Kwa hakika sijui ni kitu gani kilichokuwa kimenifanya niamini kuwa Ramadhani ya mwaka huu isingelimalizika kabla ya viongozi na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu ya Zanzibar (Uamsho) wanaoshikiliwa kwa zaidi miaka minne sasa katika magareza ya Tanzania Bara, hawajaachiliwa huru!
Ni jambo la kushangaza kuwa bila ya hata kuwa na ushahidi wowote mkononi mwangu, nilikuwa ‘najipiga dripu’ mwenyewe na kujing’ang’aniza akilini mwangu kuwa iwe iwavyo, sala ya Iddi ya Mfunguo Mosi ingeliswaliwa visiwani Zanzibar na mahabusu hao wakiwa wamejumuika na Waislamu wenzao. Wakiwa watu huru!
Bahati mbaya ni kuwa zangu zilikuwa ni ndoto za Alinacha – za kuota mchana kweupe kwa kujipa matumaini kwa jambo lisilokuwapo. Bahati nzuri ndani ya bahati hii mbaya ni kuwa niliishi na ndoto hiyo ndani yangu, sikuwahi kumuambia mtu hata mmoja – hata yule mwendani wangu.
Ningelimuambia yeyote, leo angelipata sababu ya kunisuta, maana kwa jinsi nilivyokuwa naiamini ndoto yangu hiyo, basi nina hakika ningelikuwa nimeitetea kwa kila aina ya utetezi, kama si viapo na viapizo vya kuweka hata nadhiri!
Ila ukweli ndio huu unaotukodolea macho mbele yetu hivi sasa. Viongozi na wafuasi wa Uamsho wangali “wananyelea ndooni Bara” – kwa kutumia msamiati wa Balozi Seif Ali Iddi, ambaye wala haoni haya kusema kuwa yeye na wenzake serikalini na chamani ndio waliowapeleka raia hao wa Zanzibar huko.
Hata Haji Omari Kheri, aliyepewa dhamana ya kusimamia vikosi vya serikali chini ya utawala wa Dk. Ali Mohamed Shein, naye hujifakharisha kwa hilo hilo la kuwapeleka masheikh hao kwenda kudhalilishwa kikatili katika ardhi ya Tanganyika, akitishia kuwa “na yeyote atakayejifanya kutuletea ya Uamsho, basi hayo munayosikia yanawapata wao huko Bara, naye tutampeleka yakampate hayo hayo!”

Kwa kusema “hayo yaliyowapata” masheikh wakiwa gerezani Segerea, Haji Omari alikuwa anamaanisha udhalilishwaji wa kimwili, ambapo iliwahi kuripotiwa kuwa masheikh wetu hao wanasema waliingizwa vitu kwenye sehemu zao za haja kubwa. Kama tuhuma hizi ni za kweli, basi laana za Mungu naziwashukie watendaji wa hayo na walioyasababisha.
Dua hizi za kuwalaani watu hao, hata hivyo, zimeshaombwa nyingi visiwani Zanzibar. Nadhani ni dua iliyoombwa zaidi kuliko nyengine yoyote ndani ya kipindi hiki cha miaka minne inayokwenda zake.
La kujibiwa na kutojibiwa si juu ya waziombao. Aombwaye mwenyewe ana kawaida ya kujipangia muda, mahala na namna ya kujibu maombi ya wamuombao. Hata anapochelewa, si kwa kuwa anachelea, bali huwa ana mipango yake, ambayo kila siku ni bora zaidi.
Nirudi kwenye nukta kuu. Miaka minne inakatika na wazazi hawa wanaendelea kutenganishwa na watoto wao, watoto na wazazi wao, na waume na wake zao. Familia zimesambaratishwa. Vitoto vidogo vinaendelea kukuwa bila baba zao majumbani. Madarasa ya dini yamekosa walimu wao na misikiti maimamu wake.
Kwa sisi tulio nje, huenda hata hatuhisi kupita huku kwa siku. Tuko huru huku nje. Tunaishi na familia na marafiki zetu. Tunakwenda tukirudi, tunalala tukiamka. Kwa waliomo ndani ya makuta manne, siku hizi ni kama miaka 40. Tena kwa jinsi tunavyojulishwa na yale yanayowajiria huko waliko, hii ni miaka 40 ya mateso na idhilali. Ya dharau na bezo. Miaka ya mateso na dhuluma.
Hapa na pale huwa tunapaza sauti zetu, ama kwa kuandika mitandaoni au kuripoti kinachosemwa bungeni na wabunge walioamua kujitolea kuwatetea angalau kwa maneno yao (maana ndilo pekee wawezalo kulifanya).
