بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي ﴿٢٥﴾ وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي ﴿٢٦﴾ وَاحْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي ﴿٢٧﴾ يَفْقَهُوا قَوْلِي
Ewe Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu, Na unifanyie nyepesi kazi yangu, Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu, Wapate kufahamu maneno yangu. (Suratu Maryam Aya ya 25-28)
UTANGULIZI
Mimi si mtaalamu wa lugha, wala si mweledi katika uandishi. Sikuondokea kujishughulisha na kazi ya uandishi, na bahati mbaya mpaka sasa nimebaki vivyo hivyo. Japokuwa sina ufasaha pia katika uzungumzaji, lakini huwa ninafadhilisha kufikisha makusudio yangu kwa njia ya uzungumzaji kuliko uandishi. Kwa sababu hiyo, nimekuwa nikitembea nalo kichwani mwangu kwa muda mrefu, dukuduku langu la haya nitakayoyaeleza katika andiko hili, mpaka hivi karibuni ilipotokea sababu ya heri iliyonipa msukumo wa kukaa kitako na kuchapa maneno haya.
Nimeamua kuandika kuhusu mada hii niliyoipa jina la suali la: “NI SWALA AU NI SALA?” kwa sababu moja ya msingi, nayo ni mapenzi kwa dini yangu na lugha yangu ya uzawa. Dhamira hasa ya kufanya hivi ni, chambilecho wataalamu wa Kiswahili, kuchokoza mada, ili nipanue maarifa yangu juu ya maudhui hii, kwa ama, kupatiwa suluhisho na utaratibu sahihi wa uandishi wa neno hilo, au angalau kufaidika na rai tofauti za wataalamu wa lugha, wanaotumia maneno hayo kwa uandikaji na tafsiri tofauti.
Ninakuombeni nyote mtakaosoma makala hii fupi, hasa wataalamu wa Kiswahili, mnisaidie mimi na kila mwenye dukuduku kama langu, kutupa ufahamu mpana zaidi wa maudhui hii na nyinginezo zenye utata, katika uandishi wa lugha yetu hii azizi.
Allah SW anasema katika aya ya 104 ya Suratul Baqarah:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقُولُوا رَاعِنَا وَقُولُوا انظُرْنَا وَاسْمَعُوا ۗ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ
Enyi mlio amini! Msiseme: “Raa’ina”, na semeni: “Ndhurna”. Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.
NI SWALA AU NI SALA?
Sote tunajua kuwa Kiswahili, asili yake kilikuwa kikiandikwa kwa kutumia alfabeti za Kiarabu, mpaka ulipokuja kubadilishwa uandikaji wake na kuanza kutumika herufi za Kilatini.
Suali la kujiuliza hapa ni, je yalipofanyika mabadiliko hayo, au tangu wakati huo hadi sasa, uliwahi kuwekwa utaratibu rasmi na wa kikanuni wa uandishi wa Kiswahili, unaotoa mwongozo wa jinsi ya kuyaandika na kuyasoma maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu kwa kutumia herufi za Kilatini?
Inawezekana jambo hilo limefanyika na lipo, lakini mimi binafsi sikuwahi kufundishwa skuli katika somo la Kiswahili, au kubahatika kusoma kitabu au andiko lolote linalozungumzia maudhui hiyo. Hata hivyo kwa uzoefu wangu wa kusoma na kujifunza Kiswahili, nimehisi utaratibu ufuatao ndio unaotumika zaidi katika uandikaji na utamkaji wa maneno hayo.
- A, E, I, O na U zinatumika kwa maneno ambayo herufi zake katika Kiarabu ni ALIF na AYN. Kwa mfano. Ali, elimu, ibada, isha, izara, ahueni, afadhali, ahera, akili, amani, orodha, umri, umra, umma n.k.
- T inatumika kwa maneno ambayo herufi zake katika Kiarabu ni TAA na T’AA. Kwa mfano: taifa, tabia, tabaka, tarehe, tabibu, tabasamu, taathira, tahiri, tafadhali, matilaba, matlai n.k.
