BLOG POSTS, KISWAHILI KINA WENYEWE

SIMULIZI ZA BI TIME: Hadithi za Ncha Saba

JAMII za Waswahili daima zimekuwa na mihimili inayoshikilia silka na tamaduni zake. Zimekuwa na taasisi imara za ujenzi na uendelezaji wa maisha, mitazamo, falsafa na imani zao. Kuanzia chini kabisa hadi juu kabisa, maisha ya watu wa Uswahilini huwa si matupu. Kila ombwe hujazwa kwa tanzu, bahari na mikondo ya sanaa na usanii, fasihi na ufasaha.

Hayo ndiyo maisha yaliyonikuza na kunifumbua macho tangu nikiwa kijijini kwetu, Mchangani, jimbo la Pandani, wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini kisiwani Pemba, katika taifa la Zanzibar. Naamini, hata kwenye pirika za maisha ya kuhama upande mmoja na kuhamia upande mwengine – kwanza kwenda Unguja na Dar es Salaam na kisha ndani kabisa ya Afrika ya Mashariki, ambako ingawa Kiswahili hakikuwa kwao lakini kilipokewa kwa fadhila za “mgeni awiya mwenyeji apone” – kumbukumbu hizi zimekuwa sehemu yangu. Zimekuwa hivyo hata baada ya kuhamia Ulaya nilipo sasa.

Kumbukumbu za maisha hayo hazikamiliki bila ya taswira ya Bi Time Bint Kombo Kiago, aliyekuwa msimulizi maarufu wa hadithi za paukwa- pakawa pale kijijini kwetu, Mchangani. Nakumbuka namna ambavyo tulikusanyika usiku tukiwa tumeuzunguka moto wa machanja na magubi, tukichoma kwaju mbichi, viazi vitamu na muhogo, huku Bibi huyu, aliyekuwa na ufasaha wa ajabu wa usimulizi, ulumbi na utambaji, akitusafirisha kutoka tulipo hadi kwenye  mawanda mapana ya dunia: mara akitupandisha milima, kisha akatushusha mabonde, mara akatuvuusha misitu na nyika, akatutupa katikati ya kiza kinene cha usiku na pori, akatusimamisha mbele ya mazimwi tukitetemeka kwa khofu, kisha akawaleta majini wazuri kutuokowa, na tena kutufikisha mbele ya wafalme makatili na wapole, wanyama wakali na wataratibu na kwa vibibi vikongwe vyenye maajabu.

Ninakumbuka kuwa miongoni mwa mbinu ambazo alikuwa akizitumia Bi Time ni kwamba kila hadithi aliyotusimulia aidha aliianza au aliimaliza kwa msemo ama methali. Wakati mwengine katikati ya hadithi pangelikuwa na nyimbo; naye angeiimba na sisi kuitikia na kucheza pamoja naye. Wakati mwengine angelisimama alipokuwa amekaa na kutembea uwanja mzima kutuonesha kwa vitendo kile anachotusimulia. Alimradi, ilikuwa ni sanaa ya hali ya juu ya usimulizi na maonesho kwa wakati mmoja. Katika utu uzima huu nilionao, kila nikimkumbuka huwa namuombea dua za rehema huko aliko.

Sasa ni takribani miaka 40 tangu kukaa kitako mbele ya shungu la moto kumsikiliza Bi Time akitamba kwenye simulizi zake za paukwa-pakawa. Bado kumbukumbu za sura yake na vitendo vyake zipo akilini mwangu, lakini lazima niseme kuwa sasa kumbukumbu hizo hunijia zikiwa na magazigazi – picha inayochanganyikachanganyika na maji na moshi na mvuke na hewa na kisha kupotea angani. Kisha zinaporejea, hujikuta kipande kimoja cha hapa kimejiambatanisha na kipande cha kule, zimwi wa huku kauliwa na shujaa wa pale, na au joka la pima saba limekatwa kwa kisu cha ukindu badala ya upanga wa dhahabu.

Ndio maana nimeonelea kabla sijapoteza kila kitu, nikaye kitako kuokota ncha moja moja kuziweka maandikoni. Nikiwaangalia watoto wangu ambao wanakulia mbali kabisa na nilikokulia mimi, na ambao sina njia ya kuwapa nilichopewa mimi utotoni, basi kumbukumbu hizi hutokonyeka na naona aibu kuziwacha kabla hazijapotea moja kwa moja. Na hiyo ndiyo moja ya sababu ya kuuita mkusanyiko huu “Simulizi za Bi Time: Hadithi za Ncha Saba.”

Sababu nyengine ya anwani hii ni kwamba katika jamii za Waswahili, tunaamini juu ya Nambari Saba. Vitu vingi vinapewa nambari hiyo, kama vile siku za fungate ya harusi na au matanga baada ya msiba. Hata hadithi zetu za paukwa-pakawa huwa tunasema zina mbeya saba za masilimulizi. Inawezekana kabisa kuwa hadithi moja hiyo hiyo, husimuliwa hivi Pemba, ikasimuliwa vile Bagamoyo, muhusika huyu Ngazija na ikawa na mwisho mwengine Lamu, ingawa ujumbe wake ukabakia kuwa ni ule ule mmoja. Kwa hivyo, kwa wenyeji wenzangu wa pwani ya Afrika Mashariki, wataona kwenye mkusanyiko huu kunaweza kuwapo masimulizi tafauti ya hadithi moja kutoka nyengine kama hiyo waliyokulia nayo kwao. Sababu ni kuwa hadithi zina ncha saba.

Hadithi hizi za paukwa-pakawa zina utamu wake kwenye usimulizi, maana hujumuisha kila kitu na kila mtu: fanani, muktadha na hadhira. Wakati wangu zilikuwa zinasimuliwa usiku tu. Tulikuwa hata na kitiba kuwa mtu anayesimulia hadithi hizi mchana, anaota mkia. Usiku ulikuwa una maana kubwa sana kwetu wasimuliaji. Lakini pia kwa msimuliaji, utamu wake ulikuwa pale anapoitikiwa: “Enhe!” kila baada ya sentensi mbili tatu. Kwa hivyo, panakuwa na ushiriki wa moja kwa moja baina ya fanani na hadhira. Na kwa hilo namshukuru sana swahiba na ndugu yangu, Khatib Mohammed, na watoto wangu, Said na Fatma kwa kuwa vyote – fanani na hadhira – wakati wa ukusanyaji wa hadithi hizi za ncha saba.

Unaweza kuagizia nakala ya Simulizi za Bi Time hapa: https://www.lulu.com/en/gb/shop/mohammed-ghassani/simulizi-za-bi-time/paperback/product-755dvk.html?page=1&pageSize=4

2 thoughts on “SIMULIZI ZA BI TIME: Hadithi za Ncha Saba”

  1. Asalam Aleikum. Habari za muda. Bashkiria kwa kunikumbuka na kunitumia jumbe kuhusu mambo tofauti na vitabu vipya . Je hiki kitabu chako nitakipata vipi? Shukran Mwalimu Rayya >

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.