UCHAMBUZI

Zanzibar ijifunze maana ya mapinduzi kutoka Oman

Kwa makusudi kabisa, wenye satwa ya kutunga sera na mwelekeo wa taifa letu wanataka ionekane kama kwamba uhusiano kati ya Zanzibar na Oman ulianza mwaka 1832 pale Sayyid Said bin Sultan Al-Busaid alipoanzisha utawala wake kisiwani Unguja na kisha kuhamishia rasmi makao yake makuu kutoka Maskat na kuyaleta kisiwani hapo miaka minane baadaye. Wakirudi nyuma zaidi, watakutajia 1698 baada ya kumalizika Vita vya Wareno.

Lakini ukweli ni mwengine. Mahusiano ya kijamii na kitamaduni kati ya Oman na Zanzibar hayakuletwa na Waomani waliokuja kusaidia kumuondoa mtawala wa Kireno wala waliokuja karne mbili baadaye kutawala, bali yalianza karne kadhaa kabla ya hapo. Tarehe inarejea zaidi ya miaka elfu tatu nyuma, ambapo mahusiano na maingiliano kati ya jamii za pwa za Bahari ya Hindi yalianza kushamiri na Oman na Zanzibar zikiwa sehemu ya mafungamano hayo.

Kwa hivyo, milango baina ya pande hizi haikufunguliwa kwa Vita vya Mreno wala kuhamia kwa Sultan na wala kufungwa mwaka 1964 ulipoporomoka usultani wa Jamshid bin Abdallah Al-Busaid. La hasha! Mahusiano makubwa yalishakuwepo kabla ya siasa hizo, yakiwa yameweka mizizi yake kwenye damu za watu wetu – tamaduni zao, lugha zao na imani zao. Athari iliyopo baina ya pande hizi ni kubwa na kongwe mno kuliko miaka mia mbili kasoro kidogo tangu utawala wa Kisultani uanzishwe Zanzibar.

Ni bahati mbaya sana kuwa fitina za kisiasa zilizopandikizwa mwanzoni mwa karne ya 20 zikichanganywa na hila za kidini kwa malengo ya ukoloni wa Ulaya, zilifanikiwa kuyapa jina baya mno mafungamano haya kiasi cha kwamba miaka kadhaa baadaye, chuki dhidi ya chochote kinachohusishwa na Oman ‘ikahalalishwa’, huku athari yoyote njema iliyowachwa na mafungamano hayo ikitiliwa shaka.

Bahati mbaya zaidi ni kuwa Zanzibar, kama taifa, ndiyo iliyojikuta muhanga mkubwa zaidi wa ujengwaji wa taswira hii mbaya kwa sababu tu ya kuwaridhisha wale tuliowataja awali kama ndio wenye nguvu za kuweka mwelekeo ya wapi nchi iende. Hawa, kwa maslahi yao ya kutawala, wameitia gizani Zanzibar katika jitihada zao za kuyanajisi mafungamano yake na Oman na mataifa mengine ya Bahari ya Hindi.

Lakini, miongo mingi baada ya uchafuliwaji huu wa makusudi wa historia na mualaka baina ya pande hizi mbili, sisi wa kizazi cha sasa hatuna tena sababu za kufungwa kwa minyororo yao, bali tuna wajibu wa kuangalia mbele zaidi ya pale pua zetu zinapofikishwa na kufikiri nje ya duara ambalo akili zetu zililelewa.

Lile duara la chuki, hasama na ubaguzi, lile giza la khofu na mashaka, ambalo ndani yake tulikuzwa, sasa tunapaswa kulivunja na kuyasaka yale mengi mema na mazuri ambayo Oman na Zanzibar zinayo kati yao.

Kila upande una ya kujifunza kutoka mwengine, hasa kwa kuwa kile kiungo madhubuti cha kijamii na kitamaduni kimesalia hadi leo, licha ya mkufu wa kisiasa kudumuka. Nakusudia kuwa Oman na Zanzibar zilikutanishwa kwanza na kwa karne kadhaa na jamii na tamaduni zao, mahusiano ambayo yaliweza kubakia na kuselelea hadi leo, hata baada ya mahusiano ya kisiasa yaliyokuja kuzuka na kuzimika kwa muda mchache mno wa historia hiyo.

Kwa jicho la Kizanzibari, nimeona jambo moja muhimu sana la nchi yangu kujifunza baada ya ziara yangu ya juma moja nchini Oman, nalo ni maana halisi ya mapinduzi. Mataifa haya mawili yanakutana kwenye hili pia kama yanavyokutana kwenye mengine.