Kinachosikitisha ni kuwa ni kama kwamba hili dola liitwalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilishaamuwa kuwa dhuluma dhidi ya raia wake hawa ni halali na inapaswa kuendelea. Ni kama kwamba walio madarakani wanastaaladhi kwa mateso haya yanayowapata Uamsho.
Binafsi huwa ninakaa na kujiuliza: Hivi kiongozi yeyote wa serikali na vyombo vya dola aliyehusika kwa namna moja au nyengine na dhuluma hii, huwa anajihisije kila arudipo nyumbani na kupokelewa na familia yake, katika wakati ambapo kuna mzazi kama yeye ambaye kamkomelea ndani kwa mwaka wa nne huu, akimkosesha kile ambacho yeye anakipata nyumbani pake?

Tuje kwenye upande wa dini kidogo, jukwaa ambalo viongozi hao wa Uamsho walilitumia kutuma ujumbe wa kisiasa dhidi ya mfumo wa Muungano, na kwalo wakawa wamejichongea kwa wenyewe wenye Muungano. Kila mwaka kunakuwa na huu mwezi mmoja wa Ramadhani ambao sisi Waislamu hufunga kwa ajili ya kumcha Mola wetu. Ndani yake muna mengi ambayo yanaigusa sana familia ya Muislamu moja kwa moja. Chakula cha awali baada ya mfungo, yaani futari, chakula cha mwisho kabla ya mfungo, yaani daku, swala za tarawehe, visomo vya pamoja, na kisha sikukuu. Mote humo neno familia linaongoza.
Hapo ndipo huwa najiuliza mtu kama aliyekuwa amiri jeshi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati viongozi wa Uamsho wanakamatwa, Jakaya Mrisho Kikwete, anajihisije? Anajifikiriaje? Maswali haya pia yawahusu viongozi wote wakuu wa Zanzibar wakati wa kukamatwa na kupelekwa Bara viongozi hawa, wakati huo nchi ikiwa na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa – Dk. Shein, Balozi Iddi na Maalim Seif Sharif Hamad.
Ukweli mmoja mchungu kwa dola ni kuwa kwa miaka yote hii minne ya kuwashikilia watu wa Uamsho wameshindwa kuurai umma huku nje kuamini kauli yao kuwa watuhumiwa hawa ni wakosaji.
Sehemu kubwa ya Wazanzibari na Watanzania wanafahamu kuwa jamaa wa Uamsho ni wahanga wa siasa za Muungano. Kwamba kosa lao kubwa ni vile kusimama kwao kuupinga mfumo wa Muungano uliopo na kutetea hoja ya Zanzibar kuwa taifa, dola na nchi huru, ya kuachiwa ikapumuwa – kwa kutumia msamiati wao wenyewe. Uthubutu huu kilikuwa kitu kisichoweza kuvumilika mbele ya watawala, wenyewe wenye Muungano wao.
Kwa hivyo, wakati dola inahangaika huku na kule kukusanya ushahidi wa kuungaunga ili kusimamisha madai yake ya ugaidi wa Uamsho, huku nje umma haumuangalii yeyote kati ya waliokamatwa kwa jicho hilo.
Kinyume chake ni kuwa wanawaangalia kuwa mashujaa wao waliowatetea na kuwasemea kile ambacho kimo kwenye nafsi zao, lakini wenyewe wakawa hawana njia au uthubutu wa kukisema.
Huu ni ukweli ambao dola na vyombo vyake inaujuwa fika. Pengine kuliko hata tuujuwavyo mimi na wewe, maana dola lina mikono, macho na masikio mengi zaidi. Tatizo ni kuwa kwa kutumia mikono, na macho na masikio hayo, dola hili limeamuwa kuchaguwa ukweli wa kuuamini na kuufanyia kazi, huku likiupuuzia mwengine wowote.
Na hapa pa kupuuza na kudharau, ndipo hasa iliposimama kadhia ya Uamsho. Puuzo kwamba wataendelea kushikiliwa na kudhulumiwa hadi huko ndani waliko watoke maiti mmoja baada ya mwengine, wala pasiwe chochote.
Dharau kwamba hata familia, ndugu, jamaa na wafuasi wao huku nje wakiinuka na kusema, hawawashi wala hawazimi. Nao ni vinyangarika vinavyoweza kuviringishwa kiganjani sekunde chache “yakawapata kama yawapatayo masheikh wao” – kama asemavyo Haji Omari Kheri, na wala pasiwe kitu.
Katikati ya puuzo na dharau hii, ndipo dhuluma dhidi ya Uamsho izidipo kunawiri na kushamiri. Na siku zapita, lakini kwao wao, hakuna mabadiliko yoyote yale.
Lakini hakika Mungu ni Hakimu wa mahakimu!