UCHAMBUZI

Mayatima na wajane wa kisiasa hadi lini Zanzibar?

Ali Juma Suleiman alivamiwa na kikosi kikubwa cha watu usiku wa tarehe 26 Septemba mwaka huu nyumbani kwake Mtoni, Unguja. Mke wake, Bi Rehema Nassor Juma, anasema alishuhudia askari wenye sare za vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wakiwa na mitutu ya bunduki, marungu na mapanga.

Watoto wake wanasema askari hao walikuwa na magari matatu na kuzunguka eneo lote la nyumba yao na za majirani zao usiku huo ukaribiao saa sita.

Ali Juma alipigwa ndani ya nyumba yake, kisha akatiwa pingu kwa nyuma na kufungwa kitambaa cha macho, kabla ya kutupwa kwenye gari, ambalo mwenyewe aliwasikia watekaji wake wakizungumzia habari za Masingini.

Masingini ni eneo lisilo mbali sana na kitovu cha mji mkuu wa Zanzibar, upande wa magharibi muelekeo wa kaskazini mashariki. Huko kuna msitu mkubwa.

Na Mohammed Ghassani

Aliposhushwa hapo, alipigwa na watekaji wake kwa vyuma na vitu vyenye ncha kali, ambavyo vilimpasua misuli ya miguu yote miwili, miongoni mwa majeraha na maumivu mengine mengi.

Watekaji hao walikuwa wakimpiga huku wakimuambia wanamtia adabu kwa kuwa anataka “kuipindua serikali”. Walimshushia kipigo kwa muda mrefu mpaka waliporidhika kuwa kwa namna alivyo, basi asingeliinuka tena.

Walihakikisha amepoteza damu nyingi sana na kwa mahala walipomuwacha – katikati ya msitu na usiku huo mkubwa – waliamini asingeliweza kupata msaada wowote hadi tone lake la mwisho la damu lingekauka mwilini na huo ukawa mwisho wake.

Lakini kumbe siku yake ya kuondoka duniani, Allah hakuwa ameiandika iwe Jumanne hiyo, wala malaika wa mauti hakuwa ametumwa kuitwaa roho ya Ali Juma katikati ya msitu wa Masingini.

Badala yake, Mungu alimpa nguvu za kujikongoja hadi kijiji cha karibu na msitu huo, ambako baada ya jitihada kubwa na kwanza kukataliwa msaada na wenyeji yumkini kwa woga wao, wakatokea vijana wawili kumsaidia. Ni hao walioiwezesha hadithi ya Ali Juma kuja juu, ikasimuliwa na kusikika duniani kote.

Ali Juma akiwa hospitalini Mnazi Mmoja, siku moja baada ya kifo chake.

Masaa 48 baadaye, usiku wa Alhamis kuamkia Ijumaa, Ali Juma alihitajiwa kwa Mola wake akiwa Hospitali Kuu Mnazi Mmoja. Wino ukakauka na daftari la uhai wake likawa limefungwa hapo. Innalillahi wainna ilayhir raajiun!

Hata hivyo, kitabu cha hadithi ya Ali Juma kwetu walimwengu hakikufungwa hadi pale mwenyewe alipopata fursa ya kuandika sehemu ya mwisho ya riwaya yake.

Akiwa kitandani hospitalini siku ya Jumatano, aliweza kuyasimulia masaibu yote yaliyomkumba ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita. Neno kwa neno. Tukio kwa tukio. Kama vile mkanda wa sinema, shahidi huyu alipata upumzi wa kuelezea kila kitu. Hadi saa na dakika.

Na yote aliyoyasema yakaja baadaye kuthibitishwa na watu waliomzunguka na walioshuhudia sehemu ya mwanzo na ya mwisho ya jaala yake – yaani pale alipochukuliwa na yaliyojiri wakati huo na baada ya kupatikana na kilichotokea kwenye hatua za awali za matibabu. Ya katikati yake, hapana shaka, wanayo waliomkamata na kumtesa kwenye msitu wa Masingini na Mungu wao.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Ali Juma kufuatwa nyumbani kwake na watu hawa hawa wanaoaminika kuwa wanatoka vikosi vya SMZ wakisaidiwa na vyombo vyengine vya dola. Ndio maana hata alipowaona waliokuja mara hii wakiwa na mitutu na namna walivyojipanga, aliwaambia mkewe na wanawe: “Buriani. Safari hii sirudi salama!”

