KISWAHILI KINA WENYEWE

Changi N’Kuchangizana: Tungo za Kiswahili

Ushairi ni sauti ya ndani. Ndani kabisa huko moyoni na huko kwenye chumba cha ndani cha ubongo, ambako mshairi hujisemesha na kuusemesha ulimwengu wake na wa wenzake. Ushairi ni hisia na pia ni fikira ya ndani. Kwa kuwa kwake sauti ya ndani, kunaufanya uwe kielelezo cha fikra huru za mwanaadamu, kwani huwa anajisemesha akiwa peke yake, pasina na nguvu za nje anazozikhofia kumsakamiza matambara mdomoni.

Mshairi ni ndege aamkaye kiotani mwake asubuhi na mapema, akayatumbuiza mandhari kwa njia za kuyasawiri, kuyasema, kuyasemea, na kuyatarajia, bali hata kuyasuta na kuyakosoa. Mshairi ni wimbi la bahari livumalo katikati ya mkondo na mto utiririkao milimani, ukipenya mule ambamo wenda kwa miguu wa kawaida, hawawezi kumupita. Mshairi ni maji ya mvua inyeshayo kutononesha ardhi, na pia mshairi ni jua liwakalo kukausha vilivyo juu ya ardhi hiyo.

Na Mohammed K. Ghassani
Na Mohammed K. Ghassani

Kwa bahati mbaya, hata hivyo, si kila ushairi unaoimbwa ndani ya nafsi ya mshairi hubahatika kuja kuimbwa hadharani ama kuwekwa maandikoni. Daima tungo zilizotungwa ni nyingi zaidi kuliko zile zilizowahi na zitakazowahi kutufikia sisi, hadhira, katika vipindi vyote vya historia ya mwanaadamu. Hutokea sadfa tu kwamba baadhi ya tungo hizo hupata nafasi ya kuhifadhiwa na kusambazwa, zikaenda mbali, nje ya jengo la nafsi la mshairi mwenyewe, na kufika pa kufika. Sadfa hiyo huufanya ushairi kutoka kwenye kilango chake cha ndani na kuwa nyimbo ya kughaniwa kweupeni – jahara shahara – pa kila mtu kuusikia na kuuhisi.

Lakini ushairi si kila sauti ya ndani ajisemeshayo mshairi tu, maana mshairi naye ni mwanaadamu, ambaye mawasiliano yake mengine huwa si ya kishairi. Anapouvaa ushairi wake, ndipo hapo anapotoa na kutumia sauti yenye upekee; kwanza, kutokana na mapigo yake, kwa ule muziki na mahadhi yake; na, pili, ni kwa uzito wa ujumbe wake, upeo wa fikra zake na ule ujuzi wa mafunzo yake.

Ushairi ni sauti ya furaha kama ilivyo ya huzuni, ni sauti ya hasira kama ilivyo ya nasaha, ya kupongeza kama ilivyo ya kulaumu, ya kuagiza kama ilivyo ya kuitikia maagizo. Alimradi, katika undani wa dhati yake, ushairi husimama kama kauli inayojitegemea na kujipambanua.


SAUTI NDANI YA DIWANI

Mkusanyiko huu wa Changi N’Kuchangizana ni kielelezo cha fasili hii ya ushairi kama sauti. Ndani yake, muna sauti za ndani zinazonong’onwa kimyakimya na zinazopazwa kwa mayowe na washairi hawa saba, ambao wamekutanishwa humu kwa upeo wa fikra zao na mdundo wa muziki wao. Diwani hii ni kielelezo kuwa Waswahili si wachache wa sauti tangu zama na dahari. Kwa makusudi kabisa, tumechaguwa washairi chipukizi kutoka kila kipembe cha maisha – vijana kwa wa makamu, wanaume kwa wanawake, walimu kwa wanafunzi, na wanasheria kwa mameneja.

