NJOO uniulize Mohammed Khelef Ghassani ni nani na nitakupa vitambulisho vyake kadhaa. Kila kimoja kati yavyo kitamsibu. Kitajaa kama pishi.
Wengi wanamjuwa kwa jina la “Mohammed” alilopewa na wazazi wake. Kuna wengine, kama mimi, waliozoea kumwita “Khelef” jina la baba yake. Na wapo wanaomwita Ghassani, jina la ukoo wake. Mwenyewe, mara nyingine, hujiita “Mo al Ghassani.”
Tukiviacha vitambulisho hivyo vya isimu zake, yeye pia ana vipaji vinavyomfanya awe na vitambulisho vingine tafauti: mshairi, mtangazaji wa redio ya kimataifa, mwanahabari, mwandishi, mpiga picha, mchapishaji vitabu na gwiji wa mitandao ya kijamii. Kwa ufupi, na kwa hakika, yeye ni taasisi kamili. Ni taasisi ya mtu mmoja yenye kukhusika na tasnia ya mawasiliano, kwa upana wake wote.

Mohammed Khelef Ghassani aliwahi kuandika jinsi alivyochanganya damu za makabila tafauti ya Kiafrika, na yasiyo ya Kiafrika. Mchanganyiko huo ndio uliomfanya hivi alivyo — Mpemba, Mzanzibari, Mswahili, Mtanzania. Nionavyo ni kwamba kati ya damu zake zote ni mbili zilizokoza zaidi na zinazomwenda, bila ya kusita, mishipani mwake na kwenye hisia zake. Damu zenyewe lakini si za kikabila bali ni za ushairi na uanaharakati.
Damu hizo zimemfanya awe mrithi khalisi wa yule Ghassani mwengine, mshairi maarufu wa karne ya 18, Muyaka bin Haji al Ghassani. Sijui ikiwa Maghassani hao wawili wamekhusiana, iwapo damu ya kinara wa malenga wa mashairi ya Kiswahili Muyaka wa Haji ilitiririka na kumfikia malenga wa kileo Mohammed wa Khelef.
Muhimu ni kutambua kwamba Maghassani wote hao wawili ni washairi wapambanaji au wapambanaji wa kishairi. Hawakushika panga wala bunduki bali silaha zao zilikuwa kalamu, wino na maneno. Ni wapambanaji waliotumia mishororo wakiwa mashuhuda wa taarikh (historia). Kwa kufanya hivyo wamekuwa wakitunza kumbukumbu kwenye vitabu vyao vya moyoni, chambilecho Mohamed Ghassani, Vitabu Nyoyoni:
Tuna vitabu moyoni, mengi tuliyoandika
Mengi siri za sirini, funiko ‘mezifunika
Na japo mwetu ndimini, hatuwezi yatamka
Hata mwetu akilini, hatutaki yakumbuka
Lakini kuyaepuka, hilo haliwezekani!
Humu mwetu vifuani, kurasa zajiandika
Nyingi zisizo kifani, hakuna zinachoruka
Zayaweka hifadhini, siku, saa na dakika
Kuna siku ya Manani, kurasa zitafunuka
Zifike kwa kukufika, mambo yawe hadharani!
Mashairi ya Ghassani huyu wa enzi zetu, kama yale ya Ghassani wa kale, ni mithili ya kioo. Na Ghassani wetu amekiunda kioo hicho kwa msamiati mkubwa ukiwa pamoja na ule wa lahaja ya Kiswahili cha Kipemba. Muyaka akitumia zaidi lahaja ya kimvita. Wote ni wabobezi wa kuweka neno juu ya neno, likifuatiwa na neno. Nalo likivutwa na jingine katika mpangilio wa maneno ambao hatimaye huleta maana makhsusi. Hiyo maana huzaliwa na hayo maneno.

Kwa namna anavyochagua maneno ni wazi kwamba Mohammed Ghassani ni fundi wa maneno. Ni mhunzi khasa wa kuyachukua maneno na kuyafinyanga atakavyo. Mara hayo maneno huwa silaha, huwa mshale wa kuwalengea watawala dhalimu, mara hugeuka na kuwa tasa la kutemea machungu ya madhalimu, mara huwa bakuli la kumiminia machozi yanayomtoka akiwakumbuka wanaodhulumiwa au akilalama kwa namna alivyotolewa maanani na mpenziwe wa zamani anayemuona sasa kuwa si kitu kwenye shairi N’shakuwa Alikuwa:
N’shakuwa ‘Alikuwa’, kiumbe wa hadithini
Zamani niliyekuwa, nimo mwako nafsini
Na weye kwangu ukawa, ndiye fatiha na nuni
Leo yangu anuwani, kwako miye ‘Alikuwa’
Kwako sasa ‘Alikuwa’, ndiyo yangu anuwani
Siye tena yule dawa, na barafu wa moyoni
Yule kwake ulokuwa, wamuona gilasini
Wakiuliza jirani, wawambia ‘Alikuwa!’…
Jina langu ‘Alikuwa’, wala si bini fulani
Wakata ukilitowa, likabakia nchani
Ndilo wanonitambuwa, walio Bara na Pwani
‘Menitia kikutini, niitwavyo ‘Alikuwa!’
Waniita ‘Alikuwa’, sina somo mtaani
Peke yangu nimekuwa, mwenda kimya macho chini
Kama siye ulokuwa, ‘kinibimba vitangani
Miye akhiri zamani, n’shakuwa ‘Alikuwa!’
Ghassani ana kipaji cha kuyafanya mashairi yake yashibe maana. Hayakufanyi uisikie tu bali hukufanya hata uione hali ya mambo ilivyo nchini mwake anapozungumzia maudhui ya kisiasa. Au hukufanya uuone moyo wake ulivyo anapozungumzia mambo ya mahaba yenye kuigusa nafsi yake.