- TH inatumika kwa maneno ambayo herufi zake katika Kiarabu ni THAA. Kwa mfano: thabiti, thalathini, thamani, thamini, thawabu, theluji, thibiti n.k
- H inatumika kwa maneno, ambayo herufi zake katika Kiarabu ni H’AA, KHAA NA HAA. Kwa mfano: hadhi, hadithi, hamsini, hekima, hifadhi, hija, halali, hali, hedhi, homa, huru, habari, heri, hofu, halisi, hafifu, hatibu, hati, hatari, hiliki, hitima n.k.
- DH inatumika kwa maneno ambayo, herufi zake katika Kiarabu ni DHAAL na DH’AA. Kwa mfano: dhahabu, dhambi, dhalili, dhuluma, dhalimu, dhuru, dhiki, dhahiri, dhaifu, dhana, dhani, dhamiri, dharau n.k.
- ***S inatumika kwa maneno ambayo, herufi zake katika Kiarabu ni SIIN na S’AAD. (Nimeweka msisitizo maalumu katika kifungu hiki kwa kuwa ndilo ndilo chimbuko la andiko hili). Kwa mfano: saa, saada, saba, sababu, sabahi, sabihi, sabuni, subira, sadaka, sadiki, safi, safari, safu, sahifa, SALA, SALI, sahaba, sahibu, sahihi, saliti, sarifu, sarufi, saumu, sifuri, sijida, sihi, sifa, silimu, siri, sitiri n.k.
- GH inatumika kwa maneno ambayo, herufi zake katika Kiarabu ni GHAYN. Kwa mfano: ghadhabu, ghafilika, ghaibu, ghairi, ghali, ghamu, gharama, ghariki, ghururi, ghusubu, magharibi n.k.
- K inatumika kwa maneno ambayo, herufi zake katika Kiarabu ni QAAF NA KAAF. Kwa mfano: kalamu, kitabu, kufuli, kabidhi, kaburi, kabuli, kabili, kafara, kadha, kadhi, kaimu, karaha, karama, katili, karibu, kiyama n.k.
Bila ya shaka umesha baini kuwa nimeacha kuzungumzia baadhi ya herufi, kwa sababu ya kutokuwa na utata wowote katika uandishi na utamkaji wake. Kwa mfano B=BAA, J=JIIM, D=DAAL, R=RAA, Z=ZAA, F=FAA, L=LAAM, M=MIIM, N=NUUN, W=WAAW na Y=YAA.
Lakini kabla hatujaendelea mbele, inafaa tujiulize suali moja muhimu, nalo ni: Kama mlinganisho huu tuliofanya wa utamkaji herufi za Kiarabu katika Kiswahili ni sahihi, je, inapasa au ni lazima maneno yanayotokana na herufi hizo yasomwe kama yanavyoandikwa? Uzoefu nilionao unaonyesha kuwa hali haiko hivyo. Kuna hali kadhaa za usomaji wa maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu.
Kuna kundi la kwanza la wazungumzaji wa Kiswahili, wanaosoma maneno yenye asili ya Kiarabu kama yanavyoandikwa kwa kufuata msingi huo. Yaani palipoandikwa ‘heri’ husoma heri na si ‘kheri’, kurani na si qur’ani n.k.
Kundi la pili ni la wanaojaribu kufanya hivyo, lakini wanashindwa kutokana na ugumu wa baadhi ya maneno yenye asili ya Kiarabu, kama magharibi, ghadhabu n.k.
Wako wa kundi la tatu wasiojali kutamka maneno hayo kama yanavyoandikwa, hata kama wanao uwezo wa kufanya hivyo. Kwa mfano wanasema samani (thamani), zulma (dhulma) n.k.
Wako pia wa kundi la nne wanaobadilisha utamkaji wa baadhi ya maneno kwa kuyarejesha kwenye asili ya Kiarabu, hasa yale yenye uhusiano na ibada na maadili ya dini ya Kiislamu; na wako pia wa kundi la tano wanaotamka maneno YOTE ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu, kama yanavyotamkwa katika Kiarabu.
Watu wa kundi la mwanzo na la pili, wengi wao ni wazungumzaji wa Kiswahili ambao hawana msingi wa lugha ya Kiarabu au msingi wa masomo ya dini ya Kiislamu kama usomaji Kurani (Qur’ani).
