Makala hii inazungumzia kadhia ya Zanzibar kuondolewa kwenye uwanachama wake iliokaa nao siku 128 katika Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa kugusia mule makala iliyotangulia ilimopitia, yaani “Siasa za Muungano kuelekea Zanzibar”, lakini kwa hoja kuwa siasa hizo za Muungano zinafanikishwa na uadui mkubwa uliomo ndani ya Zanzibar yenyewe.
Nitapiga mfano wa namna ambavyo siasa hizi zinaposhindwa kufanya kazi muda wowote ambao uadui huo ndani ya Zanzibar umedhibitiwa, na Zanzibar ikasimama kama moja kwenye mambo fulani makhsusi.
Kwa sababu ya suala lenyewe la michezo na kwa sababu ya historia yangu kwenye sekta ya utalii na vile vile kwamba kwa muda mrefu, Zanzibar imekuwa ikiunganisha mambo haya pamoja – yaani utalii, utamaduni na michezo, mfano wangu utaanguukia hapo.
Baina ya mwaka 2001 na 2010, nilikuwa mwajiriwa wa kampuni moja ya utalii visiwani Zanzibar, nilikoanzia kama mtembezaji wageni na kupanda ngazi hadi mwakilishi wa kampuni hiyo kwenye hoteli za mashariki mwa kisiwa cha Unguja.
Mwezi Machi 2008 ulikuwa muda mwengine wa kufanyika maonesho ya kimataifa ya utalii ya Berlin, Ujerumani, maarufu kama ITB. Kampuni za utalii visiwani Zanzibar kupitia chama chao (ZATO) na kwa kushirikiana kikamilifu na kamisheni ya utalii chini ya usimamizi wa wizara yenye dhamana ya utalii, wakaamuwa kushiriki kwa mara ya kwanza wakiiwakilisha Zanzibar kama Zanzibar.

Sababu moja kubwa kabisa ya makampuni hayo kutaka kwenda yenyewe kuitangaza nchi, ilikuwa ni ukweli kuwa kamwe Zanzibar haikuwahi kuuzwa kama Zanzibar na mamlaka ya utalii ya Tanzania Bara, ambayo hadi sasa inataka kujiaminisha kuwa ni mamlaka ya utalii ya Tanzania nzima.
Matokeo yake, Zanzibar ilikuwa inauzwa kwenye vifurushi vya safari za watalii barani Ulaya na Amerika kama sehemu tu ya mapumziko kwa wageni waliokwishatembelea mbuga za Tanzania Bara, na sio kama kituo kikuu cha utalii.
Kwa hakika, hata mamlaka za utalii za Kenya zilikuwa zikiiuza Zanzibar kwa mahadhi hayo hayo, kwa kuiunganisha na Mombasa. Hili lilimaanisha kuwa Zanzibar haikuwa ikipata fedha za kutosha, licha ya kuwa wageni walimiminika kwa wingi kwenye hoteli na fukwe zake.
Kwa kuyazingatia hayo, ndipo chini ya Amani Karume kama Rais wa Zanzibar na Samia Suluhu Hassan kama waziri wa utalii, biashara na uwekezaji, Zanzibar ikaamuwa kushiriki maonesho.
Kilichotokea kwenye maonesho yenyewe mwaka huo kilikuwa kituko cha mwaka, lakini ambacho inaonekana kilishatarajiwa na Wazanzibari. Maafisa usalama wa ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani ‘waliwavamia’ wasimamizi wa banda la maonesho la Zanzibar na kuwataka walivunje.
Hoja yao kubwa ni kwamba Zanzibar ni sehemu ya Tanzania na hivyo haikupaswa kujitangaza yenyewe kwenye maonesho hayo kama nchi. Kwamba kufanya hivyo kulikuwa ni kinyume na itifaki za kimataifa na hatari kwa Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa mmoja wa waliokuwepo kwenye banda hilo, maafisa hao wa usalama walifika mahala pa kukiita kitendo hicho cha Zanzibar kufunguwa banda lake kuwa ni sawa na ‘uhaini’.
Bahati mbaya kwa maafisa hao wa usalama kutoka ubalozini ni kwamba waliwakuta Wazanzibari wakiwa wamejitayarisha kwa lolote ambalo lingeliweza kutokezea, kwani banda halikuvunjwa hadi mwisho mwa maonesho yenyewe. Kikubwa ambacho wasimamizi wa banda hilo walikifanya, kilikuwa ni kuweka mabango ya Tanzania ndani ya banda lenyewe ili kufikia muafaka na maafisa usalama kuwa Zanzibar inabaki kuwa sehemu ya Tanzania, ingawa inaweza kujitangaza na kujiuza kama Zanzibar.
Lakini sinema hii haikuishia hapo. Mwaka 2010, wakati kampuni za utalii zinajitayarisha kwenda maonesho mengine ya ITB ya mwaka huu, mamlaka ya utalii ya Tanzania Bara ikatuma ujumbe wake visiwani Zanzibar kwenda kusaka suluhisho la hali iliyojitokeza hapo kabla.