Ndani yake muna sauti zilizovuuka kingo za mito ya mawazo na kupasua viambaza vya nyoyo za washairi hawa. Kuna mahala, msomaji anasikia sauti ya hasira dhidi yake mpaka anatamani aache papo hapo kusoma na akitupilie mbali, maana kibinaadamu, huwa hakuna anayependwa kusutwa. Kwa mfano, msikilize Said Yunus katika utungo Ingawa (Uk. 23) akizungumza moja kwa moja nawe:

Ingawa mzuri
Usiwe jeuri, na kujisifia
Jipambe vizuri, kwa njema tabia
Fanya tafakuri, la utaumia

Ingawa a’limu
Usiwe dhalimu, watu kuzuzuwa
‘Katoa hukumu, usizozijuwa
Jua hutodumu, siku wakijuwa

Mwahala mwengine, ndani ya Changi N’Kuchangizana, msomaji anakutana na sauti ya ndani ikitema ujabari na ujasiri wa kijana anayesaka maisha, akijikosoa mwenyewe kwa ugoigoi wake na sio kuwakosoa wengine. Huyo ni Amour Haji Abdallah (Uk. 55), ambaye hadi diwani hii inachapishwa umri wake ni miaka 20 tu, lakini tayari upevu wa mawazo yake umevuuka milima ya miaka 50. Msikilize hapa akijisemea mwenyewe, ndani kwa ndani, kisha akiinuka kutoka huko gizani aliko, huku akiipaza sauti yake kwa nguvu za ajabu katika utungo ‘Mechoka Kusumbuliwa (Uk. 57):

Nimechoka sumbuliwa, na unyenye muilini
Chakula cha kugaiwa,  hakinishuki kooni
Uvivu waniumbuwa, naonekwa jitu duni

Nimechoka sumbuliwa,  na mikwaruzo tumboni
Ilhali natambuwa,  kinisumbuacho ni nini
N’ache nende yatatuwa, nikalitafute peni

 Nimechoka sumbuliwa, kwa ubwabwa kiganjani
Hogo kusukumiziwa, lis‘ojaa sahanini
Huku nikisimbuliwa, nijibweteka ja kwini

Mara nyengine, sauti hii ya ndani  huja na mafumbo ambayo yanadai ufumbuwaji, kama ilivyo desturi kongwe kabisa kwenye utanzu huu wa fasihi miongoni mwa Waswahili, kiasi cha kwamba wengine huamini kuwa bila kufumba, basi ushairi usingeitwa ushairi. Mshairi Amar Ruweihy anaonekana kuzama sana kwenye eneo hili, ndio maana takribani tungo zake zote kumi ama ni mafumbo ya moja kwa moja au mafumbo yaliyofumbwa kwa mfumo wa masuali kama vile Pete Ivawe N’Nani? (Uk. 2), Bata Kosale N’Lipi? (Uk. 3) na Kunitesa Kwani? (Uk. 4).

Hapa angalia namna fumbo lililofumbwa kwenye shairi Samaki Kukosa Chumvi (Uk. 7) linavyoyasawiri maisha halisi ya samaki wa baharini, majina yao, tabia zao, na kisha kumalizikia na suali linalosaka sababu ya samaki kuishi chumvini (baharini) na bado mwenyewe akawa hana chumvi:

Chumvi hajitoshelezi, huyu samaki kwa nini?
Mavyazi hadi makuzi, kutwa yumo baharini
Lakini mbona hawezi, kuwa na chumvi mwilini?

Uzawa wake majini, chumvini ni maskani
Kakulia humo ndani, tangu aje duniani
Ila akija nchini, chumviye hatuioni

Pweza ndiye peke yake, mzawa wa baharini
Hujitosheleza vyake, chumvi i mwake mwilini
Changu ‘takupiga teke, Nguru hata Saladini

Sauti ya ndani pia ni ya mama mlezi, ambaye sio kwamba anajikosoa mwenyewe tu, bali pia jamii yake iliyomzunguka. Kwa Waswahili, misemo na methali huchukuliwa kama maagizo matakatifu ambayo hayakosei wala hayatanguki. Lakini mshairi Salama Omar Othman (Uk. 31) anasema kwenye Uchungu wa Mwana (Uk. 41) kwamba misemo na methali zetu zinapaswa kutafsiriwa na hata kukosolewa na wanaozitumia. “Uchungu wa mwana aujuwaye mzazi“ ni msemo unaotumika kuonesha yote mawili: mapenzi ya mzazi kwa mtoto wake na pia maumivu anayoyapata mzazi huyo kwa mwanawe:

Aijuaye mzazi, chungu ya kupata mwana
Ela hautuagizi, kuachia huru wana
Vyema tuoneshe wazi, kama uchungu twaona

 Kudhihirisha uchungu, sio kupiga kelele
Kwamba hili chango langu, nani kanisaidile
Ikawa kwa walimwengu, mwana lolote angile

