UCHAMBUZI

Ndiyo kwa ‘uchumagu’, hapana kwa ‘umagukrasia’

Kitu kimojawapo ambacho Rais John Magufuli anajipambanuwa nacho kwa haraka na watangulizi wake, ni tabia yake ya kutokuwa na ajizi na vile kutozingatia kwake mipaka kwenye huko kutokuwa na ajizi. Hayo ni kwa kila alisemalo na kila alitendalo. Kutokuwa na ajizi ni jambo jema kwa kiongozi, lakini kutokuzingatia mipaka si jambo la kusifiwa hata kidogo.

Hapa ndipo ambapo, kwa mwenye akili, anapoweza kirahisi kuchora mstari wa namna ya kumchambua, kumtafakari na kuchaguwa lipi ni lipi kwenye shakhsia ya Rais Magufuli, na kwayo isimuwiye vigumu kujuwa pa kuungana naye na pa kupingana naye.

Kinyume na wanavyochukulia wale wanaojiaminisha kuwa uzalendo hasa ni kumuunga mkono kiongozi wa nchi kwa lolote aliwazalo, alinenalo na alitendalo, utendaji kazi wa Rais Magufuli unawasuta sio tu kwa kutokujuwa kwao maana halisi ya uzalendo, bali pia kwa kuwaonesha kuwa hawana msaada wowote wa maana si kwa Rais Magufuli mwenyewe, wala kwa serikali yake na hata kwa chama chake kinachotawala, CCM.

Ufanyaji wake maamuzi, utoaji wa kauli zake na utendaji kazi wake unatufanya wengine kuona kuwa hata kama hatuna ulazima wa kumuunga mkono kwa kila jambo lake, bado pia hatuna ulazima wa kumpinga kwa kila kitu. Kwamba muna mwahala, kwa mtazamo wetu, anafanya vyema na anahitaji kupewa heko na kusaidiwa na muna mwengine ambamo anafanya vibaya na anapaswa kukosolewa na kuzuiwa.

Uchumagu na Tanzania inayotakiwa

Na Mohammed Ghassani

Binafsi, namuunga mkono Rais Magufuli kwenye hili ninaloliita hapa ‘uchumagu’ – uchumi wa Magufuli, dhana inayowakilisha jitihada zake binafsi kama kiongozi wa nchi kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakuwa na kuwagusa wananchi wa kawaida, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitengwa kando.

Ndani ya jitihada hizi, muna kampeni kubwa ya kupambana na ufisadi, wizi wa mali ya umma, ukosefu wa uwajibikaji na kiwango kikubwa cha uholela kwenye sekta ya umma. Muna pia jitihada zinazoonekana za kuimarisha miundo mbinu na kuwafikia watu kule waliko. Hapana shaka, mafanikio ya kampeni hii ni faida kwa umma na yana athari za moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida.

Hakuna mwenye mapenzi ya kweli kwa nchi, ambaye hataweza kuunga mkono pale, mathalani, watuhumiwa wa ufisadi wanapofikishwa mahakamani kujibu mashitaka dhidi yao. Hakuna pia atakayepinga pale siku maafisa wa serikali waliokuwa wamepewa dhamana kubwa kuwahudumia wananchi na wakazifanyia khiyana dhamana hizo ‘wanayotumbuliwa’.

Ingawa hata watu wanaweza kukosoa njia zinazotumika kwa kuhofia zisije zikawa za zimamoto na kulifanya lengo halisi kutofikiwa, lakini wanajuwa kuwa vita dhidi ya ufisadi ni jambo linalohitajika.

Baada ya zaidi ya nusu karne ya kutawaliwa na chama cha Rais Magufuli, CCM, serikali za pande zote mbili za Muungano zilishageuka kuwa jalala la uchafu wote wa kiuongozi:  kuanzia wizi wa mali ya umma, udugunaizesheni (upendeleo wa kifamilia na kieneo), ubadhirifu, uzembe na ukosefu wa uwajibikaji.

