Korona ipo. Usiwasikilize wanaoamini ushirikina na wapuuze hawa wanaoshindwa kutimiza wajibu wao kwa wenye dhamana nao. Jilinde wewe mwenyewe na walinde watu wetu. Wagonjwa wetu wa Kisukari, Shinikizo la Moyo, Moyo, Pumu, wenzetu wenye unene sana na wazee wetu wapo kwenye hatari kubwa zaidi. Wenyewe wajichunge na sisi tuwalinde sana wasije kupata korona. Wakipata maambukizo haya huwa wanaathirika sana. Wote wanaokwenda kumwona mgonjwa wavae barakoa na ni vizuri wakae nje wasiingie ndani! Kuna watu wana corona lakini hawaonyeshi dalili na huwezi kuwajuwa lakini wanaambukiza wengine. Miezi miwili iliyopita, mimi na familia yangu tulipata, japokuwa tulikuwa tunachukuwa kila jitihada. Lakini kwa kuwa tunaishi kwenye nchi inayojali afya za watu, tulihudumiwa kwa mapenzi na hisani kubwa hadi tukapona sote tukiwa nyumbani mwetu. Na hata baada ya kupona, bado tukawa tunapigiwa simu na Wizara kufuatiliwa hali zetu pamoja na kuletewa barakowa za gharama kubwa bure. Allah awape shifaa wagonjwa wetu na atulinde sote, lakini sharti kwanza tujilinde wenyewe.