UCHAMBUZI

Funzo la uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya ni kuwa demokrasia hujengwa kutokea ndani, sio nje

Uamuzi wa tarehe 1 Septemba 2017 wa Mahakama ya Juu ya Kenya kuufuta uchaguzi uliompa ushindi rais aliye madarakani na kuamuru kurejewa upya, umezua maoni mengi na yanayofanana ndani na nje ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Miongoni mwa hayo yanayofanana ni kumwagiwa sifa kwa Jaji Mkuu David Maranga kwa kuamua kwa haki – kuna waliomfananisha na Mfalme Suleiman (amani ya Mungu iwe juu yake), ambaye anasifika kwa kuwa muamuzi muadilifu wa kesi za raia wake.

Mfanano pia ni kwenye hongera kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga na timu ya wanasheria wake kwa kupigania haki yao mahakamani – kuna waliomfananisha na Mtume Daud (amani ya Mungu iwe juu yake), ambaye alisimama imara dhidi ya jitu kubwa, Goliathi, na kuliangusha chini kwa teo.

Na bila kusahau, kuna mfanano wa maneno ya heshima aliyopewa Rais Uhuru Kenyatta kwa kuruhusu demokrasia na utawala wa sheria uchukuwe mkondo wake – kuna waliompachika jina la ‘Baba ya Demokrasia barani Afrika‘.

Sehem

Na Mohammed Ghassani

u nyengine ya maoni haya yanayofanana ni upande wa lawama na kunyoosheana vidole. Kwanza kwa maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) waliosababisha uchaguzi huo kuharibika na kufutwa, pili, kwa chama tawala cha Jubilee kwa kushawishi uharibifu huo na, tatu, kwa waangalizi wa ndani na nje walioubariki uharibifu huo, hata kabla ya kufanya utafiti wa kutosha.

Nitajizuwia kupita humo wanamopita wenzangu, kwenye sifa na lawama, na nitaelekeza mchango wangu kwenye funzo moja tu miongoni mwa mafunzo mengi muhimu ambayo mataifa ya Afrika Mashariki na Kati yanaweza kuchota kutokana na hatua hii yenye maana kubwa kwa eneo hili zima.

Kama kuna jambo moja muhimu kabisa la kukopa kutoka kwa Wakenya kwenye hili, basi ni la kutufanya tukubali kivitendo kwamba demokrasia na utawala wa sheria hujengwa kutokea ndani ya taifa husika, na wala sio kutokea nje yake.

Kilichomfanya Odinga na wenzake kutoka muungano wa upinzani (NASA) kukimbilia mitaani na mahakamani, si kigeni ndani ya eneo zima la mashariki, kati na kusini mwa Afrika.

Ni kile kile kilichojiri Burundi mwezi Julai 2015, Tanzania na Zanzibar mwezi Oktoba 2015, Uganda mwezi Februari 2016, Zambia mwezi Agosti 2016, Rwanda mwezi Agosti 2017, na ambacho kimekuwa hivyo hivyo kwa muda mrefu.

Ni ile hali ya watawala wameziteka nyara chaguzi zilizotakiwa ziwe za kidemokrasia na kuzitumilia kuwa kichaka cha kujitawalisha milele madarakani, hata pale ambapo wananchi wanawakataa.

Safari hii, Odinga aliamini ametendewa hayo hayo na wale aliowaita watotoaji wa “vifaranga vya kompyuta“. Mfumo wa matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8, alihoji, ulikuwa umechezewa tangu mapema kumnufaisha mpinzani wake mkuu, Rais Kenyatta.

Wakati anatoa madai hayo, tayari waangalizi wa uchaguzi huo kutoka taasisi zinazoheshimika duniani, kama ile ya Jimmy Carter ya Marekani, walishaupa sifa uchaguzi huo kuwa huru na wa haki.

Baya zaidi, waangalizi wengi sana wakaenda mbali zaidi kumtolea wito Odinga ayatambuwe matokeo hayo na kama ana la ziada basi aende mahakamani, ingawa wenyewe wakijiaminisha kuwa Odinga hakuwa na kesi madhubuti ya kuwakilisha, maana uchunguzi wao ulikuwa unaonesha kila jambo liko sawa.

Kama Odinga angewasikiliza akina John Kerry wa Carter Center, basi leo hii Waafrika Mashariki wanaofurahikia uamuzi huu wa Mahakama ya Juu ya Kenya, wasingelikuwa na cha kufurahia, na badala yake msiba ule ule kwa demokrasia ya eneo hili ungelikuwa umejirejea.

Na haikuwa mara ya kwanza kwa Odinga kuamini uchaguzi ‘umechakachukuliwa‘ kwa maslahi ya watawala, na angalau ilikuwa mara ya pili kuamini kwenda mahakamani kupeleka malalamiko yake.

Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2013, ambapo baada ya kile kilichoonekana kama “mahakama kwa ajili ya amani“ (peace judiciary), Odinga akabwagwa chini.

Wakati huo ilikuwa ni miaka mitano tu baada ya mauaji ya 2007 na nchi ikawa kwenye mazingira ya kuhofia kujirejea kilichotokea hapo awali.