Watu wa kundi la tatu (wasiojali kutamka swasawa) na la nne ni wale walio na ufahamu wa usomaji Kiarabu au Qur’ani; na watu wa kundi la tano, aghalabu ni wale wazungumzaji wa Kiswahili wanaoishi nje ya eneo la Afrika Mashariki, hususan walioko Arabuni.
Kutokuwepo utaratibu rasmi na wa kikanuni wa jambo hili, ndio unaosababisha baadhi ya maneno yenye asili ya Kiarabu yaandikwe kama yanavyotamkwa katika makamusi na maandiko rasmi na kukiuka kanuni niliyoashiria. Mfano wa maneno hayo ni: Alhamisi (Alkhamisi), Kur-ani (Qur’ani), heri (kheri), ahera (akhera), halifa (khalifa), hitima (khitma), huntha (khuntha), habithi (khabithi), humusi (khumusi) n.k.
Inavyoonekana, hali hii imekubalika katika jamii ya wazungumzaji wa Kiswahili. Mimi binafsi nimo kwenye kundi la nne la wanaofadhilisha, inapokuwa WEPESI, kuyatamka maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu, kwa lafudhi ya Kiarabu. Kama Qur’ani, kheri, alhamdulillah, Allah, Subhanallah, khabithi, t’aghuti, hija, khumsi, magharibi, I’sha, takabali, taufiki n.k.
Baada ya utangulizi huo, tuingie sasa kwenye nukta kuu ya makala hii, yaani kujadili hoja ya utumizi sahihi wa maneno SALA na SWALA na yale yanayotokana na mzizi wa neno hilo kama KUSALI/KUSWALI, MSALA/MSWALA, KUSALISHA/ KUSWALISHA, KUSALISHWA/ KUSWALISHWA, MSALIHINA/MSWALIHINA n.k
Kama unakubaliana nami kuhusu kanuni niliyotaja ya usomaji na uandishi wa maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu, basi utakubaliana nami pia kuwa uandishi sahihi wa: Ibada inayotekelezwa na Waislamu kwa mujibu wa shuruti, nguzo na wakati wake maalumu. Au nguzo ya pili ya Kiislamu inayojumuisha vitendo k.v, kusimama, kuinama, kusujudu na kukaa. (KAMUSI LA KISWAHILI FASAHA UK: 353), ni SALA na si SWALA. Kwa kuongezea ni kwamba, katika maandiko ya baadhi ya waandishi wa Kiswahili, na hasa walio na ujuzi wa lugha ya Kiarabu, kama marehemu Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsi au marehemu Shaaban bin Robert, neno hilo limeandikwa kwa sura ya SALA na si SWALA. Kusema hivi simaanishi ninakanusha kuweko maandiko ya wataalamu wa zamani wa Kiswahili, ambao wametumia neno SWALA. Yamkini wapo, ila mimi sijabahatika kukutana nayo.
Ufafanuzi zaidi wa mtazamo wangu juu ya suala hili unatokana na maelezo yafuatayo.
Kama tutaamua kubadilisha utaratibu wa uandishi wa maneno yenye asili ya Kiarabu, yanayojumuisha herufi ya S’AAD uwe wa SW badala ya S, itabidi kimantiki na kikaida (kikanuni) tufanye hivyo kwa maneno YOTE yenye asili ya S’AAD, kama sabuni, subira, sadaka, sadiki, safi, safu, sahihi ili yawe swabuni, swubira, swadaka, swadiki, swafi, swafu, swahihi n.k. Hii ni pamoja na unyambulishaji wa vitendo (vitenzi) pia vinavyotokana na maneno hayo, na isiwe tu kwa maneno kama SWALA na SWAUMU na mfano wa hayo, yanayohusiana na ibada za Kiislamu. Kama ni kujumuisha maneno yote hayo, itabidi kuanzia sasa tuandike na kusoma hivi:
(a) Mtu huyu anaswifika kwa swifa nzuri;
(b) Tuliposwali swala ya alaswiri, swafu ya mbele haikujaa.;
(c) Si swahihi kufanya uswafi wa msikiti, wakati watu wanajiandaa kwa ajili ya swala.