Ikawa alifanyalo, mvyele halipembui
Chango lanyanyuka hilo, nguoze hazimkai
Hapo lolote liwalo, yu tayari habagui

LUGHA NA MAUDHUI

changi_nkuchangizan_cover_for_kindleLugha ndicho chombo kikuu kinachoibeba fasihi na ndicho kinachoitafautisha sanaa hii na sanaa nyenginezo. Na katika ushairi, matumizi ya lugha huwa na jambo la ziada ambalo, yumkini, halionekani kwenye tanzu nyengine za fasihi. Mshairi hujipambanua na wanafasihi wengine kwa jinsi anavyoyatumia maneno yake kwa staili apendayo. Husemwa mshairi huimiliki lugha na sio yeye kumilikiwa na lugha. Na hili jambo la ‘umiliki’ humpa nguvu na udhibiti wa kwelikweli, baadhi ya wakati hata wa kuinyonganyonga na kuinyongoa, akikiuka misingi na kawaida za kiisimu.

Hebu angalia hapa lugha ilivyosanifiwa na kusarifiwa kiasi cha yenyewe kujikuta dhalili na madhulumu ikimtumikia mshairi Amour Haji mwisho wa kutumika, utumwa wa hiyari katika Nuru Haijafifia (Uk. 63):

Walipoizima, nuru yetu kwa upinde
Wakaisakama, wakaifanyia mbinde
Wakaisukuma, chini kwenye mabonde
Nyuso zao zikicheka!

Ikaporomoka, chini huko matopeni
Ikapuruchuka, toka mwao mikononi
Ikachawanyika, vipandepande sitini
Lakini haijafifia!

Haijafifia, bado nuru inawaka
Haijapotea,  bado inaakisika
Haijazubaa, topeni yataka toka
Iwaduwaze washenzi!

Kipande hiki cha ushairi kimesheheni tamathali za semi, lugha ya picha na uteuzi wa maneno. Kwa mfano, tangu mwanzoni, msomaji anakutana na picha ya mwangaza uliozimwa na hao watu ambao mshairi hakuwataja, lakini kwa kucheza kwake na lugha, uzimaji wa mwangaza (au tuseme kitu kinachotowa mwangaza huo) haukufanyika kwa kutumia vitu vya kawaida ambavyo kwenye maisha hutumika, kama vile tuzimavyo taa au mshumaa ama kijinga cha moto. La hasha! Amour anasema wazimaji hao wa nuru walitumia upinde, jambo ambalo tawi la semantiki kwenye isimu lisingekubaliana nalo. Ila kwa kuwa hii ni fasihi, basi uwezekano wa mshairi kukiuka kanuni za lugha ili kuwasilisha ujumbe, hukubalika. Ndio maana ule upinde utumiwao na wasasi kuwindia wanyama au wapiganaji vitani, ndio hapa umetumika kuizima nuru. Hapana shaka, hapa msomaji lazima akune kichwa kutaka kujuwa nuru gani hiyo inayozimwa kwa upinde na sio upulizo au kwa kiganja cha mkono? Na zaidi, kwa nini pamoja na kuutumia upinde, bado mshairi akasema kamwe nuru hiyo haikuzimika!?

Jambo la muhimu kulielezea hapa ni kwamba licha ya uwanagenzi wa washairi hawa waliomo humu, wamejidhihirisha kuwa na uweledi mkubwa wa lugha ya kishairi. Lugha, kama ilivyokwishasemwa, ndiyo msingi mkuu wa fasihi pale inapotumika sio tu kama lugha, bali lugha zaidi ya lugha. Ama kama wasemavyo wenyewe: “kila neno kwenye fasihi, huwa neno zaidi ya neno!”

Msomaji wa diwani hii atagundua mara moja amekutana uso kwa uso na wajuzi wa Kiswahili nje ya wale wenye majina makubwa aliokuwa akiwasikia. Inawezekana, kwa mfano, jina la Ibrahim Hemed wa Mombasa, Kenya (Uk. 79), lisiwe maarufu kwako, lakini utakapoushika ubeti mmoja wa mashairi yake, hapo hapo unajiona ukikiri kuwa umekutana na mwenyewe mwenye Kiswahili:

Lalopo lalikuwepo, kwambiwa sipo halipo
Halipo wapi lilipo, na hapo ndipo liwapo
Liwapo daima papo, panginepo huwa sipo
Sipo ndipo hawambia, papo ndipo likaapo!

