UCHAMBUZI

Januari 27: Walikuwa watu, hazikuwa nambari tu

Mwandishi nguli visiwani Zanzibar, Maalim Ally Saleh, ameandika makala makhsusi kuwakumbuka wahanga wa matukio ya Januari 26 na 27, 2001. Ni makala ambayo imeshiba taarifa za kweli na kila mwenye kuipenda na kuitakia mema Zanzibar, haachi kutiririkwa na machozi iwapo ataisoma.

tomondo

Ndani ya moja ya makala hii anatajwa kijana mmoja aliyepigwa risasi barazani kwao na wala si kwenye maandamano au barabarani! Kama mara moja alivyowahi kuandika Mohammed Ghassani, “hayakuwa majina wala nambari tu, bali walikuwa watu halisi waliouawa na vyombo vya dola”, nami licha ya kuwa mshiriki wa maandamano hayo yaliyogeuzwa machinjio na serikali, pia nilimjuwa kijana huyu aliyetajwa humu. Nitasimulia kidogo.

Nilikutanishwa na kijana huyu jijini Dar es Salaam na sahibu yangu, Ahmed Miraj, ambaye anaishi London siku chache kabla ya kuuawa kwake. Ahmed na kijana huyo walifika nyumbani kwetu mishale ya saa 9 mchana, wote wawili wakiwa na wamevalia kanzu. Ilisadifu hivyo kutokana na ukweli kwamba mbali ya kuwa kwao watu wa ibada, siku hii pia ilikuwa Ijumaa.

Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris

Ndani ya uzio wa nyumba yetu mulikuwa na minazi minne aina ya Kitamli na wakati huo ilikuwa imezaa na kupangatia makole ya nazi kavu, madafu na makoroma. Baada ya Ahmed kunitambulisha kwa kijana yule na mara baada ya kujuwana, niliwakabidhi kisu ili wale madafu kiasi wapendacho.

Nakumbuka, mara baada ya kuwakabidhi kisu, kijana huyu ambaye jina lake silikumbuki tena, alifurahi na kutowa msemo ambao umeganda kichwani mwangu: “Ahmed, leo najuwa tumbili kashasusiwa shamba la muhogo”, na sote tukaanguwa kicheko. Lakini pamoja na kusema hivyo, alikula madafu mawili tu na Ahmed akala matatu, jambo lililopelekeya Ahmed amcheke sana.

Tulikaa nyumbani kwetu takribani saa nzma na tukaondoka pale baada ya kusikia adhana ya al-Asr ikiadhiniwa. Tulitembea taratibu tukikatiza kwenye chochoro za Buguruni Kisiwani, mahali ambapo mimi na Ahmed tumekulia, huku tukikumbushia mengi kwenye chochoro zile. Muda wote, mgeni wetu alikuwa akitusikiliza na kuchomekea vijineno vya maskhara hapa na pale hadi tulipofika kwenye msikiti maarufu wa Makukula, ambapo tulitia udhu na kusimama kwenye safu na wenzetu kwa sala ya al-Asr.

Baada ya kukamilisha jukumu la sala tulitoka na kuanza safari ya kuelekea Ilala Sharifu Shamba, ambako tulienda kumuona bwana mmoja, ambaye mwenzetu huyu alikuwa na mzigo wake aliokabidhiwa na mdogo wake aliyekuwa akiishi nchini Denmark na kijana yule. Nakumbuka ilikuwa ni kompyuta ya mkononi aina ya Siemens. Tulitembea kwa miguu taratibu na tukafika safari yetu muda ya saa 11:10 jioni. Tulikabidhi mzigo kwa muhusika na bila kukawia tukaondoka hadi kituo cha mabasi cha Ilala Bungoni. Hapo ndipo ilikuwa ni mara ya mwisho katika uhai wetu mimi na Ahmed kuagana na mwenzetu yule, kwani siku iliofuata alikuwa ndio anasafiri kwenda Pemba kupitia Unguja na Ahmed anasafiri kwenda kumuona kaka yake mkubwa mkoani Tanga.

Kati ya Januari 24 au 25, wakati nikiwa nimekodowa macho yangu kwenye televisheni, nikamsikia aliyekuwa mkuu wa polisi wa Tanzania, Inspekta Jenerali Alhajj Omar Mahita, akijitapa mbele ya vyombo vya habari akisema “Kama wao (CUF) ni ngangari, basi sisi ni ngunguri na nitahikikisha kwamba siku hiyo hata ndege hawatoruka angani!” Kutokana na kauli ile, nikajuwa kwamba ipo dhamira ya kweli ya kupambana na waandamanaji kwa gharama yoyote iwayo.

