Mimi sifichi msimamo wangu dhidi ya ‘siasa’ za huu tunaoaminishwa kuwa ni Muungano wa Tanzania kuelekea Zanzibar, ingawa naweka mpaka baina ya kusimama dhidi ya Muungano wenyewe na kusimama dhidi ya hizo niziitazo siasa za Muungano, maana kwangu hivyo ni vitu viwili tafauti.
Tangu mwaka 2001 nilipoanza kuandika mawazo yangu kwenye vyombo vya habari, mtazamo wangu ni kuwa siasa hiyo inaelezeka kwa sentesi moja tu: Muungano imara kwa Zanzibar dhaifu. Naamini hiyo ndiyo falsafa inayouongoza Muungano wenyewe miongoni mwa viongozi wakuu wa Muungano huo na wafuasi wao.
Kwao wao, ili kuwa na Muungano imara, basi ni lazima uwe na Zanzibar iliyo dhaifu. Ni ipi Zanzibar dhaifu na ni upi Muungano imara? Muungano imara ni ule ambao unahodhi na kumiliki kila kitu cha Zanzibar kwenye kapu lake na kuitawalisha Tanganyika kwenye udhibiti wa kapu hilo. Huo ndio Muungano hasa unaotakiwa na watawala na siasa yao inaakisi ukweli huo.
Na Zanzibar dhaifu ni ile Zanzibar isiyo na mamlaka ya kisiasa kujiamulia mambo yake yenyewe, isiyo na madaraka ya kifedha kusimamia uchumi wake yenyewe, na isiyokuwa na uthubutu wa kuiongoza jamii yake yenyewe. Hiyo ndiyo Zanzibar hasa inayotakiwa na siasa ya Muungano huu na siasa yao inaakisi pia ukweli huo.
Kwa hivyo, kuidhoofisha Zanzibar kwa kauli na vitendo ni sehemu muhimu sana ya kuufanya Muungano uwe na nguvu, uwe madhubuti na udumu milele.

Kwao wao, ukiwa na Zanzibar yenye nguvu na iliyo imara kwenye uchumi wake, siasa yake na jamii yake, una Muungano ulio dhalili. Ni kama vile wamechora mstari mwekundu baina ya viwili hivi na kisha wanakuradulisha upande mmojawapo wa mstari huo. Ama usimame upande wa Muungano na hivyo uwe sehemu ya udhalilishaji wa siasa, uchumi na jamii ya Zanzibar, au uchaguwe kusimama upande wa Zanzibar na hivyo uwe sehemu ya kuubomoa na kuuvuruga Muungano huo!
Hivyo ndivyo akili zao zinavyofanya kazi na ndivyo inavyodhihirika, kama nilivyosema, kwenye kauli na amali zao. Mifano ni mingi. Nimeiandika mingi huko nyuma tangu wakati wa Rais Benjamin Mkapa, nikafanya hivyo wakati wa Rais Jakaya Kikwete na sasa nafanya hivyo wakati wa Rais John Magufuli.
Ni kama vile ambavyo Marekani isivyoweza kubadilisha msingi wa siasa zake za nje hata akija rais gani, ndivyo ilivyo kwa siasa ya Muungano kuelekea Zanzibar isivyoweza kubadilika hata aje mtawala gani. Wanaweza kubadili kila kitu kuhusu siasa za ndani ya Tanganyika (wenyewe hawataki hata kulisikia hili jina), lakini hawatathubutu kubadili siasa ya Muungano kuelekea Zanzibar.
Leo nazungumzia mfano wa karibuni kabisa ambao umedhihirishwa na Rais Magufuli, wakati akihutubia baada ya kumuapisha Bi Anna Elisha Mghwira wa Chama cha ACT-Wazalendo kuwa mkuu mpya wa mkoa wa Kilimanjaro.
