KISWAHILI KINA WENYEWE

Baina ya mkandarasi na kandarasi – 2

Nimetangulia kusema kwamba hayo niliyoyaeleza kabla hayakuwa yamenishughulisha sana kwa sababu, mtu aweza kuwa na hiari ya kutumia maneno kandarasi/makandarasi au mkandarasi/wakandarasi, akusudiapo kuwa ni mtu. (Mimi nitaendelea kutumia kandarasi/makandarasi – tena bila ya wasiwasi wowote!)

Lakini yaliyonishughulisha, na hata kwa kiasi fulani kunishtua, ni hii kauli, na amri, ya Dkt. Chipila: “…Tunapokutana kwenye hadhara kama hizi tunapaswa kuzungumza Kiswahili Sanifu. Tunapaswa kukubali kuacha ‘viSwahili’ vyetu vya sehemu tunapotoka… Kila mmoja akizungumza ‘Kiswahili’ chake, tutapotezana.” Na kauli hii ikaungwa mkono na Bwana Majid Mswahili alipoandika, “Na hii bila shaka ndio dhima ya usanifishaji Lugha. Ama sio Dkt. Chipila?”

Na Mwalimu Abdilatif Abdallah

Baada ya dakika chache, Dkt. Chipila akaendelea, “… Nimewahi kukutana na matini moja ya lahaja ya Kimwani izungumzwayo Msumbiji. Wakija hapa wakaleta maneno yao, tutakimbiana. Tena tusiende mbali hadi kule kusini. Hapa Unguja, ukifika Makunduchi ukawasikia wanavyozungumza, wewe Mswahili huenda usiambulie mchele wala pumba.”

Bwana Majid akarudi baada ya dakika nane, na akaendelea na kuunga mkono, kwa kuandika (na namnukuu chapa kwa ya pili), “Viswahili vyetu tunavipenda sana ni kweli lakini katika upevukaji wa Kiswahili ni muhimu au ni lazima tukubali matumizi ya Lugha yetu kwa mfanano (Usanifu). Mfanano huu bila shaka utasababisha baadhi ya maneno yetu kutoka katika viswahili vyetu tusiyatumie kwenye Kiswahili. Vinginevyo, tutakuwa na tofauti kubwa katika Lugha yetu. Mathalani: tunzo na tuzo, tafauti na tofauti, nk….”

Hizi fimbo za Dkt. Chipila na Bwana Majid napigwa mimi. Bahati yangu ni kwamba nina mwili sugu! Tangu niwemo humu katika kikundi cha Watetezi wa Kiswahili Tanzania (WAKITA), sasa ni kiasi cha mwezi mmoja na kitu tu. Kwa hivyo ningali mgeni. Na, twaambiwa, mgeni hachomi pweza. Nimeingia humu baada ya Bwana Majid kunialika, nilipokutana naye Dar es Salaam mwezi wa Januari mwaka huu. Nami nikaukubali mwaliko wake. Na tangu wakati huo nimeshashiriki mara nne hivi kutoa maoni yangu kuhusu maneno yaliyokuwa yakijadiliwa.

Katika baadhi ya maoni yangu hayo, nimepata kuyafafanua au kuyatolea ushahidi niliyoyaeleza kwa kuyategemeza kwenye maneno ya asili ya Kiswahili kutoka, kwa mfano, lahaja za Pwani ya Kenya, Kimtang’ata na Kipemba. Na pia nimekuwa nikiyaandika baadhi ya maneno kwa namna ambayo pengine wengi wetu hatukuzowea kuyaona yakiandikwa au yakitamkwa hivyo: kwa mfano kuandika ‘tafauti’ badala ya ‘tofauti’; ‘marakibisho’ badala ya ‘marekebisho’; ‘harufu’ badala ya ‘herufi’; na kuyatumia maneno taazia kwa ‘tanzia’; na ‘tuzo’ kwa ‘tunzo’. Pia kuna wakati ambapo nililitumia neno ‘mwiku’ (ambalo labda halikuzowewa hapa), lakini nikaliandamiza na neno ‘kiporo’ katika mabano.

Nina hakika kwamba katika maelezo yangu hayo (mbali na kutolea mifano) sikupatapo hata mara moja kutumia hivyo ‘viSwahili’ vya sehemu ninapotoka. Au kuna mahali popote katika maelezo yangu hayo ambapo nimeandika kwamba tutumie “ ‘viSwahili’ vyetu vya sehemu tunapotoka”?

Kama nimesahau, naomba nikumbushwe. Au, kwani, hayo maelezo yangu sikuyaandika kwa Kiswahili ambacho kila mtu amekielewa bila ya kutatizika nacho? Kama ni ndivyo, basi tatizo ni lipi hapo? Je, wasomaji “hawakuambulia mchele wala pumba”? Au hicho si ‘Kiswahili Sanifu’?

YATAENDELEA, inshaAllah.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.