BLOG POSTS, UCHAMBUZI

Iwache jamii iihukumu sanaa

Mimi si mtu wa huu uitwao muziki wa kizazi kipya kwa sababu nina matatizo ya kimsingi na ufasihi wa fasihi iliyomo ndani yake na pia ufinyu na mawanda ya neno SANAA panapohusika kazi zao. Lakini nawatambua waufanyao muziki huu na nawahishimu kwa kazi yao.

Hapa naandika kwa azma ya kumuunga mkono ndugu yangu, Nay wa Mitego, makhsusi kabisa kwenye kauli yake hii ya kutokukubali kubadili chochote kwenye kazi yake aliyokwishaitowa. Naandika kuunga mkono msimamo wa msanii. Uhuru wa mawazo na uwezo wa kuyawasilisha mawazo kwa ubunifu wake wa maneno, picha, sauti, michoro, ama ishara unapaswa kuhishimiwa. Jukumu la kuihukumu kazi ya sanaa ni la hadhira yenyewe.

Maisha yamenipa fursa ya kuwamo kwenye taaluma za habari na fasihi kwa wakati mmoja. Kwa hivyo, la Nay wa Mitego linanihusu binafsi. Katika taaluma ya mawasiliano ya umma, kuna kitu kinaitwa “Nadharia ya Ubawabu” (Gatekeeping Theory), ambayo inaelezea jinsi daraja nyingi kwenye tasnia ya habari zinavyoshiriki kuzizuwia, kuzichuja, kuziunda na kuziwasilisha habari kwa umma. Kwa siku moja kuna matukio zaidi ya laki moja yanatokea, lakini yanayopewa nafasi kwenye vyombo vya habari ni machache tu, na hayo machache ni kwa njia na namna ambavyo hao “mabawabu” wanavyoamua.

Mabawabu ni akina nani? Wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, wakusanyaji, waandishi, wawasilishaji na, juu ya yote, mamlaka ya nchi. Kila mmoja kati ya hao anashiriki kwenye sehemu yake ya kufungulia na kuzuwia habari ya kutoka na kuufikia umma. Hawa kwa ufupi ni wachujaji wa habari kwa kutumia taratibu walizojiwekea wenyewe. Ndio maana kwenye taaluma ya Mawasiliano ya Umma, watu hufundishwa namna ya kulinganisha na kutafautisha UANDISHI WA HABARI na UHANDISI WA HABARI. Kwa nadharia hiyo, Baraza la Sanaa la Tanzania Bara (BASATA) ni chombo cha ubawabu, chombo cha uchujaji wa kazi za sanaa. Kimeichuja kazi ya Nay wa Mitego na ikakwama kwenye chujio lao.

Kwenye fasihi, nishawahi binafsi kukumbwa na kadhia kama hii na nikachukuwa msimamo kama huu wa Nay wa Mitego. Zaidi ya miaka kumi iliyopita, Marehemu Profesa Ken Walibora aliniomba nimpelekee hadithi fupi ili aiweke kwenye mkusanyiko ambao ungekuja kuwa kwenye mtaala wa masomo ya sekondari nchini Kenya. Nikampelekea hadithi niliyoiita wakati huo “HALALI KUUWA?” ambayo ni mkasa wa msichana aliyebakwa na baba yake mzazi na hatimaye msichana huyo akamuuwa baba yake.

Baada ya muda Profesa Walibora akaniletea barua yenye maoni ya mhariri mkuu (bawabu) akiisifia kazi hiyo kwa matumizi ya lugha na mtiririko wa visa LAKINI akisikitika kwamba isingeliweza kutumika kwenye mkusanyiko huo ikiwa sikubadilisha HITIMISHO la hadithi yenyewe, yaani KIFO kama malipo ya UBAKAJI kwa sababu kufanya hivyo ni kutoa ujumbe usio sawa kwa hadhira.

Profesa Walibora akaniuliza ikiwa niko tayari kutekeleza ushauri wa mhariri mkuu ili kazi iweze kuchapishwa. Ushauri ungekuwa labda yule baba akamatwe na polisi kisha afungwe jela. Jibu langu likawa ni hapana. Siwezi kubadilisha hilo. Baba alikuwa lazima AFE na auawe kwa mikono na binti yake aliyembaka. Profesa Walibora akaniunga mkono na hadithi yangu ikarejeshwa. Hiyo ndiyo baadaye niliyoiongeza nyama ikawa novela na kuja kuichapisha mwenyewe miaka mingi baadaye kwa jina la MJA WA LAANA.

Ndiyo maana namuunga mkono Nay wa Mitego kwamba ni bora kazi yake isitoke kabisa au akaitowa kwa njia nyengine kuliko kukubali kupangiwa ujumbe anaotaka kuufikisha kwa hadhira yake na “mabawabu”. Iwache hadhira iamue ikiwa kazi yake ni nzuri ama la. Kama ni nzuri itapokelewa na kutukuzwa na kudumu. Kama ni mbaya, hadhira wataidharau na kuiwacha ife kifo cha kawaida kama ambavyo zimekufa kazi nyingi sana.

Kwa hakika hasa, kuna kazi nyingi ambazo zinapitishwa na BASATA lakini hazipokelewi na umma. Na zipo nyingi zaidi ambazo hupitishwa na umma ukazipokea lakini kwa muda mfupi tu zinapitwa na wakati hata mwaka haujafika. Hazidumu. Hii ndiyo inarudi kwenye ile kauli yangu ya mwanzo ya mashaka ya ufasihi na mawanda ya sanaa ya kazi zenyewe.

Je, kwa kuyasema haya, mimi ni mtu ambaye napendelea UHOLELA? La hasha! Nachukia uholela kwenye jambo lolote lile, si sanaa peke yake. Napendelea ufuatwaji wa taratibu na kawaida za kijamii. Naunga mkono sana maisha yenye kanuni. Lakini napingana sana na kuingilia uhuru na ubunifu wa msanii. Napingana na ubawabu usiozingatia mawanda ya sanaa. Usiojali vipimo vya fasihi. Na unaotumika kulilinda tabaka moja dhidi ya jengine. Sanaa ya fasihi ni mali ya jamii. Iwachiwe jamii yenyewe iihukumu.

1 thought on “Iwache jamii iihukumu sanaa”

  1. Nimefarijika sana baada kusoma waraka wako. Bila shaka mwenye kutaka kuelewa ataelewa, ama yule mwenye kizingiti sikioni mwake hata umuelimishe kwa lishe yenye wazo bora kwa hakika , huyo kamwe hawi miongoni mwa wenye kufahamu.

    Asante sana kwa kuwa maalim mzuri.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.