Jamii ya Kizanzibari inapitia kwenye vipindi vyake vya mabadiliko kama zilivyo jamii nyengine zozote za kibinaadamu. Kubadilika kwa jamii huwa ni sehemu muhimu ya maisha na, kwa hakika, si adui wa maisha ya mwanaadamu.
Lakini ili mabadiliko yawe na maana kwa maisha ya jamii inayohusika, yanapaswa kuakisi ipasavyo misingi iliyoijenga jamii hiyo katika imani yake, falsafa yake, na taasisi zake. Taasisi kuu ya malezi ya kila jamii duniani ni familiya, majirani, skuli au madrasa, na masuhuba ama marafiki.
Familiya ndio chimbuko la jamii, ndio skuli na madarasa ya mwanzo ambayo mwanaadamu huhudhuria na kujifunza. Familiya ikikaa sawa, kwa kiasi kikubwa sehemu nyengine za jamii hufuata njia hiyohiyo. Jamii ya Kizanzibari, ikiwa sehemu ya jamii pana ya Waswahili wenyeji wa Upwa wa Afrika Mashariki – inatoa nafasi ya pekee kwa familiya katika maisha ya watu.
Kuna hadithi, methali, misemo na masimulizi mengi kuhusiana na hayo, kwa mfano, nafasi ya wazazi kwenye maisha yetu, malezi ya mtoto, na mahusiano baina ya wanafamiliya. Waswahili huadhiana: “Mama ni mama, japo akiwa rikwama” kuonesha nafasi ya mama kwenye maisha ya mtu. Hutunga piya kitendawili: “Titi la mama litamu wala halinishi hamu” ambalo jawabu lake nij usingizi, kuonesha ladha ya malezi ya mama zetu. Lakini piya kwa wazazi huaswa kwa misem kama vile: “Samaki mkunje angali mbichi” kuwataka wawape mafunzo mazuri watoto wao tangu wakiwa wadogo, na au “Ukicha mwana kulia, utalia weye” unaoonya kuwa mzazi asiyetaka kumrekebisha mwanawe tangu akiwa mdogo, basi atakuja kulia kwa kumkuta mwanawe huyo amepotea ukubwani.
Baada ya familiya, taasisi za malezi ni majirani. Namo piya Waswahili wana hekima kubwa na nyingi sana zinazoutukuza ujirani na kuupa haki yake. Husemwa, kwa mfano, “Wema mtendee jirani” au “Jirani ndiye ndugu”, tukihimizwa nafasi ya jirani kwenye maisha yetu, maana ni yeye ndiye tunayemkimbilia tunapopatwa na matatizo au faraja, kabla ya hata ndugu wa damu, ambaye anaishi mbali nasi. Piya, kwa sababu ya umuhimu wake huo, ndipo piya wahenga hutuasa kwa kutuambia: “Hala hala na jirani”, yaani tuchukuwe tahadhari sana kwenye kuishi na majirani zetu kusudi tusije kuwakera na kuondosha mapenzi baina yetu.
Katika mapokezi ya Dini ya Kiislamu, ambayo ndiyo dini inayofuatwa na zaidi ya asilimiya 98 ya Wazanzibari, tunasimuliwa kuwa kiongozi wa dini hiyo, Mtume Muhammad (S.A.W) alikaribia kumuweka jirani kuwa mmoja wa warithi wetu kutokana na namna ambavyo alikuwa akihimizwa kumtendea ihsani na Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, ujirani mwema ni taasisi muhimu ya malezi na ujengaji wa maadili.
Ukiondoa familiya na majirani, malezi hufanywa piya na vituo vya elimu ambavyo watoto wetu huhudhuria, iwe ni elimu ya skuli au ya madrasa. Mote humo huwa munapandikizwa misingi muhimu kwenye vichwa vya watoto wetu, ambavyo ndivyo baadaye vinavyojenga jengo zima la ubinaadamu wao.
Wajapani husema: “Ukitaka kujuwa kinachoendelea mitaani, tazama kinachoendelea darasani”. Usemi huu unamaanisha kuwa, elimu wanayopata watoto wetu huakisika moja kwa moja na maisha watakayokwenda kuyaishi huko mbele ya maisha yao. Kutengenea kwa taasisi za kielimu huwa ni kutengenea kwa jamii zetu na kuporomoka kwake, huwa ni kuporomoka kwa jamii hizo.
Mbali ya familiya, ujirani na taasisi za elimu, nafasi nyengine muhimu ya malezi na makuzi ya jamii inatekelezwa na masuhuba walionao watoto wetu. Waarabu husema kuwa: “Nioneshe marafiki zako, nikuambie wewe ni mtu wa aina gani”, wakimaanisha kuwa masuhuba wanaombatana kwenye maisha huwa wana tabia ya kuathiriana na hatimaye khulka zao huwa moja. Kama wasemavyo Waswahili kuwa “Mkaa karibu na waridi, hataacha kunukia”, basi piya ni sawa kuwa mkaa karibu na karo, hatakosa kunuka uvundo!
Tamthiliya hii ya Tafrani inawahusu vijana wa Kizanzibari na namna wanavyoyaishi maisha yao katika jamii hii iliyojengwa kimaadili. Inalitazama kundi hili muhimu kwenye jamii na namna ambavyo taasisi zake za malezi – familia, majirani, skuli na masuhuba – zinavyoyagusa na kuyaathiri maisha hayo kwa namna ya kukinzana, kuachana na piya kushikana. Inauchambua uwezo na nguvu za kila taasisi kwenye yote mawili – kheri na shari – na kisha inatuongoza kwenye jawabu lake.
Kupitia mazungumzo na matendo ya wahusika wa tamthiliya hii, suali kubwa linalojaribu kujibiwa ni: Nini hasa kilichosababisha hata baadhi ya vijana hawa waliofunzwa maadili mema wakawa katika tafrani?
Katika gamba la nje kwenye picha neno Tamthiliya limeandikwa Tamtiliya “h” haipo
Ahsante Bwana Salmin. Marekebisho yanafanywa.