Kwa lugha na utamaduni wangu, magharibi ina maana nyingi: ndiko jua linakotulia likaibadilisha leo kuwa jana na kuitayarisha kesho kuwa leo. Ndicho kielelezo pia cha kumalizika kwa maisha ya mwanaadamu ya hapa duniani, maana magharibi kawaida huja na giza, na giza ni alama ya mauti. Magharibi pia ni nadharia ya kisiasa kwenye medani za kilimwengu na lugha yangu imeipokea hivyo hivyo – kuwa ni mataifa ya Ulaya na Marekani yanayoambiwa yameendelea kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Naam, mimi ninaishi magharibi kwa maana zote hizo zitambuliwazo na lugha na utamaduni wangu. Ninaishi huku ambako kunaambiwa kuwa ni kielelezo cha maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia. Huku ambako kuna makato makubwa ya kodi kwenye pato nichumalo kiasi cha kwamba nashindwa kuweka akiba kwa ajili ya waniangaliao huko kwetu nitokako, lakini ambako pia nikiumwa nitatibiwa kwa kiwango cha juu ya tiba, ibaki ya Mungu tu, ambako wanangu watasoma kiwango cha juu cha elimu ya kidunia, ibaki akili na majaaliwa yao tu, ambako mimi na wao tutakamuliwa hadi tone la mwisho la damu na mfumo usiotambua uhuru wa kifedha, bali unaoheshimu sana uhuru wa kutumika.
Ndiko huku magharibi ambako kunawapa sasa watoto wangu ulimi mwengine zaidi ya ule ambao nyumbani kwetu kuliwapa. Lakini huku kukiwapa ulimi huo, kunaufuta kabisa sio tu ulimi wa awali bali pia fikra, mawazo, hisia, na maana ya kuwa wao. Kwamba licha ya yote itupayo, Magharibi hii inajitahidi kuniambia mimi ni wanangu kwamba sisi si wa hapa. Hapa si petu.
Ninaishi magharibi ambako ni kweli jua linatua na mchana unamalizika kuukaribisha usiku. Giza gizani. Ni gizani licha ya mataa yawakayo kila mahala na kila wakati. Yumkini ndio maana mwanafalsafa aaminiwaye sana hapa, Socrates, mara moja aliwahi kukutwa akitembea na taa mchana kweupe sokoni, na alipoulizwa kulikoni, akajibu: “Licha ya mwangaza wote huu, kuna wengi hapa sokoni wasioona!“ Na, naam, naishi huku kwenye wengi tusioona licha ya mwangaza, maana ni magharibi. Ni gizani.
Wengi wetu hatuoni kwamba faraja ya kiuchumi na kimaisha tuliyoikimbilia huku haipo. Na hata tunapoona, tunajipumbaza kwamba ni “bora kuwa paka wa Ulaya, kuliko binaadamu wa Afrika.“ Matokeo yake, kile tunachojuwa kukifanya kwa usahihi utukutapo kwenye mikusanyiko yetu, ni kauli za kukuzodoa kwetu tulikotokea – mifumo yetu ya maisha, tabia za wetu wetu, imani zetu za kidini, mjengeko wa familia zetu, na kadhaa wa kadhaa. Husemi kama kwamba mtu anayezodoa hivyo hakuzaliwa, akakuzwa, akafundwa kwenye pachiko za wazee na watu wake mwenyewe. Ghafla moja, imani yake ni kuwa kila kitu kuhusu Afrika ni kinyesi. Afanaalek!
Wengi wetu tunajipumbaza kwamba tumeukata na tumepata kwa kuwa tuko kwenye giza la mchana. Hatutaki kukiri hata katikati ya giza la usiku, ndani ya mablanketi yetu, kwamba tumeyachezea maisha yetu na wenetu pata-potea – kamari ambayo kwa kila kumi wanaoingia kwenye mchezo, ni mmoja tu anayewafuta wenziwe, naye akafutwa kwenye duru ijayo.
Nitakupa mfano. Wiki hii hapa magharibi habari kubwa ni ile ya mwanamitindo na mtangazaji wa vipindi vya televisheni nchini, Kimberly “Kim” Kardashian, kupiga picha ya kuonesha makalio yake wazi kwa kile alichosema anakusudia kuivunja tabia ya kutumwa picha za utupu za wasanii mitandaoni kuwadhalilisha. Eti anawakomesha watu wenye tabia hiyo ambayo imekuwa mashuhuri na hata kuigizwa hadi Afrika katika siku za karibuni. “Watajiju“ kwa Kiswahili cha kwetu. Mwenyewe anaiita hiyo ni sanaa.
Wala usidhani kuwa hii ni mara ya mwanzo kufanya hivyo. Wala usidhani kuwa Kim ni pekee. Wala usidhani kuwa “msanii“ huyu hatopata wafuasi na watu wa kumtetea. Tayari kampeni ya “Breaking the Internet“ imeivunja kweli intaneti, maana mamia ya wafuasi wameanza ama kupiga picha za makalio yao kuzituma mtandaoni, au kuichukua picha ya makalio ya Kim na kuisarifu kwa kila namna na kuisambaza. Miongoni mwetu ni sisi watu wa habari, tuambiwao ati ni waandishi wa habari wa Magharibi. Waandishi wa gizani. Umagharibi wa magharibi (soma ugiza wa gizani) unataka nione kwamba hiyo ni sahihi, walau niivumilie kama siwezi kuipigia chapuo.
