KISWAHILI KINA WENYEWE

Ni “tanzia” au “taazia”?

_dsc1163Chembelecho (au chambilecho, au chambacho) msemo wa Kiswahili, “Kipya kinyemi, kingawa kidonda.” Ni dasturi ya baadhi ya watu kuvutiwa na kipya kitokacho kwengine, hata kama tangu hapo wanacho chao wenyewe kifananacho na hicho cha kigeni. Hili swala la maneno kama “mubashara” lina tanzu mbili. Utanzu wa kwanza ni huo wa kupenda kukimbilia maneno  ya kigeni, hata kama tunayo yetu wenyewe yenye maana hiyo hiyo. Kama ilivyokwisha elezwa, kabla ya habari “mubashara” tumekuwa tukisema habari/ ripoti za moja kwa moja, au za papo kwa papo (wala si “papo” pekee).

 

Hata hivyo, maadamu neno, au maneno, yameshaanza kutumiwa katika lugha fulani – na yakawa hayendi kinyume na sarufi au mawako ya lugha hiyo iliyoyapokea – hapana ubaya kuyatumia maneno kama hayo kuwa ni visawe. Kudumu au kutodumu matumizi yake kutategemea wazungumzaji na waandikaji wa lugha hiyo. Wakiendelea kuyatumia yatadumu, na wakitoyatumia yatasahaulika na kupotea. Hatuwezi kuyalazimisha yabakie au yapotee.

Utanzu wa pili watokana na ile tabia ya watu wengine kupenda kufasiri neno kwa neno. Yaani watu kama hao huwa na lazima ya kupata neno moja tu la Kiswahili ili liwe ni tafsiri ya neno la lugha ya kigeni. Kuna baadhi ya maneno ambayo huwa hayakubali kufasiriwa hivyo, haswa iwapo lugha mbili hizo hazina asili au mzizi mmoja. Iwapo neno kama hilo halifasiriki kwa neno moja la Kiswahili, basi ni vizuri zaidi kulifasiri kwa zaidi ya neno moja, au kwa kishazi cha maneno. Wala huwa hakuna haja ya kuanza kubuni maneno ambayo watu hawatayatumia, bali yatabaki vitabuni tu.

Mosi, ni muhimu tuelewe kwamba si wazungumzaji wote wa Kiswahili walitumiao neno “tanzia.” Katika sehemu nyengine neno lijulikanalo ni “taazia”. Kwa mfano, Pwani ya Kenya neno tulitumialo ni “taazia.” (Kama ambavyo wengine husema “tunzo” na kitenzi chake ni “kutunza,” hali ya kwamba sisi twasema “tuzo” na “kutuza”). Haya ni miongoni mwa maneno ya asili yaliyobadilishwa matamshi na baadhi ya watumiaji. Sitalishughulikia swala hili leo, kwa sababu nataka kurudi kwenye maana ya tanzia/taazia.

Pili, nakubaliana kabisa na maelezo ya kwamba bila ya kifo hakuna tanzia/taazia. Kwa sababu maana ya tanzia/taazia ni habari zilizopokewa za kifo kilichotokea mahali mbali na pale habari hizo zilipopokewa. Kwa mfano, mimi niliyeko Ujerumani niletewapo habari ya kifo kilichotokea Tanzania, nitakuwa nimepokea tanzia/taazia. Na nikimpa pole aliyefiliwa na mtu wake, nitakuwa ninampa mkono wa tanzia/taazia, au ninamtaazii (kitenzi kitokanacho na nomino “taazia.” Sidhani kama kuna kitenzi kitokanacho na “tanzia.” Na hili latuonyesha dalili ya kwamba neno la asili ni “taazia”).

Asili ya neno hilo ni lugha ya Kiarabu; na mzizi wake ni -‘azza. Mzizi huu una maana zisizopungua tisa. Miongoni mwa maana hizo ni kusikitika/kuhuzunika kwa sababu ya lililotokea; kwa mfano, kifo. Ndiyo sababu katika Uislamu unapokwenda kumpa mkono wa taazia/ kumtaazii aliyefiliwa, wazungumzao Kiarabu humwambia huyo aliyefikwa na msiba, “A’adhwama-Llahu ajraka wa-ahsana ‘azzaaka wa-ghfir limayyitika.” Maana yake: Mwenyezi Mungu azifanye kubwa thawabu za msiba wako, na akupe kizuri cha kukuliwaza, na amghufirie maiti wako.” Na aliyefiliwa hujibu, “Istajaaba-Llahu minka waghfir laka wa-liwaalidayka.” Yaani “InshaAllah Mwenyezi Mungu ataikubali dua yako na atakughufiria wewe na wazazi wako.”

Tatu, hiyo maana ya tanzia/taazia iliyotolewa (na Bwana Majid Mswahili (?) hapo juu, ni maana ya taaluma ya Fasihi, ambayo kwa Kiingereza huitwa tragedy.

Kwa hivyo, basi, ikiwa katika hiyo ajali ya treni hakuna aliyekufa, hakuna tanzia/taazia ya kupokewa; itakuwa ni ajali tu.

1 thought on “Ni “tanzia” au “taazia”?”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.