Likaapo nijuwapo, si popote ila hapo
Hapo ndipo liwekwapo, napo ndipo lifaapo
Lifaapo huwa lipo, nijuwavyo  likiwapo
Likiwapo hamuwapo, mulipo nyote hamupo

Hamupo na mukiwa’po, hamuoni lililopo
Lilipo nanyi muwepo, musinene halilopo
Halilopo kwapi l’lopo, ambapo  mulionapo?
Napo ndipo liwekwapo, kwanginepo huwa sipo

Jambo jengine la muhimu kulitaja chini ya kipengele hiki ni uteuzi wa maneno, jambo ambalo ni lina umuhimu wa pekee kwenye sanaa ya ushairi. Maneno huchaguliwa kwa sababu ya kufaa kwake na pindi yanapotumika hukifu maana yake. Kwa mfano, angalia ubeti huu ulivyotumia neno “chombo” katika utungo Manahodha Wetu (Uk. 26):

Chombo kimeshika kasi
Abiria wana wasi wasi
Nahodha hana kisisi
Amepandwa na bilisi
Usukani umemnogea

Waswahili wanatumia neno chombo kwa maana tatu za kawaida na nyengine kadhaa zisizo za kawaida: (i) usafiri wa baharini na hata wa nchi kavu, ila wanapotumia wa nchi kavu husema chombo cha moto, wakikusudi gari, basi, treni na kadhalika, (ii) kifaa cha jikoni kama sahani, bakuli, sufuria na kadhalika, na (iii) kifaa chochote chengine. Katika maana zisizo za kawaida, ni kutumia neno chombo kumaanisha mtu mwenye sifa za aina ya kipekee kama uzuri sura, ujasiri, ujabari na kadhalika.

Mshairi Salama Omar anaandika shairi alilolipa jina La Mgambo, neno ambalo limeteuliwa kutokana na msemo wa Kiswahili “La mgambo likilia kuna jambo“ unaotumika kutoa tahadhari ya kujiri jambo au kutendeka kitu kisicho cha kawaida. Dhana ya mgambo imo zamani kwenye jamii za Waswahili wakikusudiwa watoaji indhari kwa kupita na ngoma kubwa au pembe mitaani. Baada ya tawala za kigeni zilizounda vyombo vya kisasa vya dola, dhana hiyo ikabadilika na kuwa askari rasmi wa serikali wanaoogopewa na kuchukiwa na watu. Uteuzi huu wa maneno una maana kubwa sana kwenye sanaa ya ushairi.

Katika shairi lake jengine, Yasiyomea kwa Mvua (Uk. 42), mshairi huyu huyu anatumia neno kipando, ambalo kwenye Kiswahili lina maana mbili katika matumizi ya kawaida: (i). chombo cha usafiri wa nchi kavu kama gari au baiskeli. (ii). mimea inayopandwa kwa ajili ya kupata chakula kama vile muhogo, viazi, na kadhalika:

Miche ya kila aina, hima tukaiatika
Vijimbi, viazi tona, navyo vikajumuika
Vipando  kila aina, mihogo yebahatika

Katika ‘Mechoka Kusumbuliwa (Uk.57), mshairi Amour Haji Abdullah, anadondoa maneno maalum ya kuyatumia kuwalikisha machungu yake ya kutokuwa na kazi akitumia chakula:

Nikatafute vibuwa, nikavuwe baharini
Ama nizimwage chuwa, nikalime mabondeni
Nipigwe juwa na mvuwa, nirowe jasho mwilini

Wali ni chakula muhimu kwa Waswahili, na hivyo lugha yao imejaa misamiati ya kuelezea viwango, aina, na hali mbalimbali za mchele, tangu ukiwa shambani unapoitwa mpunga, ukishatangwa huitwa mchele, ukidondolewa ule ambao hubakia na magamba yake huitwa chuwa, na hata huo wali uko wa aina kwa aina. Alimradi hakuna chakula chenye majina mengi kwenye Kiswahili kama wali.