Baada ya kusoma sentensi hizo mbili, nina imani utakubaliana nami kwamba, kwa kuanzisha utaratibu huo, Kiswahili kitakuwa kigumu kuandikika; lakini zaidi kusomeka na kuzungumzika. La kama sisitizo la watetezi wa hoja ya SWALA ni kutaka mtu anapozungumza TU, alitamke neno hilo kwa lafudhi ya Kiarabu, hilo halina mgongano wowote na kuheshimu kanuni tuliyotaja ya kuandika Sala lakini tukasoma Swala, au kuandika Sahaba, tukasoma Swahaba n.k.
Lakini inapasa tujue pia kwamba KIUHALISIA, utamkaji wa SWALA katika uandishi wa Kiswahili, yaani ‘SWA’ umeshadidishwa zaidi, kuliko hata namna Waarabu wenyewe wanavyaoitamka herufi ya S’AAD! Pengine mtu anaweza kusema, anataka tuandike SWALA na KUSWALI ili itafautike ibada hiyo ya Waislamu na ile wanayofanya Wakristo kanisani, ambayo mimi binafsi, sijui asili yake inaitwaje!
Yaani, iwe kama inavyoonekana kwenye baadhi ya makamusi, ikiwemo Kamusi ya Kiswahili Sanifu, ambayo imeandika: Sala (katika Ukristo) 1. Maombi kwa Mwenyezi Mungu; dua. 2. Shughuli za kumshukuru Mungu. (uk: 247). Katika ukurasa wa 248 imeandikwa: Sali: (katika Ukristo) Omba dua kwa Mwenyezi Mungu. Kisha katika kueleza maana ya SWALA imeandika: Swala (A) Ibada maalumu katika dini ya Kiislamu iliyochanganya visomo na vitendo fulani k.v. kurukuu, kusujudu, n.k na ambayo ni ya lazima kutekelezwa; mojawapo ya nguzo tano za Uislamu. Swala: Jambo linalotakiwa kujadiliwa na kukatiwa shauri. Swala: 1. Mnyama wa jamii ya kurungu na tohe. 2. Mnyama afananaye na mbuzi mkubwa anayeketi porini. 3. Mbuzi pori. Kisha kamusi hiyo ikaandika tena: Swali: (A) jambo linalotakiwa kujulikana jawabu yake; jambo linaloulizwa; ulizo. Swali: (B) tekeleza ibada ya swala. (uk: 269).
Kusema kweli, niliposoma maelezo hayo kwa mara ya kwanza katika KATIKA KAMUSI YA KISWAHILI SANIFU, ambayo ilichapishwa kwa mara ya mwanzo mwaka 1981, nilipigwa na butwaa, nikabaki nimeduwaa!!! Nishindwa, na hadi sasa ninashindwa kuelewa hekima na falsafa ya watungaji wa kamusi hiyo kuanzisha ubunifu wa aina hii, ambao ninahisi ni wa KIPEKEE, wa kulichukua neno moja, lenye asili moja kiuandishi na kimaana katika Kiarabu, wakaubadilisha muundo wa uandishi wake na maana yake pia, wakati neno hilo lina maana ya tendo la IBADA katika dini mbili tofauti na zinazokinaza! Ajabu kubwa zaidi ni kuwa, ibada hiyo tukufu zaidi ya WAISLAMU, imeamuliwa uandishi wake ubadilishwe kutoka hali yake ya asili ya SALA na kubatizwa sura mpya ya uandikaji, yenye hali sawa na maneno mengine mawili yenye maana tofauti, moja likiwa ni la MNYAMA! Je, kwa mtazamo wa wabunifu wa jambo hili, huku ni kuipa hadhi SALA??!! Ikiwa Sala au Swala asili yake ni neno la Kiarabu na sote tunajua kuwa maandiko ya asili ya Ukristo si Kiarabu, vipi imeonekana neno lenye asili ya Kiarabu na lenye hali ya kipekee kiuandishi katika Kiswahili, yaani SALA litumiwe kueleza maana ya ibada ya Kikristo, dini ambayo ni NGENI katika lugha na utamaduni wa Kiswahili, na lile lenye maana kadhaa, ikiwemo ya mnyama lipendekezwe kwa ajili ya ibada tukufu zaidi ya Waislamu? Tuna msingi na mwongozo wowote katika mafundisho ya Uislamu na majina ya ibada zake tuliotumia kubuni jambo hili?