Kwa ujumla, ufisadi umekuwa ni wa kimfumo ndani ya serikali hizi, kuanzia juu kabisa hadi chini kabisa kwa kipindi kirefu sasa. Hata hizo enzi za Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume, ambazo wengine hutaka kutuaminisha kuwa zilikuwa zama za usafi wa kimaadili, ushahidi unaonesha kuwa zilikuwa na makandokando yake mengi na ndiyo hayo yaliyoasisi uovu uliokuja kudhihirika baadaye.

Mwenyewe Mwalimu Nyerere alikuwa akikiri kuwa hata katika uongozi wake kulikuwa na rushwa, lakini alitaka tukubali kuwa yeye na wenzake wachache waliokuwa juu walikuwa hasa wakiichukia rushwa kwa vitendo, na kwamba kila walipopata mashaka na mteule yeyote aliye chini yao kuhusika na rushwa, basi walimchukulia hatua hapo hapo bila kuchelewa na bila kuchelea.

Kwa hivyo, kwamba leo Rais Magufuli anaongoza vita vya kuukomboa uchumi kutoka mikononi mwa ufisadi wa ndani na wa kimataifa na dhidi ya uporaji wa rasilimali unaofanyika kupitia mikataba ambayo serikali zilizoongozwa na chama chake ziliingia huko nyuma, ni wazi kuwa anapigana vita ambavyo anastahiki sifa na kuungwa mkono, hata kama ni vita vinavyotokana na uchafu uliotendwa na chama chake mwenyewe huko tutokako.

Kwa kutumia maneno yake ya tarehe 1 Julai 2017, wakati akifungua Maonesho ya Sabasaba: “Tanzania tumechezewa sana kwa sababu tulitaka kuchezewa. Lakini sasa kuchezewa basi!” Nami nafanya hivyo: namsifu na namuunga mkono. Tanzania kama taifa lilichezewa sana kwenye uchumi wake kwa kuwa wao kama watawala walitaka taifa hili lichezewe. Kufanikiwa kwa Rais Magufuli kwenye vita hivi, ni kufanikiwa kwa taifa zima.

Tanzania haiuhitaji umagukrasia

Lakini kando ya vita vyake hivi, Rais Magufuli anapigana pia vita vyengine, ambavyo mpigaji hasa ni peke yake kwa kuwa ana nyenzo za kumuwezesha kupiga pasi yeye kushambuliwa, na anaowapiga vita hivyo ni mamilioni ya Watanzania ambao hawakubaliani na siasa zake wala dhamira yake. Hapa nitatumia dhana ya ‘umagukrasia’ kuelezea vita vyake hivyo na namna ambavyo mimi siviungi mkono.

Umagukrasia ni aina ya utawala wa kisiasa ambao Rais Magufuli anaujenga, ambao unalenga kumtukuza yeye na chama chake juu ya kila kitu kwa gharama ya kuwadhalilisha wengine wote wasiokuwa wa chama chake au wasiomuunga mkono yeye. Kwa imani kwamba yeye – kama kiongozi mkuu wa dola na chama tawala – anamiliki pekee maarifa yote ya mwelekeo wa taifa na anaongozwa na nia safi isiyo doa kwenye kila anenalo na atendalo, Rais Magufuli hana uvumilivu hata chembe kwa wale wanaomuona tafauti.

Ukosefu wa uvumilivu wake unadhihirika kwa ayasemayo na ayatendayo dhidi ya sauti za ukosowaji ndani ya nchi, akitumia mikono yake aliyonayo kama mkuu wa dola, serikali, chama, na hivyo mwenye kauli ya juu kwenye mihimili mingine yote ya nchi.