Wenyewe, Wakenya, wanasema sio tu majaji, bali hata waandishi wa habari, wote, walikuwa kwenye ‘peace journalism‘ – uandishi wa habari kwa ajili ya amani.

Kwa maslahi ya amani, kwa hivyo, kila mtu akawa anaona bora tu mambo yaende kama yaendavyo lakini pasiwe na damu itakayomwagika.

Hata Odinga, licha ya kutokuridhika na uamuzi huo wa mahakama, akakubali kurejea kwenye kitu cha upinzani, kutoka nafasi ya uwaziri mkuu wa nchi aliyokuwa nayo kabla ya hapo.

Hiyo haimaanishi kwamba hakuwa na njia nyengine ya kufanya. Alikuwa nayo. Siasa za ndani kupitia umma.

Miaka miwili baada ya Odinga kushindwa kesi ya 2013, nilikutana na mmoja wa majaji waliokuwemo kwenye kesi hiyo jijini Nairobi. Nilitambulishwa kwake na rafiki yake mkubwa ambaye nami ni rafiki yangu.

Nikatumia fursa hiyo kumuuliza la kesi ile, naye akanijibu kwa kutumia mkasa tafauti wa walimu waliokuwa wakigoma na wakawa wameshinda kiwango fulani cha madai yao mahakamani, lakini yeye mwenyewe jaji huyo, akamuambia mmoja wa viongozi wa mgomo huo kuwa: „“Sasa mshahinda mahakamani, kauendelezeni ushindi wenu mitaani kuhakikisha kuwa kilichoamuliwa mahakamani kwa manufaa yenu, kinatimizwa. Mkilala, hapana kitakachotekelezwa!“

Lakini hadi kufikia mahala pa kwenda mahakamani, Wakenya wamepitia mengi kuijenga hiyo mahakama yenyewe. Yakiwemo mapambano ya kuipata katiba mpya mwaka 2010.

Ukimsikia leo Rais Kenyatta akiwaambia wapinzani: “Andamaneni mtakavyo, muhimu tu msiharibu mali na kuumiza wengine!“ si kwa kuwa Kenyatta ni mwanademokrasia sana, bali ni kwa kuwa Wakenya walipigania na kujenga taasisi imara za kusimamia demokrasia na utawala wa sheria, ambazo lazima yeye aziheshimu akataka asitake.

Huwezi kuwa na wapinzani ambao wanapangiwa na mtawala namna ya kumpinga nao wakawa wanamfuata mtawala huyo atakavyo, kisha ukatarajia kusimama kwa taasisi imara za kidemokrasia na utawala wa kisheria.

Huwezi kuwa na upinzani ambao unashiriki uchaguzi, unashinda kura lakini unaamini kuwa baada ya kuibiwa kura zao, haki hiyo itarejeshwa na waangalizi wa kimataifa, bila ya wenyewe kuendeleza shinikizo hilo, na bado ukatazamia kuna siku kura itakuwa na maana kwenye maisha ya watu.

Odinga aliwakaidi waangalizi wa kimataifa, wakiwemo wa mataifa makubwa ya Marekani  na Uingereza, na akawaambia mbele ya macho yao: “Shame on you!“ – Nyie musiokuwa na haya!

Wakati wao wakisisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, Odinga alishikilia kuwa matokeo yaliyotangazwa na IEBC yalikuwa “vifaranga vya kompyuta“ na kwamba angeliwathibitishia hivyo.

Hii ni kwa kuwa, mbali ya ushahidi madhubuti aliokuwa nao, Odinga alikuwa pia na uhakika wa nguvu ya ndani aliyonayo – umma. Aliapa kuwa angeliisaka haki mahakamani na mitaani, kama vile yule jaji wa mahakama ya juu alivyowahi kuniambia aliwashauri walimu waliogoma nchini Kenya.

Kwa hivyo, mafanikio makubwa ambayo Kenya imeyapata kupitia uamuzi huu wa Mahakama ya Juu hayatokani na nia njema tu ya majaji kwenye mahakama hiyo, wala huruma ya Rais Kenyatta kuwaruhusu kufikia hatua ya kwenda mahakamani au kuandamana mitaani, bali unatokana na mapambano ambayo upinzani na asasi za kijamii nchini Kenya zimeyapigana kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Haya ni mapambano ya ndani, ya watu wenyewe, ambayo yana gharama kubwa lakini ambayo matunda yake pia ni makubwa.

Ikiwa wanademokrasia wa mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Kati wanayatamani  yanayojiri Kenya, basi watende kama walivyotenda wenzao huko.

Wajipange na wajijenge ndani yao, na wapambane kwa imani kuwa wao peke yao ndio wa kubadilisha hali iliyopo.

Si Muingereza wala si Mmarekani!

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 4 Septemba 2017.

 

1 thought on “Funzo la uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya ni kuwa demokrasia hujengwa kutokea ndani, sio nje”

  1. Ukweli Kenya nikama wamefungua lango la ustaarabu situ kwa Afrika Mashariki bali kwa Afrika nzima na kwa vile ustaarabu ndio vazi la sasa nilazima kwa ulimwengu wa sasa basi lazima na wengine watapita tu katika lqngo hilo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.