Kitu chengine ambacho ni rahisi kukigundua kwenye diwani hii, ni namna ambavyo ushairi hutumika kuelezea kila kitu kwenye maisha – iwe siasa, yawe mapenzi, uwe uchumi, iwe elimu, na kadhaa wa kadha, na hayo huwa kwa viwango mbalimbali. Muktadha na mazingira aliyomo mshairi huiumba sauti yake na njia za kuitoa sauti hiyo. Msikilize, kwa mfano, Othman Ali Haji, ambaye wakati akimaliza masomo yake ya Kidato cha Sita (Darasa la Kumi na Nne)  visiwani Zanzibar, alijikuta uso kwa macho na uhalisia wa maisha. Kwa mfumo wa elimu wa kwao, Darasa la Kumi na Nne ni la mwisho kwa sekondari ya juu. Baada ya hapo, wahitimu ama huendelea na masomo ya vyuo vikuu au hurudi nyumbani kusaka ajira, naye wakati anarejea nyumbani akajikuta hapana mahala ambapo angeliajirika, si kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kielimu, lakini kwa kwa sababu zilizo nje ya hapo. Ndipo kutoka ndani kabisa ya chembe chake cha moyo, akausuta mfumo aliopambana nao kwa kuuzaba kibao cha uso:

Cha Sita  nisaza, kidato n’lonacho
Sauti nipaza, isikike kwacho
Ila nibaki naranda, ajira imekimbia!

Ajira sinayo, mitaani nazurura
Nijawa na choyo, nipandwa hasira
Elimu wasio elimu, ajira wanapatiwa!

Udugu kigezo, elimu si kitu
Wa chini apizo, huipati katu
Ila tunachodanganywa, elimu kujisomea!

Urasimu sera, bango la taifa
Hujuliki bora, elimuyo ufa
Ila twamba nchi changa, ajira hazijapea!

Hali ni sawa na kwenye kigawe cha mahusiano ya kimapenzi, kigawe kilichotungiwa tungo nyingi kabisa miongoni mwa watungaji wa fasihi duniani kote, yumkini kwa kuwa kwake sehemu moja muhimu sana ya maisha ya watu. Suleiman Mkubwa Khamis (Uk. 45) ana njia zake za kuyasawiri na kuyawasilisha, akiengaenga na wakati huo akirusha maneno ya hapa na pale yanayoashiria udhati na ukweli wa mapenzi yake akiutumia msemo wa kale “mapenzi kama asali” katika shairi lake Asali Ina Hadaa (Uk. 52):

Katika kupitapita, kwenye  yangu matembezi
Macho yangu yalipata, kuona kitu azizi
Na moyo bila kusita, sega wetaka lienzi

Denda likanidondoka, asali kutaka onja
Sega lilotakasika, ‘lojawa sifa za haja
Ila nyuki wanawaka, kusogea ni kiroja

Nitumie njia gani, kuonja hii asali?
Moyo umeshatamani, kuikosa ni muhali
Niibugie kinywani, ila nyuki ni wakali

USHAIRI NA UTAMADUNI

Kama zilivyo kazi nyengine za fasihi, ushairi nao ni kipimo cha namna jamii fulani inavyoutafsiri ulimwengu uliowazunguka na pia chombo cha kuhifadhia utamaduni wao. Waswahili ni watu wenye tareikh (historia) inayorudi nyuma sana na yenye mizizi mirefu kwenye upwa wa Afrika Mashariki. Utamaduni wao na utambuzi wao wa ulimwengu unaakisika kwenye namna wanavyoitumia lugha yao kuuelezea ulimwengu huo, mambo yanayojiri, yanayoingia na kutoka, na hata wanayoyapenda na kuyachukia. Hiki ni kipengele muhimu kinachoakisika kwenye diwani hii. Wangawa wanagenzi kama walivyo, washairi hawa wamethibitisha kwamba ni Waswahili wenyewe, wanaozijuwa kunga na akida za lugha, utamaduni na maana kwenye lugha yao.

Angalia, kwa mfano, wanavyozitumia nahau, kama ile ya kutema mate chini iliyo kwenye shairi Bata Kosale N’Lipi? (Uk. 3) la Amar Ruweihy Nassor:

Vipi bata umseme, pachafu ni maskani?
Ni vipi umsakame, kuwa yeye ndege duni
Na mate chini uteme, nyamaye usitamani?
Bata ni ndege jamali, wamfuga majumbani

Kwa utamaduni wa Waswahili, kutema mate chini unapokiona kitu au mtu ni ishara ya kukidharau kitu hicho au mtu huyo. Haya hayafahamiki ila kwa Mswahili mwenyewe, ambaye anayaishi maisha ya Waswahili hao.

