BLOG POSTS, ZANZIBAR DAIMA PUBLISHING

Dhuluma Iliyodumu na Kudamirisha

Mwaka wa nane sasa huu, Wazanzibari walio wengi wamekataa kushawishika kuwa viongozi wa Uamsho wanaoshikiliwa na dola walitenda kosa lolote linalotajwa na dola hiyo. Kwa miaka yote hii minane, msimamo wao umesalia kuwa ule ule mmoja: kwamba hii ni dhuluma ya kisiasa iliyotendwa kwao na adhabu waliyobebeshwa kwa niaba ya Wazanzibari wenzao. Walipelekwa “wakanyelee ndooni” (kwa maneno ya Balozi Seif Ali Iddi) ili liwe funzo kwa wengine wenye mtazamo wa kisiasa waliokuwa wakiuhubiri viongozi hawa hadharani – msimamo wa ZANZIBAR HURU.

Waliingizwa korokoroni wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikitawaliwa na Jakaya Kikwete na Zanzibar chini ya Ali Mohamed Shein. Kikwete akaondoka, akaja John Magufuli, na Shein akaondoka akaja Hussein Ali Mwinyi. Wao wamo ndani wakiendelea kunyelea ndooni. Sasa Magufuli naye ameondoka, amekuja Mama Samia Suluhu Hassan. Haijulikani ikiwa na Mama Samia na Dk. Hussein nao wataondoka na kuwaacha humo humo ama la!

Linalofahamika wazi ni kuwa hii ni dhuluma. Dhuluma iliyodumu kwa muda mrefu. Na kama isemwavyo: “Dhuluma haidumu na ikidumu hudamirisha”, hapana shaka hii imeshadamirisha na inaendelea kudamirisha wengi na vingi.

Kwa upande wa mahabusu hawa, zinadamirika afya zao, zinadamirika nyumba zao, wanadamirika watoto wao – yanadamirika maisha kwa ujumla wake. Ninachowaombea ni kuwa zisidamirike akili na dhamira zao njema.

Kwa upande wa walioamini kuwa wanawapigania – namaanisha Wazanzibari wenzao – umedamirika uthubutu na fakhari yao. Ile hamasa waliyokuwa wakiionesha kwenye mikusanyiko ya Uamsho na moyo wa kutaka Uhuru zaidi kwa nchi yao, vimedamirika.

Nilipokuwa likizo wakati fulani nilihudhuria mikutano hiyo kwa ajili ya kuchukuwa picha. Nakumbuka ulifanyika Mfenesini, Magharibi ya Unguja. Umma ulikuwa mkubwa na hamasa ilikuwa ya juu. Walikuwa wakijitolea kwa hali na mali kukusanya walichonacho ili kulipeleka vuguvugu mbele. Nakumbuka lilipopita “kapu” la michango, licha ya umasikini wao, walilijaza noti za elfu moja moja, mbili mbili, tano tano na wengine hata kumi kumi. Hivi leo, Wazanzibari hawa hawa wanashindwa kujikusanya kuziafu familia za viongozi wao walioswekwa ndani kwa ajili ya kupigania dhamira ya pamoja. Wamedamirika!

Kwa waliowachukuwa na kuwapeleka Bara wakanyelee ndooni, nao pia wamedamirika. Hishima yao mbele ya jamii ya Wazanzibari walio wengi imeshuka kwa kasi ya ajabu na haijawahi tena kupanda hadi sasa. Niliwahi kupewa dondoo za moja ya tafiti zilizoagizwa na watawala kuelekea uchaguzi wa 2015, ambapo utafiti ulieleza wazi athari kubwa ya kisiasa kwa watawala kutokana na dhuluma hii. Upande wa kaskazini mwa kisiwa cha Unguja ulidamirika moja kwa moja. Si ajabu kwamba kuanzia hapo, walipaswa kutumia uharamia ule ule wanaoutumia kisiwani Pemba.

Kwa waliojifanya kuibeba dhuluma hii mabegani mwao, mintarafu ya serikali ya Muungano, nao ni hivyo hivyo. Wanajuwa kuwa hawana kesi ya kuwafungulia. Wanajuwa kuwa hakuna ugaidi uliotendeka. Wanajuwa kuwa hawana haki ya kuwashikilia. Matokeo yake, siku zinakatika na tope la aibu limewakaa usoni pao. Labda, kuna wakati hutaka kuwaachia huru, lakini kwa dhuluma waliowatendea hukhofia kitakachojiri baada ya hapo. Kwa hivyo, wakaamuwa kuiendeleza dhuluma ili kuilinda dhuluma ya awali na kukwepa mwisho wa dhuluma yao. Wanadamirika.

Dhuluma haidumu na ikidumu hudamirisha. Kwa hakika, Zanzibar nzima imedamirika kwa dhuluma hii dhidi ya viongozi wa Uamsho. Imekuwa kama laana kwa nchi na viongozi na watu wake – walio kwenye madaraka na walio nje ya madaraka. Hali ya kiuchumi ya nchi na wananchi wake ni mbaya sana. Kisayansi ni shida kuhusisha dhuluma dhidi ya Uamsho na ugumu huu, maana hali pia haikuwa nzuri kabla ya dhuluma kutendeka. Lakini kiroho ni rahisi kuuona uhusiano baina ya dhuluma na dhiki.

Tuna wiki moja na kidogo kuingia kwenye Ramadhani, mwezi wa msamaha, rehema na huruma. Ombi langu kwa wenye mamlaka kote Tanzania na Zanzibar: tuondoleeni dhuluma hii. Watoweni viongozi wa Uamsho.

Mohammed Ghassani
3 Aprili 2021
Bonn

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.