Januari 26, mara baada ya sala ya Ijumaa yalianza mauwaji ya kwanza, ambapo imamu wa Msikiti wa Mwembetanga aliuawa ingawa maandamano hasa yalikuwa yamepangwa Januari 27! Kwangu hii ilikuwa ni salamu nyingine kwamba kazi ingelikuwa ya gharama kubwa.

Pamoja na vitisho vya Mahita, nilishuhudia siku ya tarehe 27 Januari maandamano yakifanyika kwenye jiji la Dar es Salaam, ambapo polisi ‘walirambwa chenga ya mwili’ baada ya wao kutanda kila mahali kwenye mtaa wa Uhuru na waandamanaji kupita na mabango kwenye mtaa wa Lindi ambapo walitembea hadi jirani na viwanja vya Kidongo Chekundu na kufanikiwa kuongea na wanahabari!

Baada ya hapo wakatawanyika na punde kazi ikaanza kwenye eneo la Kariakoo, ambako walikamatwa watu wengi hasa waliokuwa wamevalia kofia za baraghashia hata kama hawakuwa waandamanaji. Ukweli ni wengi walikuwa wazee waliokuwa maeneo yale kwa kazi zao nyingine, lakini kwa vile ilishajengwa kwamba CUF ni chama cha Waislamu, kila mvaa kofia siku iyo alikiona cha mtema kuni!

Binafsi nilishuhudia raia wa kawaida wakikamatwa kwa wingi na kushushiwa vipigo vya kinyama na naweza kuthibitisha kuwa hao hawakuwa waandamanaji. Waandamanaji walikuwa na umakini wa ziada ambapo hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyenaswa.

Eneo la Kariakoo lilivurugika na punde mji ukazizima baada ya maduka yote kufungwa. Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, mimi na mwandishi mmoja wa gazeti la An-Nuur tulilazimika kuondoka mahali pale na mimi nikashika njia kurejea Buguruni huku macho yangu yakiwa yameshiba sumu ya gesi ya machozi.

Ilikuwa muda wa saa 6 mchana kamili nilipowasili nyumbani kwetu. Mara nilipoingia ndani, mlango wangu ukagongwa na shemegi yangu mkubwa ambaye mara baada ya kuniona, alianguwa kilio kubwa. Nilimtuliza ili anieleze kilichotokea. Ndilo akanieleza kwamba yule jamaa aliyekuja nyumbani na Ahmed wakala madafu, alikuwa a mepigwa risasi barazani kwao na kufariki papo hapo. Hii ni baada ya Ahmed kunipigia simu mara tatu akiwa na lengo la kunifahamisha juu ya dhulma aliyofanyiwa kijana mbichi akiwa mbele ya uso wa mama yake mzazi!

Pamoja na mengine mengi, lakini naikumbuka Januari 27 ndani ya kichwa changu mukiwa na dowa hilo. Walioyafanya haya hawakuguswa lakini tuwakumbushe kwamba Mwenyezi Mungu ametowa maneno haya ambayo wanapaswa kuyazingatia vichwani mwao. Anasema “Layyadum dhalimin illa khasara. Layyadum dhalimin illa dhalalah. Layyadum dhalimin illa tabbara” Hii ni ahadi ya Allah kwa kila mwenye kufaidi pumzi yake pasi kuilipia kodi.

Ewe Mwenyezi Mungu, hakika sisi waja wako ni madhaifu wa kupitiliza. Twakuomba tuondoshee dhulma hizi kwenye ardhi yetu ya Unguja na Pemba. Tumeuawa, tumelawitiwa, tumebakwa, tumepigwa, tumeumizwa na tumefanywa wakimbizi. Tumefanywa yote hayo na viumbe vyako ambavyo vinalinda madaraka yao kwa gharama yoyote iwayo.

Basi twaja kwako tena na tena kukuomba utupe utulivu wako, kwani hao wenye kutufanyia haya si lolote si chochote mbele yako. Tumechoka waja wako na idhilali hizi za kuteswa kwa sababu tu ya kupigania haki zetu.

Tupe nusura yako Ya Ilahi na uibariki Zanzibar na watu wake!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.