UCHAMBUZI

Taazia: Kwaheri Maalim Suleiman Shkeli wa Pandani

Mauti ewe mauti, ukija kama hujaja
Huwa waja katikati, ya maisha yetu waja
Katikati ya wakati, na kati ya zetu haja
Na hata tukikutaja, wewe khabari hupati

Nimepokea habari ya Kaka yangu, Mzee wangu, Muhisani wangu, Sheikh Sulaiman Al Shukaili, kuitikia wito wa Aitaye akalazimika kuitikwa. Asubuhi hii karudi kwa Mola wake. Allah Ampokee ilhali keshamsamehe makosa yake na aifanye pepo iwe nyumba yake. Amin Yaa Rabb.

Mtoto wake, Immu Shkellý, (mtoto wa ndugu yake Nassor Ali Salim Al Shukaili – Bondia) alinitumia picha hii hapa akaniuliza ikiwa nimepata habari ya msiba. Nikamuuliza wa nani, akaniambia wa huyo uliyenaye pichani. Zaidi ya dakika 40 baadaye, nami nikawa najiona siamini.

Kwa hakika, Oman imeondokewa, lakini imeondokewa pia Zanzibar. Imeondokewa Pandani, ambako anajulikana kama Maalim Suleiman Shkeli. Hadithi yake ya maisha yaliyokuja kuwa ya rubani na mwanaanga wa Oman mwenye mafanikio makubwa ilianzia kijiji hiki ambacho mimi pia ninatokea.

Taswira ya kijiji hiki, hata harufu ya udongo wake, ninaamini ameondoka nayo kwenda nayo kwa Muumba wake. Alikuwa kila mara ananisimulia maisha yake ya huko, na hata alipokuwa akirudi kwa likizo kuwasalimia wazee, ndugu na jamaa, alikuwa akinisimulia anavyoumizwa na hali duni ya maisha.

Kila wakati, licha ya kuwa kwake mtu mwenye mafanikio makubwa kwa kila hali nchini Oman, roho yake iliishi Pandani. Mule mule mikarafuuni, minazini, miembeni, mifuuni, mibungoni, na alikuwa haoni tabu kukiri hivyo. Huyu ni mtu aliyeathirika sana na kulikozikwa kitovu chake.

Ni Pandani ndiko alikoanza kazi ya ualimu wakati mimi ndio kwanza nazaliwa, na baadaye akahajiri kuenda Oman, ambako alisomea urubani na kupanda cheo hadi kuwa mmoja wa marubani wa ndege za Mfalme Qaboos bin Said Al Said. Akastaafu kwa heshima zote za kijeshi kama mwanaanga bingwa na mtaalamu. Kisha akaendelea na shughuli zake za maisha. Ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuwa mkulima, kazi aliyoiinukia kwenye mabonde ya Msaani na Kijipu na Bibi Wa Tele.

Alinisimulia haya yote wakati nilipokutana naye mwaka jana miezi kama hii nyumbani kwake, alikonialika rasmi.

Ukiangalia masafa baina yangu na yeye, unaweza kudhani kuwa palikuwa na ukuta mkubwa baina yetu. Kwa vyovyote, mimi nilikuwa mdogo sana kwake kwa kila jambo – umri, elimu, uzoefu, uwezo, haiba, na yote mengine. Mimi nilikulia na kucheza na ndugu zake wawili wa mwisho – Hafidh na Ahmed.

Lakini masafa haya hayakuwa kitu kwake. Alikuwa mtu wa kujishusha sana sana. Tangu aliponifahamu kupitia hapa ukurasa wa Facebook, basi alinikurubisha kwake kwa hali na mali, kwa mawaidha na nasaha, na hata kwa matani pia, kama vile tuko rika moja.

Alinialika mara kadhaa kwenda Oman kumtembelea, nami nikawa sijapata wasaa, hadi mwaka jana nilipopata nafasi ya kwenda kuwasilisha mada kuhusu Mchango wa Waomani kwenye Fasihi ya Kiswahili, naye alipofahamu kuwa ningelikuwa na safari ya huko, akaniambia kuwa nisingeruhusiwa kuondoka bila kufika kwake. Na ikawa hivyo, akanialika kwanza kwenye klabu yao ya wanajeshi wa anga kwa chakula cha usiku, lakini akaona haitoshi. Siku nyengine akanialika nyumbani kwake mchana mzima.

Nakumbuka takrima kubwa aliyonikirimu mimi na familia yangu. Hata baada ya kurudi hapa Ujerumani, tukaendelea kuwasiliana. Mara ya mwisho ikiwa ni siku tatu nyuma, ambapo alinijulisha kupitia kwa swahibu yetu wa pamoja kuwa angekuwa na safari ya China. Na ni China, ambako roho yake asubuhi hii imetenganishwa na kiwiliwili, akirudi kwa Mola wake.

Nimeanza andiko hili kwa ushairi. Ni kwa kuwa Maalim Suleiman alikuwa shabiki mkubwa wa ushairi. Vitabu vyangu vyote vya ushairi aliviagizia na nilipokwenda Oman nikamkuta tayari anavyo. Wakati mwengine alikuwa akiniandikia ujumbe kwa kutumia beti zangu mwenyewe, au kujibizana nami kwa beti za kishairi. Kwa hivyo, kadiri ya alivyokuwa Muomani na Mwarabu, huyu pia alikuwa Mswahili na Mzanzibari. Na utambulisho huu ulikuwa umemganda nyama na mfupa.

Ubeti huu nimaliziao hatausoma, kitabu changu kijacho, Mfalme Yuko Uchi hatakipata, lakini wacha kauli yangu hii kwake ibakie:

Kake Selemani, moyo wanipwita
Kun’kwenda Sini, tiba kutafuta
Na kumbe Manani, ndiyo akikwita
Nawe kushamuitika!

Kwa idhini yake Allah, awe amekuridhia amali zake zote za kheri, na akuweke kwenye kundi la waja wake wema peponi!

Innalillah wainna ilayhir raajiun!

Mohammed Ghassani
12 Aprili 2018
Bonn, Ujerumani

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.