UCHAMBUZI

Uhuru Kenyatta: Mtu mzima akivuliwa nguo, huchutama 

 Ni bahati mbaya sana kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kuwa majaji wa Mahakama ya Juu wameamua kuufuta ushindi wa asilimia 54 aliotangaziwa na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwenye uchaguzi wa Agosti 8 wakisema haukuwa halali na kwamba uchaguzi mpya lazima ufanyike ndani ya siku 60 kuanzia tarehe 1 Septemba 2017.

Bahati mbaya zaidi kwake ni kwamba sasa anaanza kuacha njia safi aliyokuwa akitembea na anaingia machakani. Onyo la mapema kwake ni kuwa huko maguguni anakojitia, atakuja kukujutia katika wakati ambao atakuwa ameshachelewa, maana majuto ni mjukuu, daima huja mwishoni.

Awali alikuwa ameanza kubebeshwa sifa za kuwa “Baba wa Demokrasia barani Afrika” kwa kauli zake za awali za kuunga mkono maandamano ya wapinzani waliokuwa hawakuridhishwa na ‘ushindi’ huo na baadaye hata kusema angeliuheshimu uamuzi wa Mahakama ya Juu kuufuta ushindi wake ingawa hakuridhika nao.

Lakini masaa machache baada kuhutubia taifa akiwa Ikulu ya Nairobi akiwa amesisitiza umoja, udugu na amani ya Wakenya, Rais Kenyatta akaelekea mitaani na huko ndiko alikoanza kuonesha rangi tafauti na ile aliyokuwa kajipakaza mwanzo.

Na Mohammed Ghassani

Kwenye mitaa ya Nairobi na Nakuru, Rais Kenyatta alizungumza lugha ya kibabe, lugha ya kupotosha na kupotoka na, baya kuliko yote, lugha ya kutisha na kuchonganisha.

Anawaita majaji wa Mahakama ya Juu kuwa ni “wakora”, neno la Kiswahili cha Kenya linalomaanisha watu wakorofi wasiokuwa na maana.

Anamtisha Jaji Mkuu David Maranga kwamba asijidhani akishavaa joho la ujaji anakuwa na nguvu ya kuogopwa.

Anajilabu kuwa akina Jaji Maranga wanapaswa kujuwa kuwa kwa uamuzi wao huo, sasa yeye, Uhuru Kenyatta, ni rais aliyepo madarakani na si rais anayesubiri kuapishwa tena.

Anauita uamuzi wa Mahakama hiyo ya Juu kuwa ni kauli ya watu wanne watano wasiochaguliwa wanaokiuka matakwa ya Wakenya milioni 15 waliompigia yeye kura.

Zaidi ya yote, anaitishia idara nzima ya mahakama kwamba ina tatizo na ambalo wakimaliza uchaguzi ulioitishwa atalishughulikia. Tatizo ni kutoa uamuzi wa kufuta ushindi wake wa Agosti 8, uliokuwa na utata.

Kwenye hotuba yake mbele ya magavana wa chama chake cha Jubilee, Kenyatta anafikia umbali wa kumtisha Jaji Maranga kwamba asithubutu kuingilia majukumu ya IEBC, licha ya kuwa mahakama ina wajibu wa kusikiliza hoja za wale wanaoamini kuwa Tume hiyo imepoteza uaminifu wake mbele ya umma.

Sasa hapa Kenyatta lazima aambiwe naye aambilike kuwa amefika mbali. Muelekeo aliokuwa amechukuwa mwanzoni ulikuwa sahihi na ulimpatia heshima na sifa kutoka kwa kila mpenda amani, haki na demokrasia.

Ikiwa kweli ni muumini wa demokrasia na utawala wa sheria, kama ambavyo awali alitufanya tumuamini, kauli zake hizi za sasa zinamuweka mbali sana na sifa hizo.

Kwa kauli hizi za kibabe, sasa Kenyatta anajiweka kwenye kundi moja na watawala wenziwe wa Afrika Mashariki na Kati, akina Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunziza wa Burundi na John Magufuli wa Tanzania, ambao hupenda kujikweza juu ya mihimili yote ya utawala, wakiamini kuwa wao ndio mwanzo na mwisho.

Wengine hata wanahoji kuwa Kenyatta sasa anathibitisha rangi yake halisi – ya mtoto wa kitajiri aliyelelewa na kukulia Ikulu akidekezwa mno na wazazi wake kiasi cha kwamba haujuwi msamiati wa kukosa. Neno “sina” kwake yeye halimo kwenye kamusi. Ni mwana akipataye akitakacho kwa namna yoyote ile.

Gazeti la Daily Nation la tarehe 3 Septemba lilichapisha habari ya uchunguzi inayoonesha kuwa kumbe maafisa wa serikali na chama tawala cha Jubilee walikuwa wamejaribu, bila mafanikio, kuwafanya majaji watowe uamuzi ambao ungeibeba IEBC naye Kenyatta.

Hata kauli yake ya kuwaita majaji wa Mahakama ya Juu “wakora” inaakisi kuwa kiongozi huyo amekasirishwa kupita kiasi na kuona kuwa kanyimwa anachoamini ni chake peke yake, miliki yake.

Kauli hii pia imewakumbusha Wakenya na wanaofuatilia siasa za Kenya ile kauli ya baba yake, Marehemu Mzee Jomo Kenyatta, dhidi ya wapinzani wake, aliyekuwa akiwaita “vinyangarika!”

Hapana shaka, wanaomsema hivyo wanapuuzia ukweli kuwa huyu ni mpambanaji mwenye mbinu na mikakati yake, ambaye kukulia kwake Ikulu kulimpa wasaa wa kujinoa kisiasa.

Lakini, kwa vyovyote viwavyo, Uhuru Kenyatta ameteleza pakubwa na bahati mbaya kwake ni kuwa juu ya kichwa chake panatembea bango la kuwahi kutuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa jukumu lake katika machafuko ya mwaka 2007 yaliyoangamiza maisha ya Wakenya zaidi ya 1,000, kuwajeruhi kadhaa na maelfu ya wengine kugeuzwa wakimbizi wa ndani.

Ingawa mashitaka dhidi yake yalilazimika kufutwa na Mahakama hiyo, lakini si kwa kuwa waendesha mashitaka walishawishika kuwa Kenyatta hakuwa na kesi ya kujibu.

Mwezi Aprili mwaka huu wakati nikihudhuria mkutano wa utawala bora barani Afrika uliofanyika mjini Marrakesh, Morocco, nilimuuliza Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, juu ya kushindwa kwake kwenye kesi ya akina Uhuru Kenyatta, na jibu lake lilikuwa moja tu: “Hatukushindwa na kesi haikufungwa. Muda wowote hali ikiruhusu, tutairejesha mahakamani!”

Lau ni kiongozi wa mfano – kama ambavyo alianza kuchukuliwa na wengine, basi Kenyatta ana siku za kuyameza matapishi yake na kuomba radhi kwa Wakenya na Waafrika Mashariki wote waliomchukulia kuwa kigezo chema.

Kenya haimuhitaji Kenyatta asiyeihishimu Mahakama. Afrika Mashariki haina haja ya kuendeleza tawala za viongozi wasiopima athari za kauli na matendo yao.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mwelekeo la tarehe 5 Septemba 2017

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.