Pafukapo moshi, moto wakaribia
Kipwagacho jikoni,mezani chasubiriwa
Kieleacho baharini, pwani kitawadia
Hakuna liso mwisho, toka zama daharia
Chema kisitrini, tuhali kuharibia
Mwendo kama tausi, shwari yake tabia
Sie hasa afiriti, vya watu kuvidowea
Hakuna liso mwisho, toka zama daharia
Kibibi wetu mzuri, kwa sifa katimilia
Mwendo wake na sauti, katimia malkia
Rangi yake zifuri, mwendo wake wa ngamia
Hakuna liso mwisho, toka zama daharia
Wamsemao kwa chuki, kwa kweli wamkosea
Kweli kasoro hakosi, aloumbwa na jalia
Ila mwamtia nyingi dhiki, mabaya kumzulia
Hakuna liso mwisho, toka zama daharia
Mulosema si kweli, afiriti mumezua
Ati kakwapua mali, sio yake ilokuwa
Kwa ushahidi lukuki, muloleta kupalilia
Hakuna liso mwisho, toka zama daharia
Mlosema yamejiri, asilani kumtokea
Kwa viapo na takbiri, mupate kuaminiwa
Awe kiumbe dhalili, kwa watu jumuiya
Hakuna liso mwisho, toka zama daharia
Amedhirisha Jalali, ya uongo mlozua
Haikumfika idhilali, mulopanga kumtia
Imewafika simanzi, aibu kubwa ya dunia
Hakuna liso mwisho, toka zama daharia
Azuliwaye maiti, hawezi kujitetea
Hukumu yake siratwi, kwa Mola wetu Jalia
Huko ‘tapewa haki, kila alodhulumiwa
Hakuna liso mwisho , toka zama daharia
Suleiman Shaaban Suleiman
23 Agosti 2016
Napenda mnavyofanya mambo nyie wakuu wangu.kazi kuntu.