Katika nyanja zote hizo mbili, za siasa na za huba, Ghassani anafanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu huwa anakijua anachokieleza. Labda ameufuata wasia wa Gabriel García Márquez, mzawa wa Colombia aliyekuwa mwandishi mahiri wa riwaya. Wasia wake kwa mwandishi au anayetaka kuwa mwandishi ulikuwa: “Andika unachokijua.”
Kukhusu siasa, Ghassani anayajua mengi kutokana na kazi yake ya uanahabari. Ayajuayo yanaliza. Humfanya alie moyoni. Na vilio vya ndani ya moyo huwa ni vya sampuli ya kipekee. Huwa na mapigo yake, mayowe yake na kwikwi za aina yake. Vilio hivyo tunavisikia katika baadhi ya mashairi yaliyomo kwenye diwani hii, “Mfalme Yuko Uchi”.
Kalima hii ya ‘mfalme yuko uchi’ aghalabu hutumika katika muktadha wa kisiasa. Huwa inawahusisha walio wengi katika jamii wenye kuukanya ukweli licha ya kwamba ukweli wenyewe uko wazi unawakodolea macho. Wenye kuukataa ukweli hufanya hivyo kwa kujipendekeza kwa mtawala ambaye naye pia huwa hataki kuuamini ukweli ulio wazi. Kinachotokea ni kwamba mtawala, aghalabu wa kidikteta, huughilibu umma. Umma nao, kwa kujipendekeza, hukubaliana na ayasemayo mtawala.
Jamii hugeuka na kuwa jamii ya kudanganyana. Mtawala anaudanganya umma na umma unamdanganya mtawala. Mfano mzuri ni wakati wa uchaguzi inapodhihirika kwamba mtawala anang’ang’ania madaraka ijapokuwa hakushinda. Mtawala wa kidikteta huwa anajua kwamba hakushinda. Umma nao huwa unajua kwamba mtawala hakushinda lakini wote hujidanganya kwamba ameshinda.

Inayumkinika kwamba kalima ya ‘mfalme yuko uchi’ ilitokana na hekaya moja ya mafunzo ya Kisufi lakini baada ya kupokewa na masikio ya tamaduni tafauti hadithi hiyo ilizidi kupata umaarufu katika nchi za Magharibi iliposarifiwa na mwandishi wa Denmark, Hans Christian Andersen. Mwandishi huyo aliandika hekaya fupi mwaka 1837 aliyoiita ‘Nguo Mpya za Mfalme’. Hadi sasa imefasiriwa kwa lugha zaidi ya mia moja.
Hekaya hiyo ilipomfikia Mohammed Ghassani aliinyaka na akaisarifu kivyake kama ilivyo kwenye mukhtasari wake wa kitabu hiki. Isitoshe aliitungia shairi lenye anuwani ya “Mfalme Yuko Uchi” ambayo pia ndiyo anuwani ya kitabu hiki.
Huu ni mkusanyiko wa mashairi 63 ya Mohammed Ghassani na ni diwani yake ya saba kuchapishwa. Ya mwisho kabla ya hii aliipa anuwani ya “Mfalme Ana Pembe”. Na ya tano, “N’na Kwetu”, ilishinda tuzo adhimu ya fasihi ya Kiswahili ya Mabati-Cornell kwa mwaka 2015.
Machache miongoni mwa mashairi yaliyomo kwenye diwani hii “Mfalme Yuko Uchi” aliyatunga wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2020, uchaguzi uliowashuhudia wapinzani, pamoja na wanaoshukiwa kuwa wapinzani, “wakishughulikiwa” na vyombo vya dola.
Kwa upande wa Zanzibar, polisi pamoja na vikosi maalumu vya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na magenge ya waitwao “Janjawid” waliwatesa na kuwaua kinyama wananchi wasiopungua 15. Wengine walikamatwa kwa makumi na kuwekwa kwenye kambi maalumu ambako waliteswa kinyume na sheria za nchi na kwa ukiukwaji uliokubuhu wa haki za binadamu.
“Mfalme Yuko Uchi” ni diwani yenye mashairi mazito yanayotulazimisha tutafakari kukhusu dhima ya fasihi katika maisha yetu ya kijamii na ya kisiasa.
Ahmed Rajab
London,
Novemba 16, 2020
Asalam Aleikum. Natumai umzima na mwaka umeanza vyema. Je Nita Ipara vipi hii Diwali yako mpya? Salam kwa jamaa. Rayya Timammy Sent from my iPhone
>
Alaykum salaam warahmatullah Profesa. Nitakuletea nakala yako wiki mbili zijazo InshaaAllah. Shukrani. Wasalimie pia hapo nyumbani.
Habari mshairi wetu tunapataje nakala?
Itakuwa kwenye Amazon na Lulu.Com karibuni. Lakinni pia unaweza kuagizia nakala yako kwangu. Ahsante sana.