Alianza na bunge, chombo kinachopaswa kuwa muhimili huru wa kuisimamia serikali. Kwa namna kilivyotekeleza wajibu wake wa kuikosoa na kuisimamia serikali kwenye awamu iliyopita, inaonekana Rais Magufuli anaamini kuwa ndiko kulikopelekea kwa mara ya kwanza kabisa, chama chake cha CCM kushindwa kuvuuka asilimia 60 ya kura za urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2015.

Kwa hivyo, kitu cha mwanzo kabisa alichofanya, ni kuliminya bunge kwa kulitenganisha na wananchi wa kawaida, ambao wanaonekana kuathirika na kinachoendelea Dodoma.

Kisha akaenda kwenye vyama vya kisiasa ambavyo vinaonekana kumpinga. Tunashuhudia sio tu kupigwa marufuku kwa mikusanyiko ya vyama hivyo, bali pia kuandamwa kwa viongozi wake wa ngazi mbalimbali, wakikamatwa, kuadhirishwa, kuadhibiwa, kufunguliwa kesi na hata kufungwa jela.

Kisha akaja kwenye vyombo vya habari vya kawaida (televisheni, redio na magazeti) na vya kisasa (hasa mitandao ya Facebook, WhatsApp na blogu), ambako sauti mbadala ya wananchi wa kawaida huwa inasikikana bila kupitia taratibu za kawaida za uchujaji.

Ndani ya kipindi hiki kifupi cha kuwapo kwake madarakani, redio na magazeti kadhaa yameshafungiwa na watumiaji kadhaa wa mitandao hiyo ya kijamii wameshakamatwa, huku wengine wakiripoti kuteswa, wengine wakifunguliwa mashitaka na wengine wakiwa wametoweka bila kujuilikana walipo hadi leo.

Inavyoonekana ni kuwa sasa mkono wa Rais Magufuli unazielekea asasi za kijamii ambazo zinajihusisha na masuala ya haki za binaadamu kwa ujumla wake ama haki za makundi maalum, kama vile vijana, wasichana na wanafunzi.

Haya na mengine ambayo yanafanywa na utawala wa Rais Magufuli katika jitihada zake za kupunguza duara la ukosowaji dhidi yake na kutanuwa duara la ama uungaji mkono wa kulazimisha au ukimya wa khofu, ndicho hicho ninachokiita ‘umagukrasia’.

Mwelekeo unaostahiki

Umagukrasia si jambo la kusifiwa wala kuungwa mkono na yeyote mwenye mapenzi ya kweli na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taifa hili ilikuwepo kabla ya Rais Magufuli hajakuwa rais na misingi yake ya kitaifa, ikiwemo demokrasia, haki za binaadamu, kijamii na kisiasa na hishima kwa mawazo mbadala – licha ya mapungufu makubwa yaliyokuwa nayo – bado ilianzishwa na kuanza kuengwaengwa kidogo kidogo na waliomtangulia.

Rais Magufuli amekuja madarakani zaidi ya nusu karne tangu Watanzania waanze safari ya kuelekea kwenye utawala wa watu, unaotokana na watu na uliopo kwa ajili ya watu, wakiimarisha hatua kwa hatua taasisi zao za utawala – vyama vya siasa, vyama vya kiraia, vyombo vya habari, bunge, mahakama na serikali yenyewe.

Kama kiongozi mkuu wa dola, serikali na taifa, ana muda wake maalum wa kuwapo hapo. Ukifika atapaswa kuondoka kama walivyoondoka wenzake, lakini hataondoka na nchi hii. Jamhuri hii itabakia na itaendelea baada ya yeye.

Kwa hivyo, anatakiwa sio tu kuiwacha salama kisiasa kama alivyoikuta, bali pia ana wajibu wa kuongezea thamani kwenye misingi hiyo ya kitaifa na kikatiba aliyoikuta na sio kuiangamiza kama anavyoonekana sasa akifanya.

Ndio maana, kwa hilo la umagukrasia, mimi simuungi mkono kabisa kabisa.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa mara ya kwanza na gazeti la Mwelekeo la tarehe 4 Julai 2017.

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.