KISWAHILI KINA WENYEWE

Kuhusu Mwanamajumui

Kabla ya kuelezaa maana ya neno “mwanamajumui”, kuna mambo mawili ambayo ni muhimu kuyaeleza. La kwanza, ni kwamba kuna wasemao “mwanaumajumui”; na baadhi ya watu huidondosha hiyo u walitumiapo neno hilo.

La pili, kama tulionavyo, hilo ni neno lililokusanya maneno mawili – mwana na (u)majumui. Na, kama tujuavyo, neno mwana liwapo pekee huwa lina maana ya mtoto. Lakini  mwana lijumuishwapo na neno jengine ambalo ni nomino (jina), huwa lina maana ya mtu ashughulikaye na, au aliye na sifa ya, au aliye na asili ya, hicho kilicho na maana ya neno lililounganishwa nalo. Ndipo tukapata maneno kama vile mwanaadamu, mwanamke, mwanamume, mwanamaji, mwanachuoni, mwanasheria, mwanaanga, mwanamichezo, mwanaharakati, mwanamapinduzi, mwananchi, mwanasiasa, na kadhalika.

Na Abdilatif Abdalla

Kwa hivyo, kulipatia maana neno “mwana(u)majumui”, itabidi mwanzo tuijue maana ya “(u)majumui”. Neno hili lina asili ya lugha ya Kiarabu, na ambalo latokana na mzizi wa harufu (herufi)  j-m-‘ – yaani konsonanti ambazo kwa Kiarabu zaitwa jim (ﺟ), miym (ﻣ),‘ayn (ﻊ) ► ﺟﻣﻊ. (Tuandikapo Kiswahili kwa haya maandishi ya Kirumi tuyatumiayo, huwa hatuna harufu iwezayo kuiwakilisha sauti itokanayo na ‘ayn. Kutokana na ukosefu huo, tuandikapo neno lenye harufu hiyo, hutubidi kuandika irabu a, au i, au u – kutegemea kama hiyo ‘ayn imeribizwa fat-ha (a), au kasra (i), au dhwamma/dhwumma (u)).

Miongoni mwa maana za jumla zipatikanazo kutokana na mzizi huo wa jim, miym na ‘ayn, zahusiana na mkusanyo/kukusanya, muungano/muunganisho/kuunganisha, umoja/kuweka pamoja, kukutanisha vitu viwili au zaidi, au kukutanisha watu wawili au zaidi, na kadhalika. Ndipo katika Kiswahili kukapatikana maneno (ambayo ni nomino) kama vile jamaa, ujamaa, ujima, jamii, jumuiya, ijtimai (jitimai), ijimai, jimai, juma, ijumaa – maneno ambayo yote yana dhana za maana zilizoelezwa hapa juu. Pia, tukawa na vitenzi kama vile kujamii, kujumuika, kujumuisha.

Kwa hivyo, basi, neno “umajumui” litakuwa na maana ya aina fulani ya mkusanyiko au mjumuiko wa watu wanaotokana na jinsi au asili moja, au walio na msimamo au mtazamo mmoja kuhusu jambo fulani, walioungana katika chombo fulani – kwa mfano chama au jumuiya – kwa ajili ya kutimiza au kutekeleza malengo fulani. Ndipo tukawa na neno “mwana(u)majumui”.

 

W. E. B DuBois

Matumizi ya neno hili katika Kiswahili ni ya kisiasa, na hutumika katika kishazi cha maneno, “umajumui wa Afrika”, na “mwana(u)majumui wa Afrika” ili kufasiri maneno ya Kiingereza, Pan Africanism na Pan Africanist. Na matumizi haya hayana umri mrefu. Ndiyo sababu maneno hayo yakawa hayamo hata katika makamusi ya hivi karibuni kabisa – kwa mfano, Kamusi Kuu ya Kiswahili (BAKITA: Longhorn, 2015) na Kamusi Elezi ya Kiswahili (Jomo Kenyatta Foundation, 2016).

Na hili neno Pan Africanism, liliingia katika msamiati wa kisiasa mwaka 1900. Aliyelibuni ni mwanasheria mwenye asili ya Kiafrika kutoka Trinidad, Henry Sylvester Williams, ambaye mwaka huo alipokuwa London aliandaa mkutano wa watu wenye asili ya Afrika ili kupinga kitendo cha wakoloni cha “…wizi wa ardhi katika makoloni, (kupinga) ubaguzi wa rangi, na kushughulikia maswala mengine yawahusuyo, na yenye maslahi na, watu wenye asili ya Afrika” waishio nje ya Afrika au makwao kwengine. (Tizama makala ya W.E.B. Du Bois, ‘Origins of the Pan African Movement’ (yaani, Asili ya Vuguvugu la Umajumui wa Afrika), katika 7th PAC News,i 1993. Wanaotaka maelezo zaidi kuhusu chanzo cha Vuguvugu hili, waweza kuyapata katika kitabu cha V.B. Thomson, Africa and Unity, Longmans, London, 1969; makala ya Kwame Nkrumah, ‘Towards African Unity’, katika kitabu chake, Africa Must Unite, Panaf, London, 1963;  kitabu cha George Padmore, Pan Africanism or Communism, Denis Dodson, London, 1956; na pia kitabu kilichohaririwa na Tajudeen Abdul-Raheem, Pan Africanism: Politics, Economy and Social Change in the Twenty-First Century, Pluto Press, London, 1996.)

