Ikiwa ni vigumu kusema kwa kinywa kipana ushairi ni nini, si vigumu kamwe kulitambua shairi zuri ni lipi. Mara unapolikabli (au tuseme linapokukabili), hukuvaa kwa nguvu za ajabu na kukupenya kwa hisia ya raha isiyoweza kuelezeka.
Au bora tuseme hukuchukua na kukugandisha kwenye kurasa hata usiwe na nafasi ya kutoka nje ya ulingo wake – na hayo yote kwa maneno machache tu ushairi unayotumia.
Huu mimi nauita uchawi wa ushairi – mgumu kufafanulika na adimu kupatikana katika fani nyingine za maandishi – uchawi ambao mara uliniteka nilipokuwa nikiyapitia mashairi ya chipukizi huyu.

Kwa mshairi wa aina hii, hakuna kabisa wazo wala fikra kongwe. Tungo zake huanza kwa ‘fikra’ ipevukiayo akilini na kumwagikia karatasini. Na hii iwe fikra yoyote, ikiwa kongwe, anaweza kwa uchawi wake, kuigeuza mpya. Tazama kwa mfano, mshairi huyu anavyoipa upya fikra kongwe ya ‘kurudi nyumbani’ (Uk. 7):
Tarudi
Acheni kulia, kujipa machungu
Kuwa mwaumia, ni dhahiri kwangu
Ila namwambia, kila al’o wangu
Akivumilia, ni furaha yangu
Mwisho tarudia, kitovuni pangu
Tarudi!
Hili si tamko tu la ‘kurudi’, bali pia ni ishara ya maumivu pande mbili. Ni kilio cha kote kuwili; kwa walioondokewa na kwa aliyeondoka. Ndani ya maumivu na kilio hiki cha pande mbili, mnazuka mambo mawili – ‘mapenzi’ makubwa na ‘mwanya mpana wa utengano’. Masuala yasiyotamkwa na ambayo yamejificha ndani ya mbavu za “acheni kulia kujipa machungu” bila shaka kwa aliye ugenini, ni “lini nitakuwa nao tena?” Na kwa walio nyumbani “lini tutakuwa naye tena?”
Kwa hakika hili ni suala moja lenye maelekeo mawili; suala moja lenye mizani sawa katika kusakarika kwa hamu na ukiwa wa kutengana. Shida kubwa inayojitokeza imo katika ile kauli ‘mwisho tarudia kitovuni pangu’. Shida ni mwisho ni upi? Mpaka lini utaendelea utengano? Mpaka lini litaendelea vumilio? Mpaka lini kitovu kitangojea kurutubishwa?
Shairi hili bila ya shaka linavuka ulingo wake na kwenda mbele kupita mipaka ya kibinafsi. Ni shairi linalozungumzia vuta n’kuvute ya ‘mhajiri’ yeyote yule, pahala popote pale, wakati wowote ule. Mhajiri ambaye nyuma ameacha pande zima la uyeye; uzazi wake, malezi yake, michezo yake, masomo yake, tarihi yake, wazee, ndugu, jamaa, rafiki na uzowefu wa mazingira yake. Kila akiamka asubuhi na kutazama mbele anakuta kumetanda wingu la balaa kule anakokuita “kitovuni pake”- afanye nini? Kila siku anataka kurudi, lakini kila siku kuna kughairi kwa sababu kitovuni hakurudiki. Tazama namna gani mshairi hodari anavyoichukua mada ndogo na kuifinyanga upya kutoa michirizi na milizamu ya tafakuri kwa msomaji. Hili ndilo ninaloliita mimi shairi – liwe lina vina na mizani au linatiririka huru tu.
Inahitaji sifa nyingi kwa mshairi kuweza kumteka msomaji namna hii! Kwanza, anahitaji kuwa na ukwasi wa lugha, na Ali Abdulla Ali anao wa kumiminika. Pili, ni jinsi mshairi anavyojua kuyatumia maneno yanavyostahiki mwahala mwake – katika miktadha ambayo msomaji angeungama kwamba yasingeliweza kutumika bora pahala pengine popote.
Tuchukue mfano mmoja wa shairi la Unayempenda (Uk. 2) ambamo Ali Abdulla Ali anaonyesha yote mawili: ukwasi wa lugha na namna anavyojua kuyatumia maneno kwenye miktadha maneno hayo yanamostahiki. Hebu tutulizie jicho maneno yaliyomo kwenye yombo:
Unayempenda
Mtu unayempenda, kwa dhati uliyonayo
Akakufanyia inda, karaha na jaka moyo
Huzidi ila kukonda, na kusumbua rohoyo
‘Sitangamane na huyo!Lau kumwacha waweza, wamng’ang’ania nini?
Lolote lile fanyiza, umkopoe moyoni
Mtu aliyekutweza, wewe ukashindwe kwani?
Dawaye mfanye duni!
