Nilibahatika kumjua Marehemu Khatib Said Haji katika Bunge la 2015-2020 yeye akiwa wa Konde na mimi wa Malindi kwa tiketi ya Civic United Front. Sikuwa namjua uso kwa uso kabla.
Siku ya kwanza kumuona ilikuwa ni baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 na tukakusanyika Ofisi ya CUF ya Vuga ili kukutana na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kutupa msimamo na mwelekeo wa Chama tukielekea Bungeni.
Ikumbukwe sisi tulikuwa tunaelekea Bungeni wakati CUF ilikwisha tangaza kususia Baraza la Wawakilishi na kutoitambua Serikali ya Mapinduzi baada ya uharamia katika uchaguzi uliojaa ghilba na wizi.
Khatib alikuwa ni msemaji, mchangamfu na mchekeshaji. Na akiwepo pahala utamjua na sauti lake la kuhanikiza.
Alikuwa pande la mtu ungedhani angeweza kuwa mgomvi kwa kutegemea umbo lake, lakini sivyo ilivyo. Khatib alikuwa mtaratibu na mwenye imani na huruma, na hayo nimeyaona mara nyingi akionyesha ukarimu panapo shida anavyoweza kutia mkono, pesa na hata moyo wake.
Lakini ana vishindo. Wenzangu walinichagua kuwa Mnadhimu wa Kambi na kwa hivyo nilikuwa na wajibu wa kuwasoma na kujua kwa hakika ni Mbunge yupi nitamtumia kwa kazi ipi au kupeleka ujumbe gani.
Khatib alikuwa ni yule Mbunge ambaye ana uwezo wa kubeba mabomu kupasua miamba. Wewe mwambie tu unataka ujumbe gani ufike…
Naam utafika tena kwa kishindo. Sifa moja kubwa ya Khatib ilikuwa ni orator. Yaani waliozaliwa na kipaji cha kutiririka bila ya kuwa na karatasi au maandishi yoyote.Kwa hivyo mimi Mnadhimu nilimtumia mara nyingi kwa kazi ya kupasua miamba na hakuwahi kuniangusha.
Ila wakati mwengine alikuwa na “nno”, chembilecho Wapemba, lakini ulipomwita pembeni na kumwambia alikiri kosa.
Khatib alikuwa mwanasiasa mzuri sana. Wakati mmoja alikuja kwangu na wazo la “kumbomoa” Maalim Seif pale mgogoro ndani ya CUF uliiuma na kesi inarindima Mahakamani. Nikamuelewa.
Ila wengi hawakumuelewa pale alipotaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa “amkabe koo” Maalim ili aeleze matumizi ya Chama yameendaje. Ilibidi nifanye mkutano na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kwamba alichotaka Khatib ni kumtengenezea jukwaa Maalim Seif. Aliweka mtego, lakini Msajili hakuusogelea.
Khatib alikuwa na busara. Akiwa anajijua ana bomu la kupasua basi huanza kwa kupaka mafuta. Iko siku alimpaka mafuta mwendazake Magufuli mpaka Bunge zima likazizima. Kisha kitu!!!! Akapasua.
Wakati wa mgogoro wa ndani wa CUF alikuwa na mrengo wa kushoto kabisa ambapo hakutaka hata kuwakaribia wale Wabunge walioamua kubaki kwa Profesa Lipumba na kila mara aliwarushia maneno hasa pale walipotunyima fursa za kuchangia Bungeni.
Mpaka mwisho kabisa alikuwa na ghamidha na Serikali ya Zanzibar na hasa Dk Ali Mohamed Shein aliyeongoza katika CUF kunyimwa haki ya Urais.
Ila litalomsindikiza mno Khatib ni mambo mawili ambayo mimi namvulia kofia kwayo. La kwanza ni uzalendo wake kwa Zanzibar ambao aliusimamia, aliusemea na aliutetea kila alipopata fursa. Na fursa wakati mwengine akizilazimisha ili apate kipaza sauti na alitumia uwezo wake kupata kipaza sauti awepo kitini Ndugai, Tulia, Najma, Zungu au Chenge.
Pili ni mapenzi yake kwa Masheikh wa Uamsho. Sote tuliwasemea ila yeye alizidi na kupitiliza. Hivi sasa kama ni kufiwa basi walofiwa zaidi ni Masheikh wa Uamsho na Wananchi wa Konde.
Bila ya shaka Khatib alikuwa ni moja ya nembo yetu toka zama za CUF hadi sasa ACT na natumai ataenziwa kadri itavyowezekanaMbunge Khatib alikuwa mwana michezo bungeni na mchezo wake ulifanana na umbo lake… Kuvuta kamba…. na Bunge likawa kinawavuta wale wa Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kama mchezo.
Ilikuwa ni rahisi kufanya urafiki na Khatib. Hakuna ambaye hakushawishika kucheka nae, kutaniana nae. Ila akiwa rafiki yake ujitayarisha kukuambia jambo la kweli hata kama litakuudhi.
Naamini Bunge litakuwa na majonzi makubwa. Wabunge ambao hawakurudi watasikitika kuwa Mola hakuwajaalia fursa ya kumzika rafiki na komredi mwenzao. Nilipata fursa nzuri ya kufanya kazi na Khatibu na nakiri ni vigumu kumpata Mbunge wa sifa za aina yake, lakini ndio matakwa ya Jala Jalali.
Askari wetu muhimu, mjasiri na mwenye uzoefu amefia vitani. Na vita vinaendelea mpaka demokrasia itamalaki.
Tumuenzi Khatib Said Haji kwa kuendeleza mapambano haya maana bila hivyo hatatulia katika kaburi lake. In shaa Allah atatusalimia Maalim Seif na amwambie umma bado unataka mabadiliko na ndoto yake bado tunayo nyoyoni mwetu.
Tanbihi: Ta’azia na Ally Saleh (Alberto) aliyekuwa Mnadhimu Kambi ya Upinzani Bungeni kutoka 2015 hadi 2020