Uandishi wa hadithi fupi unafanana na uandishi wa ushairi. Mote muwili, mwandishi hulieleza jambo kubwa na zito kwa maneno machache. Bila ya shaka hadithi fupi ni refu sana kuliko shairi, lakini ni fupi sana kuliko riwaya au hata novela. Mshairi hutafautiana na mwandishi wa hadithi fupi kwenye matumizi ya lugha, mapigo ya sauti na muziki wa ndani. Kwenye mawili yote hayo, Ally Saleh si mwepesi. Ameandika tungo kadhaa za ushairi kama ambavyo ameandika hadithi kadhaa fupifupi. Msome hapa kwenye mkusanyiko huu wa La Kuvunda.
Anaandika kwenye dibaji yake:
“Wakati naendelea kushukuru kupewa pumzi na mwenye uwezo nazo Mwenyenzi Mungu, ambazo zinaambatana na uzima, afya na akili zilo razini, napenda mniruhusu nilete kwenu kazi yangu nyengine ya sanaa iitwayo La Kuvunda, ikiwa kazi yangu ya pili ya mkusanyiko wa hadithi fupi kufuatia Jumba Maro.
“Huwa inasemwa msanii ni kioo cha jamii, na mara nyingi hutarajiwa kuwa msanii ana jicho la tatu ambalo linaitizama jamii yake kwa kina zaidi, na kutokana na uwezo wa majaaliwa ya utumizi wa kalamu, basi mwandishi hutarajiwa kuandika mambo ambayo yataakisi yanayotokea katika jamii yake kwa maana nyingi tu; na chache zake ikiwa kuonyesha uovu, udhaifu, na upindaji wa mambo ambayo jamii hiyo imekubaliana.
“Kwa maana nyengine kazi ya sanaa inatakiwa izindue, ionyeshe jamii au itanabahishe, ijapokuwa kazi hiyo itakuwa pia, bila ya shaka, na burudani, ufundi wa lugha na hata virutubisho mbalimbali vyenye kuonesha uweledi falsafa na tamaduni za jamii husika.
“Kazi hii imeangalia matatizo ambayo mwandishi kwa jicho lake anaona yanaisokota jamii na ama hayasemewi, au yanasogezwa upenuni kwa kudharauliwa yakionekana ni ya kawaida: na watu husema cha kawaida huwa desturi.
“Lakini desturi mbovu ni mbovu tu na hazifai kulelewa au kufugwa. Na jamii ambayo haisimami au haiiunuki kupinga desturi hizo, basi nayo huoza kimaadili. Hakuna abishaye kuwa jamii yetu ya Zanzibar ina ustaarabu wenye tareikh kubwa, dini na uzingativu, lakini pia afanaleik tunakolekea sasa siko kabisa.
“Kwa hivyo, katika hadithi hizi nimejaribu kuchukua upana wa jamii na kuyatizama yale ambayo yanatutanza na kutosokota. Iwe ni utovu wa maadili, upotokaji, uonevu wa haki, utumiaji mbaya wa madaraka, ung’ang’anizi wa madaraka, ukandamizaji wa wanawake, ukandamizaji wa kisiasa, na jumla ya mambo mengine chemvu kizima ambayo ati yanachukuliwa ni ya kawaida na siku zinakwenda na zinapita.
“Hapana shaka, kwa kuwa jamii inaishi na mambo hayo, hayatamalizika kwa kuandikwa wala kuandikwa na mwandishi mmoja. Kazi na wajibu mkubwa wa msanii ni kuandika kutokana na wakati wake na fursa azipatazo na mwengine ajaye kuendeleza palipobakia.
“Kama vile aliyeonywa ataendelea kuonywa na anayeonya hatasita kwa kuwa ameonya, ndivyo binaadamu walivyo ni waja wa kukumbushwa. Na sanaa ina dhima hiyo hiyo ya kuendelea kukumbusha, asaayakunkher jamii itazinduka, maana kama sivyo, msanii mwenye atazongwa na kusutwa na dhamira yake mwenyewe, kwa sababu iwavyo vyovyote, msanii anatarajiwa ayaone yanayopita katika jamii yake kwa jicho pana na la ndani zaidi.
“Kwa hivyo kama wapo watu watatupuuza, watatubeza na au kutotoa maana kwa kila mara kusema, kuonyesha na kuelekeza kuwa tunakokwenda siko, basi angalau sisi tutafurahi, maana tumesema. Sisi ni bora zaidi kuliko wale waliokaa kimya na akhasi zaidi kuliko wale wenye kudhulumu, kutesa na kunyakuwa na wakaendeleza wanayoyafanya ilhali wanajua wanafanya sivyo. Wao huwa nguvu zimewapa kiburi, ila nasi tunajua kuwa kiburi ni cha Mwenyenzi Mungu tu.”
Zanzibar Daima Publishing ina fahari kupata fursa ya kuwa mchapishaji na msambazaji wa diwani hii ya hadithi fupi fupi. Inapatikana sasa ulimwenguni kote kupitia mtandao wa Amazon na Kindle.
Unaweza pia kuagizia moja kwa moja kama uko mataifa ya Afrika Mashariki kupitia kghassany@gmail.com.