Maneno gani mengine yanayosisitiza kina cha mapenzi kuliko maneno dhati uliyonayo? Ni maneno yanayochora upeo wa mapenzi kwa mtu. Lakini mara kadha mapenzi kama haya hayajibiwi hata chembe ya mapenzi ila inda; na si inda tu, bali karaha ya mambo na jaka la moyo. Hili likitokezea, mtu huzidi kukonda na kusumbua roho yake. Afikapo hapo mtu katika maweko ya mapenzi, ni ujinga kubaki mapenzini. Ni ujinga ambao mwandishi anatuonya nao anapotuuliza wamng’ang’ania nini? Na kutuhimiza tufanye lolote ili tumkopoe tumpendaye moyoni ili kuepukana na matwezo yake. Ndani ya mbavu ya maneno aliyoyateua mshairi tunaonyeshwa si mapenzi tu, bali idhilali na ujuha wa mapenzi, unaomtia huruma mshairi na kumfanya atuchochee kufanya kitu.
Sifa nyingine ni ile ya kuyagonga upya maneno ili kuyapa mng’aro mpya kiumbo, kiujumi na kimaana – mfano umo katika shairi Damu si Namna Moja, ambamo neno aenende limegongwa upya kiumbo na kiujumi kwani linasikika upya kuliko tulivyolizowea katika umbo alienda. Neno damu limechukua maana mpya katika mjazo wa kauli damu si namna moja na katika hadi kwenye damu yake ambamo limechukua maana mpya: ya watu katika damu si namna moja na ndugu katika hadi kwenye damu yake.
Mshairi huyu pia anatumia ile sifa muhimu ya ushairi ya kutumia maneno machache kufumbata dhana pana. Tazama katika shairi la Moyo wa Kupenda (Uk. 18), jinsi dhana ya mapenzi inavyogeuzwa kuchukia kwa maneno machache tu katika ubeti mmoja:
Moyo wa Kupenda
‘Mependa mwenyewe, hukulazimishwa
Sio mwenginewe, wengi ‘meonyeshwa
Cha nini kiwewe, au umechoshwa?
Kumbe,
Moyo wa kupenda, na kuwiza huwa?
Ndani ya maneno haya machache kuna hadithi ya mapenzi ya hiari yaliyoanza mbali, kwa tunu na tamasha, kwa kulilia na kusisitiza na kuishia kero, uchofu na chuki – jambo linalomshangaza mshairi: kumbe, moyo wa kupenda na kuwiza huwa? Yote haya hayasemwi, bali yanaashiriwa kwa maneno machache ya ubeti huu.
Sifa ya mwisho ni ile ya miundo na maumbo tofauti ya mashairi haya – kiubeti na mistari yake, kimistari na migawiko yake, kimizani (8:8, 4:8, 3:8, 6:6 n.k), kivina, kiarudhi na kimtiririko huru. Hii naiita sifa kwa sababu kutunga mashairi katika maumbo na miundo mbalimbali kunamwepushia msomaji kuchoshwa na mashairi yenye maudhui yanayojirejea hayo kwa hayo au maumbo na miundo inayorudiwarudiwa katika diwani nzima.
Mchanganyisho wa mashairi ya kawaida ya vina na mizani na yale yanayoitwa huru kama yanavyojitokeza katika diwani hii, unafanana na mchanganyisho wa diwani ya Jicho la Ndani ya Said A. Mohamed, ambamo mshairi huyo anabainisha wazi kwamba maana ya ushairi ni kubwa zaidi kuliko vina na mizani.
Katika diwani hii pia Ali Abdulla Ali kama Said A. Mohamed anazungumzia maana ya ushairi katika tungo zake. Kusema kweli, mshairi anaanza kwa kuuliza swali: Upi kwako ushairi, au nauwe uwao? Jibu la swali hili linapatikana katika utungo wake huohuo:
Kwangu kila ushairi, wanipendeza yakini
Kwani una kubwa siri, kueleza kwa undani
Ukasaza na athari, licha kuvuta makini (Uk. 59)
Kauli hii inaelekea kukubali kwamba aina zote mbili za mashairi ni ushairi mradi tu zikiwa zinatimiza sifa za ushairi … Kwani una kubwa siri, kueleza kwa undani … Ukasaza na athari, licha kuvuta makini … Lakini hatosheki na kufumba, mwisho anahalalisha fani zote mbili ikiwa zinakidhi masharti:
Ama wa kimapokeo, wenye utamu wa fani
Kwa beti ujigawao, taswira kusheheni
Ni wengi wausifuo, huimba na kuughaniNa wanamaendeleo, kwa nini si washairi?
Sheria za mapokeo, japo haziwaathiri
Ni nzito tungo zao, si jambo baya kukiri
Kama anwani ya diwani inavyoelekeza, kuna mashairi kadha ya Kilio cha Usumbufu (Uk. 61) ndani yake: Wastara (Uk. 1), Damu si Namna Moja (Uk. 1), Kitu N’nachokipenda (Uk. 1), Unayempenda (Uk. 2), Utengano (Uk. 2), Kilio (Uk. 4), Tarudi (Uk. 7), n.k.
Mbali na mashairi ya kilio mna mashairi ya mapenzi na mambo ya kidunia ndani ya diwani hii: Ua la Moyoni (Uk. 12), Pendo Letu (Uk. 13), Muhibu Wangu (Uk. 16), Ua (Uk. 16), Amani Tunda la Haki (Uk. 23), Radhi ya Mama (Uk. 24), Sigara (Uk. 25), Hasidi (Uk. 26), Asali (Uk. 27), n.k.
Kupata nakala yako ya diwani hii, tafadhali bonyeza hapa.
1 thought on “Kilio cha Usumbufu: Diwani mpya ya Kiswahili inayoangazia majanga ya kijamii”