Ndipo nikasema kwamba naishi huku magharibi, huku gizani ambako hayo ni mambo ya kawaida kwenye maisha. Ambako ndugu na jamaa zangu wanakisia kuwa nimeukata kuacha maisha ya dhiki na tabu ya nyumbani kwetu, Zanzibar, kuja “kula kuku kwa mrija“ kwenye ardhi ya wakoloni wetu wa zamani. Ambako nao, masikini, wanatamani lini itakuwa zamu yao ya kuja kufaidi kama nifaidivyo kijana wao. Masikini, mimi na wao!!
Ila watu wangu wana mawazo hayo kuhusu mimi na magharibi yangu niliko kwa kuwa – juu ya yote – siiwaambii ukweli kuhusu giza lililonitanda. Kwa mfano, siwaambii kwamba huku niliko sitakuja kuwa na hiyari (Mungu apishe mbali) pindi mwanangu akinijia na mchumba wa jinsia kama yake, akaniambia anataka kuona naye.
Siwaambii kuwa mimi na wanangu huku tuliko kila siku tu wageni, ambao tangu tukiamka asubuhi hadi tukilala usiku hutaka kuthibitisha ukubalifu wetu kwa mifumo na tabia za huku ili nasi tupate kukubaliwa nako, lakini ambako kamwe hatutakuwa wao wala nako hakutakuwa kwetu.
Siwaambii kuwa sina uhuru wala utulivu wa kiuchumi, maana haidhuru pato nipatalo ni mara kumi ya nililokuwa nikilichuma kihalali nyumbani kwetu, makato nikatwayo ni mara mia moja ya niliyokuwa nikikatwa kwetu.
Siiwaambii kuwa mimi, kijana wao, kama walivyo mamia ya wenzangu wengine, tumenasa kwenye mitego ya kimagharibi: pesa, kazi, maisha, madeni. Katika mitego hiyo, hamuna msamiati wa faraja, hamuna wa uhuru, hamuna wa starehe.
Je, nina hasira na Magharibi? Ndilo swali ambalo utaniuliza sasa. Jibu langu ni hapana. Sina hasira nako wala chuki nako. Sikuchukii huku jua lizamako, ambako nilikukimbilia mwenyewe kwa hiari yangu. Tafauti na miaka 200 nyuma, wakati wazee wetu wa Kiafrika walipolazimishwa kuingia kwenye mabedeli ya Kizungu kuvuuka Bahari ya Atlantiki kuelekea utumwani Amerika, mimi kirembwe chao nilipigania mwenyewe “kukwea pipa” nikaja kujitia utumwani kwa hiyari yangu.
Na, kwa hakika, angalau mimi ninaweza kuambiwa nina afadhali. Maelfu kwa maelfu ya vijana wenzangu kutoka Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara hivi sasa wanahatarisha maisha yao kuvuuka Bahari ya Kati kwa mitumbwi kuingia kisiwa cha Lampedusa katika safari yao ya kukimbia jaala wasioijua Ulaya. Maiti zao huwa chakula cha papa wa pwani ya Aden na upwa wa Mwana wa Mwisho.
Kama ni hasira na chuki basi ni dhidi yangu mwenyewe, na ambazo zaidi zinatokana na khofu zangu kwa mustakabali wangu na wa kizazi change mwenyewe. Katikati ya usiku, chini ya guo la baridi, huwaona wamekuwa na wametambua uchaguzi ambao mzazi wao niliufanya kwa ajili yao. Uchaguzi wa kuwalea na kuwakuza katika upande wa dunia, ambao sio tu unawageuza mbele-nyuma, lakini ambao kamwe hautawakubali hata baada ya kuwageuza huko, na matokeo yake pia hawatakubaliwa kule iliko asili ya wazazi wao. Uchaguzi wa kuwageuza wageni kwa kila maana ya neno hilo.
Sina chuki pia na nchi yangu ya uzawa, Zanzibar, iliyo upande wa mashariki mwa dunia – kule dunia lichomozako na siku ianzako na sio lituwako na siku imalizako. Kule nuru – alama ya maisha – iangazapo, na sio giza – alama ya mauti – litandako.
Siichukii Zanzibar, bali kwayo nina masikitiko na majuto. Baada ya kunisomesha kwa jasho, damu na usaha, sikuheshimu jitihada yake kwangu. Ni kweli kuwa nilisomea chini ya miembe, wakati mwingi nilikaa kwenye mabanda yasiyo sakafu wala dari, walimu wangu walikosa motisha kwa sababu mishahara dhaifu, mtaala wa elimu ulikuwa haupimwi mafanikio yake. Lakini baada ya yote hayo, iliweza kunizalisha mtoto wake miye, ambaye watu wa Ulaya waliona haja ya kuniita na kuniajiri kuwatumikia.
Mfumo wa aina ya kwetu, licha ya mapungufu yote uliyonayo, unatoa nguvu-kazi ambayo iko tayari kutumiwa huku Magharibi, nayo ikatumika laisalkiyasi, halafu bado mimi mtoto wake nimeihama eti kwa kisingizio cha kutafuta kilicho bora zaidi.
Hayo ndiyo majuto yangu kwa nchi yangu, Zanzibar. Kwamba ilinipa ilichoweza kunipa, nami nimeipoka nilichoweza kuipoka. Nimeipoka mtoto wake nikampeleka magharibi, gizani!
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 katika mtandao wa zanzibardaima.org.