Tunajuwa kuwa mnamo mwaka 1964, visiwani Zanzibar kulifanyika kile ambacho wale niliowataja hapo juu kuwa ndio wenye nguvu za kuamua muelekeo wa nchi wanakiita mapinduzi. Japokuwa sio sote tunaokubaliana na dhana hiyo – ya kukiita kilichotokea siku ya tarehe 12 Januari 1964 kuwa mapinduzi, maana wengine tunaamini ulikuwa ni uvamizi wa dola moja dhidi ya nyengine – lakini ukweli usiopingika ni kuwa tukio hilo ndilo lililiondowa madarakani serikali ya muungano wa vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) na kwalo ukaanguka mfumo wa utawala wa Kisultani, ambao chimbuko lake ni mwaka 1832.

Miaka sita baadaye, yaani mwaka 1970, nchini Oman nako kulitokea tukio la kubadilisha utawala wa nchi kwa kutumia nguvu. Haya yakaitwa ‘Mapinduzi ya Kasri’ kwa kuwa mtoto wa Sultan Said bin Taimur Al-Said aitwaye Qaboos bin Said ndiye aliyemuondoa baba yake madarakani.

Kwa hivyo, panapohusika dhana ya kuuondoa utawala ulio madarakani kwa kutumia nguvu, zote mbili – Zanzibar na Oman – zilifanya hivyo kwenye historia yake ya hivi karibuni. Lakini nchi hizi mbili zinatafautiana pakubwa kwenye dhana yenyewe – yaani utokeaji wa tukio lenyewe, sababu zake, utekelezwaji na watekelezaji wake: na tafauti hizo zinafanya kuwe na utafauti pia kwenye matokeo yake.

Kwanza, Sultan Qaboos aliingia madarakani kwa nguvu akimuondoa baba yake kwa sababu aliamini mzee wake huyo hakuwa akifanya ya kutosha kutumia rasilimali za mafuta na gesi asilia kulifanya taifa lake kuwa la kisasa. Raghba ya maendeleo aliyokuwa nayo nafsini mwake ilikuwa inamuambia kuwa mzee wake hakuwa tena uwezo wa kuipeleka mbele nchi zaidi ya pale alipokuwa ameshaifikisha na kwamba kama angelisubiriwa hadi aondoke duniani ndiyo taifa lisonge mbele, huenda ingelizidi kurudi nyuma.

Sera za baba yake zinatajwa na wanahistoria kuwa ziliifanya Oman ya wakati huo kuwa na asilimia 75 ya vifo vya watoto wadogo, huku maradhi yanayotokana na njaa na uchafu yakisambaa. Hadi Sultan Qaboos anaingia madarakani, nchi nzima ilikuwa na skuli tatu tu, ambapo Waomani waliojuwa kusoma na kuandika walikuwa asilimia tano tu na ni meli 6 pekee za barabara ndizo zilizokuwa zimetengenezwa.

Hii ni kusema kuwa msingi wa Mapinduzi ya Qasri ya tarehe 23 Julai 1970 ulikuwa ni kiu ya maendeleo tu na si chengine. Haikuwa kupapia madaraka, haikuwa chuki dhidi ya aliyeshikilia madaraka. Haikuwa hisia za ubaguzi dhidi ya waliopo.

Sultan Qaboos na waliomuunga mkono kwenye mapinduzi yake yasiyo umwagaji damu hawakumuona baba yake kuwa mtawala wa kigeni au kibaraka wa wageni, na wala hakuwachukulia waliomuunga mkono baba yake kuwa walikuwa wasaliti na wasiokuwa wazalendo kwa nchi yake. Baada ya yote, Taimur alikuwa baba yake, naye ndiye mwana pekee wa kiume, na wengine wote kwenye utawala walikuwa ndugu na jamaa zake. Walikuwa Waomani.

Ndio maana, mara tu baada ya kuingia madarakani, Sultan Qaboos alijielekeza moja kwa moja kwa lile alilokuwa limempeleka pale, ambalo ni kuleta maendeleo kwa taifa lake. Leo hii, hata nusu karne bado, Oman ni moja ya mataifa yenye mfumo imara kabisa wa kiafya duniani, ambapo asilimia 99 ya wakaazi wake milioni nne unusu wana fursa ya huduma bure na bora za matibabu, ikishikilia nafasi ya nane duniani, kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Wastani wa kuishi ni miaka 76.