Lakini kabla sijaendelea mbele na kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu nukta hii, ambayo ndicho kiini kikuu cha hoja yangu, tuipitie kwa pamoja kamusi ya A Standard Swahili-English Dictionary iliyotungwa na jopo liitwalo Inter-Territorial Language Committee for th East African Dependencies, chini ya mwongozo wa Fredrick Johnson na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1939. Katika ukurasa wa 408 wa kamusi hiyo iliyoandikwa na wasio Waislamu, neno SALA limeelezwa kama ifuatavyo: Prayer. The five prescribed hours of prayer of the Muhammadans are (1) alfajiri, at first signs of dawn; (2) adhuhuri, noon; (3) alasiri, afternoon; (4) magharibi, sunset; (5) isha or esha, about 8 p.m. Kisha ikaeleza pia maana ya kitendo (kitenzi) SALI kwa kuandika: (1) pray; (2) use the prescribed forms of Muhammadan prayer in public or private.
Ajabu ni kuwa, kinyume na ilivyo kwenye baadhi ya kamusi za sasa, ambazo zimetumia neno SWALA kwa vitu vitatu tofauti, ndani ya kamusi ya A Standard Swahili-English Dictionary neno hilo limetajwa mara moja tu na kwa maana ya kitu kimoja TU, ambacho ni jina la mnyama. Hii inanipa dhana kwamba, ubunifu wa SALA kuwa ya Wakristo na SWALA kuwa ya Waislamu, ni jambo jipya lililobuniwa na wataalamu wetu wa Kiswahili, kwa madhumuni ambayo, mimi ambaye si mtaalamu wa lugha, ninashindwa kuyafahamu. Labda niulize tena suali moja. Ikiwa mtu mathalani, anataka kumpa jina mtoto wake, akachagua jina lililompendeza kwa utamkaji wake tu, kama ilivyozoeleka sana siku hizi, lakini baada ya kuuliza kwa wajuzi maana yake, akaambiwa jina hilo lina maana tatu. Mbili ni maana ya sifa nzuri, lakini maana yake ya tatu inamaanisha kitu duni na kibaya, je mtu huyo atashikilia kumpa jina hilo mwanawe? Imani yangu kubwa ni kuwa la, hatofanya hivyo. Kama ni hivyo, kwa nini basi imeonekana si tatizo kuipa ibada ya Waislamu jina ambalo, lina maana nyingine mbili tofauti, ikiwemo ya aina ya mnyama, kwa hoja tu pengine ya kutaka kuwapatia Wakristo neno linalohusu ufanyaji ibada zao? Kama ndani ya kamusi ya mwaka 1939, hakukuwepo neno Swala isipokuwa la maana ya mnyama, na leo hii Swala imekuwa na maana ya ibada ya Waislamu, ina maana jina la mnyama Swala ni kongwe zaidi katika Kiswahili kuliko ibada hiyo ya Waislamu, na ibada SALA, ambayo sasa ni ya Wakristo, ni ya kale zaidi katika utamaduni wa Waswahili???!!!
Nitauliza tena suali jengine. Kama mantiki hiyo ni sahihi, kwamba kuongeza herufi ‘W’ TU, kwenye neno SALA kunapambanua ibada za dini mbili kinzani, na ikiwa kwa sasa Kitabu kitakatifu cha Waislamu kimeanza kuandikwa kwa sura ya Qur’ani, je itakuja kuwa sahihi katika siku za usoni kubuni neno KUR’ANI liwe na maana ya kitabu kitakatifu cha Wakristo badala ya Biblia? Yaani cha Waislamu TUKITAMKE QUR’ANI, cha Wakristo KUR’ANI, sawa kabisa na SALA na SWALA???! Au kama wao pia wana aina yoyote ya funga, yetu sisi ya Kiislamu iwe SWAUMU na yao wao SAUMU?