Akionekana kuwajibu wale ambao walimuona kuwa ni mtu wa kigeugeu juu ya uamuzi wake wa kuteua wapinzani kuingia kwenye serikali yake baada ya kujiapiza kuwa kamwe asingelimuigiza Dk. Ali Mohamed Shein wa Zanzibar ambaye amefanya, Rais Magufuli alisema wanaomkosoa hivyo wanapaswa kwanza kujuwa mazingira ambayo alitoa kauli hiyo.
Mwaka mmoja na kidogo uliopita, akiwa kwenye mkutano wa hadhara kuwashukuru wapigakura kisiwani Unguja, Rais Mafuguli akiwa mbele ya Dk. Shein na viongozi wengine wa chama chake na vyama vichache vijiitavyo vya upinzani, alimshangaa Dk. Shein kwa kuwaingiza ‘wapinzani’ kwenye serikali yake.
“Rais uchaguliwe upate asilimia 92, bado unawachukuwa watu wa vyama vingine unawaingiza kwenye serikali yako. Mimi nilipata asilimia 58, hakuna wa chama chengine kule ndani yangu. Na wala hataingia.”
Sasa akihalalisha hatua yake ya kumteua ‘mpinzani’ kuingia kwenye serikali yake, Rais Magufuli akataka aeleweke kimuktadha anapotoa maneno yake.
“Ni lazima watu waelewe nilizungumza hilo nikiwa mahali gani. Nilizungumza nikiwa Zanzibar. Lakini pia msimamo wa kutoteuwa mpinzani kwenye nafasi zangu kumi za wabunge, sitafanya hivyo kweli. Nilishateuwa tisa, nimebakiza moja, na hiyo nafasi moja haitakuwa ya wapizani.”
Kama kuna kitu amekisema kweli kwenye hili basi ni hilo la muktadha wa kutoa kauli zake zinazopishana. Kwenye viwanja vya Kibandamaiti kisiwani Unguja katika ardhi ya Zanzibar, kauli ni kuwa umoja wa kitaifa kwenye serikali hauna maana, madhali huyo aambiwaye ni mshindi ana uhalali wa kuzoa na kukokozoa vyote. Kwenye jengo la Ikulu, katika ardhi ya Tanganyika, kauli ni kuwa nchi inapaswa kujengwa na wananchi wote bila kujali vyama vyao, maana nchi kwanza.
Kwa nini kauli mbilimbili? Jibu limo kwenye ufafanuzi wa awali wa namna siasa ya Muungano inavyofanya kazi yake kuelekea Zanzibar. Waswahili husema kuwa: “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”, na kwa mantiki yake ni kuwa kama Zanzibar itakuwa na umoja huo, basi itakuwa na nguvu, na ikiwa na nguvu basi Muungano utakuwa dhaifu.
Kwa hivyo, kwa kiongozi wa juu wa Jamhuri ya Muungano kushadidia utengano wa Wazanzibari kwenye muktadha huu wa uendeshaji nchi, anakusudia hasa kutekeleza kwa vitendo siasa hiyo ya Muungano kuelekea Zanzibar – Zanzibar dhaifu kwa Muungano imara!
Kwa kusema kuwa ahukumiwe kauli zake hizi mbili kwa msingi wa mwahala alimozizungumza, Rais Magufuli anatupa ujumbe wa wazi, ambao kwetu wengine unafahamika kitambo, kwamba linapokuja suala la mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, basi viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano si sehemu ya suluhisho, bali sehemu ya tatizo.
Nimesema kuwa huu ni mfano mmoja tu kati ya mingi iliyokwishatokezea huko nyuma, na ambayo mingine kati yao nilipata fursa ya kuielezea. Katika miaka ya mwisho mwisho ya utawala wake, Rais Mkapa alialikwa kwenye shughuli mbili muhimu visiwani Zanzibar – moja ni kuadhimisha Mapinduzi na nyengine Muungano, na mote muwili aliakisi siasa hiyo hiyo ya Muungano kuelekea Zanzibar.
