UCHAMBUZI

Demokrasia na haki zinapotekwa nyara kwa gharama za amani na utulivu

Kilichotokea nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Agosti 2017, si kitu cha kuungwa mkono. Mauaji dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi sambamba na ghasia zinazofanywa na waliojiunga na maandamano hayo ni mambo yanayozidi kuliweka taifa hili la Afrika Mashariki kwenye mkwamo zaidi.

Bahati mbaya ni kuwa sababu za kutokea kwa haya si ngeni ndani ya eneo zima la mashariki, kati na kusini mwa Afrika. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu tu, mataifa yapatayo sita kwenye eneo hili yameingia uchaguzini – Burundi Julai 2015, Tanzania Oktoba 2015, Uganda Februari 2016, Zambia Agosti 2016, Rwanda Agosti 2017 na Kenya Agosti 2017 – na takribani yote yalikumbwa na matokeo yanayofanana ingawa si yote yaliyochukuwa njia moja kwenye kukabiliana na matokeo hayo. Mote watawala wamerejea madarakani na mote wapinzani wamelalamika kuwa hazikuwa chaguzi huru, haki wala za wazi.

Nchini Burundi, baada ya kuisigina katiba ya nchi yake na makubaliano ya amani ya Arusha na kulazimisha kuwania muhula wa tatu madarakani, Rais Pierre Nkurunziza, alirejea madarakani kwa asilimia 69 ya kura. Vyama vikuu vya upinzani viliugomea uchaguzi huo.

Na Mohammed Ghassani

Kabla na baada ya uchaguzi huo, taifa hilo limeshuhudia maandamano, machafuko na mauaji ya hapa na pale, huku maelfu wakiikimbia nchi yao kuelekea mataifa jirani. Upinzani rasmi unaendelea kutoa matamko ya mara kwa mara dhidi ya utawala na baadhi ya mataifa ya nje yameiwekea nchi hiyo vikwazo.

Nchini Tanzania, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulimsimamisha aliyewahi kuwa mwanachama wa ngazi za juu wa chama tawala (CCM), Edward Lowassa, kupambana na mwanachama asiyekuwa na mizizi mirefu ndani ya chama hicho, John Magufuli, katika uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano, na matokeo yake Magufuli akatangazwa ushindi kwa asilimia 58.6, huku UKAWA ukiamini kuwa mgombea wao ndiye hasa aliyeshinda, lakini matokeo yakabadilishwa kwa manufaa ya chama kilichotawala kwa zaidi ya nusu karne, CCM.

Hata hivyo, katika uchaguzi wa Zanzibar, hali ilikuwa tafauti kabisa. Chama cha upinzani, CUF, kinasema CCM ilishindwa kabisa kubadilisha matokeo licha ya kukaa siku tatu nzima kukusanya na kuhakiki kura zisizofika 600,000 na hatimaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha, akaufuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba 2015 na kisha kumrejesha madarakani Dk. Ali Mohamed Shein kwa asilimia 91.8 kupitia kilichoitwa ‘uchaguzi wa marudio’ wa Machi 2016 uliosusiwa na vyama vikuu vya upinzani.

Baada ya uchaguzi kumalizika na Magufuli kujiimarisha madarakani, kuna jitihada kubwa kabisa za utawala wake kuuwa upinzani na yumkini kwa mahisabu ya kutokukumbana na yaliyojiri mwaka 2015 ifikapo uchaguzi wa 2020. Viongozi kadhaa wa upinzani wamekamatwa, kupigwa, kuteswa, kufungwa, kunyang’anywa ama kuharibiwa mali zao na hata vyombo huru ya habari vinatishwa.

Kwa upande wa Zanzibar, kabla na baada ya Dk. Shein kurudi madarakani, kulitanda visa vya kamatakamata, pigapiga, na kuwekwa watu ndani kwa muda usiojuilikana, huku baadhi ya mataifa ya nje yakiweka vikwazo laini na upinzani unaoshikilia kutokuitambua serikali ya Dk. Shein ukitoa matamko ya hapa na pale dhidi ya utawala huo.

Lakini lazima kutaja hapa kuwa chama kikuu cha upinzani, CUF, ambacho kinaamini kuwa kilishinda tena uchaguzi wa Oktoba 2015, sasa kimeingizwa kwenye mgogoro mkubwa kabisa ambao una kila dalili za kusimamiwa na vyombo vya dola na ambao unaweza ukaififisha nafasi ya wapinzani kusimama tena imara dhidi ya utawala mwaka 2020.

Nchini Uganda, ambako Rais Yoweri Museveni amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, alitangazwa mshindi wa asilimia 60.62 kwenye uchaguzi wa tarehe 18 Ferbruari 2016, ikiwa ni mara ya nne mfululizo kumshinda mpinzani wake mkuu, Kizza Besigye. Upinzani unasema Besigye alishinda lakini kwa mara nyengine akazuiwa na kuiongoza nchi hiyo.

Hata hivyo, tafauti na wapinzani wenzake wa mataifa mengine ya Afrika Mashariki, Besigye aliamua kujitangaza na kuapishwa kuwa rais wa Uganda, kisha akakamatwa na kuwekwa ndani kwa uhaini. Lakini nako pia, kabla na baada ya uchaguzi wenyewe, kulikuwa na kamatakamata, pigapiga na fungafunga dhidi ya wapinzani.