Mke wake, Bi Rehema, anasema hii ilikuwa mara ya nne kufuatwa na kupigwa mumewe. Hana imani kabisa na serikali, kwani anaamini ndiyo inayohusika moja kwa moja na mauaji ya mumewe. “Hakuna raia mwenye bunduki, wala bastola, wala pingu. Ni hao hao. Walikuwa wamevaa sare za vikosi vya serikali. Dhuluma kubwa imepita. Mume wangu kadhulumiwa!”

Kauli ya kudhulumiwa inatolewa pia na Seif Ali, mtoto wa Marehemu Ali Juma, ambaye anasema hana shaka na hilo, ingawa haongezi kitu zaidi ya kumuombea mzazi wake asamehewe makosa yake na Mungu amuweke peponi!

Lisilo shaka ni kuwa Ali Juma hakufa kifo cha kawaida. Aliuawa. Na sababu ya kuuawa ni msimamo wake wa kisiasa. Nje ya nyumba yake, huyu alikuwa mwanasiasa wa upinzani, akiwa mwanachama na muanzilishi wa Chama cha Wananchi (CUF) tangu kilipoasisiwa mwaka 1992.

Nusu nzima ya umri wake wa miaka 50, Ali Juma aliitumia akikitumikia chama chake hicho kwenye ngazi mbalimbali, kuanzia za chini kabisa huko matawini hadi juu kabisa kwenye vikao vya kitaifa. Umri wake umekatishwa wakati akiwa mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama chake katika Wilaya ya Magharibi ‘A’.

Hadithi ya Ali Juma ni moja tu kati ya hadithi nyingi za aina hii tangu Zanzibar irudi tena kwenye mfumo wa vyama vingi. Bahati mbaya ni kuwa hadithi zote za aina hii zinasimuliwa kutoka upande mmoja wa kisiasa – upinzani.

Miguu ya Ali Juma iliyovunjwavunjwa na watekaji.

Kama kuna kitu ambacho uongozi wa CUF ni mahodari kwacho, basi ni uwezo wake wa kuwajengea wanachama wake uvumilivu wa kuachiwa mayatima, vizuka na vilema. Yalianza na Shumba ya Mjini, Micheweni, ambako siku bendera inapandishwa mlingotini kwa mara ya kwanza wilayani humo mwaka 1992, iliondoka na roho ya mwanachama wao, mwenye jina kama hili la Ali Juma.

Kuanzia hapo, ikawa mitutu ya dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshaonja damu ya wana-CUF na haiwezi tena kuiacha. Ndani ya nusu karne hii ya vyama vingi, idadi ya maiti zilizozikwa kwa jina la siasa upande wa CUF zinapindukia 100, waliowekwa vilema ni maelfu na waliowachwa vizuka na mayatima hawana idadi.

Takribani kila familia ya mwana-CUF ina mtu wake ambaye amekuwa muhanga wa vyombo rasmi na visivyo rasmi vya dola. Kama inakosa aliyeuawa moja kwa moja, itakuwa na aliyejeruhiwa. Kama imekosa majeruhi, itakuwa na aliyefukuzwa kazi, kuvunjiwa nyumba au kukoseshwa fursa za kimaisha na kimasomo kwa sababu ya msimamo wao wa kisiasa.

Juu ya yote, kuna malaki ya wengine wanaotembea na majeraha ya rohoni mwao – hayaonekani, lakini yapo ndani kabisa ya miili yao na yanauma kila uchao. Majeraha, majonzi na machozi ndiyo gharama halisi inayolipwa na wale wenye maoni tafauti ya kisiasa na watawala visiwani Zanzibar.

Na katikati ya makovu haya, CUF imejaaliwa kuwa na uongozi ambao unaamini kwenye subira na busara. Unaamini kwenye kuwapa matumaini wanachama na wafuasi wake kuwa haya yote ni mambo ya kupita. Kwamba Zanzibar haitajengwa kwa siasa za kutoana macho na kung’oana meno, bali za Maridhiano na Umoja wa Kitaifa.

Bahati mbaya ni kuwa kadiri uongozi huo unavyojikita kwenye kutaka kuitakasa mikono yao isije ikachirizika damu za Wazanzibari, ndivyo wapinzani wao, ambao ndio watawala, wanavyoona fursa ya kuwasukuma ukutani zaidi na zaidi, hadi sasa wameshawachupisha upande mwengine kabisa, ambako hawawezi kujitetea wala kushambulia.

Swali kubwa ambalo kifo hiki cha karibuni kabisa, miongoni mwa roho nyengine nyingi zilizolazimishwa kuhama kabla ya wakati, kinatuachia ni ikiwa hadi lini Zanzibar itaendelea kuangamiza watu wake na kuwaacha watoto mayatima na wake vizuka? Hadi lini siasa zetu zitaendelea na kusinzwa kwa damu ya watu wetu?

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.