoto iliyo mbele yetu kwa sasa ni ukweli kwamba hatua za tatu, nne na tano zinakuja kwa kasi na, yumkini, hatuna matayarisho mazuri kuzikabili. Kwa mfano, hatua ya tatu, ambayo ni ya kuharibika kwa mahusiano makongwe, kwa mintarafu ya kuharibika kwa muundo wa sasa wa Muungano, ina matatizo yake. Mojawapo ni kwamba, wenye maslahi na mahusiano haya hivi sasa, watajitahidi kutumia nguvu zao za ziada kuzuia yasiharibike. Na ingawa, kutokana na matakwa ya kiwakati hawataweza kufanya hivyo, lakini kama ilivyo kawaida ya mti mkubwa unapoanguka, husababisha maafa kwa pale unapong’okea (panaweza kuchimbika shimo kubwa) na kule unakoangukia (unaweza kuelemea nyumba au wapita njia na kuwajeruhi kama si kuwatoa roho zao).
Wakati huu ambapo mahusiano makongwe baina ya Syria na Lebanon yanaharibika, kwa mfano, ni Lebanon ndiyo inayoonekana kulipia gharama za kipindi hiki kwa wale wanaharakati wake walio mstari wa mbele katika kusaidia maharibiko hayo, kukabiliwa na vitendo vya kigaidi vinavyoaminika kusimamiwa na kuongozwa na Syria ndani ya ardhi ya Lebanon.
Lakini mara tu kipindi hiki kinapoanza, hutanguliwa haraka sana na kipindi cha ujenzi wa mahusiano mapya. Huu ni mfano wa ujenzi wa nyumba mpya juu ya kongwe, ambapo mwenye nyumba huendelea kujenga nyumba mpya, huku yeye akiwemo ndani. Huvunja kiambaza kimoja kwanza na kusimamisha kipya mahala pa kilichovunjwa, kabla hajakwenda katika kiambaza chengine. Ingawa huweza kuchukua muda mrefu kwa nyumba kukamilika, kutegemea na uwezo wa kifedha, kiufundi na mazingira ya ujenzi; lakini ni staili ya ujenzi ambayo ina faida moja kubwa: hakuna wakati ambapo mwenye nyumba analazimika kulala nje, hata kama katika kipindi cha ujenzi huwa hakai katika makaazi mazuri sana.
Hapo ndipo, kwa maoni yangu, nchi hii inapoelekea. Muungano huu utaingia kwenye kuvunjika na kuundika kwa wakati mmoja, yaani tunakwenda katika kipindi ambacho hatutasema kuwa hatuna Muungano moja kwa moja, lakini pia hatutakuwa na Muungano huu.
Mwisho tutaingia kwenye kuimarisha mahusiano mapya tutakayoyajenga; maana ukweli ni kwamba Zanzibar na Tanganyika, bali pamoja na mataifa mengine ya karibuni, yataendelea kuwa katika mahusiano dumu daima. Lakini tafauti na sasa, mahusiano yajayo kwa sababu ya mapinduzi haya, yatakuwa na sura nyengine na matakwa mengine.
Hata hivyo, tuzinduke Wazanzibari, kwamba jambo pekee linaloweza kutufikisha hapo ni moja tu, nalo ni mkono mmoja kuyashikilia Mapinduzi yetu na mwengine kuishikilia Zanzibar yetu. Yaani isiwe tu Mapinduzi Daima, lakini iwe pia Zanzibar Daima; maana Mapinduzi Daima hayana maana ikiwa hatuna Zanzibar!
MAREJEO:
- Nabwa, A. (2002), Tanganyika Yatumiliwa Kukandamiza Zanzibar, makala katika gazeti la Dira Zanzibar la Juni 12, 2002, Zanzibar International Media Company
- Barua ya Edwin Mtei kwa Katibu wa EACB ya tarehe 29 Disemba, 1965, Kumb. Na. TYC.46/01/582
- Barua ya Amir Jamal kwa Mwenyekiti wa Bodi ya EACB ya tarehe 22 Machi, 1966, Kumb. Na. TYC.46/01
- Duni, J. H. (2008), Baada ya Miaka 50 ya Muungano Wazanzibari Wana Lipi la Kujivunia?, makala katika Kongamano la Wazanzibari, London
- Ghassany, M. (2003), Kazi Yao Kukanusha tu, makala katika gazeti la Dira Zanzibar, Toleo Na. 11, Februari 14-20, 2003, Zanzibar International Media Company
- Taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Juu ya Mapendekezo ya Uendeshaji wa Kazi za Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar Ilivyowasilishwa na Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi ya Zanzibar katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, tarehe 2 Aprili 2009
- Hansard ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, tarehe 18 Septemba 2008
- Uganda Community Support (2000), Zanzibar: A Drain on Union Economy, from http://www.ugandaruralcommunitysupport.org/2000/06/07/zanzibar-a-drain-on-union-economy-7-june-2000/ on 20th April, 2009
- Rule, S. (1987), Zanzibar Journal: Easygoing Isle, An Uneasy Match with Mainland, makala katika gazeti la New York Times la Aprili 22, 1987
- Talbot, A. (2000), Nyerere’s Legacy of Poverty and Repression in Zanzibar, makala katika mtandao wa Socialist Website, kama ilivyochukuliwa kutoka http://www.wsws.org/articles/2000/nov2000/zanz-n15.shtml tarehe 19 Aprili, 2009
- Ghassany, M. (2008), Tamko la Mzanzibari, Mswaada wa Utenzi ambao haujapishwa
- Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984
- Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977
- Shivji, I. (2008), Pan Africanism or Pragmatism: Lessons from Tanganyika-Zanzibar Union,
- Walton, L. A. & Wenzake (2002), In the Balance: Themes in Global History, McGraw Hill, New York, U.S.A
- Barua kutoka kwa H. R. Hirst kwenda Ubalozi wa Uingereza ya tarehe 21 Machi, 1964, Kumb. Na. INV/EA/F/196
- McNiven, M. & Khan, R. (1990), An Introduction to Political Science, Nelson Canada
*Mada ya Mohammed Ghassani katika Kongamano la Kuadhimisha Miaka 45 ya Muungano wa Tanzania lililoandaliwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu katika ukumbi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar, tarehe 26 Aprili 2009.