Wakale kenda safari kwa ndege, usukani marubani wawili
Mwengine leo hii vyereje, kwa msururu wa gari?
Njiani kihanikiza vishindo na shangwe, keli ya kubana hali
Ninaomba nielezwe, kubana matumizi ni nini?
Mguu mosi mguu pili, wingi wa tarishi na wafuasi
Ndani chungu ya motokari, pia wamo mawaziri na polisi
Wakipita mwendo wa kasi, safari yao Kigali
Sasa hebu munieleze, kubana matumizi ni nini?
Wakayachoma mafuta, kwa wingi wa utitiri
Eti kwao hiyo maana, ni nafuu ya matumizi
Asojua maana hapewi maana, hili ni ya kale yetu kauli
Naomba leo nielezwe, kubana matumizi ni nini?
Wakafika yao safari, kwenye mji wa Kigali
Shughuli kubwa ni uzinduzi, wa buruji la njia za gari
Ikafatia ya pili, ni maadhimisho ya kimbari
Basi japo munieleze, kubana matumizi ni nini?
Kigali msururu ulifika, madereva, mawaziri na tarishi
Wote wahitaji zao huduma, maakuli na hoteli za malazi
Kisha wapatiwe na wao ujira, safari nje ya nchi kikazi
Kwa uwazi munieleze, kubana matumizi ni nini?
Ugeni ulikhitimu yake ziara, kwa zawadi adhimu ya Ankoli
Ila bado mwenzenu natatizwa, Ankoli alipanda eropleni?
Au utitiri wa msafara, walirudi nazo garini?
Hebu sasa nieleze, kubana matumizi ni nini?
Safari ya kurudi ikawadia, mkuu akadapia eropleni
Kwa safu usiku akalakiwa, Daslama usiku wa manani
Je ni kweli ameziacha Kigali, Au zilibeba Ankoli?
Ningependa nielezwe, kubana matumizi ni nini?
Ni wa gubi huu ureda, chambilecho mafanani
Sipati jawabu ya kung’amua, mawaziri, madereva na polisi?
Kwa kubana matumizi, iwe kawaacha Kigali?
Naomba nielezwe, kubana matumizi ni nini?
Suleiman Shaaban Suleiman
01 Oktoba 2016
Zanzibar