Kwenye elimu, idadi ya wajuwao kusoma na kuandika ni asilimia 90 kutoka ile ya asilimia tano na kwenye miundombinu, Oman sasa imewekeza dola bilioni 20 kwa kipindi cha miaka 15 ijayo kuimarisha muenekano wake. Hivi leo, Oman imesimama kama taifa linalokwenda mbele kimaendeleo kwa kuwa msingi wa mapinduzi yake ulikuwa ni maendeleo. Fikra kuu iliyosukuma mapinduzi hayo ilikuwa ni kuiondoa nchi kutoka ilipo kuipeleka pengine pazuri zaidi. Hakika, hata katika kuiadhimisha kwake, tarehe 23 Julai inaitwa “Siku ya Mwamko wa Oman” na sio “Siku ya Mapinduzi ya Oman”.

cofHali ilikuwa tafauti kwa kile kilichotokea kisiwani Unguja tarehe 12 Januari 1964, ambapo waliohusika nacho wanadai kilikuwa ni kitendo cha kumuondoa ‘mtawala mgeni ‘kwenye ‘ardhi ya mwenyeji’, na ndiyo maana – kwa itikadi hiyo ya kumuondoa mgeni – yakajiri mauaji makubwa ya kikatili na matendo mengi ya kinyama dhidi ya waliotafsiriwa kuwa wageni, yakifuatiwa na kukinajisi kila kilichonasibishwa na ‘mgeni’ huyo.

Mapambano dhidi ya ‘mgeni’ huyo na ‘ugeni’ wake, kwa hivyo, yakawa ndiyo falsafa na dira ya utawala uliongia madarakani baada ya hapo na ambayo yameyaathiri maisha ya Zanzibar kama taifa, Uzanzibari kama utaifa na Wazanzibari kama raia tangu hapo hadi leo.

Tangu hapo hadi leo, fikra ya kinachoitwa “Mapinduzi ya Zanzibar” ni vita dhidi ya mgeni – kimaneno, kisilaha, kisiasa na kisaikolojia. Waumini wa “Mapinduzi” hayo wanajiona kama kwamba bado wangali wamesimama kwenye uwanja wa mapambano dhidi ya mgeni waliyemtengeneza akilini mwao, nao wakijifanya ndio hao ati ndio wenyeji wenyewe.

Miaka 50 iliyopita, ungelichukuwa picha za Oman na Zanzibar na kuziweka kwenye fremu moja, ungelipata taswira ya utafauti mkubwa mithali ya mchana na usiku – ya Zanzibar ungeliifananisha na kito cha thamani kwenye nuru, ya Oman kito cha thamani gizani.

Bahati mbaya, miaka 50 baadaye, taswira imegeuka kama anavyosema mshairi mashuhuri wa karne ya 19, Muyaka bin Hajj Al-Ghassany: “Kwinamako hwinuka, kwinukako kukainama.” Zanzibar ndiyo sasa iliyo upande wa gizani na Oman iliyo nuruni.

“Kila (cha kimaendeleo) unachokiona mbele ya macho yako leo, hakikuwepo miaka 47 iliyopita,” aliniambia mwenyeji wangu mmoja wakati akinitembeza kwenye viunga vya mji mkuu wa Oman, Masqat. Jibu langu lilikuwa: “Hapa hasa ndipo yalipofanyika mapinduzi!”

Tanbihi: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 4 Aprili 2017.

3 thoughts on “Zanzibar ijifunze maana ya mapinduzi kutoka Oman”

 1. Kweli bwana Ghassani uliyo andika ni ukweli mtupu kwa kuwa uliweka buti lako Oman na ukajionea mapinduzi ya kweli ambayo wananchi wake wanafurahia matunda ya miaka takriban 47 sasa…ahsante mkuu.

 2. Ya Zanzibar hayakuwa Mapinduzi bali ni Uvamizi wa wageni kuvamia nchi yetu.

  Mapinduzi siku zote huletwa na raia au wazalendo wa nchi husika.
  Inapokuwa wahusika ni Wageni waliotoka nchi jirani, huwa ni Uvamizi ( Invasion).

 3. COMPARE & CONTRAST
  ZANZIBAR NA OMAN
  Kwakuwa nime bahatika kuishi katika nchi zote hizi mbili, nimekuwa na nafasi nzuri ya kulinganisha maendeleo ya nchi hizi.
  Ki maendeleo, tafauti ya Oman na Zanzibar ni kama mbingu na ardhi.
  Oman ikiwa juu na Zanzibar ikiwa chini kwa kila sekta.
  Kabla ya Mavamizi ya tarehe 12 January 1964, Zanzibar ilikuwa juu kimaendeleo kuliko Oman na nchi nyengine za Bara Arabu.
  Ama kwa desturi na silka tunalingana sana isipokuwa kwa sasa desturi na silka zetu Zanzibar zinaharibika kwa kasi kubwa sana kwasababu ya ujio mkubwa
  wa wageni.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.