Sikitiko, ni simanzi kwa mengi mateso
Sikitiko, tamaa tele mbele majuto
Sikitiko, hujaa moyoni na kekefu ya joto
Sikitiko, mbegu ya jana zao la kesho
Sikitiko, la nafsi idhilali na jekejeke la roho
Siktiko, latia ndwele na mengi mateso
Sikitiko, mwanzo nuru kiza huwa mwisho
Sikitiko, mbegu ya jana zao la kesho
Sikitiko, ladumaza kiwiliwili seuze macho
Sikitiko, halichagui mvyele wala mtoto
Sikitiko, likiwa kwako kwa wenzio ni kicheko
Sikitiko, mbegu ya jana zao la kesho
Sikitiko, kiumbe haliwezi kwa uzito
Sikitiko, hujaanamia dhalili mja kuliko
Sikitiko, halina shuja wa medali na vito
Sikitiko, mbegu ya jana zao la kesho
Suleiman Shaaban Suleiman