Nchini Zambia, Edgar Lungu alirejea madarakani kwa ushindi wa asilimia 50.35 dhidi ya 47.63 za mpinzani wake mkuu, Hakainde Hichilema, ambaye naye ana uhakika wa ‘kuibiwa’ kura kwa maslahi ya watawala.

Upinzani nako unaandamwa kabla na baada ya uchaguzi huo wa tarehe 11 Agosti 2016 kwa vipigo, kamatakamata na vifungo. Ndio kwanza Hichilema ametolewa juzi jela alikokuwa anasubiri kesi ya uhaini dhidi yake, kosa lake likiwa kushindwa kuupisha msafara wa magari ya Lungu.

Hadithi ya Rwanda haistahiki hata kusimuliwa kwa upana wake, si kwa sababu haina mengi ya kusimuliwa, bali kwa kuwa ni shida kuchaguwa cha kusimulia kwa namna ilivyojengeka.

Katika taifa ambalo kuwa mpinzani wa kweli ni sawa kujiandikia hati ya kifo, mateso na ukandamizwaji, si ajabu kuwa kila uchaguzi, mgombea wa chama tawala hupata asilimia 90 kwenda juu.

Mwaka 2003, Paul Kagame alipata asilimia 95, mwaka akashuka kidogo kwa asilimia 95 lakini huu wa tarehe 4 Agosti 2017 akapanda tena hadi asilimia 98.7, kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi.

Kabla na baada ya uchaguzi, Rwanda hubakia kuwa ile ile. Machache hubadilika kwenye taswira ya kisiasa, ikiwa yapo.

Uchaguzi wa mwisho wa Kenya wa tarehe 8 Agosti 2017 umerejesha hali ile ile iliyozoeleka kwenye mataifa ya Afrika Mashariki – walio madarakani hawawezi kurejea kosa la kushindwa kwenye uchaguzi waliouandaa wenyewe.

Inaonekana ni kama kwamba kile watawala wanachokiona ni kosa lililowahi kufanyika Zambia mwaka 1991 alipoangushwa Kenneth Kaunda na hapo Kenya penyewe mwaka 2002, ambapo Uhuru Kenyatta akiwa chama tawala cha wakati huo, KANU, alishindwa na mgombea wa muungano wa upinzani aliyeikimbia KANU, Mwai Kibaki, hakipaswi kujirejea milele.

Huenda kweli, watawala katika eneo la kusini, kati na mashariki mwa Afrika wanafanya kazi nzuri ya kuzijenga nchi zao na wanakubalika sana na wapigakura kiasi cha kurejeshwa madarakani kila mara wanapofanya uchaguzi.

Lakini pia inawezekana kuwa watawala hawa wamejiimarisha sana kwenye taasisi na mifumo ya kidola kiasi cha kwamba kura za wananchi hazimaanishi chochote. Ni bahati mbaya sana kwamba huu wa pili unaonekana kuwa uhalisia zaidi.

Sikusudii kuhukumu kuwa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC), ambayo imesifiwa na waangalizi wa ndani na nje kwa kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa licha ya changamoto za hapa na pale, imejigeuza kuwa moja ya taasisi ya kidola ambazo amri kuu inatoka kwa mtawala.

Lakini pia sitaki kuhukumu kuwa muungano wa upinzani wa NASA unadanganya kwenye madai yake ya kuibiwa kura kwa mara nyengine.

Ninachokiona ni kuwa tabia inayojengeka kwenye mataifa yetu, hata baada ya takribani miaka 30 ya kuijaribu demokrasia ya vyama vingi, inaakisi ukweli kuwa demokrasia hii imetekwa nyara na watawala, ambao wanatumia bango la amani na utulivu kama kisingizio cha kuendelea kuwapo kwa madarakani.

Kwa maslahi ya kutunza amani, wapinzani visiwani Zanzibar wanaendelea kumalizwa na matumaini ya mabadiliko kuvunjwa kabisa. Kwa tamaa kuwa utulivu ndio njia na shabaha ya maendeleo, wapinzani Uganda nao ni hivyo hivyo. Yayo yanaweza kusemwa kwa kwengineko.

Mataifa ya Magharibi, ambayo yanahusika pakubwa na hili dubwashikana liitwalo ‘demokrasia ya vyama vingi’ ni kama kwamba nayo yameamua kuwa yalifanya kosa kushawishi kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, na sasa kisirisiri yanaungana na watawala wanaoikandamiza demokrasia kwa kuwa tu makampuni yao ya kibiashara yanapata kuvuna rasilimali kirahisi chini ya mifumo iliyopo.

Ninapoangalia kufeli kwa kile kilichoitwa “Mapinduzi ya Arabuni” kuanzia Tunisia, Libya, Yemen, Syria na kwengineko, naona imesharasimishwa sasa kuwa demokrasia si jambo muhimu kwa mataifa hayo na yetu ya Afrika, na hivyo muelekeo wa siasa za kilimwengu sasa ni kuiteka nyara demokrasia changa iliyokwishaanza kuchipuwa kwa maslahi ya kulinda amani na utulivu unaoambiwa upo.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mwelekeo la tarehe 14 Agosti 2017.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.