Sasa turejee kwenye aya ya 104 ya Suratul Baqarah ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقُولُوا رَاعِنَا وَقُولُوا انظُرْنَا وَاسْمَعُوا ۗ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ
Enyi mlio amini! Msiseme: “Raa’ina”, na semeni: “Ndhurna”. Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.
Almarhum Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani ameandika yafuatayo katika maelezo ya aya hii. “Enyi mlio amini! Tahadharini na hawa Mayahudi. Msimwambie Mtume pale anapo kusomeeni ufunuo: “Raa’ina” kwa kukusudia akuwekeni pahala pa uangalizi wake, yaani (Tuchunge, Turai), na akupeni muda katika kusoma kwake mpaka mzingatie na mhifadhi. Kwani watu makhabithi miongoni mwa Mayahudi husaidiana kutaka kukuigeni na kupindua ndimi zao kwa neno hilo mpaka likawa neno la matusi wanalo lijua wao. (1) Na wao humkabili Mtume kwa neno hilo kwa kumfanyia maskhara. Lakini nyinyi tumieni neno jingine wasilo weza Mayahudi kulipatia njia ya kufanya ukhabithi wao na maskhara yao. Tumieni neno: “Ndhurna” yaani “Tuangalie”. Na sikilizeni vyema anayo kusomeeni Mtume. Na Mwenyezi Mungu anawadundulizia adhabu kali kwa Siku ya Kiyama hawa wanao mfanyia maskhara Mtume.
Katika lugha ya Kiyahudi ya Kiebrania lipo neno “Rai’nu” ambalo limejengwa na neno “Ra'” kwa maana ya “Shari” na neno “nu” linaonesha jamii, wingi. Na maana ya neno lote ni kuwa “Wewe ni shari yetu”, wakikusudia kumwambia Mtume hayo.
Almaruhm Sheikh Abdulla Saleh Al-Farsy, yeye ameandika maelezo yafuatayo chini ya tarjumi ya aya hiyo:
Waislamu walikuwa wakati mwingine wakimwambia Mtume”Raainaa” (Yaani kuwa ukituchunga kama mchungaji mzuri anavyowachunga wanyama wake, kwani sisi ni wajinga, hatujui la madhara wala la maslaha).
Na tamko hili linashabihi tamko la Kiyahudi, ambalo maana yake ni “Wewe mjinga mpotofu!”
Basi Mayahudi wakaona wamepata njia nzuri ya kumtukana Mtume kipunjo pasina mwenyewe kujua wala watu wake kutambua. Ikawa wakifika barazani kwa Mtume hukithirisha kumwambia Mtume ‘Raainaa’; na wanakusudia maana ya ‘Wewe mjinga mpotofu!’
Mwenyezi Mungu akakataza kutumiwa hilo tamko la Raainaa katika kumsemeza Mtume, watumie tamko jengine lenye maana ile ile. Nalo ni ‘Ndhurnaa;’ na maana yake ni ile ile ya kuwa “Tutazame kama mchungaji mwema anavyotazama wanyama wake.”
Wakaikosa Mayahudi fursa hii ya kumtukana Mtume kipunjo mbele ya macho yake na mbele ya watu wake.
Kwa uono wangu finyu, ninalichukulia tukio hili lililotokea katika historia ya Uislamu na kuzungumziwa ndani ya Qur’ani kama ilhamu na funzo muhimu kwa Waislamu la kuwataka wachunge utumiaji wa maneno na majina yao ya kidini katika lugha zao, ili wasije wakawapa mwanya wowote maadui wa kutumia majina yenye UTAMKAJI MMOJA NA MAANA TOFAUTI kuikejeli dini yao, kama walivyowahi Mayahudi kumfanyia Bwana Mtume Muhammad SAW. Na kwa kweli nikiri kwamba, aya hiyo ndiyo iliyonishajiisha kuandika maelezo haya kuhusu utumiaji uliokithiri wa neno SWALA, na ambao unafanywa zaidi na Waislamu wenyewe, ili labda kuonyesha kuwa, kufanya hivyo kunalipa neno hilo hali ya Kiarabu zaidi!