Kwenye sherehe za Mapinduzi, aliwataka waliohudhuria katika viwanja vya Amani, waitikie kwa nguvu “Mapinduzi Daima”, hadi vitukuu na vijukuu vya Waarabu na masultani wa Kiarabu wasikie kuwa kweli Waafrika weusi wa Zanzibar wamechukuwa hatamu za nchi yao. Kwenye jukwaa siku hiyo alikuwepo Rais Amani Karume, mke wake Shadia na watoto wao, ambao kwa hakika ni vijukuu na vitukuu hivyo vya hao Waarabu. Sadfa ni kuwa takribani miaka 10 baadaye, vijana wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM), walipita na mabango yanayowataka “Machotara na Mahizbu” kutafuta nchi ya kwenda kutawala, maana Zanzibar si pao.
Wakati akifungua bunge la kwanza kwenye utawala wake mwaka 2005, Rais Kikwete naye akasema kwamba ni ajabu kwamba Wapemba ambao wanafaidika na fursa kadhaa za Muungano huo, wanakuwa wa kwanza kuonesha kujitenga, akirejea matokeo ya chaguzi, ambazo kila mara watu wa kisiwa cha Pemba hupiga kura kuikataa CCM kwa ujumla wake.
Sadfa ikaja ikawa kwamba wakati anaondoka madarakani mwaka 2015, serikali ya umoja wa kitaifa ambayo iliundwa kwa shinikizo la Wazanzibari wenyewe ndani ya kipindi cha mwisho cha muhula wake wa urais, inakufa. Kilichoiuwa ni kuharibiwa kwa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na chama chake, CCM, kupitia vyombo vya dola vilivyokuwa chini yake kama amiri jeshi mkuu.
Kwa hivyo, alichokisema Rais Magufuli kinaakisi kabisa siasa za Muungano kuelekea Zanzibar. Mtazamo wa kuiona Zanzibar iliyozidi kudhoofika, iliyozidi kugawika, na hivyo iliyo rahisi kutawalika na kudhibitika.
Binafsi simuoni kuwa Rais Magufuli, akiwa kama msimamizi mkuu wa siasa hiyo, ana kosa lolote. Kwa hakika hasa, huyu ni kiongozi ‘anayetekeleza’ wajibu wake katika hili, kwa kiwango kile kile ambacho rais wa Marekani anapotekeleza wajibu wake kwenye siasa za nje za taifa lake akiuma na kupuliza kwenye mizozo ya mataifa ya Ghuba na Mashariki ya Kati.
Kosa kubwa litakuwapo pale ambapo yeye na wenzake watataka kutulazimisha sisi kuamini kinyume na hiki wanachokihubiri. Kwa mfano, wakitulazimisha sote tuwaone kuwa wao ni watetezi wa amani, maendeleo na utangamano wa Zanzibar, na kutuadhibu pale tunapowaeleza kuwa hivyo sivyo kabisa walivyo, hapo watakuwa wanatuonea vikubwa!
Kosa jengine kubwa ni kwa hao wanaoelekezewa siasa hii ya Muungano, yaani Wazanzibari wenyewe. Ikiwa zaidi ya nusu karne tangu kubuniwa na kutekelezwa kwa siasa hii, bado hawajang’amua kuwa ipo na inatumika dhidi yao, taifa lao na utambulisho wao, basi hiyo ni dhambi kubwa. Ikiwa wameng’amuwa na wanaipendelea iendelee, basi huo ni uhaini mkubwa dhidi ya taifa lao.
Ama endapo wameng’amuwa na wanaipinga isiwepo, japo kama hadi sasa hawajafanikiwa, hayo ni mapambano ya fakhari. Waendelee nayo hadi pale siasa ya Muungano huu kuelekea nchi yao itakapobadilika, na watawala wafahamu kwamba unaweza kuwa na Zanzibar imara na yenye nguvu, kwa upande mmoja, na wakati huo huo Muungano madhubuti wenyevheshima na adabu kwa pande zote.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 13 Juni 2017