Baada ya mkutano huo ulioandaliwa London na Henry Sylvester Williams, kuanzia tarehe 23 mpaka 25 Julai, 1900, mkutano wa kwanza wa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika (Pan African Congress), uliandaliwa na mwanachuoni na mwanaharakati Mmarekani mwenye asili ya Afrika, Dakta W.E.B. Du Bois, tarehe 17 mpaka 21, 1919, mjini Paris, Ufaransa. Wa pili, ulifanyika Septemba 1921 katika miji mitatu – London, Brussels na Paris. Wa tatu ulifanyika katika miji miwili (London, tarehe 7 na 8 Novemba, 1923; na Lisbon, Ureno, tarehe 1 na 2 Disemba, 1923. Wa nne ulifanyika Agosti 1927, New York, Marekani. Wa tano ulikuwa tarehe 15 mpaka 19, 1945, Manchester, Uingereza.

Tafauti na hiyo mikutano mine ya kwanza, ambayo ilihudhuriwa na watu wenye asili ya Afrika waishio katika nchi za Ulaya, huu mkutano wa tano ndio uliokuwa wa kwanza kuhudhuriwa na wajumbe waliosafiri kwenda Manchester kutoka Afrika kwenyewe; na pia ulikuwa ndio wa kwanza, katika mfululizo wa mikutano hiyo, kulikabili na kulijadili swala la kupinga ukoloni na kupitisha azimio la nchi za Afrika kupigania uhuru.

Miongoni mwa wajumbe hao walikuwa ni viongozi wa vyama vya wafanyakazi na vya wanafunzi, wanaharakati na viongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa nchi za Afrika, na ambao baadhi yao wakaja wakawa ni viongozi wa nchi zao baada ya uhuru kpatikana. Kwa mfano, Wallace Johnson (Sierra Leone), Obafemi Awolowo, Nnamdi Azikiwe na Jaja Wachukwu (Nigeria), Jomo Kenyatta (Kenya), Hastings Kamuzu Banda (Malawi), Peter Abrahams (mwandishi wa riwaya kutoka Afrika ya Kusini), na Kwame Nkrumah na Ako Adjei (Ghana).  Hiyo mikutano yote mitano ya kwanza iliongozwa na Dakta W.E.B. Du Bois.

Mkutano wa sita wa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika ulifanyika Dar es Salaam, Chuo Kikuu (Nkrumah Hall), mwezi wa Juni 1974. Kwa vile wakati huo nilikuwa nafanya kazi hapo, nilipata bahati ya kuhudhuria baadhi ya vikao vya mkutano huo, uliofunguliwa na Mwalimu Julius Nyerere. Na mkutano wa sabaa ulifanyika kuanzia tarehe 3 mpaka 8 Aprili, 1994, Kampala, Uganda, uliofunguliwa na Rais Yoweri Museveni. Mkutano huu nao niliuhudhuria na pia kuuhutubia, kutokana na wadhifa wangu wa kuwa kiongozi wa Umoja wa Kupigania Demokrasia Kenya (United Movement for Democracy in Kenya), ulioundwa London mwaka 1987, kutokana na muungano wa vyama vyote vya wanaharakati Wakenya vilivyokuwa uhamishoni katika nchi mbalimbali duniani. Tangu mkutano huo wa Kampala, hakujafanyika mkutano mwengine wa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika.

Kwa hivyo, kwa ufupi, mwana(u)majumui wa Afrika atakuwa ni mtu ambaye, kwa mfano,  yuwaamini moyoni – na kwa vitendo – kwamba Afrika ni moja;  kwamba nchi za Afrika zahitaji kuungana na kushirikiana; na kuuondoa, au angalau kuupunguza, mgawanyiko ulioko sasa uliosababishwa na mipaka ya kijiografia  tuliyowekewa na wakoloni; kuwa na sauti moja kuhusu maswala ya bara la Afrika muda nchi hizo zikabilianapo na nchi za mabara mengine, badala ya kila nchi kujifanyia mambo kipekee.

1 thought on “Kuhusu Mwanamajumui”

Leave a Reply to Mualim Cancel reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.