Bado, ujumbe huo ulikuwa na kauli ile ile, kwamba Zanzibar haipaswi kujitangaza kama Zanzibar kwenye jukwaa hilo la kimataifa, kwamba kinachofanywa na Tanzania Bara kwenye maonesho kama hayo ni kwa ajili ya Tanzania nzima na kwamba, kwa hivyo, Zanzibar iwe sehemu tu inayowakilishwa na Tanzania Bara na siyo kujiwakilisha na kujitangaza yenyewe.
Nao pia, kama walivyokuwa wale maafisa wa usalama wa ubalozini mjini Berlin, walikuwa na kauli zinazofanana juu ya kampuni za utalii za Zanzibar “kuuhatarisha Muungano”. Baada ya kutoka kwenye Kamisheni ya Utalii, sasa ukawa wakati wa wajumbe hao kutoka Bara kukutana na wamiliki wa kampuni za utalii kwenye ukumbi wa hoteli ya Bwawani.
Inayumkinika kuwa, kutokana na tabia ya woga waliyonayo baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali ya Zanzibar pale wanapokutana uso kwa uso na wenzao kutoka taasisi kama hizo kutokea Bara, huenda wakuu wa Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar (siku hizo chini ya Katibu Mkuu Alhalil Mirza), hawakuwaambia wenzao wa Bara kwamba suala la Zanzibar kwenda ITB lilikuwa suala la serikali nzima ya Zanzibar na sio la ZATO tu.
Ndio maana, walipoanza maafisa kutoka Bara ilikuwa moja kwa moja kuwashambulia jamaa wa ZATO kwamba wanataka kuharibu nchi kwa kujipeleka kwao Ujerumani kama Zanzibar wakati Zanzibar ni sehemu ya Tanzania. Hili jamaa wa ZATO hawakuwacha lipite hivi hivi. Wakawaeleza kinagaubaga nini kilichopo na kipi kinapaswa kufanyika.
Kwamba, kwanza, utalii si jambo la Muungano, kwa hivyo Zanzibar haihitaji kuwakilishwa na Tanzania kwenye jambo ambalo si la Muungano; pili, hata kama lingelikuwa la Muungano, basi taasisi za Tanzania Bara sio taasisi za Jamhuri ya Muungano, kwa hivyo hazina haki ya kukiwakilisha cha Muungano, na tatu; hata banda ambalo Zanzibar hukodi kwenye ITB huwa linachangiwa kwa pamoja kati ya Kamisheni ya Utalii na ZATO, kwa hivyo hii ni hatua ya pande zote zinazohusika visiwani Zanzibar, na sio ya ZATO pekee.
Msimamo huu wa Bwawani 2010 ndio ambao umesalia hadi hivi leo, miaka minane baadaye. Zanzibar imeendelea kujiwakilisha kila mwaka kwenye maonesho hayo, na imekuwa ikijiuza yenyewe kwa njia zake.
Hadithi hii ya Zanzibar, ZATO na ITB ina mafunzo makubwa sana kwenye hii kadhia ya Zanzibar kuvuliwa uwanachama wa CAF. Inawezekana kuwa ni kweli kwamba, kwanza, CAF inatumia hoja ya kuwa nchi haiwezi kuwa mwanachama wake kama si mwanachama wa FIFA. Kwa hivyo, Zanzibar ilipaswa kwanza kuwa kwenye FIFA.
Pili, CAF na FIFA – kwa pamoja – zilimeelezwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja tu na ambayo chombo chake cha uwakilishi kwenye soka ni Shirikisho la Soka la Tanzania Bara (TFF), na kwa kuwa mashirikisho hayo ya kimataifa humtambua mwakilishi mmoja kwa kila nchi, basi TFF aliyejipeleka kama mwakilishi wa Tanzania nzima, ndiyo keshajaza nafasi hiyo.
Kwenye utalii, hoja za waliokuwa hawakutaka Zanzibar ijiwakilishe na kujiuza yenyewe kimataifa zilikuwa zinafanana na hizi. Lakini tafauti ni kuwa uongozi wa juu wa serikali ya Zanzibar na kampuni za utalii, kwa pamoja, ulisimama imara kujenga hoja ya kipi ni kipi, na hivyo ndivyo ikawa.
Kwenye hili la soka pia, hoja ni zile zile ambazo zinaweza kutumiwa na Zanzibar, kwanza kwa mamlaka za ndani ya Zanzibar na Tanzania, kisha kwa mashirikisho hayo ya soka ya kimataifa, ukiacha mbali hoja nyengine zinazohusiana na undumilakuwili wa FIFA na CAF yenyewe kwenye suala hili la uwanachama wa Zanzibar.
Ni kweli kuwa siasa za Muungano zinataka kuiona Zanzibar ikiwa dhaifu ili kuweka mizani ya umadhubuti wa Muungano huo, lakini ni siasa dhaifu za ndani ya Zanzibar zenyewe ndizo hasa zinazoziruhusu siasa hizo za Muungano kufanikiwa.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 7 Agosti 2017.