KISWAHILI KINA WENYEWE

Ni “kiasi cha…” sio “kiasi ya…”

AbdilatifKwa uchache wa nifahamuvyo, lugha fasaha ni kusema “kiasi cha…”, basi haidhuru iwe ni kwa watu au kwa vitu. Yaani, kiasi cha watu kumi, au kiasi cha miti kumi. Kama  ambavyo twasema, kitabu cha…, kisa cha…, kiatu cha…, kitambo cha…, na kadhalika, wala hatusemi kitabu ya…, kisa ya…, kiatu ya…, wala kitambo ya… Na ni hivyo kwa sababu maneno yote hayo yamo katika ngeli ya KI/VI. Basi ikiwa kwa maneno hayo niliyoyatolea mfano hatuyatumilii “ya”, kwa nini iwe kwa neno “kiasi”?

Nionavyo mimi ni kwamba hayo ni katika jumla ya yale makosa yanayorudiwarudiwa kwa miaka mingi, mpaka mwisho watu wakayazoea na wakafikiri, au wakafikirishwa, kuwa ni matumizi sahihi.

Ni kama ule mfano wa neno “vita” litumiwavyo na baadhi ya watu. Twawasikia au kuwaona watu wengine wakisema au wakiandika “vita hii”, au “vita ya…” badala ya “vita hivi” au “vita vya…” – ambayo ndiyo fasaha. Kwa asili, neno “vita” ni wingi wa neno “kita”, ambalo lilikuwa likitumika katika lugha ya kale. Baadaye, kutokana na mabadiliko yanayozipitia lugha zote, neno “kita” likapungua matumizi yake na hatimaye kupotea kabisa. Hivi leo ni watu wachache mno wajuao kwamba kulikuwa na neno/ nomino “kita”, na kwamba kitenzi chake kilikuwa ni -ta: (kuta = kupiga).

Kwa mfano, kitenzi hiki kimetumiwa katika Utenzi wa Inkishafi, utenzi maarufu uliotungwa katika karne ya 19 na Sayyid Abdallah A. Nassir. Katika ubeti wa 14 wa utenzi huo, mtunzi anayafananisha maisha ya duniani na kisima kisichokuwa na ukingo, na ambacho karibu yake kuna mwana ng’ombe ambaye humpiga pembe mtu yoyote anayekikaribia kisima hicho. Ubeti huo ni huu:

Ni kama kisima kisicho ombe
Chenye mta paa mwana wa ng’ombe
Endao kwegema humta pembe
Asipate kamwe kunwa maiye

Kuna mwenzetu mmoja aliyependekeza kwamba kwa binadamu kutumiwe neno “idadi” badala ya “kiasi”. Maneno haya mawili yana tafauti ya maana. Usemapo, kwa mfano, “Walikuja kiasi cha watu kumi” maana yake ni kwamba watu waliokuja yaweza kuwa walitimia kumi, au

walikaribia kumi, au walizidi kidogo ya kumi. Hali ya kwamba ukisema,”Idadi ya watu waliokuja ni kumi,” maana yake ni kwamba walikuwa kumi – hakuzidi hata mmoja wala hakupungua hata mmoja.

Hayo ndiyo niyafahamuyo kwa uchache wangu.

 

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.