Huyu huyu Amar Ruweihy anasema na kasuku katika shairi lake Kasuku Koma Kusema (Uk. 6), na ndani yake anamzungumzia mtamba, ambaye ni moja ya majina yanayotumika kumuelezea kuku, ingawa si kila kuku. Waswahili wanawagawa kuku kwenye makundi mengi kwa mujibu wa jinsia, umri, na hata maumbile. Mtamba ni kuku mke ambaye bado hajawahi kutaga. Kuku mke ambaye ameshataga anaitwa koo. Lakini kuku anavyotumika kwenye Kiswahili kuna maana zaidi ya maana. Jogoo, ambaye ni kuku wa kiume, humaanisha mwanamme shababi, kijogoo humaanisha mwanamme anayependa wanawake, na huyu mtamba anayetajwa hapa, humaanisha mwanamke mwanamwari. Hata huyo kasuku anayesemwa hapa na mshairi, kwenye Kiswahili ni nahau itumikayo kumuelezea mtu asiyeweza ulimi wake, mtu m’mbeya.

Angalia pia shairi Kubadilisha Majina (Uk. 8), ambalo linazungumzia mila ya kubadilisha majina ya maharusi, hasa ya mabiharusi, inayoendelezwa kwenye miji mingi ya kusini mwa pwani ya Afrika Mashariki. Mila hii inaambatanishwa na utabiri wa nyota, ambapo wahusika huamini kuwa kama mtu akibakia na jina lake la asili, basi ndoa yake inaweza kuwa na matatizo. Hiki ni kitu cha ndani ambacho kukifahamu kwake na kukitumia kwenye fasihi kunamlazimu mtu awe ama ni mzawa au amekaa sana na kuutafiti utamaduni wa Mswahili.

Ndani ya shairi hilo hilo, munatumika neno Rusha Roho, ambayo ni aina mpya ya muziki wa taarabu inayojumuisha mipasho na mara nyingi inayohusu ugomvi wa kimapenzi baina ya wanawake. Huchezwa kwenye mikusanyiko ya harusi, sherehe za kitamaduni na hata kisiasa, kidogo kidogo ikichukuwa nafasi ya msondo ya ngoma ya msondo.

Katika shairi Tumbo Mchongea Domo (Uk. 17), Said Yunus anatumia misemo ya Ambari na Zinduna na chanda na pete, akisema:

Mimi na yeye tulivyo, ni kama chanda na pete
Nikipata apendavyo, sharti yeye apate
Hata kama ni cha ovyo, naye pia kimpite
Yamekuwa mazoea, ya Ambari na Zinduna

Hekaya za Kiswahili zinasema hawa Ambari na Zinduna walikuwa mtu na  mkewe – Ambari mume na Zinduna mke – ambao walipendana sana na kuishi na kwenda kila mahala pamoja na hata siku ya kufa pia wakafa wakiwa pamoja. Kuna msemo wa Kiswahili: “Ukimuona Ambari, na Zinduna yuko nyuma“ ukiashiria maisha ya wapenzi hawa wawili. Misemo mingine iliyomo kwenye lugha ikiakisi mkasa huu, ni pamoja na “chanda na pete“ (ambao pia umetumika kwenye ubeti wa tatu) na “kifa kifanana“.

Mahala pengine, mshairi huyu huyu anatumia nahau kugonga mwamba, pale anaposema:

Sasa nimegonga mwamba, sijui vya kufanyiza
Kila ninayemuomba, kwake yeye kunibeza
Nimebaki omba omba, mahaba yaniumiza
Mapenzi yananitimba, yanila yaniumiza
(Uk. 24)

Waswahili ni watu wa pwani na misemo yao mingi inaakisi maisha ya pwani. Kugonga mwamba katika lugha ya kawaida ni kitendo cha chombo cha baharini kupinduka kwenye maji makubwa baada ya kupigwa na wimbi zito, lakini katika matumizi ya ziada, hii ni nahau inayomaanisha mtu kushindwa baada ya kujaribu sana.

