KISWAHILI KINA WENYEWE, UCHAMBUZI

Baina ya Mkosaji, Mkoseaji na Mkosefu

Mkosaji, mkoseaji na mkosefu ni watu watatu tafauti kwa Kiswahili, ingawa kuna mahala panaweza kuwa na mgusano wa kimantiki.

Mkosaji (kutokana na kitendo “kukosa) ni mtu aliyekuwa akitaka jambo na akalikosa, ndiyo maana kuna msemo “Maneno ya Mkosaji”. Kuna kisa mashuhuri cha bweha aliyezilaani zabibu baada ya kujaribu mara kadhaa azipate lakini akawa hazipati. Akasema: “Zabibu zenyewe mbaya, mbovu, chafu!” Hayo ndiyo maneno ya mkosaji. Kilugha, kitendo “kukosa” kina wahusika wawili tu: aliyekosa (mtenda) na alichokikosa (mtendwa). Kwenye kisa chetu; mkosaji ni BWEHA na alichokikosa ni ZABIBU.

Mkoseaji ni kutokana na kitendo “kukosea” yaani “kutenda kosa”. Tunaambiwa kuwa: “Kila mmoja ni mkoseaji na mbora wa wakoseaji ni yule mwenye kuomba msamaha.” Kilugha, kitendo “kukosea” kina wahusika watatu: aliyetenda kosa (mtenda), kosa lililotendwa (mtendwa) na yule ambaye kosa hilo limetendwa kwake (mtendewa).

Mara kadhaa watumiaji wasiozingatia matumizi sahihi ya maneno, husema mkosaji (aliyekosa kitu) wakimaanisha mkoseaji (aliyetenda kosa), na hali ya kuwa hawa ni watu wawili tafauti. Mtu anaweza kulikosa jambo si kwa sababu ametenda kosa. Bweha wetu amezikosa zabibu si kwa kuwa ametenda kosa, lakini kwa sababu zilipowekwa ni mahala pa juu sana, naye kila akirukia hapafikii kwa sababu ya udogo wake. Maumbile yake si kosa lake. Ndivyo alivyoumbwa.

Hata hivyo, kama nilivyosema kabla, kunaweza kuwapo mgusano wa kimantiki baina ya wawili hao (mkosaji na mkoseaji). Bweha wetu alipoamua sasa kuzilaani zabibu kwa ubovu, ubaya na uchafu alikuwa anakosea (anatenda kosa). Anazikosea zabibu kwa kuzizulia, anajikosea mwenyewe kwa kujijengea sababu za uongo badala ya kutafuta njia nyengine mpya za kuzipata zabibu au kukiri kuwa kwa kimo chake kilivyo hana uwezo wa kuzipata. Hapa ndipo maneno mawili haya (kukosa na kukosea) yanapounganika. Katika uhalisia wa maisha, tupo wengi baada ya kuwa wakosaji kwa kukosa tunalolitaka, tunajipandisha (au kujishusha) daraja na kuwa pia wakoseaji.

Ama mkosefu (kutokana na kitendo “kukoseka”) liko mbali zaidi ya yote mawili – mkosaji na mkoseaji. Hili hutumika zaidi kwenye lahaja yangu ya Kipemba, ambapo mtu akiitwa mkosefu (hakika tunasema NKOSEFU) huwa ameshushwa sana hadhi yake. Maana yake ni mtu asiyekuwa na maana, ambaye hana analolifanya likawa la manufaa kwake wala kwa wengine. Huwa mtu aliyekula hasara, aliyehasirika.

Kilugha, kitendo “kukoseka” hakina mtenda wala mtendewa wala mtendwa, bali kina mtendeka. Kwa kuwa ni kitenzi kilichomo zaidi kwenye lahaja ya Kipemba, hata uambishi wake huwa unafuata lahaja hiyo. Vyenginevyo, hakina ladha au kinakuwa na maana nyengine tafauti kabisa unapokiambisha kwa kutumia kiitwacho Kiswahili Sanifu. Kwa Kipemba, huwa tunasema: miye n’nakoseka, weye kun’koseka, yeye kan’koseka, siye tun’koseka, nyiye mun’koseka, wao wan’koseka. Lakini ukikitia kwenye Kiswahili Sanifu ukasema: “Mimi nilikoseka” utakuwa unamaanisha “mimi nilinusurika” au “mimi niliokoka.” Na ukiongeza kiambishi -na mwisho wake, ukasema: “mimi nilikosekana”, utakuwa unamaanisha kuwa “mimi sikuonekana” au “mimi sikuwepo mahala hapo!”

Lakini kama yalivyo maneno mawili ya awali (kukosa na kukosea) na hili nalo (kukoseka) linaweza kuwa na muunganiko wa kimantiki na wenzake. Ukosefu ni matokeo ya muda mrefu wa kuyakosa mambo unayoyataka na kukosea (kutenda makosa) baada ya kuyakosa huko. Sababu za kuyakosa unayoyataka zinaweza kuwa nje ya uwezo wako, lakini kwa kutokujitathmini kwako, ukawa unafanya makosa yale yale kuyatafuta na unarejea mule mule mwenye kuyakosa, hatimaye unakuwa mzoefu wa kukosa na kukosea, na ndiye huyo MKOSEFU.

Kwa hivyo, Bweha wetu alianza kwa kuwa mkosaji tu na hakuwa na kosa lolote, lakini kisha akawa mkoseaji kwa kutenda kosa la kuzilaumu zabibu alizozikosa badala ya kuchunguza sababu za kuzikosa na kuzirekebisha (kama anaweza) na mwisho naye akawa mkosefu – mzoefu wa kukosea, hana maana, ama kama mama yangu alivyokuwa akisema: HAFAI PESA MBILI, SI WA KUPIKIA WALA WA KUOPOLEA!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.