Uchambuzi huu unakusudia kuonesha – kwa nadharia – uhusiano mkubwa uliopo baina ya ukosefu wa demokrasia na kushamiri kwa ufisadi. Hoja ni kwamba kadiri demokrasia inavyokosekana ndivyo ufisadi unavyojiimarisha na kisha nao ufisadi ukazuwia demokrasia kufanya kazi yake.
Kwenye uchambuzi huu, demokrasia na utawala wa sheria zinawekwa kwenye kapu moja kama vile ni kitu kimoja, kwa mintarafu ya kwamba kilipo kimoja, huwapo pia chengine na kila kimoja hukifanya chengine kiishi – bali pia kinapokosekana kimoja, chengine hakiwezi kudumu.
Kwenye uchambuzi huu pia, ufisadi haudogoshwi kwenye jambo moja tu la rushwa – ambayo ni utowaji na au upokeaji wa kitu (mara nyingi huwa fedha) kwa ajili ya mpokeaji kutowa na mtowaji kupatiwa huduma (ambayo kimsingi ingelikuwa haki kutolewa bila ya kitu hicho). Hapana, ufisadi ni zaidi ya rushwa!
Neno ‘rushwa‘ la Kiswahili halifasiri neno ‘corruption‘ la Kiingereza, bali fasiri halisi ya ‘corruption‘ ni ‘ufisadi’ – neno ambalo limelichukuliwa kutoka Kiarabu ‘fasada‘ linalomaanisha uovu unaoharibu na kuangamiza.
Kwa hivyo, kwa dhati yake, ufisadi hufanywa na wale wenye uwezo wa kuharibu na kuangamiza na ndiyo maana mahala pake hasa ni penye nguvu – penye madaraka. Ufisadi haufanywi na mnyonge.
Kwa sababu unahusisha nguvu na maamuzi, kwa hivyo, ufisadi ni dhana ya kisiasa, na hapa tunauzungumzia ‘ufisadi wa kisiasa‘ – ambao ni utumiaji mbaya wa madaraka unaofanywa na maafisa wa serikali, taasisi za kisiasa au za umma kwa maslahi binafsi.
Ufisadi huu wa kisiasa ndio mama wa maovu mengine yote kwenye jamii: uvunjwaji wa haki za binaadamu, udugunaizesheni, rushwa, wizi wa mali ya umma, ubadhirifu na uhalifu.
Bahati mbaya ni kuwa ufisadi wa kisiasa una khulka moja ya hatari: kuzoeleka. Kila anayechukuwa nafasi ya uongozi wa umma, huona ni sawa kwake kuwa fisadi na jamii humtarajia awe hivyo. Kwamba atumie fursa ile kujinufaisha binafsi.
Ndio maana tume za uchaguzi huiba kura, wagombea hununua wapiga kura, polisi hula mkono kwa mkono na wahalifu, maprofesa hupasisha au kufelisha wanafunzi vyuoni kwa kuzingatia maslahi yao binafsi, daktari hatibu mgonjwa isipokuwa kwa makubaliano ya kupewa chake na mengine mengi.
Ufisadi wa kisiasa huzalisha jamii ya mchafukoge yenye utamaduni wa chukua chako mapema, wa iba ulindwe, wa kemea udhibitiwe. Ufisadi huu una hatari kubwa, kwa sababu huingia katika kila eneo la maisha.
Katika siasa, hufifisha na kuua kabisa mfumo wa kidemokrasia na utawala wa sheria, kwa sababu una ufisadi una kiburi cha kuingilia kati chochote kilicho dhidi yake. Demokrasia na utawala wa sheria ni kinyume cha ufisadi; na kilipo kimoja chengine hakikai.
Katika jamii kama ambayo imejikita ufisadi, mafisadi ambao ndio wenye nguvu na madaraka hawataki kuona mfumo wa demokrasia ukistawi ama utawala wa sheria ukisimama. Si ajabu kuwaona wanaingilia kati taratibu za kawaida na za kidemokrasia na za utawala wa sheria kila pale wanapoona zinachukuwa mkondo wake. Mojawapo, ni njia ya kuingia na kushikilia madaraka, yaani uchaguzi.
Ufisadi katika chaguzi hupelekea ofisi za umma kukaliwa na watu wasiotokana na ridhaa ya umma, ambao huzigeuza ofisi hizo kuwa zao binafsi na za wale waliowawezesha kuzishikilia lakini sio za umma. Unapopokea taarifa za wakaguzi zinazoonesha jinsi waliokaa kwenye ofisi za umma wanavyojichukulia mabilioni ya shilingi bila kisisi, rejea kwenye namna wizi hao walivyofikia kushikilia afisi hizo. Je, ni kwa demokrasia au kwa ufisadi wa kisiasa?
Ufisadi wa kisiasa katika vyombo vya kutunga sheria huondosha kabisa uwajibikaji na uwakilishi wa kweli wa wananchi katika vyombo hivyo. Hata viongozi wa vyombo hivyo vya kutunga sheria huwa wameingia kwenye nafasi hizo si kupitia ridhaa ya wananchi bali kwa mfumo ule ule walioingia kwenye serikali kuu. Badala ya kuwa chombo cha kuidhibiti na kuielekeza serikali, kinadhibitiwa na kuongozwa na serikali, ambayo ndiyo iliyowaweka kwenye viti vyao.
Ufisadi wa kisiasa kwenye mahakama huiweka rehani haki ya wananchi kwa kukosekana uadilifu katika utowaji haki na matokeo yake huimarisha mfumo wa dhuluma.
Kwa jumla, ufisadi wa kisiasa hukokozoa kabisa uwezo wa kitaasisi wa serikali, kwani husababisha taratibu kupuuzwa, rasilimali kuporwa, na ofisi za umma kuuzwa na kununuliwa kama bidhaa nyengine yoyote.
Ufisadi wa kisiasa ukipevuka huufanya uhalali wa serikali iliyopo madarakani uhojike na vivyo misingi ya userikali wake itoweke, kwa sababu maedeleo ya kiuchumi na kijamii (jukumu la msingi la kila serikali) huwa hayapo, na badala huwa pana umasikini na ongezeko la uhalifu mkubwa na mdogo. Mali za nchi zinaibiwa ovyo ovyo.
Kilele cha ufisadi huu ni utamaduni uitwao kleptocracy (rule by thieves), yaani utawala wa wizi – wizi wa kura, wizi wa mali, wizi wa matumaini, wizi wa kesho ya wanyonge walio wengi.