Muakisiko wa lugha, utamaduni na maana ya ulimwengu pia unaonekana kwenye utungo uitwao Masikini Roho Yako (Uk. 19), pale mshairi anaposema:

Umedhamiria nini, jamii yako, kuifanyia?
Utawaeleza nini, watu wako, wakikujia?
Utawambia nini, wazee wako, wakija kukushtakia?
Utawafanya nini, watoto wako, wakikuambia?
Mbona unajitia pambani?
Tuseme husikii?

Asili ya nahau kutia pamba masikioni unatokana na kisa cha kale kwenye moja ya nchi za Waswahili, ambao pindi mtawala alipokuwa akiwaita watu wake kuwaamuru jambo ambalo hawakutaka kulifanya, walikuwa wanakwenda kumsikiliza huku wakiwa wamejiweka vipamba masikioni mwao, na kisha wanarudi nyumbani na hawafanyi jambo hilo, na siku wanapoulizwa wanasema hawakusikia kwani wakati mfalme alipokuwa akizungumza wao walikuwa wanaumwa na masikio na wakawa wamewekwa vipamba masikioni.

Utungo La Mgambo wa Salama Omar (Uk. 32) linaakisi uhalisia mwengine kwenye jamii za Kiswahili. Wote mzima umeandikwa kwa mazingira ya uganga wa kienyeji ambao unahusisha matibabu ya kuondosha mashetani au kupambana na uchawi dhidi ya mgonjwa. Jamii za Waswahili zinaamini sana juu ya uwepo wa dunia ya siri inayokaliwa na viumbe wenye nguvu za ajabu na ambao baadhi ya wakati huingia kwenye ulimwengu wa kawaida wanaoishi wanaadamu na kuwadhuru au kuwasaidia kwa mujibu wa kiumbe aliyeingia. Wana misamiati kadhaa inayohusu majina ya viumbe hao kama vile majini, mashetani, pepo, vibwengo, makomanzi, na kadhalika.


Hilo linaakisika kwenye tungo nyengine ziliozomo humu, kama vile  Mtambwe Yeanza Kale (Uk. 10),  ambapo mshairi Amar Ruweihy anazungumzia mkasa wa Bi Kirembo (wengine humuita Bi Kirembwe) na Bi Mwanaache Bint Hassan. Mkasa huu ni sehemu ya ngano zinazosimuliwa sana kisiwani Pemba. Mtambwe ni rasi maarufu kaskazini mwa kisiwa hicho, ambayo kuna wakati fulani kwenye historia yalikuwa makao makuu ya utawala wa eneo hilo. Bi Kirembo anaaminika na wakaazi wa nchi za Uswahilini kuwa ndiye aliyekuwa mkuu wa wachawi wote wa upwa wa Afrika ya Mashariki, akiwa mzaliwa wa Kiuyu, kaskazini ya Pemba, mwenye makao yake makuu Ging’ingi, kusini Pemba. Mwanaache Bint Hassan alikuwa pia bingwa wa uchawi ingawa si kwa kiwango cha Bi Kirembwe.

Usimulizi wa mkasa huu unachora picha ya historia ya Pemba na pia kuelezea imani za watu kwenye masuala haya, kama vile ambavyo utungo wake mwengine wa N’ache N’chagawe (Uk. 13) unavyosindikiza ukweli huu. Utungo huu mzima umeandikwa kwa kutumia mazingira ya uganga na uchawi:

N‘ache n‘chagawe, apande kichwani
Naaje mwenyewe, kwenu insani
Anene mujuwe, anenacho nini

Ulimi wa kwake, kashapasuliwa
Si mume si mke, nyote awajuwa
Si pepo mheke, yuajielewa

Kama zilivyo jamii nyingi duniani, Waswahili nao wanaamini pia juu ya kuwepo kwa ulimwengu wa siri ambao huingiliana na kuishi na ulimwengu wa dhahiri. Viumbe vinavyoishi kwenye ulimwengu huo wa siri huitwa majina mbalimbali kama vile pepo, shetani, majini, vibwengo, makomanzi, na kadhalika. Pale kiumbe mmoja kati ya hao anapokuja kwenye ulimwengu wa dhahiri, Waswahili wanaamini hufanya hivyo kupitia binaadamu wa kawaida, na ndipo husema kuwa binaadamu huyo aliyetumiliwa amechagawa au amekumbwa. Au pale binaadamu mwenyewe kwa hiyari yake ama kushawishiwa anapoingia kwenye ulimwengu huo wa siri, husemwa kuwa ameingia uchawini au ametolewa kikowa.