Sote tunajua kama, tutake tusitake, Kiarabu, na kwa mkazo zaidi Uislamu, una taathira kubwa katika lugha na utamaduni wa Kiswahili. Lakini leo hii tunashuhudia jinsi athari hizo zinavyofutwa, kupinduliwa na kupotoshwa hatua kwa hatua, iwe ni kwa makusudi au bila ya kukusudia. Kuna mifano kadhaa ya jambo hili, lakini hapa nitaitaja michache.
Katika kamusi karibu zote za Kiswahili, neno HIJA limeelezwa kuwa ni: Ibada ya Muislamu anayoifanya mara moja katika umri wake huko Makka mwezi wa Mfunguo Tatu. Na HIJI: Kitendo cha kutekeleza ibada ya Hija (Kamusi la Kiswahili Fasaha; uk: 116). Lakini leo tunasikia katika baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kuwa, katika dini yao, Wahindu, nao pia huwa wanakwenda kuhiji! Je haitakuja kufika siku ikaamuliwa H’ija inayotamkwa kwa HAA ya baada ya JIIM katika alfabeti za Kiarabu kuwa ibada ya Waislamu, na wasio Waislamu wachukue neno Hija??!!
MSAHAFU: Kamusi hilohilo la Kiswahili Fasaha limeeleza maana ya neno hilo kuwa ni: Kitabu kitukufu cha Kur-ani. Kamusi ya Kiswahili Sanifu imefafanua zaidi kwa kuandika: Kitabu kitakatifu cha Waislamu, kilichokusanya juzuu thalathini za Kurani; mkusanyiko wa sura mia na kumi na nne za Kurani. Lakini leo limekuwa jambo la kawaida kusikia ikisemwa: Kur-ani ni msahafu wa Waislamu, na Biblia ni msahafu wa Wakristo!
KIDOLE CHA SHAHADA: Inajulikana tokea asili na jadi kuwa, katika Kiswahili, kidole cha baada ya kidole cha gumba cha mkono, kinaitwa kidole cha shahada; na sababu ya kuitwa hivyo inajulikana kuwa ni suala la itikadi ya Kiislamu la tamko analotoa mtu anayesilimu. Lakini leo tuanasoma kwenye vitabu vya lugha jina jingine jipya la kidole cha PILI! Utadhani majina ya vidole vyote vya mkono ni cha kwanza, cha pili, cha tatu, cha nne na cha tano!!
HITIMISHO
Kama nilivyotangulia kueleza kwenye utangulizi wa andiko hili, mapenzi ya dini yangu ya Uislamu na lugha yangu ya Kiswahili, ndivyo vilivyonipa msukumo wa kuandika haya niliyoandika, japokuwa ni kwa tabu na mashaka makubwa, kwa kuwa si mtaalamu wa Kiswahili wala sina mazoea ya kuandika. Ninamwomba msomaji, hasa aliye mtaalamu wa lugha, ajikite zaidi kuyahakiki madhumuni ya makala yenyewe, kuliko udhaifu uliomo katika uandishi, ambao najua una kasoro na mapungufu mengi kitaalamu. Inshallah niwe nimeweza kufikisha yale niliyoyakusudia.
Kwa kumalizia ninatoa ushauri kwa wataalamu wetu wa lugha na watungaji wa kamusi ya Kiswahili, kama upo uwezekano wa kufanya marekebisho, walirejeshe neno la asili la ibada na nguzo ya pili ya Uislamu yaani SALA ambalo lina hali maana moja pekee kiuandishi; na neno SWALA libakie kutumika kwa maana yake pia ya asili ya jina la ‘mnyama’. Kwa upande wa Wakristo, wao wabuniwe jina jengine litakalofikisha maana ya ibada zao, kama ni maombi, dua, misa… au hata kama hapana budi, watumie hilo neno SWALA ambalo utumikaji wake katika maana ya ibada katika Kiswahili ni mpya.
إِنْ أُرِيدُ إِلَّا الْإِصْلَاحَ مَا اسْتَطَعْتُ ۚ وَمَا تَوْفِيقِي إِلَّا بِاللَّـهِ ۚ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ
Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyo weza. Na sipati kuwezeshwa haya ila na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye naelekea. (Surat Hud aya ya 88)
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Abdulfatah Mussa Iddi, ni mwandishi wa habari na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Tehran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.