Lakini imani hii ya masuala ya uchawi kwa Waswahili inakwenda sambamba na imani yao kwenye masuala ya dini, jambo ambalo linaweza kutafsirika kwa wengine kuwa ni kinyume-mbele, ingawa ndio uhalisia. Mwahala mwingi kwenye diwani hii, utakutana na athari za imani ya dini ya Kiislamu, imanii inayofuatwa na asilimia kubwa na Waswahili wenyewe. Katika shairi la Wabaini Waja (Uk. 11), kwa mfano, kuna ubeti huu:

Shujaa siye mwengine, bali muweza nafusi
Matendo yako yapime, utende kwa ufanisi
Jitahidi uwe sime, alani mwako jikisi

Nasaha hii inatokana na kauli ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwamba shujaa si yule mtu anayempiga na kumshinda adui yake, bali yule anayeidhibiti nafsi yake inapokuwa na hasira.

BAINA YA ‘UWANAMAPOKEO’ NA ‘USHAIRI HURU’

Bila ya kuingia ndani kwenye mjadala mkongwe wa fasili ya ushairi wa Kiswahili, ambao katika siku zake za unyemi kwenye miaka ya ’70 hadi ’90 ulizua kambi mbili zilizolumbana sana kitaaluma juu ya sifa halisi za ushairi, washairi waliomo humu wamekuja na majawabu yao wenyewe. Ingawa tungo zao nyingi zimeandikwa kwa bahari ya tarbia – ambayo ni mashuhuri mno miongoni mwa washairi wa Kiswahili – wamo pia walioandika kwa mitindo mingine ya ushairi inayoelekea sana kwenye kile kinachoitwa “mashairi huru”.

Hata hivyo, kiwango cha uhuru wanachoamini washairi hawa, na yumkini ndiyo ilivyo sehemu kubwa ya washairi wa Kiswahili, kimeshikiliwa kwa vikuku ndani vya kile tunachoweza kukiita “umapokeo-mwepesi”, yaani kiasi fulani cha urari wa vina na au wa mizani. Hili linasema ukweli mmoja muhimu sana katika ushairi wa Kiswahili, kwamba si vina na mizani pekee vinavyoufanya utungo kuwa utungo, bali pia mantiki yake na mahadhi yake.  Kwa mfano, katika utungo Kataani (Uk. 20), Said Yunus anatumia mbinu hii:

Haiwi, na wala haitokuwa
Kataani nakataa
Kuonewa!
Kubugudhiwa!
Kusulubiwa!
Kamwe haitokuwa

Kwa jicho la kawaida, mtu angeweza kuuita utungo huu kuwa ni hilo “shairi huru” kwa kuwa halimo kwenye bahari zilizozoeleka za tarbia, tathlitha, takhmisa au tasdisa, lakini kwa mwenye kuujuwa usuli wa utungo wa Kiswahili, itamuelea haraka kuwa hata utungo huu nao unaangukia kwenye uitwao “umapokeo” kwa uzingatifu wa vina vya mwisho (-a na –wa), ambavyo kiimbo chake kinawiana, hata kama mizani zinatafautiana baina ya mshororo na mshororo wa kila ubeti.

Mitindo mfano wa hii pia imetumiwa na Othman Ali Haji kama kwenye utungo Kwa Jina la Uzanzibari? (Uk. 75):

Nchi hii yashangaza
Elimu watu waviza
Udugu wao wakuza
Urasimu waongoza
Majina wao wajiita –
“Wazanzibari!”


Mwisho, diwani hii imepewa jina la Changi N’Kuchangizana kwa kuakisi msemo na utamaduni wa Waswahili ambao pindi wanapokuwa na shughuli ya kijamii – hasa harusi – basi husaidiana kwa hali na mali ili kuifanikisha. Kila familia, ndugu, jamaa, marafiki na majirani, hutoa walichojaaliwa na kuifanya harusi ya mwana wa mwenzao kuwa yao. Kinachotolewa huitwa changi.

Na ndio maana, mbali ya kuwa sauti yao ya ndani iliyopata sadfa ya kusikika hadharaani kupitia diwani hii, changi hizi ni sehemu ya walichojaaliwa washairi wetu hawa saba katika kuongeza utajiri wa fasihi yetu ya Kiswahili. Ipokeeni!

2 thoughts on “Changi N’Kuchangizana: Tungo za Kiswahili”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.